STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, April 3, 2013

Mashabiki Msondo walilia albamu mpya

Baadhi ya wanamuziki wa Msondo Ngoma wakiburudisha jukwaani

BAADHI ya mashabiki wa bendi ya Msondo Ngoma 'Baba ya Muziki' wameutaka uongozi wa bendi hiyo uwaeleze ni lini utawatolea albamu mpya, kwa kile walichodai kuwa siyo desturi ya bendi hiyo kukaa muda mrefu bila kutoa albamu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti juzi kwenye viwanja vya Leaders jijini Dar es Salaam, baadhi ya mashabiki hao walisema ni vyema uongozi ukawaeleza tatizo linalokwamisha kutoa albamu mpya.
"Siyo kawaida Msondo kukaa muda mrefu bila kutoa albamu mpya, ni vyema uongozi ukatueleza tatizo ni nini?" Said Habib alihoji huku Joseph 'Job' Matiku, akisema ukimya huo inawakosesha raha.
MICHARAZO iliwasiliana na baadhi ya viongozi wa bendi hiyo, ambapo Shaaban Dede aliwatuliza mashabiki akidai wanaendelea kurekodi nyimbo mpya, hivyo mashabiki hao hawapaswi kuwa na presha.
"Tunafahamu mashabiki wana kiu ya albamu, lakini kwa sasa wanapaswa kukaa mkao wa kula kwani tupo jikoni tunaiandaa," alisema Dede.
Aliongeza mbali na kukamilishwa kwa albamu hiyo, pia vibao vipya vimeanza kuandaliwa kikiwamo alichotunga yeye (Dede) kiitwacho 'Nidhamu'.
Msondo kwa mara ya mwisho ilifyatua albamu mwaka 2010 iliyoitwa 'Huna Shukrani' iliyokuwa na nyimbo za mwisho za marehemu Joseph Maina.
Enzi za uhai wa nyota wake Tx Moshi William, Msondo ilikuwa ikitoa albamu kila mwaka.

No comments:

Post a Comment