STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, September 17, 2013

Hawa ndiyo wanawake vinara wa dawa za kulevya!

KUNA dhana iliyojengeka kuwa wanawake ni watu laini, wapole na wasioweza kufanya mambo ya hatari. Hata hivyo pia kuna wengine wanadai kuwa wanawake ni daraja hatari sana. Machoni huonekana laini lakini wanaweza kutenda mambo ambayo ni vigumu kwa mtu wa jinsia ya kiume kuyafanya. Biashara ya madawa ya kulevya inahitaji watu hatari, katili, wenye roho isiyotishika. Huwezi amini miongoni mwa watu wanaonekana jamali na wapole usoni ndiyo wakali katika biashara hiyo. Wasome vigogo 10 wanawake duniani wanaotisha kwa biashara ya 'bwimbwi' a.k.a ugoro, unga sembe nk
Mireya Moreno Carreon.
Nancy Botwin katika ‘siriz’ yake ya Weeds kwenye TV, anajaribu kuonesha jinsi mwanamke anaweza kuwa hatari katika biashara ya bangi na madawa ya kulevya kwa jumla, hata hivyo katika uhalisia, hajawafikia hata chembe wanawake hawa hatari ambao wameitikisa dunia.
Hawa ni maharamia 10 wauza unga, wametengeneza fedha nyingi na kila mmoja ameshahusika kwa namna moja au nyingine na mauji. Kwa muuza madawa ya kulevya, kitendo cha kutoa roho ya mtu kipo jirani yake sana.
1. GRISELDA BLANCO
Inawezekana huyu ndiye akawa muuza unga mwanamke katili, mwenye uwezo mkubwa kuliko wote kuwahi kutokea katika historia ya dunia. Ameshahusika na mauaji ya watu zaidi ya 200. Ni raia wa Colombia, akiwa na miaka 11, tayari alishahusika na tukio la utekaji wa mtoto. Baadaye alihamia Marekani, kwenye Jimbo la Florida ambako alitengeneza mtandao wa madawa ya kulevya ambao ulimpa utajiri mkubwa.

2.  SANDRA AVILA BELTRAN
Ni raia wa Mexico, alizaliwa mwaka 1960. Aliwahi kupewa jina la Mungu wa Kike wa Madawa ya Kulevya. Vyombo vya habari nchini mwake vikamwita Malkia wa Pacific. Serikali za Marekani na Mexico zinamtaja kuwa kiungo wa magenge ya unga ya Sinaloa Cartel la Mexico na Norte del Valle Cartel la Colombia. Anadaiwa kujipatia mabilioni ya dola kwa usafirishaji wa unga kati ya Colombia, Mexico na Marekani. Kwa sasa yupo gerezani nchini Mexico kwa kosa la utakatishaji wa fedha haramu.

3. ANGIE SANCLEMENTE VALENCIA
Ni raia wa Colombia, aliwahi kushika taji la urembo la taifa katika nchi hiyo lakini alinyang’anywa baada ya kubaini ameshaolewa. Mume wake alikuwa mmoja wa vinara wa unga na walipoachana, alitumia njia zilezile kujipatia utajiri haramu. Alikuwa na genge kubwa la wasafirishaji wa cocaine na kila mtu alimlipa dola 5,000 kwa safari moja. Alisafirisha zaidi Argentina, Uingereza na Mexico. Ana umri wa miaka 35, yupo gerezani Argentina tangu Oktoba 27, 2010.

4. KATH PETTINGILL
Alizaliwa mwaka 1935. Jina lake la utani ni Bibi Kizee Shetani (Granny Evil). Ni mwenyeji wa Jiji la Melbourne, Australia. Alianza kama kahaba kabla ya kugeukia madawa ya kulevya. Alipoteza jicho moja baada ya kupigwa risasi katika moja ya matukio ya uharamia, akimtetea binti yake, Vicky, aliyekuwa anadaiwa dola 300 na maharamia wenzake. Nguvu ya mtandao wa unga aliyoitengeneza, ni hatari na imehusika na mauaji mengi nchini Australia.

5. ENEDINA ARELLANO FELIX
Katika genge ambalo lilikuwa linaongozwa na kaka zake, Ramon na Eduardo, mwanzoni yeye alishika nafasi ya umeneja wa fedha. Baada ya Ramon kuuawa na Eduardo kukamatwa, alishika uongozi. Maofisa usalama wa Mexico waliwahi kukiri kwamba Enedina ndiye alikuwa dira ya kaka zake. Ana umri wa miaka 52, ni msomi mwenye shahada ya uhasibu. Marekani imempiga marufuku kuingia nchini humo. Amebadili mfumo na sasa anaendesha kazi zake kisayansi,
hakuna fujo za magenge ya wahuni kiasi kwamba inakuwa ngumu kumtia hatiani.

6.  BLANCA CAZARES SALAZAR
Ni raia wa Mexico, alianza kujihusisha na utakatishaji wa fedha haramu, aliponogewa akajikita kwenye unga. Ana umri wa miaka 37. Biashara yake ameitanua na yupo makini sana. Anaongoza mtandao mkubwa wenye makundi 42. Ni ngumu kumkamata kwa sababu hahusiki moja kwa moja. Marekani imempiga marufuku kuingia nchini humo.

7. MARIA JIMENEZ
Ana umri wa miaka 27. Alikuwa kiongozi wa genge lililokufa la La Tosca. Baada ya kufanya biashara kwa muda mrefu, alikamatwa mwaka jana nchini kwake Mexico kwa tuhuma za usafirishaji wa unga na mauaji. Baadaye alikiri kuua watu 20 na mpaka sasa yupo jela.

8.  EDITH LOPEZ LOPEZ
Anajulikana kama Malkia wa Kusini. Amekuwa kinara wa madawa ya kulevya tangu alipoolewa na haramia wa unga, Raul Nunez Morales, maarufu kama The Cowboy. Tangu mwaka 2000, Edith amebaki kuwa mmoja kati ya wanawake tisho kwa biashara hiyo haramu duniani.

9. THELMA WRIGHT
Alishirikiana na marehemu mumewe, Jackie Wright katika biashara ya unga kati ya miaka ya 1980 na 1990. Mwaka 1986, mumewe aliuawa, kwa hiyo akashika usukani kwa kulisuka genge lao la Black Mafia ambalo lilifanya matukio mengi. Hata hivyo, kwa kuhofia maisha ya mtoto wake, Jackiem,  kuharibika, aliachana na kazi hiyo na kufanya shughuli nyingine halali. Ni mara chache sana kutokea.

10. MIREYA MORENO CARREON
Ndiye mwanamke pekee kushika nafasi ya juu kwenye Genge la Zetas. Ndani ya kipindi kifupi alifanya matukio mengi ya utakatishaji wa fedha haramu na usafirishaji wa unga. Akiwa nchini kwake, Mexico, mwaka 2010, maofisa usalama wa siri walimkamata akiwa akiwa na gari lenye cocaine na bangi na mpaka leo yupo korokoroni.

Sheikh Ponda akwama kupata dhamana Morogoro  Sheikh Ponda Akishuka kwenye basi la Magereza tayari kuingia Mahakamani Kusikiliza kesi yake inayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoani Morogoro.
Sheikh Ponda anashtikiwa katika Mahakama hiyo akikabiliwa na Mashtaka Matatu ambayo inadaiwa aliyatenda Mkoani Morogoro katika Mkutano hadhara mwezi uliopita.
Kiongozi huyo wa umma wa Kiislam Tanzania amenyimwa dhamana na hivyo kurejeshwa tena rumande mpaka kesi yake itakaposomwa tena Oktoba  Mosi.


 Sheikh Ponda akiwa Chini ya Ulinzi Mkali wakati akiingia Mahakamani kusikiliza kesi yake inayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoani Morogoro.
 
Sheikh Issa Ponda akiingia Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoani Morogoro leo kusikiliza kesi yake


 Wafusi wa Sheikh Ponda wakiwa wakiwa mahakamani leo kusikiliza kesi ya Kiongozi wao iliyokuwa imetajwa mahama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro.


Ulinzi mkali ukiwa umeimarishwa mahakamani leo wakati kesi hiyo ikiendelea mjini Morogoro.

Newz Alert: Shule ya Ilboru yafungwa, kisa...!

Waziri Majaliwa alipowahi kwenda kuutuliza mgogoro wa wanafunzi wa Ilboru mwaka jana
TAARIFA zilizotufikia hivi punde zinasema kuwa, serikali imeamua kuifunga kwa muda usiojulikana Shule Maalum ya vipaji ya Ilboru ya jijini Arusha, baada ya kuwepo kwa tishio la kuchomwa moto kutokana na mgogoro uliodumu kwa muda mrefu shuleni hapo.
Imedokezwa wanafunzi wapatao wanne wanahojiwa kutokana na tishio hilo huku wengine karibu 800 wamerudishwa makwao mpaka watakapotangaziwa vinginevyo.
Tangu mwaka jana shule hiyo imekuwa na mgogoro baina ya wanafunzi na uongozi wake kiasi Naibu waziri wa Tamisemi (Elimu), Kassim Majaliwa kulazimika kuingilia kati, lakini hali haijatengemaa hadi hivi karibuni tena kiliponuka tena.

Msiba tena! Prince Ahmed Mgeni hayupo nasi afariki Zenji

Prince Ahmed Mgeni

TASNIA ya sanaa imeendelea kupata misiba baada ya muimbaji nyota wa zamani wa Zanzibar Stars, Prince Ahmed Mgeni kufariki dunia visiwani Zanzibar na jioni hii alitarajiwa kuzikwa.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka visiwani humo zinasema kuwa, marehemu Mgeni aliyetamba na kuziba nafasi ya Mzee Yusuf alipojiengua katika kundi hilo na kuunda Jahazi, alifariki usiku wa kuamkia leo katika Hospitali ya Mnazi Mmoja alipokuwa amelazwa.
Taarifa za awali zinasema marehemu alikuwa akisumbuliwa na kifua kikuu (TB) na kulazwa hospitalini hapo kwa muda mrefu.
Mpaka mauti yalipomkuta jana marehemu Mgeni alikuwa mwanamuziki wa kundi la Zanzibar Njema Taarab.
Kifo cha msanii huyo ni muendelezo wa misiba katika tasnia ya sanaa kuanzia mwishoni mwa mwaka jana ambapo imeshuhudiwa waigizaji na waimbaji wakipoteza uhai kwa sababu mbalimbali ikiwamo ajali na maradhi. Mungu aiweze mahali pema peponi roho ya marehemu Ahmed Mgeni na MICHARAZO inawapa pole familia, ndugu, jamaa na rafiki wa msanii huyo pamoja na wadau wote wa sanaa Tanzania. 

Sunday Kayuni kuhudhuria kozi ya wakufunzi CAF

Sunday Kayuni
MKURUGENZI wa Ufundi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Sunday Kayuni atashiriki warsha ya wakufunzi wa makocha wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) itakayofanyika kuanzia Oktoba 22-24 mwaka huu.

Warsha hiyo iliyoandaliwa na CAF kwa ajili ya wakufunzi wake itafanyika nchini Cameroon. Wakufunzi 18 wa CAF kwa upande wa makocha watahudhuria warsha hiyo.

Madhumuni ya warsha hiyo ni kuainisha majukumu yao, kubadilishana uzoefu. Pia kuwapa methodolojia mpya ya ufundishaji na muongozo kuhusu mfumo wa leseni za makocha ambao watautumia katika nchi wanazotoka.

Mbali ya Kayuni Tanzania, wakufunzi wengine ni Ahmed Babiker (Sudan), Amadou Shaibu (Nigeria), Boy Bizzah Mkhonta (Swaziland), Duodu Fred Osam (Ghana), Edussei Anthony (Ghana), Fathi Nossir (Misri), Faouzy Altaisha (Sudan) na Fran Hilton Smith (Afrika Kusini).

Wengine ni Francis Oti-Akenteng (Ghana), Honour Janza (Zambia), Kasimawo Laloko (Nigeria), Mahmoud Saad (Misri), Paul Hamilton (Nigeria), Serame Letsoaka (Afrika Kusini), Shawky Abdel Shafy (Misri), Thondoo Govinder (Mauritius) na Ulric Mathiot (Seychelles),

Tembo Mtoto, nyota iliyozimika ghafla katika ngumi za kulipwa

Bondia Yohana Mathayo 'Tembo Mtoto' (kulia) akichuana na Fadhili Awadh 'Mnyama Chui' katika moja ya mapambano yake enzi za uhai wake.
 Na Magendela Hamisi
SEPTEMBA 12 tasnia ya mchezo wa masumbwi ilimpoteza bondia mahili wa uzito wa kilo kilo 66, Yohana Mathayo 'Tembo Mtoto' (23), akiwa mazoezini kujindaa na pambano lake la ubingwa wa Taifa dhidi ya Abdallah Mohammed 'Prince Nassib'.
Pambano hilo lilipangwa kufanyika Oktoba mwaka huu, jijini Dar es Salaam na kusimamiwa na Shirikisho la Ngumi za Kulipwa Tanzania (PST), lilionekana kuvuta hisia za mashabiki wengi.
Bondia huyo mahili ambaye jina lake lilianza kujulikana baada ya kufanya vema katika mapambano yake mengi, tena kwa kushinda kwa KO, wengi walimtabiri mafanikio makubwa kupitia mchezo huo.
Katika vitongoji vya Jiji la Dar es Salaam, hasa kwenye chimbuko la mchezo masumbwi yakiwemo maeneo ya Keko, Manzese, Tandale, Mburahati, Mabibo, Mwananyamala na maeneo mengine hakuna asiyefahamu jina la Tembo Mtoto.
Kwani kabla ya kuanza kushiriki katika ndondi za kulipwa na kuwatwanga mabondia wengi alitokea katika ujenzi wa mchezo huo kwenye ngumi za ridhaa ambako ndiko wanapotokea mabondia bora Tanzania na ulimwengu kwa ujumla.
Prince Nasseb ambaye ndiye anashikilia mkanda wa taifa wa PST, na ndiye alitakiwa kuzitwangwa na Tembo Mtoto,  anasema kifo cha bondia huyo ni pigo kubwa kwake kwani aliamini ndio alikuwa mpinzani wake aliyebaki katika uzito huo wa kilo 66, kutokana na wengi kuwa dhaifu kwake.
"Sikuweza kuamini baada ya kusikia kifo cha mpinzani wangu,  hali ambayo ambayo hadi leo bado inanipa shida kuamini kama ni kweli Tembo Mtoto amefariki, lakini kikubwa ni kumuombea Mungu ampumzishe kwa amani katika makazi ya milele," alisema.
Mratibu wa pambano hilo ambaye ndiye alikuwa kocha wa Tembo Mtoto, Faraji Ndame anasema kifo cha bondia huyo ni pigo katika klabu yake ya Kwame iliyopo Mburahati kutokana na kuw,a kinara wa kusshinda mapambano mengi.
"Ni bondia ambaye alikuwa na namtegemea katika mapambano mengi na siku ambayo anafariki, kwa kweli sikuamini hadi nilipothibitishiwa na daktari wa Hospitali ya Mwananyamala, kwani kabla hajaanguka wakati alipokuwa akifanya mazoezi ya kupiga begi nilikuwa nikimtazama kwa karibu.
"Hadi anaanguka nilikuwa nikimwona, nilipomfuata kumpa huduma ya kwanza alikuwa akitokwa povu na kizuia meno akawa ameking'ata, mdomo ukawa mgumu kufunguka, tulimtoa kizuia meno na kumvua viatu, kisha tukampeleka Hospitali ya Mwananyala, lakini tukaambiwa  amefariki," anasema.
Rais wa PST, Emmanuel Mlundwa akizungumza na Jambo Leo, kuhusu kifo hicho, alisema wamepokea kwa mshtuko,  lakini kazi ya Mola haina makosa, kinachopaswa kila mmoja kumuombea.
Ninachokifahamu kwa Tembo Mtoto ni kwamba, alikuwa bondia bora mwenye umri mdogo ambaye ndio kwanza alikuwa akiyafuta mafanikio, kwani mapambano mengi aliyocheza alikuwa akishinda kwa KO.
"Katika pambano lake la mwisho ambalo alipigana na Kea Kea alishinda kwa KO, nilikuwa mwamuzi wa mchezo huo, kikubwa ambacho naweza kusema, alikuwa bondia mzuri na atakumbukwa kwa kufanya vema," alisema.
Kocha wa kimataifa wa mchezo huo, Rajabu Mhamila 'Super D', anasema kifo cha Tembo Mtoto ni pigo kubwa katika tasnia ya ngumi kutokana na bondia huyo kuonesha kila dalili za mafanikio katika mapambano yake mengi.
"Kifo cha Tembo Mtoto, hakika kimenishtua kwani ni bondia niliyekuwa nikimfahamu tangu akiwa katika ridhaa, alikuwa akifuata ushauri kwangu," alisema.
"Alikuwa akiupenda mchezo husika, aliuheshimu, aliuthamini kama sehemu ya kazi yake, huku akifanya  mazoezi ya kutosha na kuuthamini mchango wake," anasema Super D.
Dk. Kulwa Killaga ambaye mara nyingi huwapima mabondia kabla ya mapambano, anasema kifo cha Tembo Mtoto kimemshtua, hasa baada ya kukubaliana mambo mbalimbali.
"Nilipozungumza naye mara ya mwisho, aliniomba niwe meneja wake, nikamshauri awe mbali na vitu vilivyo kinyume na maadili ya mchezo wa ngumi kwa lengo la kuepuka athari zinazoweza kujitokeza," anasema.
Anasema kuwa, mara nyingi alikuwa akilalamika kuhusu waratibu kuwapiganisha mabondia bila kufuata utaratibu wa muda wa pambano hadi pambano, madhara yake ni vifo.
"Mfano bondia kapigana wiki moja au mbili, kabla hajafikisha miezi mitatu anapigana tena, hali hiyo ni mbaya sana," anasema.
Anasema kuwa, waratibu wanatakiwa kudhibitiwa katika hilo ili kulinda maisha ya mabondia ambao wengi wao hawana elimu ya kutosha katika hilo na ndicho kinachowagharimu wengi. Pia, anawataka waachane na utumiaji wa bangi.
"Bangi ni kitu kingine kibaya kinachosababisha vifo kwa mabondia, hivyo wadau wa mchezo huo wanatakiwa kuwashauri mabondia wanaotumia madawa ya kulevya," anasema.
Bondia Fadhili Awadhi wa klabu ya Jitegemee, aliyewahi kutwangana na Tembo Mtoto, mwanzoni mwa mwaka huu, alisema kifo cha mwanamasumbwi huyo kimemhuzunisha.
"Niliwahi kupanda ulingoni na marehemu Tembo Mtoto enzi za uhai wake, nikamshinda kwa KO katika raundi ya nne, kifo chake kinanipa majonzi na wakati mwingine nashindwa kuamini," alisema.
Rekodi ya bondia huyo alipigana mapambano saba ya ngumi za kulipwa, alishinda mara nne na kupigwa mara moja na  kutoka sare mara mbili.
Tembo Mtoto alijiunga na ngumi za kulipwa mwaka 2011, akianza safari yake ya masumbwi kutwangana na Seba Temba wa Morogoro, pambano lingine lilikuwa Agosti na kufanikiwa kumtwanga Shujaa Keakea kwa TKO.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi, Amin

Kitimtim cha Ligi kuendelea kesho, Yanga kuvuna nini Mbeya, Simba kupigishana kwata na Mgambo, Azam,Ashanti Dar


Simba
Yanga

Azam
Ashanti United
 
Mgambo JKT

Na Boniface Wambura 
KIVUMBI cha Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara kitaingia raundi ya nne kesho (Septemba 18 mwaka huu) kwa mechi saba katika viwanja saba tofauti.

Vinara wa ligi hiyo, JKT Ruvu wanaonolewa na Kocha Mbwana Makata watakuwa ugenini Uwanja wa Mabatini, Mlandizi Pwani kuumana na 'ndugu' zao Ruvu Shooting ya Charles Boniface Mkwasa. 

Mechi hiyo inatarajiwa kuwa kivutio kikubwa kwa washabiki mkoani Pwani kutokana na aina ya soka inayochezwa na timu hizo.

Baada ya sare dhidi ya Mbeya City wikiendi iliyopita, Yanga inaendelea kubaki Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya ambapo itacheza na Tanzania Prisons katika mechi itakayochezeshwa na mwamuzi Simon Mbelwa kutoka Pwani.

Nayo Simba itaumana na Mgambo Shooting Stars ya Tanga katika mechi itakayopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000. Mechi hiyo itakuwa chini ya Kamishna David Lugenge kutoka Iringa.

Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Oljoro JKT kutoka Arusha na wenyeji Kagera Sugar wakati Azam na Ashanti United zitakwaruzana kwenye uga wa Azam Complex ulioko Chamazi jijini Dar es Salaam.

Mwamuzi Jacob Adongo kutoka Mara ndiye atakayechezesha mechi kati ya Coastal Union na Rhino Rangers itakayofanyika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. 

Mtibwa Sugar inarejea uwanja wake wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro ambapo inaikaribisha Mbeya City ya Kocha Juma Mwambusi.

Wakati huo huo, Ligi Daraja la Kwanza (FDL) nayo inaendelea kesho (Septemba 18 mwaka huu) kwa mechi moja ambapo Lipuli ya Iringa ambayo wikiendi iliyopita ilicheza Mkamba mkoani Morogoro inapita mjini Morogoro kuikabili Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri.

Kamati yafafanua uwakilishi wa wajumbe Mkutano Mkuu TFFNa Boniface Wambura
KAMATI ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imesema uwakilishi wa ujumbe kwenye Mkutano Mkuu unaanzia kwenye chama cha mpira wa miguu cha mkoa, kufuatiwa na chama shiriki na baadaye klabu ya Ligi Kuu.

Mwongozo huo juu ya uwakilishi wa wajumbe kwenye Mkutano Mkuu umetolewa kutokana na maombi ya Sekretarieti ya TFF kwa kamati hiyo iliyokutana jana (Septemba 16 mwaka huu) baada ya kubaini baadhi ya wajumbe wanashikilia nafasi mbili kwenye vyama tofauti.

Kwa mujibu wa Ibara ya 5 ya Katiba, kuna makundi ya aina tatu ya wanachama wanaounda TFF. Makundi hayo ni vyama vya mikoa, vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu.

Sekretarieti ya TFF imebaini kuwa kuna baadhi ya viongozi wa kuchaguliwa wa mikoa ambao pia ni viongozi wa vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu, hivyo wana nafasi zaidi ya moja ya kuingia kwenye Mkutano Mkuu.

Hivyo, kutokana na mwongozo huo ushiriki wa wajumbe kwenye Mkutano Mkuu wa TFF utaanzia chama cha mkoa, kufuatiwa na chama shiriki na baadaye klabu za Ligi Kuu.

Pia nafasi ambazo zinaweza kuwakilishwa kwenye Mkutano Mkuu kama mhusika hayupo ni za Mwenyekiti atakayewakilishwa na Makamu Mwenyekiti, na Katibu atakayewakilishwa na Katibu Msaidizi.  Nafasi za ujumbe wa Mkutano Mkuu na ile ya mwakilishi wa klabu hazina uwakilishi kama mhusika hayupo.