STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, March 19, 2014

Mashetani Wekundu leo ni kusuka au kunyoa Ulaya

Manchester United
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Englan ambao wapo kwenye msimu mbaya, watakuwa na kazi nzito leo mbele ya Olympiakos ya Ugiriki, ili kuamua hatma yao ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwakani.
Kipigo cha 2-0 ilichopewa ugenini wiki mbili zilizopita zimeifanuya Mashetani Wekundu hao kulazimika kushinda nyumbani kwenye uwanja wa Old Trafford ikiwa ndiyo nafasi pekee kwao kuweza kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao kutokana na kupoteza nafasi ya kushiriki michuano hiyo msimu ujao kupitia nafasi nne za juu katika msimamo wa Ligi Kuu England.
Man United kwa sasa inashika nafasi ya saba katika msimamo wa Ligi Kuu  ikiwa ponti 12 nyuma ya timu inayoshika nafasi ya nne, Man City ambayo hata hivyo ipo nyuma mechi mbili dhidi ya Man U.
Timu inayoongoza msimamo huo ni Chelsea ikiwa na pointi 66, ikifuatiwa na Liverpool na Arsenal ambazo zina pointi 62 huku Tottenham ikishika nafasi ya nne kwa pointi 53 ikifuatiwa na Everton yenye pointi 51 tatu mbele ya Man U.
Kwa mantiki hiyo kama United itashindwa kuibuka na ushindi dhidi ya Olympiakos leo na kisha kucheza kwa 'jihadi' hadi kutwaa ubingwa, itakuwa imepoteza nafasi ya kushiriki michuano hiyo msimu ujao kutokana na matumaini yao ya kumaliza nafasi ya nne kutoweka.
Tangu klabu hiyo ianzishwe imeshiriki michuano hiyo ya Uefa mara 26 huku ikiutwaa ubingwa huo  mara tatu, hivyo kuikosa michuano ya msimu ujao itakuwa mwanzo mbaya zaidi kwa David Moyes tangu alipomrithi Sir Alex Ferguson aliyeiongoza timu hiyo kwa mafanikio makubwa kuanzia 1986-2013. United imeutwaa ubingwa Uefa msimu wa 1967–68, 1998–99 na 2007–08
 Kadhalika hii itakuwa mara ya pili mfululizo kwa Man United kutolewa katika hatua ya 16 bora baada ya msimu uliopita kutolewa na Real Madrid kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya mechi ya awali Santiago Bernabéu kumalizika kwa sare ya 1-1 na mechi ya marudiano Old Trafford Madrid kushinda 1-2.
Hata hivyo, Man United itashuka katika Uwanja wao wa Old Trafford ikichukua tahadhari kubwa dhidi ya mshambuliaji wa Arsenal anayeichezea Olympiakos kwa mkopo, Joel Campbell ambaye alitupia moja kati ya mabao hayo mawili.
Campbell ambaye tayari amepania kuonyesha makali yake kwenye dimba hilo, amesema ni vema kwenda Old Trafford na kuonyesha kiwango kwa kuwa wanaamini kuna mafanikio makubwa wanakaribia kuyapata.
"Tunajua tunakaribia kupata mafanikio fulani makubwa," mshambuliaji huyo wa Olympiakos raia wa Costa Rica alisema.
"Kuonyesha uwezo Old Trafford ni kitu muhimu sana. Ninaamini ni ndoto kubwa za wachezaji."
Jana usiku miamba minginine ya England, Chelsea ilikuwa na kibarua kigumu nyumbani dhidi ya Galatasaray baada ya mechi ya awali kutoka sare ya bao moja, huku Real Madrid ikikamilisha ratiba nyumbani dhidi ya Schalke 04 kutokana na kushinda 6-1 ugenini katika mchezo wa kwanza.
Borussia Dortmund ni timu nyingine ambayo itakuwa nyumbani leo kuikaribisha Zenit St Petersburg bada ya awali kushinda ugenini 4-2.
Galatasaray ambayo ilikuwa ikihofiwa kuhitimisha safari ya Chelsea katika michuano hiyo, kutokana na kuwa na mshambuliaji wa zamani wa miamba hiyo ya England, Didier Drogba, kama itakuwa imefanikiwa kuitoa 'The Blues', itajiwekea rekodi nzuri dhidi ya timu za England kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya 16 bora baada ya misimu iliyopita kuzitoa Arsenal na Manchester City.
United ambayo Jumapili ilikubali kipigo cha mabao 3-0 nyumbani dhidi ya Liverpool, matumaini yake yapo zaidi katika michuano hiyo ya Ulaya baada ya kuonekana kuwa katika wakati mgumu kutinga nne bora kwenye Ligi Kuu England ili kupata nafasi ya kushiriki ligi hiyo yenye utajiri mkubwa kwa ngazi ya klabu msimu ujao.
Licha ya kuwa katika wakati mgumu, Kocha David Moyes amesema kikosi chake kitapigana kutoka kwenye kucha hadi katika meno ili kuuweka msimu hai.
"Wachezaji wapo makini zaidi wakiwa wanamaanisha Jumatano (leo) na nini tunachotakiwa kukifanya," Moyes alisema.
"Tumepata jambo la kwenda kulifanya, kwa hiyo tunatumai tutalifanya hilo."
United ina rekodi ya ushindi nyumbani ya alisimia 100 dhidi ya wapinzani wao wa Ugiriki, kwani  Olympiakos imepoteza mechi 11 ilizocheza katika ardhi ya England.
Man United inaogopwa kutokana na rekodi yake ya kupindua matokeo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya 2007 'kuichenjia kibao'  AS Roma kwa kuichapa 7-1 baada ya mechi ya awali kufungwa 2-1.
Olympiakos pia itashuka uwanjani ikiwa na hamasa ya ushindi wa mabao 2-0 iliyoupata Jumamosi dhidi ya Panathinaikos na kuzidi kujihakikishia kutwaa ubingwa wa Ugiriki.
Pambano jingine la leo litazikutanisha timu za Borussia Dotmund itakayoikaribisha Zenith iliyowafungwa nyumbani kwao kwa mabao 4-2

No comments:

Post a Comment