STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, March 19, 2014

Breaking News: Goli la Kavumbagu laua shabiki Taifa

KAVUMBAGU (KULIA) AKISHANGILIA NA WENZAKE BAADA YA KUIFUNGIA YANGA BAO DHIDI YA AZAM FC KWENYE UWANJA WA TAIFA, DAR, LEO.
Shabiki anayeaminika ni wa Azam FC, ameanguka na baadaye kupoteza maisha, dakika chache baada ya mshambuliaji wa Yanga,  Didier Kavumbagu kuifungia timu yake bao.


Baada ya Kavumbagu kufunga bao hilo, shabiki huyo aliyekuwa amevaa jezi nyeupe na kutambulishwa kwa jina la Deodatus Isaya Mwakiangula.
Imeelezwa Mwakiangula ni meneja wa baa ya Rose iliyo katika eneo la Kimara jijini Dar es Salaam.
Mmoja wa madaktari viongozi waliokuwa kwenye Uwanja wa Taifa, leo na kumhudumia Mwakiangula kabla ya kupoteza maisha, Nassor Matuzya alithibitisha kuhusu kifo hicho.
Madaktari hao walifanya juhudi kuokoa maisha ya MWakiangula lakini hata hivyo ilishindikana.

Kavumbagu alifunga bao lake katika dakika ya 14, hata hivyo baadaye Azam FC walisawazisha zikiwa zimebaki dakika 8 mpira kwisha kupitia Kelvin Friday.

SALEHJEMBE

Yanga yabanwa Taifa, Azam yaendeleza rekodi

* Hamis Kiiza 'Diego' akosa penati
Wachezaji wa Yanga wakishangilia bao lililofungwa na Didier Kavumbagu (wa pili kulia), wakati wa mchezo wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara ilipopambana na Azam  FC kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo. Timu hizo zilitoka sare ya 1-1. (Picha na Francis Dande)
Heka heka: Golikipa wa timu ya Azam FC, Aishi Salum akiokoa moja ya hatari langoni mwake.
Mfungaji wa bao la Yanga, Didier Kavumbagu akitafuta mbinu za kuwatoka mabeki wa Azam FC.
Beki wa Azam FC, Gadiel Michael akimiliki mpira (kushoto) akiwania mpira huo ni mshambuliaji wa yanga, Hamis Kiiza. 
Mashabiki wa Yanga, wakiwa hawaamini timu yao ikibanwa na Azam
Mshambuliaji wa Yanga, simon Msuva akimtoka beki wa Azam FC, Kipre Bolou

BAO la dakika ya 83 lililofungwa na kinda Kelvin Friday lilizima ndoto za Yanga za kutaka kuvunja rekodi ya Azam ya kutopoteza mchezo wowote katika Ligi Kuu Tanzania Bara na kuisaidia vinara hao kupata sare ya bao 1-1 dhidi na watetezi hao.
Yanga waliokuwa wakitaka kulipa kisasi cha kulazwa mabao 3-2 katika mechi ya kwanza bao la uishindi likifungwa pia na kinda mwingine wa Azam, Joseph Kimwaga, watajilaumu baada ya kupata penati iliyopotezwa na mshambuliaji Hamis Kiiza 'Diego'.
Kipa Aishi Manula aliyekuwa nyota wa mchezo huo kwa leo alipangua mkwaju wa Diego na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda kabla ya beki wake wa pembeni, Erasto Nyoni kulimwa kadi baada ya kuzozana na mwamuzi Hashim Abdallah.
Bao la Yanga lililowapa matumaini ya kupunguza pengo la pointi baina yao na vinara hao wa ligi hiyo, liliwekwa kimiani dakika ya 14 kupitia kwa Didier Kavumbagu bao lililodumu hadi mapumziko.
Washambuliaji wa Yanga watajuta kwa kuikosesha mabao timu yao baada ya kukosa mabao mengi ya wazi wakiongozwa na Kiiza, Emmanuel Okwi na Kavumbagu kabla ya Husseni Javu kuingia.
Kwa matokeo hayo ya leo, Azam wameendelea kujiimarisha kileleni kwa kufikisha pointi 44, nne zaidi ya Yanga inayokamata nafasi ya pili ikiwa na pointi 40 na kufuatiwa na Mbeya City yenye pointi 39.
Hata hivyo Yanga bado ina mchezo mmoja mkononi baada ya klucheza mechi 19 wakati Azam imecheza 20.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea wikiendi kwa michezo kadhaa ambapo Yanga itasafiri hadi Tabora kuvaana na Rhino Rangers na Simba itaumana na Coastal Union Mkwakwani Tanga.

Yanga, Azam ni vita tupu taifa

Azam Fc

Yanga SC
VITA tupu na pambano la kisasi baina ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga na vinara wa sas wa ligi hiyo, Azam wakati wababe hao wawili watakaposhuka dimbani leo kupepetana katika pambano pekee litakalochezwa uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Yanga itashuka dimbani leo ikiwa na kumbukumbu ya kipigo cha mabao 3-2 iliyopewa na wapinzani wao ambap hawajapoteza mchezo wowote mpaka sasa katika ligi ya msimu huu ikiweka rekodi tangu walipopanda Ligi Kuu msimu wa 2008.
Azam inayoongoza msimamo wa ligi ikiwa na pointi 43 itaikabili Yanga ikiwa na kumbukumbu ya ushindo mnono iliyopata kwa mabingwa wa zamani wa kandanda Coastal Union waliowacharaza mabao 4-0, huku Yanga ikishuka Taifa ikitoka kulazimishwa suluhu na mabingwa wa 1990-2000 na 2000-2001,  Mtibwa.
Watetezi wanahitaji ushindi katika mechi hiyo ili kulipa kisasi na pia kupunguza pengo la pointi na wapinzani wao waliowazidi pointi nn4, kwani wenyewe wana pointi 39 licha ya kuwa na mchezo mmoja mkononi.
Hata hivyo mechi hiyo ni ngumu kutabirika kutokana na ubora wa klabu zote mbili ambazo zitawakosa baadhgi ya nyota wao walio majeruhi.
Yanga wenyewe wataikabili Azam ikiwa imekamilika baada ya kurejea dimbani kwa nyota wake kama Haruna Niyonzima, Mrissoh Ngassa na Mbuyi Twitte, licha ya kukosa huduma za kipa Deo Munishi 'Dida;.
Makocha wa timu zote mbili wamenukuliwa kuwa vijana wao wapo tayari kwaajili ya pambano hilo, huku viongozi wa Azam wakiwa na imani kubwa ya kuibuka wababe kwa Yanga ili kutimiza lengo lao la kuwa mabingwa wapya wa Tanzania Bara baada ya kukwama misimu miwili mfululizo wakishika nafasi ya pili.
Je ni Yanga watakaoibuka kidedea na kulipa kisasi katika mechi hiyo itakayochezeshwa na mwamuzi Hashim Abdallah au ni Azam itakayoendelezaubabe na kuking'ang'ania kiti cha uongozi wa ligi hiyo leo? Tusubiri

Abdallah Juma alia na Yondani, refa red card aliyolimwa Jamhuri

Abdallah Juma enzi akiichezea Simba
MSHAMBULIAJI wa Mtibwa Sugar, Abdalla Juma amelia na mwamuzi Zakaria Jacob na beki wa kati ya Yanga, Kelvin Yondani kutokana na kadi nyekundu aliyopewa kwenye mchezo wao na Yanga wikiendi iliyopita ulioisha kwa suluhu.
Juma, alisema alilazimika 'kuchapa' Yondani baada ya kushindwa kuvumilia vitendo alivyokuwa akifanyiwa na beki huyo uwanjani alivyovilalamikia kwa refa, lakini alipuuzwa mpaka alipandwa na hasira na kulimwa kadi hiyo.
Mshambuliaji huyo, mmoja wa wachezaji watatu waliofunga hat trick kwenye Ligi Kuu ya msimu huu, alisema Yondani alikuwa akimchezea kibabe wakati mwingine kumfinya, kumpiga makusudi na hata alipolalamika alipuuzwa.
"Laiti mwamuzi angekuwa 'fair' na kusikiliza malalamiko yangu juu ya uhuni nilikuwa nafanyiwa na Yondani naamini nisingefia pale, sijawahi kupewa kadi ya njano wala nyekundu kabla ya tukio hilo la Jamhuri, nimeumia sana," alisema.
Hata hivyo aliwaomba radhi wachezaji wenzake wa Mtibwa kwa kadi hiyo na kuelezwa ni vigumu mtu kuvumilia katika mazingira aliyokutana nayo siku ya mchezo huo kutokana na kuichachafya ngome ya Yanga na kumdhibi kihuni.
"Baada ya kuonekana tishio kwao waliamua kutumia 'uhuni' kunidhibiti na kwa kuwa refa alikuwa upande wao, walifanikiwa kunitoa mchezoni na kulimwa kadi hiyo ambayo ni ya kwanza kwangu tangu nianze kucheza soka," alisema Juma.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa AFC Arusha, Kagera Sugar na Simba alilimwa kadi hiyo nyekundu na mwamuzi Jacob dakika ya 53 baada ya kumchezea rafu mbaya, Yondani, kabla ya hapo ndiye mchezaji aliyekuwa tishio kwa Yanga.

Mwisho

Askari kanzu, Camera maalum kulinda pambano la Kaseba, Mashali PTA

Kaseba

Mashali
ASKARI kanzu na Kamera Maalum ndizo zitakazotumika kudhibiti hali ya ulinzi katika pambano la kimataifa la ngumi za kulipwa kuwania mkanda wa UBO Afrika kati ya Japeph Kaseba 'Champion' na Thomas Mashali 'Simba Asiyefugika' litakalofanyika Machi 29.
Pambano hilo la uzani wa kati litafanyika kwenye ukumbi wa PTA-Sabasaba jijini Dar es Salaam ambapo kutokana na mabondia hao wawili kuwa na mashabiki wengi, waratibu wake wamepanga kuimarisha ulinzi ili kuwafanya mashabiki watakaofika ukumbini kutokuwa na hofu juu ya usalama wao.
Akizungumza na MICHARAZO, promota wa pambano hilo litakalosindikizwa na michezo mingine kadha ya utangulizi, Ally Mwazoa alisema ili kulinda usalama siku ya mchezo huo watatumia kamera maalum kunasa matukio ndani na nje ya ukumbi ili ikitokea tatizo iwe rahisi kuwabaini wahusika.
Pia alisema mbali na kamera hizo, pia watatumika askari kanzu ambao watakuwa wakifuatilia matukio ndani na nje ya ukumbi ili kuweza kudhibiti uvunjifu wowote wa amani kwenye pambano hilo linalowakutanisha kwa mara ya kwanza Kaseba na Mashali.
Mwazoa alisema utaratibu huo pia utatumika katika pambano litakalofanyika April 26 ambaloo pia ameiandaa yeye kati ya Francis Miyeyusho dhidi ya mtoto wa bingwa wa zamani wa dunia wa WBU, Rashid Matumla, Mohammed Matumla 'Snake Boy Jr'.
Kuhusu maandali ya pambano la Kaseba na Mashali, Mwazoa alisema kila kitu kimekaa vyema na kwamba michezoi ya utangulizi siku hiyo itakuwa ni katika ya Haji Juma dhidi ya Juma Fundi, wakati Fred Sayuni atapambana na Rajabu Mahoja na Zuber Kitandula atamenyana na Issa Omar wakati Bakari Dunda ataoneshana ubabe na Baina Mazola
Pambano jingine lililokuwa liwakutanishe Allen Kamote wa Tanga dhidi ya Fadhil Awadh la kuwania ubingwa wa UBO-Mabara limefutwa kutokana na kifo cha Awadh aliyefariki jijini Dar es Salam baada ya kuugua ghafla na kuzikwa juzi mjini Morogoro.

Mashetani Wekundu leo ni kusuka au kunyoa Ulaya

Manchester United
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Englan ambao wapo kwenye msimu mbaya, watakuwa na kazi nzito leo mbele ya Olympiakos ya Ugiriki, ili kuamua hatma yao ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwakani.
Kipigo cha 2-0 ilichopewa ugenini wiki mbili zilizopita zimeifanuya Mashetani Wekundu hao kulazimika kushinda nyumbani kwenye uwanja wa Old Trafford ikiwa ndiyo nafasi pekee kwao kuweza kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao kutokana na kupoteza nafasi ya kushiriki michuano hiyo msimu ujao kupitia nafasi nne za juu katika msimamo wa Ligi Kuu England.
Man United kwa sasa inashika nafasi ya saba katika msimamo wa Ligi Kuu  ikiwa ponti 12 nyuma ya timu inayoshika nafasi ya nne, Man City ambayo hata hivyo ipo nyuma mechi mbili dhidi ya Man U.
Timu inayoongoza msimamo huo ni Chelsea ikiwa na pointi 66, ikifuatiwa na Liverpool na Arsenal ambazo zina pointi 62 huku Tottenham ikishika nafasi ya nne kwa pointi 53 ikifuatiwa na Everton yenye pointi 51 tatu mbele ya Man U.
Kwa mantiki hiyo kama United itashindwa kuibuka na ushindi dhidi ya Olympiakos leo na kisha kucheza kwa 'jihadi' hadi kutwaa ubingwa, itakuwa imepoteza nafasi ya kushiriki michuano hiyo msimu ujao kutokana na matumaini yao ya kumaliza nafasi ya nne kutoweka.
Tangu klabu hiyo ianzishwe imeshiriki michuano hiyo ya Uefa mara 26 huku ikiutwaa ubingwa huo  mara tatu, hivyo kuikosa michuano ya msimu ujao itakuwa mwanzo mbaya zaidi kwa David Moyes tangu alipomrithi Sir Alex Ferguson aliyeiongoza timu hiyo kwa mafanikio makubwa kuanzia 1986-2013. United imeutwaa ubingwa Uefa msimu wa 1967–68, 1998–99 na 2007–08
 Kadhalika hii itakuwa mara ya pili mfululizo kwa Man United kutolewa katika hatua ya 16 bora baada ya msimu uliopita kutolewa na Real Madrid kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya mechi ya awali Santiago Bernabéu kumalizika kwa sare ya 1-1 na mechi ya marudiano Old Trafford Madrid kushinda 1-2.
Hata hivyo, Man United itashuka katika Uwanja wao wa Old Trafford ikichukua tahadhari kubwa dhidi ya mshambuliaji wa Arsenal anayeichezea Olympiakos kwa mkopo, Joel Campbell ambaye alitupia moja kati ya mabao hayo mawili.
Campbell ambaye tayari amepania kuonyesha makali yake kwenye dimba hilo, amesema ni vema kwenda Old Trafford na kuonyesha kiwango kwa kuwa wanaamini kuna mafanikio makubwa wanakaribia kuyapata.
"Tunajua tunakaribia kupata mafanikio fulani makubwa," mshambuliaji huyo wa Olympiakos raia wa Costa Rica alisema.
"Kuonyesha uwezo Old Trafford ni kitu muhimu sana. Ninaamini ni ndoto kubwa za wachezaji."
Jana usiku miamba minginine ya England, Chelsea ilikuwa na kibarua kigumu nyumbani dhidi ya Galatasaray baada ya mechi ya awali kutoka sare ya bao moja, huku Real Madrid ikikamilisha ratiba nyumbani dhidi ya Schalke 04 kutokana na kushinda 6-1 ugenini katika mchezo wa kwanza.
Borussia Dortmund ni timu nyingine ambayo itakuwa nyumbani leo kuikaribisha Zenit St Petersburg bada ya awali kushinda ugenini 4-2.
Galatasaray ambayo ilikuwa ikihofiwa kuhitimisha safari ya Chelsea katika michuano hiyo, kutokana na kuwa na mshambuliaji wa zamani wa miamba hiyo ya England, Didier Drogba, kama itakuwa imefanikiwa kuitoa 'The Blues', itajiwekea rekodi nzuri dhidi ya timu za England kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya 16 bora baada ya misimu iliyopita kuzitoa Arsenal na Manchester City.
United ambayo Jumapili ilikubali kipigo cha mabao 3-0 nyumbani dhidi ya Liverpool, matumaini yake yapo zaidi katika michuano hiyo ya Ulaya baada ya kuonekana kuwa katika wakati mgumu kutinga nne bora kwenye Ligi Kuu England ili kupata nafasi ya kushiriki ligi hiyo yenye utajiri mkubwa kwa ngazi ya klabu msimu ujao.
Licha ya kuwa katika wakati mgumu, Kocha David Moyes amesema kikosi chake kitapigana kutoka kwenye kucha hadi katika meno ili kuuweka msimu hai.
"Wachezaji wapo makini zaidi wakiwa wanamaanisha Jumatano (leo) na nini tunachotakiwa kukifanya," Moyes alisema.
"Tumepata jambo la kwenda kulifanya, kwa hiyo tunatumai tutalifanya hilo."
United ina rekodi ya ushindi nyumbani ya alisimia 100 dhidi ya wapinzani wao wa Ugiriki, kwani  Olympiakos imepoteza mechi 11 ilizocheza katika ardhi ya England.
Man United inaogopwa kutokana na rekodi yake ya kupindua matokeo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya 2007 'kuichenjia kibao'  AS Roma kwa kuichapa 7-1 baada ya mechi ya awali kufungwa 2-1.
Olympiakos pia itashuka uwanjani ikiwa na hamasa ya ushindi wa mabao 2-0 iliyoupata Jumamosi dhidi ya Panathinaikos na kuzidi kujihakikishia kutwaa ubingwa wa Ugiriki.
Pambano jingine la leo litazikutanisha timu za Borussia Dotmund itakayoikaribisha Zenith iliyowafungwa nyumbani kwao kwa mabao 4-2

Dar Modern kuuza sura videoni


KUNDI la Dar Modern 'Wana wa Jiji' lipo wilayani Lushoto-Tanga likirekodia video za nyimbo za albam zao mbili walizozizindua hivi karibuni wakati wakiwatambulisha wasanii wao wapya.
Akizungumza na MICHARAZO kutoka Lushoto, mmoja wa waimbaji nyota wa kundi hilo, Hassan Kumbi 'Hassani Vocha', alisema tayari asilimia kubwa ya video hizo zimesharekodiwa.
Albamu hizo ni; 'Oh My Honey' na 'Kitwitwi' zenye nyimbo kama 'Oh My Honey', 'Naenda kwa Mume Wangu', 'Sikuamini Macho Yangu' na 'Malipo Duniani', 'Kitwitwi', 'Ngoma Imepasuka' na 'Siwanyimi Uzuri'.
Dar Modern ilianzishwa mwaka 2006 na imeshatoa albamu zaidi ya tano zikiwamo za 'Ni Vijimambo Tu', 'Sote Twasaka Riziki', 'Gharika la Moyo (Pembe la Ng'ombe)', 'Ndugu wa Mume Mna Hila', 'Toto la Kiafrika' na 'Nauvua Ushoga'.

Baby Madaha aachia mbili akiwa Kenya

 



MICHARAZO MITUPU
Baby Madaha katika pozi tofauti
NYOTA wa filamu na muziki nchini anayefanya shughuli zake kwa sasa nchini Kenya, Baby Madaha, ameachia kazi mpya mbili akiwa nchini humo.
Kazi hizo mbili moja ni ya filamu na nyingine ya muziki, fani iliyomtambulisha baada ya kushiriki shindano la kusaka vipaji vya kuimba la BSS.
Akizungumza na MICHARAZO, nyota huyo wa 'single' ya 'Summer Holiday', alisema filamu aliyoiachia inafahamika kwa jina la 'Gell Bladder' aliyoigiza na wasanii kadhaa nyota wa hapa Tanzania akiwamo Mariam Mndeme 'Mamushka' na wengine kutoka Kenya.
Baby alisema kwa upande wa muziki, ameachia 'single' iitwayo 'Mr DJ' ambayo ameirekodia katika studio za Candy Records zinazomilikiwa na 'mabosi' wake anaofanya nao kazi kwa sasa.
"Nimeachia kazi mbili moja ya muziki na nyingine ya filamu. Wimbo unaitwa 'Mr DJ' nimerekodi katika studio za Candy na filamu nimecheza na wasanii kadhaa maarufu wa Kenya na nyumbani yupo Mamushka na mimi mwenyewe," alisema.
Baby Madaha aliyewahi kufunika na wimbo wake wa 'Amore' uliokuja kuzaa albamu yenye jina kama hilo, alisema pamoja na kuachia kazi hizo yupo mbioni kuendelea kuwapa burudani mashabiki wake

Chelsea hiyoo robo fainali, Real yaua tena Wajerumani


Etoo akifunga bao la kwanza la Chelsea
Bale akimpongeza Ronaldo baada ya kutupia mpira kambani kutokana na pasi yake
VINARA wa Ligi Kuu ya England, Chelsea imedhihirisha kiu yao ya kutwaa taji la Liugi ya Mabingwa Ualaya kwa mara nyingine baada ya usiku wa jana kuikwangua Galatasaray ya Uturuki kwa mabao 2-0 na kutinga Robo Fainali.
Mabao ya Samuel Eto'o katika dakika ya nne na jingine la Gary Cahil kwenye dakika ya 43 yalitosha kuivusha vijana na Jose Mourinho na kuwafuta machozi mashabiki wa England ambao wiki iliyopita walishuhudia timu zao mbili za Arsenal na Manchester City ziking'olewa mashindanoni.
Kwa ushindi huo wa jana, Chelsea imeweza kuitupa nje timu ya nyota wa zamani Didier Drogba kwa jumla ya mabao 3-1 kwani katika mchezo wa kwanza walifungana bao 1-1 nchini Uturuki.
Katika mechi nyingine ya michuano hiyo, Real Madrid waliendeleza moto wao kwa kuizabua Schalke 04 ya Ujerumani kwa mabao 3-1 na kusonga robo fainali kwa jumla ya mabao 9-2.
Madrid ikiwa uwanja wa nyumbani wa Santiago Bernabeu ilipata mabao yake kupitia kwa nyota wake ambaye amezidi kuweka rekodi ya mabao kati ligi hiyo Cristiano Ronaldo katika dakika ya 21 na 74 na jingine likifungwa na Alvaro Morata.
Bao la kujifutia machozi la wageni lilitupiwa kambani na Tim Hoogland dakika ya 31 na kuwafanya Schalke kuaga kwa aibu michuano hiyo kwa msimu huu.
Katika mfululizo wa mechi za ligi hiyo kumaliza timu za mwisho za kutinga robo fainali, Manchester United itakuwa nyumbani kuikaribisha Olympiacos ya Ugiriki waliowatambia kwao kwa mabao 2-0  nayo timu ya Borussia Dotmund itaikaribisha Zenit.  Katika mechi yao ya kwanza Wajerumani walishinda ugenini kwa 4-2
Timu sita za kwanza kufuzu robo fainali ya michuano hiyo kwa mwaka huu ni watetezi Bayern Munich, Barcelona, Atletico Madrid, PSG, Chelsea na Real Madrid