STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, April 3, 2013

Toto yajinasua mkiani yailamba Prisons 1-0


BAADA ya kuwadindia Simba, timu ya Toto African jioni ya leo imejinasua mkiani kufuatia kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Prisons ya Mbeya katika mechi pekee ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Toto ikicheza kwenye dimba lake la nyumbani kama ahadi iliyotolewa na makocha wake, John  Tegete na Athuamn Bilal 'Bilo' iliweza kupata ushindi huo uliowapa pointi tatu na kutoka mkiani.
Bao pekee la pambano hilo linaloelezwa lilikuwa kali lilitumbukizwa na bekio wa Prisons katika harakati za kuokoa hatari langoni mwake na kuifanya Toto ikifikse pointi 21 na kuchupa hadi nafasi ya 11 wakiishusha Prisons iliyosaliwa na pointi zake 20.
Kujinasua kwa Toto mkiani kumeifanya Polisi Moro iliyokuwa imelowea katika nafasi hiyo duru la kwanza lote kurejea tena huko.
Baada ya pambano hilo la leo Ligi itasimama mpaka wiki ijayo kwa michezo kadhaa, ili kupisha pambano la kimataifa la Kombe la Shirikisho kati ya Azam na wageni wao Barracks YC II Jumamosi.
Msimamo wa Ligi hiyo kwa sasa baada ya matokeo ya jioni ya leo ni kama ifuatavyo:

                                         P     W     D     L     F     A     D      P
    1.  Young Africans  21     15     4     2     37    12    +25  49
    2. Azam                   21     13     4     4     36     16   +20  43   
    3 . Kagera Sugar      22     10     7     5     25     18    +7   37    
    4.  Simba                  21     9      8     4     30     19     +11  35
    5.  Coastal Union     22     8      8     6     23     20     +3     32   
    6.  Mtibwa Sugar     22     8      8     6     24     22     +2     32   
    7.  Ruvu Shooting    21     8      5     8     21     19     +2     29    
    8.  JKT Oljoro FC    22     7      7     8     22     24     -2     28    
    9. JKT Mgambo       21     7      3    11    14     21     -7     24
    10. Ruvu Stars         21     6      4    11    19     34     -15     22
    11. Toto Africans     23     4      9    10    20     30     -10     21
    12.Tanzania Prisons 22     4      8    10    11     21     -10     20     13. African Lyon     22     5      4    13    15     32     -17     19
    14. Polisi Morogoro  22     3     9   10    11     21     -10     18   
              

Chuji, Tegete wakwama kuanza mazoezi kuiwinda Oljoro JKT

Chuji anayeumwa mafindofindo

Wakali wengine kama hawa wapo fiti wakiendelea kujifua kuisubiri JKt Oljoro
NYOTA wanne wa vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakiwamo Athuman Idd 'Chuji' na Jerryson Tegete ndio pekee waliokosekana kwenye mazoezi ya timu hiyo yaliyoanza jana kujiandaa na pambano lao lijalo dhidi ya JKT Oljoro litakalochezwa wiki Jumatano ijayo.
Yanga wanaoongoza msimamo wa ligi hiyo wakiwa na pointi 49, ilianza mazoezi yake kwenye uwanja wa Mabatini, Dar es Salaam baada ya mapumziko mafupi ya sikukuu ya Pasaka.
Mbali na Chuji na Tegete ambao mmoja ni mgonjwa na mwingine majeruhi, wakali wengine hao wa Jangwani waliokosekana kwenye mazoezi hayo yanayoendelea jijini ni pamoja na kipa Said Mohammed na Mbuyu Twitte ambaye anauguliwa na mkewe.
Twitte ndiye aliyeizamisha Oljoro katika pambano la awali lililochezwa kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Wachezaji waliohudhuria mazoezi hayo yanayosimamiwa na kocha Ernst Brandts ni pamoja na makipa Ally Mustafa 'Barthez' na Yusuph Abdul, Shadrack Nsajigwa 'Fusso', Stephano Mwasika, Oscar Joshua, Juma Abdul, Godfrey Taita, Kelvin Yondani 'Vidic' na Nadir Haroub 'Cannavaro'.
Wengine ni viungo; Omega Seme, Salum Telela, Nurdin Bakari, Frank Domayo, Rehani Kibingu, David Luhende na Haruna Niyonzima 'Fabrigas', Said Bahanuzi, Simon Msuva, Hamis Kiiza 'Diego', George Banda, Nizar Khalfan na Didier Kavumbagu ambao ni washambuliaji.
Vinara hao wamesaliwa na mechi tano ikiwemo hiyo ya Oljoro kabla ya kumaliza msimu wa Ligi Kuu 2012-2013.
Mechi nyingine ni dhidi ya Mgambo Shooting utakaochezwa ugenini mjini Tanga, JKT Ruvu Stars, Coastal Union na watani zao wa jadi Simba zitakazochezwa dimba la Taifa, Dar es Salaam.

BARRACK YC II YATUA BONGO NA MKWARA MZITO KWA AZAM


Wachezaji wa Barack Young Controllers wakiwa na Afisa wa Shirikisho la soka nchini, Mzee Mshangama baada ya kutua uwanja wa ndege leo asubuhi


Wakipanda basi lao


Kocha mkuu Robert Lartey



Kocha na wachezaji ndani ya basi tayari kwa safari ya hotelini



Mtoto wa Rais wa Liberia  Robert Alvin Sirleaf , aliyevaa koti la suti akiwa na mmoja wa mtu ambaye alikuwa kwenye msafara


Wakishuka kwenye basi kuingia hotelini

Wakiwa ndani ya Saphirre court hotel

TIMU ya Barrack Young Controllers II ya Liberia imetua leo asubuhi huku ikiwa na matumaini kibao ya kuwafunga wapinzani wao Azam FC.

 Naye kocha wa timu hiyo, Robert Lartey, amejigamba kuwa uwezo wa kuifunga Azam FC kwenye mchezo wa marudiano wa  kombe la Shirikisho utakaochezwa jijini Dar es Salaam jumamosi kwani makosa yaliyoigharimu timu amekwisha yafanyia marekebisho

 “Mchezo huu ni muhimu kwa timu yangu na naamini nitashinda”, alisema Lartey.

Pia alijigamba kuwa na kikosi chenye wachezaji wenye vipaji ambao pia wapo timu ya taifa ya Liberia ya Vijana, akina Ezekiel Doe, Benjamin Gbamy na George Dauda.
Wachezaji wa timu hiyo wameonekana kuwa nyuso zao kutokuwa na furaha sijui ni kwa kutafakari kuwa walipoteza mchezo wa awali wakiwa nyumbani na sasa wanacheza ugenini.

Young Controllers imetua leo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 2:30 kabla ya muda wa 3.35 asubuhi ambao ulitarajiwa  kwa ndege ya PrecisionAir ikitokea Nairobi, Kenya inapounganisha safari hiyo inayoanzia Monrovia kupitia Accra, Ghana.

 Kocha huyo amesema hali ya hewa ya Dar es salaam haijatofautiana sana na hali ya hewa ya Liberia jana amekiri Dar es Salaam kuwa na joto kuzidi Monrovia

Msafara wa timu hiyo umetuwa na  watu 37,  wachezaji 21 na unaongozwa na Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa klabu hiyo Robert Alvin Sirleaf ambaye ni mtoto wa Rais wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf, Samuel Sumo wakati Meneja wa timu ni Clarence Murvee. Daktari wa timu ni Samuel Massaquoi.

 Wachezaji waliomo kwenye kikosi hicho ni Abraham Andrew, Alfred Hargraves, Alpha Jalloh, Benjamin Gbamy, Cammue Tumamie, Erastu Wee, Ezekiel Doe, George Dauda, Hilton Varney, Ishmail Paasewe, Joekie Solo, Joseph Broh, Junior Barshall, Karleo Anderson, Mark Paye, Prince Jetoh, Prince Kennedy, Randy Dukuly, Raymond Blamonh na Winston Sayou.

Lady Jaydee kuanzisha kituo cha Radio kitaitwa 'Kwanza FM’

Hatimaye tumepata jibu la kwanini Judith Mbibo aka Lady Jaydee amekuwa akitweet vitu vizito weekend iliyopita. Kama hukufaniwa kuziona tweets hizo ni kwamba mwanadada huyo alishusha mfululizo wa mabomu kuelekea kwa kituo kimoja cha radio na kujikuta akiongeza aka mpya, Anaconda.
Na sasa imebainika kuwa mwanamuziki huyo mkongwe na mjasiriamali anakuja na kituo chake cha radio kiitwacho Kwanza FM. Habari hiyo aliibreak mwenyewe jana na bila shaka haihusiani na April’s Fools Day.
Kwanza FM coming soon. Yangu mwenyewee
— Lady JayDee (@JideJaydee) April 1, 2013
Inaonesha kuwa mchakato wa kuanzisha radio hiyo unaenda vizuri kiasi cha kuweka wazi na kuwa hiyo ndio sababu alichukua uamuzi huo wa kuandika mambo ambayo yangeweza kuiharibu career yake ya muziki.
Huwezi kuanza mapambano km hujajizatiti, si utapigwa ufe.? Vita ni pale tu unapokuwa tayari. Sikuwa tayari huko nyuma ndio maana sikuongea
— Lady JayDee (@JideJaydee) April 1, 2013
Kila lakheri Lady Jaydee. Kwa usimamizi wa mumewe Gadner G Habash ambaye ana uzoefu mkubwa kwenye masuala ya radio, kituo hicho huenda kikafanya vizuri.
source:bongo5

SKYLIGHT Band yapagawaisha jiji la Mwanza



Vijana wa Skylight Band Kutoka kushoto ni Sam Mapenzi, Joniko Flower na Sony Masamba wakijitambulisha kwa mashabiki wa Band hiyo kwa staili ya aina yake jijini Mwanza katika ukumbi wa Villa Park Resort Jumatatu ya Pasaka
Aneth Kushaba AK 47 , Sam Mapenzi na Mary Lukas wakitoa burudani kwa wazi wa Mwanza.
Mary Lukas, Sony Masamba na Aneth Kushaba AK 47 wakitoa burudani kwa wakazi wa Mwanza.
Mashabiki wakicheza huku wakichukua picha za ukumbusho.
Dr. Sebastian Ndege akimtunza mijihela Sony Masamba.
Kikosi kazi cha Skylight Band kikicheza Sebene.
Nyomi la wakazi wa Mwanza ambao ni mashabiki wa Skylight Band wakijimwaga ndani ya Villa Park Resort.
Kwaito ilihusika pia.
Aneth Kushaba AK 47 akicheza na shabiki wake jukwaani.

Coast Modern Taarab wafanya 'Surprise' wakipika albamu

Mkurugenzi wa Coast Modern Taarab, Omar Tego
KUNDI la muziki wa taarab la Coast Modern 'Watafiti wa Mipasho' limefyatua wimbo mpya uitwao 'Surprise', ikiwa ni wiki chache tangu iwapoteze wanamuziki wake kadhaa.
Mkurugenzi wa kundi hilo, Omar tego 'Special One' aliiambia MICHARAZO kuwa, wimbo huo mpya ambao ameutunga na kuimba mwenyewe ni maandalizi ya Coast kupakua albamu mpya.
Tego alisema wimbo huo tayari ameshausambaza katika vituo kadhaa vya redio na kuanza kurushwa hewani tangu Jumapili na kwa sasa wanafanya mipango ya kutoa video yake.
"Baada ya ukimya kidogo, Coast Modern tumekuja na wimbo mpya uitwao 'Surprise' ambao tayari umeanza kusikika hewani tangu Jumapili. Wimbo huo ni mwanzo wa harakati za kupakua albamu yetu ya tano," alisema Tego.
Kundi hilo kwa sasa linatamba na albamu iitwayo 'Mwanamke Kujiamini' ambayo imefuata baada ya 'Damu Nzito', 'Kupenda Isiwe Tabu' na 'I'm Crazy 4u'.

Extra Bongo kunogesha Media Day

Wanamuziki wa Extra Bongo wakiwajibika
BENDI ya Extra Bongo imeahidi kuwaburudisha vilivyo waandishi wa habari wanaotokea katika vyombo mbalimbali vya habari katika tamasha la Media Day linalotarajiwa kufanyika Jumamosi.
Kwa mujibu wa kiongozi wa bendi hiyo, Rogert Hegga, Extra Bongo imefurahi kuteuliwa kutoa burudani kwenye tamasha hilo na hasa kwa kuzingatia kwamba ni mara yao ya kwanza.
Tamasha hilo limendaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo (TASWA), litafanyika kwenye viwanja vya TCC Club Chang'ombe jijini Dar es Salaam, ambapo litashirikisha michezo mbalimbali.
"Tumejiandaa kuwapa burudani ya kutosha kwa sababu tuna nyimbo nyingi tu zikiwamo za albamu Extra Bongo ya mwanzo na sasa na pamoja na nyimbo nyingine zinazoandaliwa kwa ajili ya albamu mpya," alisema Hegga.
Kiongozi huyo alisema kuwa TASWA hawakukosea kuiteua Extra Bongo, kwa madai kwamba wamesoma ishara za nyakati na kutambua kuwa ndiyo bendi yenye mashabiki wengi kwa sasa.
"Kwa kujali jinsi walivyotuthamini na kutupendekeza kutoa burudani kwenye tamasha lao, hatuna budi kuwapa kile ambacho kitawafanya watualike kila wanapofanya matamasha yao," alisema.
Bendi hiyo kwa sasa ina albamu za 'Mjini Mipango' na 'Mtenda Akitendeewa', ambapo pia imekamilisha nyimbo mbili mpya za 'Mgeni' na 'Hafidh' ambazo zinasikika kwenye maonyesho ya bendi hiyo.

Mashabiki Msondo walilia albamu mpya

Baadhi ya wanamuziki wa Msondo Ngoma wakiburudisha jukwaani

BAADHI ya mashabiki wa bendi ya Msondo Ngoma 'Baba ya Muziki' wameutaka uongozi wa bendi hiyo uwaeleze ni lini utawatolea albamu mpya, kwa kile walichodai kuwa siyo desturi ya bendi hiyo kukaa muda mrefu bila kutoa albamu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti juzi kwenye viwanja vya Leaders jijini Dar es Salaam, baadhi ya mashabiki hao walisema ni vyema uongozi ukawaeleza tatizo linalokwamisha kutoa albamu mpya.
"Siyo kawaida Msondo kukaa muda mrefu bila kutoa albamu mpya, ni vyema uongozi ukatueleza tatizo ni nini?" Said Habib alihoji huku Joseph 'Job' Matiku, akisema ukimya huo inawakosesha raha.
MICHARAZO iliwasiliana na baadhi ya viongozi wa bendi hiyo, ambapo Shaaban Dede aliwatuliza mashabiki akidai wanaendelea kurekodi nyimbo mpya, hivyo mashabiki hao hawapaswi kuwa na presha.
"Tunafahamu mashabiki wana kiu ya albamu, lakini kwa sasa wanapaswa kukaa mkao wa kula kwani tupo jikoni tunaiandaa," alisema Dede.
Aliongeza mbali na kukamilishwa kwa albamu hiyo, pia vibao vipya vimeanza kuandaliwa kikiwamo alichotunga yeye (Dede) kiitwacho 'Nidhamu'.
Msondo kwa mara ya mwisho ilifyatua albamu mwaka 2010 iliyoitwa 'Huna Shukrani' iliyokuwa na nyimbo za mwisho za marehemu Joseph Maina.
Enzi za uhai wa nyota wake Tx Moshi William, Msondo ilikuwa ikitoa albamu kila mwaka.

PSG yaing'ang'ania Barca, Bayern ikiua 'Kibibi cha Turin'

HAPA LAZIMA NIPITE: Messi akiwatoka wachezaji wa PSG

KAMA KAWA KAMA DAWA: Messi akiifungia Barca bao la kuongoza

TIMU ya soka ya Barcelona usiku wa kumakia leo iling'ang'aniwa na PSG iliyokuwa na kiungo wa kimataifa wa Uingereza, David Beckham na kutoa sare ya mabao 2-2 ugenini katika pambano la kwanza la Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Pambano hilo lililochezwa kwenye Uwanja wa Parc des Princes, lilishuhudiwa hadi mapumziko mabingwa hao wa zamani wa Ulaya wakiwa mbele kwa bao 1-0 lililotupiwa kambani na 'Mchawi Mweupe' Lionel Messi katika dakika ya 38.
Zlatan Ibrahimovic aliifunga timu yake ya zamani kipindi cha pili katika dakika ya 79 na kuisawazishoa PSG, kabla ya Xavi kuongeza bao la pili kwa mkwaju wa penati dakika ya 89.
Hata hivyo dakika moja baadaye PSG ilirejesha bao hilo kupitia Matuidi na kufanya mchezo huo uishe kwa sare hiyo ya 2-2.
Wakati Barcelona wakipumua kwamba pambano la marudiano uwanja wao wa Camp Nou huenda ikawa rahisi, vinara wa Ligi ya Seria A, Juventus wenyewe walikiona cha moto mbele ya wenyeji wao, Bayern Munich ya Ujerumani kwa kulazwa mabao 2-0.
Bao la kushtukiza la dakika ya kwanza ya mchezo huo lililofungwa na David Alaba na jingine la Thomas Mulller katia kipindi cha pili yalitosha kuizamisha 'Kibibi Kizee cha Turin' ambao watakuwa na kazi kubwa katika mechi ya marudiano wiki ijayo nyumbani.

Drogba, Sneijder uso kwa uso na Mourinho UEFA leo

Didier Drogba katika uzi wa klabu yake mpya ya sasa
Mourinho na Drogba walipokuwa pamoja Chelsea

MADRID, Hispania
MZUNGUKO wa maisha ya soka utakuwa umekamilika kwa mshambuliaji wa Galatasaray, Didier Drogba wakati atakaposhuka uwanjani nyumbani kwa Real Madrid katika mechi ya leo ya robo fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.
Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Ivory Coast, ambaye ametimiza umri wa miaka 35 mwezi huu, alicheza mechi yake ya kwanza kabisa ya michuano hiyo mikubwa ya Ulaya kwenye Uwanja wa Bernabeu Septemba 2003 wakati huo akiichezea klabu ya Olympique Marseille ya Ufaransa akiwa kijana mdogo.
Ingawa aliifungia Marseille goli la kuongoza katika dakika ya 26, magoli kutoka kwa Roberto Carlos na Luis Figo na mawili kutoka kwa Mbrazil Ronaldo de Lima, yaliwapa "Magalactico" wa Real ushindi mwepesi wa 4-2 katika hatua ya makundi.
"Itakuwa ni 'spesho' kwangu, siwezi kusahau siku ile," Drogba alikaririwa akisema katika jarida la klabu ya Galatasaray wiki hii.
"Ilikuwa ni muhimu sana kwa maisha yangu ya soka," aliongeza nyota huyo wa zamani wa Chelsea.
Drogba alikuwa nguzo kuu ya Chelsea katika safari yao ya kutwaa ubingwa wao wa kwanza wa Ligui ya Klabu Bingwa Ulaya msimu uliopita kabla ya kuondoka klabu hiyo ya London na kutimkia China na kisha kuhamia Uturuki.
Alifunga penlati ya ushindi katika hatua ya 'matuta' wakati wa mechi yao ya fainali dhidi ya Bayern Munich akiwa tayari mapema aliirejesha Chelsea mchezoni kwa goli kali la kichwa dakika mbili kabla ya dakika 90 za mchezo kumalizika ambalo lilifanya sare ya 1-1.
"Niliichangamkia fursa hii ya kucheza soka la ngazi ya juu Ulaya kwa mara nyingine bila ya kujiuliza," alisema. "Ndiyo maana niko hapa. Kupata fursa ya kushinda tena."
Mechi ya leo, ambayo inazikutanisha klabu hizo kwa mara ya nne katika michuano ya UEFA, pia inamweka Drogba dhidi ya kocha wake wa zamani Chelsea, Jose Mourinho, ambaye anapigania kuiongoza Real kutwaa ubingwa wa 10 wa Ulaya ambao umetoweka klabuni hapo tangu mwaka 2002.
Wawili hao walikuwa pamoja Stamford Bridge kuanzia 2004 hadi 2007 na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya England mwaka 2005 na 2006.
Drogba alisema Mourinho na kocha wa Galatasaray, Fatih Terim ni watu wanaotoa ushawishi mkubwa.
"Fatih Terim ana mambo mengi sana kama Mourinho kwa sababu yuko karibu na wachezaji na daima anazungumza nao," alisema.
"Suala la saikolojia ni muhimu sana kwenye soka na Terim yuko vizuri sana katika hilo."
Wakati Real wamekwama katika hatua ya nusu fainali katika misimu yote miwili iliyopita, kwa Galatasaray ni takribani robo karne tangu walipotinga hatua hiyo ya nne bora.
Pamoja na Drogba, mchezaji mwingine mkubwa katika kikosi hicho ni Mholanzi Wesley Sneijder, ambaye alishindwa taji la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya akiwa na Mourinho klabuni Inter Milan mwaka 2010.
Safu yao ya ushambuliaji inakamilishwa na Burak Yilmaz, ambaye anaongoza kwa kufunga magoli mengi kwenye Ligi ya Klabu Bingwa msimu huu akiwa sawa na Cristiano Ronaldo wa Real, wakiwa na magoli nane.
"Silaha yetu kubwa dhidi ya Real Madrid ni kwamba hatuwahofii," Terim, kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Uturuki na klabu za AC Milan na Fiorentina, aliwaambia waandishi wa habari Jumamosi.
"Hivyo ndivyo ambavyo tumekuwa tukicheza daima," aliongeza. "Umadhubuti wetu ni kwamba hatuhofii kufungwa, au kutolewa kwenye michuano."

Vikosi vinavyotarajiwa:

Real Madrid: 41-Diego Lopez; 17-Alvaro Arbeloa, 3-Pepe, 4-Sergio Ramos, 5-Fabio Coentrao; 6-Sami Khedira, 14-Xabi Alonso; 22-Angel Di Maria, 10-Mesut Ozil, 7-Cristiano Ronaldo; 9-Karim Benzema

Galatasaray: 1-Fernando Muslera; 27-Emmanuel Eboue, 26-Semih Kaya, 13-Dany Nounkeu, 11-Albert Riera; 14-Wesley Sneijder, 10-Felipe Melo, 8-Selcuk Inan, 4-Hamit Altintop; 17-Burak Yilmaz, 12-Didier Drogba

Refa: Svein Oddvar Moen (Norway)


---