STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, March 2, 2011

PAMBANO LA WATANI J'MOSI Furaha kubwa inasubiriwa *Ni Msimbazi au Jangwani?

VIGOGO wa soka nchini Simba na Yanga zinakutana Jumamosi katika 'big match' ya pekee kwa aina yake msimu huu wa Ligi Kuu ya Vodacom, huku Wekundu wa Msimbazi wakipania kulipa kisasi cha kufungwa katika mechi ya kwanza, na Yanga wakitamba kuendeleza ubabe.
Pambano hili la marudiano baada ya lile kwanza mwishoni mwa mwaka jana kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza na Simba kuloa bao 1-0, linafanyika kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Vita ya mechi hii ambayo tayari imeteka hisia za mashabiki wengi wa soka inatokana na namna timu hizo zinavyopokezana kukalia kiti cha uongozi wa ligi hiyo pamoja na Azam FC.
Kigogo kitakachoshinda katika mechi hiyo, kitakuwa kimejiweka kwenye mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa wa soka ambao kwa sasa uko mikononi mwa Simba.
Yanga ndio inayoongoza ligi hiyo kufuatia ushindi wake wa bao 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting na kuiengua Simba waliokuwa kileleni kwa masaa tangu walipoichabanga Mtibwa Sugar mabao 4-1.
Jerry Tegete ndiye aliyekuwa shujaa kwa kufunga bao zuri wakati Simba ikilala 1-0 kwenye mechi ya kwanza, na amepania kurejesha tena huzuni kwa Simba kwenye mechi ya kesho.
Hata hivyo Yanga pia watashuka uwanjani kesho wakiwa na machungu ya kipigo cha mabao 2-0 ilichopewa na watani zao hao katika pambano la fainali la Kombe la Mapinduzi mapema mwaka huu visiwani Zanzibar.
Kipigo hicho hakikuonekana kuwauma sana Yanga, kwani walijitetea kwa kusema wachezaji wake wengi walikuwa na timu ya taifa iliyokuwa ikishiriki michuano ya Mto Nile nchini Misri.
Simba itashuka dimbani ikitokea chimbo lake la kawaida mjini Zanzibar, na Yanga wakiingia kusaka pointi mbili wakitoka Bagamoyo.
Simba kupitia nyota wake kadhaa kama Juma Jabu, Rashid Gumbo na Mohammed Banka wamesema hawana hofu ya pambano hilo.
Wamesema wamejiandaa kushinda mechi hiyo, na hakuna shaka matarajio yao yatatimia ili iwe sehemu nzuri ya maandalizi dhidi ya pambano lao la Klabu bingwa dhidi ya Mazembe.
"Hatuna hofu na Yanga, tutawafunga ili tukienda Lubumbashi kuvaana na TP Mazembe tukiwa na ari ya ushindi kama tunavyowakabili Yanga kufuatia kuilaza Mtibwa mabao 4-1," alisema Banka.
Hata hivyo Yanga kupitia Afisa Habari wao, Louis Sendeu alisema wachezaji wake watacheza kufa na kupona na kuifunga Simba ili kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa.
"Kama tulivyofanya Mwanza ndivyo tutakavyorejea tena Jumamosi, timu ipo katika hali nzuri na tuna uhakika wa kuilaza tena Simba," alisema Sendeu.
Kama Yanga itashinda itazidi kujikita kileleni, lakini kama itakubali kipigo kwa watani zao maana yake wataporomoka na kuwapisha Simba warejee kileleni.
Timu hizo zinakutana Yanga ikiwa na kocha mpya, Sam Timbe kutoka Uganda, huku ikiwa na wachezaji wawili wapya ambao kwenye fainali za Kombe la Mapinduzi hawakuonyesha makali yoyote nao ni Davies Mwape na Juma Seif 'Kijiko'.
Simba kwa upande wao, itashuka dimbani ikiwa na mshambuliaji mwenye uchu Mbwana Samatta na Ally Ahmed 'Shiboli' ambao katika mechi ya Mwanza hawakuwepo.
Nani atakayeibuka na ushindi katika pambano la kesho na kuzima ngebe za wenzake? Bila shaka ni suala la kusubiri dakika 90 za mchezo huo.

INAFRIKA WAREJEA NA MBELEKO TOKA ULAYA




BAADA ya ziara ya miezi miwili na nusu ya maonyesho ya burudani katika nchi mbalimbali za Ulaya, bendi ya InAfrika imerejea nchini, ikijinadi kuwa, ziara yao ilikuwa ya mafanikio makubwa.
Bendi hiyo iliwasili jana majira ya saa 4 asubuhi, kupitia mmoja wa viongozi
na wanamuziki wake, Bob Rudala imesema itatumia siku chache kupumzika
kabla ya kuanza kuitambulisha albamu yao mpya mikoani.
Akizungumza na Micharazo mara baada ya kuwasili kwenye uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, alisema albamu hiyo ya pili kwao baada ya ile ya 'Indege', inaitwa 'Mbeleko'.
Rudala aliyewahi kutamba na nyimbo binafsi kama 'Nimekuchagua Wewe', alisema albamu hiyo ina nyimbo 10 zilizopigwa katika miondoko mbalimbali ya ngoma asilia za Tanzania.
Rudala alisema utambulisho wa albamu hiyo utaanzia mkoa wa Arusha wiki ijayo, kabla ya uongozi wa bendi hiyo kupanga mahali pengine pa kufanya hivyo.
Kuhusu ziara hiyo, Rudala alisema ilikuwa ya mafanikio makubwa na kwamba watatumia utambulisho wa albamu hiyo kuudhibitishia umma wa Tanzania kuwa walienda kujifunza mambo mengi kuendeleza muziki nchini.
"Tunashukuru tumerejea salama, ila kwa kifupi tumefarijika na mafanikio makubwa tuliyopata katika ziara hiyo na tunapumzika kwa siku kadhaa kabla ya kabla ya kuanza kuitambulisha albamu yetu ya Mbeleko," alisema.
Alizitaja baadhi ya nyimbo zilizopo kwenye albamu hiyo kuwa ni Mbeleko, Hatushangai, Jamila, Kitchen Party, Mimi Muafrika, Amina, Jua Limetua na kadhalika.
Aliongeza kuwa ziara yao waliyoifanya kuanzia Desemba mwaka jana, ilihusisha nchi tano za Uholanzi, Ujerumani, Uswisi, Austria na Romania ambapo mbali na bendi, pia InAfrika iliambatana na kikundi chao cha wanenguaji na wacheza sarakasi.
InAfrika ilianzishwa mwaka 1992 ikiwa na albamu ya kwanza ya 'Indege' ambayo pia hufahamika kama 'Omunwa'ambayo ilisaidia kuipandisha chati kwa nyimbo zake mchanganyiko zikiwemo zenye miondoko ya asili.