STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, April 3, 2013

Drogba, Sneijder uso kwa uso na Mourinho UEFA leo

Didier Drogba katika uzi wa klabu yake mpya ya sasa
Mourinho na Drogba walipokuwa pamoja Chelsea

MADRID, Hispania
MZUNGUKO wa maisha ya soka utakuwa umekamilika kwa mshambuliaji wa Galatasaray, Didier Drogba wakati atakaposhuka uwanjani nyumbani kwa Real Madrid katika mechi ya leo ya robo fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.
Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Ivory Coast, ambaye ametimiza umri wa miaka 35 mwezi huu, alicheza mechi yake ya kwanza kabisa ya michuano hiyo mikubwa ya Ulaya kwenye Uwanja wa Bernabeu Septemba 2003 wakati huo akiichezea klabu ya Olympique Marseille ya Ufaransa akiwa kijana mdogo.
Ingawa aliifungia Marseille goli la kuongoza katika dakika ya 26, magoli kutoka kwa Roberto Carlos na Luis Figo na mawili kutoka kwa Mbrazil Ronaldo de Lima, yaliwapa "Magalactico" wa Real ushindi mwepesi wa 4-2 katika hatua ya makundi.
"Itakuwa ni 'spesho' kwangu, siwezi kusahau siku ile," Drogba alikaririwa akisema katika jarida la klabu ya Galatasaray wiki hii.
"Ilikuwa ni muhimu sana kwa maisha yangu ya soka," aliongeza nyota huyo wa zamani wa Chelsea.
Drogba alikuwa nguzo kuu ya Chelsea katika safari yao ya kutwaa ubingwa wao wa kwanza wa Ligui ya Klabu Bingwa Ulaya msimu uliopita kabla ya kuondoka klabu hiyo ya London na kutimkia China na kisha kuhamia Uturuki.
Alifunga penlati ya ushindi katika hatua ya 'matuta' wakati wa mechi yao ya fainali dhidi ya Bayern Munich akiwa tayari mapema aliirejesha Chelsea mchezoni kwa goli kali la kichwa dakika mbili kabla ya dakika 90 za mchezo kumalizika ambalo lilifanya sare ya 1-1.
"Niliichangamkia fursa hii ya kucheza soka la ngazi ya juu Ulaya kwa mara nyingine bila ya kujiuliza," alisema. "Ndiyo maana niko hapa. Kupata fursa ya kushinda tena."
Mechi ya leo, ambayo inazikutanisha klabu hizo kwa mara ya nne katika michuano ya UEFA, pia inamweka Drogba dhidi ya kocha wake wa zamani Chelsea, Jose Mourinho, ambaye anapigania kuiongoza Real kutwaa ubingwa wa 10 wa Ulaya ambao umetoweka klabuni hapo tangu mwaka 2002.
Wawili hao walikuwa pamoja Stamford Bridge kuanzia 2004 hadi 2007 na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya England mwaka 2005 na 2006.
Drogba alisema Mourinho na kocha wa Galatasaray, Fatih Terim ni watu wanaotoa ushawishi mkubwa.
"Fatih Terim ana mambo mengi sana kama Mourinho kwa sababu yuko karibu na wachezaji na daima anazungumza nao," alisema.
"Suala la saikolojia ni muhimu sana kwenye soka na Terim yuko vizuri sana katika hilo."
Wakati Real wamekwama katika hatua ya nusu fainali katika misimu yote miwili iliyopita, kwa Galatasaray ni takribani robo karne tangu walipotinga hatua hiyo ya nne bora.
Pamoja na Drogba, mchezaji mwingine mkubwa katika kikosi hicho ni Mholanzi Wesley Sneijder, ambaye alishindwa taji la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya akiwa na Mourinho klabuni Inter Milan mwaka 2010.
Safu yao ya ushambuliaji inakamilishwa na Burak Yilmaz, ambaye anaongoza kwa kufunga magoli mengi kwenye Ligi ya Klabu Bingwa msimu huu akiwa sawa na Cristiano Ronaldo wa Real, wakiwa na magoli nane.
"Silaha yetu kubwa dhidi ya Real Madrid ni kwamba hatuwahofii," Terim, kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Uturuki na klabu za AC Milan na Fiorentina, aliwaambia waandishi wa habari Jumamosi.
"Hivyo ndivyo ambavyo tumekuwa tukicheza daima," aliongeza. "Umadhubuti wetu ni kwamba hatuhofii kufungwa, au kutolewa kwenye michuano."

Vikosi vinavyotarajiwa:

Real Madrid: 41-Diego Lopez; 17-Alvaro Arbeloa, 3-Pepe, 4-Sergio Ramos, 5-Fabio Coentrao; 6-Sami Khedira, 14-Xabi Alonso; 22-Angel Di Maria, 10-Mesut Ozil, 7-Cristiano Ronaldo; 9-Karim Benzema

Galatasaray: 1-Fernando Muslera; 27-Emmanuel Eboue, 26-Semih Kaya, 13-Dany Nounkeu, 11-Albert Riera; 14-Wesley Sneijder, 10-Felipe Melo, 8-Selcuk Inan, 4-Hamit Altintop; 17-Burak Yilmaz, 12-Didier Drogba

Refa: Svein Oddvar Moen (Norway)


---

No comments:

Post a Comment