STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, March 23, 2014

Atletico yaibutua Betis, yaiengua Real kileleni kwa muda

Atletico Madrid
Atletico Madrid wakishangilia moja ya mabao yao
IKIWA imesalia kama saa moja na ushei kabla ya mahasimu wa Ligi Kuu ya Hispania, Real Madrid na  Barcelona kupepetana katika pambano lao la El Clasico, Atletico Madrid imekalia uongozi kwa muda baada ya hivi punde kutoka kuifua Real Betis ikiwa kwao kwa mabao 2-0 na kuiengua Real.
Atletico imefikisha pointi 70 sawa na Real Madrid lakini imekwea kileleni kwa uwiano wa mechi baina yao huku uwiano wa mabao Real wakiwa zaidi ya wapinzani wao hao wa jiji moja la Madrid.
Mabvao yaliyozidi kuwapa tumaini la kuwa mabingwa kwa vijana hao wa Diego Simon yaliwekwa kimiani na Gabi katika dakika 58 kwa pasi ya Turan kabla ya Diego Costa kuongeza la pili dakika sita baadaye akimalizia kazi ya Koke.
Katika mchezo huo wenyeji walijikuta wakicheza pungufu baada ya mchezaji wake mmoja Rodriguez kuonyeshwa kadi ya pili ya njano na kufuatiwa na nyekundu katika kipindi cha kwanza.
Hivi sasa uwanjani zipo timu za  Valencia inayoikaribisha Villarreal kabla ya Real Madrid na Barca kuonyesha kazi uwanja wa Santiago Bernabeu ambapo taswira ya ubingwa kwa timu hizo mbili kubwa itafahamika.

Aston Villa yafa nyumbani yagongwa 4-1 kwa Stoke City

Peter Crouch
Peter Crouch akifunga bao lake dhidi ya Aston Villa
Peter Odemwingie
Peter Odemwingie
TIMU ya soka ya Aston Villa imeshindwa kutamba nyumbani baada ya kufumuliwa mabao 4-1 na Stoke City katika mechi ya Ligi Kuu ya England iliyomalizika hivi punde.
Villa ikiyoiduwaza Chelsea wiki iliyopita kwa kuilaza bao 1-0, ilikuwa ya kwanza kupata bao katika dakika ya tano tu ya mchezo kupitia kwa Christian Benteke akimalizia kazi ya Delph.
Hata hivyo wageni walirejesha bao hilo katika dakika ya 22 kupitia Peter Odemwingie aliyemaliza kazi ya mshambuliaji ngongoti, Peter Crouch, ambaye dakika nne baadaye aliipatia Stoke bao la tatu na dakika atatu kabla ya mapumziko N'Zonzi alifunga bao la nne.
Stoke iliongeza bao la nne lililoifanya iiporomoshe Villa katika nafasi ya 10 na kuikalia wao wakibadilishana na wapinzani wao hao wanaowapokea nafasi ya 11 kutokana na kufikisha pointi 37, lilifungwa dakika ya  90 na Cameron.

AS Vita yaifyatua Kaizer Chiefs 3-0

http://www.michezoafrika.com/NewsImages/VIta-club-of-Congo.jpg
KLABU YA AS Vita ya DR Congo imeifumua Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini kwa mabao 3-0 katika mechi za 16 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika, huku AC Leopards ya Kongo ikilazimishwa sare nyumbani na Al Hilal ya Sudan.
mabao yote ya Vita katika pambano hilo yalifungwa na Firmin Ndombe Mubele na kuiweka katika nafasi nzuri timu yake ya kufuzu robo fainali ya michuano hiyo iwapo itakomaa kwenye mechi ya marudiano wiki ijayo nchini Afrika Kusini.
Katika michuano ya Kombe la Shirikisho, Zesco ya Zambia ikiwa ugenini nchini Ghana imechezea kichapo cha mabao 2-0 toka kwa wenyeji wao Medeama, huku Ismailia ya Misri na Petro du Luanda ya Angola zikishindwa kutambiana kwa kutoka suluhu.
Nayo timu ya Warri Woriors ya Nigeria imelazimishwa sare tasa na Bizertin ya Tunisia katika pambano jingine la mkondo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho.
Mechi nyingine za ratiba ya mkondo wa kwanza zinaendelea kuchezwa kwa sasa ukiwamo pambano la TP Mazembe dhidi ya wenyeji wao Sewe Sports ya Ivory Coast.

Inter Milan yapigwa nyumbani, Sampdoria yaua Italia

 http://www.iberita.com/wp-content/uploads/2013/04/inter.jpg
MABINGWA wa zamani wa Ulaya, Inter Milan licha ya kucheza nyumbani, imejikuta ikikong'otwa na Atalanta kwa mabao 2-1katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Seria A.
Milan watakuwa wanamuota Giacomo Bonaventura, aliyefunga mabao yote katika kila kipindi na kuipa ushindi timu yake ugenini.
Bonaventura alianza kuwashutua wenyeji kwa kufunga bao la kuongoza katika dakika ya 35 kabla ya Inter Milan kuchomoa dakika moja baadaye kupiyia kwa Mauro Icardi na kwenda mapumziko wakiwa nguvu sawa.
Kipindi cha pili timu zote zilishambuliana kwa zamu na hasa baada ya kufanya mabadiliko ya wachezaji na wageni wakajiandikia bao lao la pili katika dakika ya 90 lililofungwa tena na Bonaventura.
Katika mechi nyingine za ligi hiyo, Parma ikiwa nyumbani ililazimishwa sare ya 1-1 na Genoa, Bologna ikaifumua Cagliari kwenye uwanja wao wa nyumbani na Sampdoria  ikautumia vyema uwanja wake wa nyumbani kwa kuisambaratisha Hellas Verona kwa mabao 5-0 na Udinese ikiwa nyumbani ikapata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Sassuolo.
Baadaye watetezi Juventus watakuwa ugenini kuumana na Catania, Napoli itapepetana na Fiorentina na Lazio wataumana na AC Milan ambao msimu huu wamekuwa wakipepesuka katika ligi hiyo.

Jahazi la Ashanti Utd lazidi kuzama, yapigwa 2-0

* Mgambo JKT yakomaa Mkwakwani
Ashanti waliyonyukwa 2-0 na Ruvu Shooting

Mgambo waliokomaa Mkwakwani na kutoka sare ya Mtibwa Sugar
Ruvu Shooting walioinyoa Ashanti Utd
TIMU ya soka ya Ruvu Shooting imeutumia vyema uwanja wake wa nyumbani baada ya kuifumua Ashanti Utd kwa mabao 2-0 katika mfululizo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, huku Mgambo JKT ikibanwa nyumbani na Mtibwa Sugar kwenye uwanja wa Mkwakwani-Tanga.
Elias Maguli ambaye alikuwa hajafunga bao lolote tangu duru la pili lianze alifunga bao la kwanza katika dakika ya sita na kuongeza jingine katika dakika ya 63.
Hata hivyo Ruvu iliyokuwa kwenye uwanja wa Mabatini-Mlandizi walijikuta wakicheza pungufu baada ya mchezaji wao Ali Kani kutolewa kwa kadi nyekundu.
Ushindi huo umeifanya Ruvu kufikisha jumla ya pointi 31 na kushika nafasi ya sita pointi moja dhidi ya Kagera Sugar wanaokamata nafasi ya tano.
Katika mechi ya Mkwakwani, Mgambo na Mtibwa zilitoka sare ya 1-1 katika pambano linalodaiwa lilikuwa kali.
Wenyeji walitanguliwa kufungwa bao na Vincent Barnabas kabla ya kuchomoa baadaye kupitia kwa Peter Malianzi na kufanya mchezo huo kuisha kwa sare ya 1-1 na timu zote kuambulia pointi moja kila moja.
Katika pambano hilo mshambuliaji nyota wa Mgambo, Fully Maganga aliwaweka roho juu mabeki wa Mtibwa kwa muda mrefu wa pambano hilo licha ya kwamba hakufanikiwa kufunga bao kwa kukosa bahati siku ya leo.

Timu ya Babi yafufuka Malaysia yashinda 1-0

BAADA ya kupoteza mechi tatu mfululizo hatimaye timu anayoichezea kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Abdi Kassim 'babi' ya UiTM imeona mwezi baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya 'vibonde' wa Ligi Kuu ya Malaysia, PBAPP.
Ushindi huo uliopatikana kwenye uwanja wa Bandaraya katika mji wa Penang, umeifanya UiTM kufikisha pointi saba baada ya kucheza mechi saba, ikishinda mechi mbili na kutoka sare moja na kupoteza mechi nyingine tatu na kushika nafasi ya 10 kati ya timu 12 zinazoshiriki ligi hiyo.
UiTM iliyoingia mkataba wa mwaka mmoja na nyota huyo wa zamani wa Yanga, Mtibwa Sugar, Azam, KMKM na Taifa Stars, itashuka tena dimbani kesho Jumatatu kwa kuumana na Felda United itakayoialika kwenye uwanja wao wa Mini UiTM uliopo mji wa Shah Alam.

Spurs yaizamisha Southampton yaipumulia Arsenal

Christian Eriksen scores Tottenham's second goal
Eriksen akitupia bao lake la pili kimiani dhidi ya Southampton leo
Christian Eriksen
Eriksen akishangilia baada ya kufunga
MSHAMBULIAJI Christian Eriksen leo ameibuka kuwa shujaa wa Tottenham Hotspur baada ya kuhusika na mabao matatu yaliyoizamisha Southampton katika pambano la Ligi Kuu ya England lililochezwa jioni hii.
Mdenish huyo alifunga mabao mawili katika kila kipindi na kutengeneza jingine lililopachikwa wavuni na katika dakika za 'jioni' na Gylfi Sigurdsson na kuipa ushindi murua wa mabao 3-2 Spurs ikiwa kwenye uwnaja wake wa nyumbani.
Eriksen alifunga bao la kwanza katika dakika ya 31 kabla ya kuongeza jingine dakika moja baada ya kuanza kipindi cha pili.
Hata hivyo wageni ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 16 lililofungwa na Jay Rodriguez kabla ya Adam Lallana kuongeza la pili dakika ya 28 na kuwapa wasiwasi wenyeji kwamba huenda wakalala tena nyumbani kama mechi zao kadhaa zilizopita.
Hata hivyo Eriksen alifufua matumaini kwa bao la dakika 31 na kuifanya Spurs kwenda mapumziko wakiwa nyuma kwa mabao 2-1.
Kwa ushindi huo Spurs imerejea kwenye nafasi ya tano iliyokuwa imeteremshwa na Everton iliyoishinda Swansea City jana kwa mabao 3-2 kwa kufikisha pointi 56, sita pungufu na ilizonazo mahasimu wao Arsenal waliopo nafasi ya tanoi baada ya jana kukumbana na kipigo cha paka mwizi mbele ya Chelsea.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea muda mfupi baadaye kwa pambano kati ya Astin Villa dhidi ya Stoke City na Jumanne kushuhudia michezoi mingine ukiwamo wa Manchester City dhidi na Manchester United.

Simba yapigwa kidude na Coastal, Azam haishikiki

Mshambuliaji wa Simba, Ramadhani Singano 'Messi' akijaribu kumtoka mchezaji wa Coastal katika mechi yao ya leoi (Picha kwa hisani ya Bin Zubeiry
WEKUNDU wa Msimbazi, Simba wamejikuta wakiangukia pua mbele ya 'ndugu' zao kutoka Tanga, Coastal Union kwa kudunguliwa bao 1-0 na kuwafanya wapoteze matumaini ya kuendelea kuwepo kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.
Simba, inayonolewa na kocha Zdrakov Logarusic, ilikumbana na kipigo hicho cha kushtukiza kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Bao pekee la mchezo ambao Coastal waliamua kuchezesha wachezaji wengi vijana badala ya wazoefu waliozoeleka, liliwekwa kimiani na beki Hamad Juma katika dakika ya 45 kwa shuti lililomshinda kipa Ivo Mapunda aliyerejea baada ya kuwa nje baada ya kupatwa na msiba wa baba yake mzazi.
Simba pamoja na kucharuka ili kutaka kurejesha bao hilo ilijikuta ikishindwa kumtungia kipa Fikirini Suleiman, aliyekuwa makini kwa dakika zote 90.
Ushindi huo wa Coastal Union umekuja baada ya 'Wazee hao wa Oman'  kutoka kupokea kipigo cha aibu cha mabao 4-0 toka kwa Azam na kujengeka hisia kwamba kuna hujuma iliyofanywa ndani ya kikosi hicho na ndicho kinachoelezwa kimemfanya kocha Yusuph Chipo kufanya mabadiliko katika kikosi chake kilichoivaa Simba.
Katika mechi nyingine, Azam imeendelea kuonyesha dhamira yao ya kutwaa ubingwa msimu baada ya kuinyuka Oljoro JKT kwa bao 1-0, bao lililofungwa na John Bocco 'Adebayor' katika dakika ya 71.
Mechi hiyo ilichezwa kwenye uwanja wa Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam na kuifanya Azam kufikisha pointi 47 nne zaidi na ilizonazo Yanga ambayo haya hivyo ina mchezo mmoja mkononi.
Kwa kuinyuka Simba, mabingwa hao wa Tanzania wamefikisha pointi 29, huku Simba wakisaliwa na pointi 36 wakisalia nafasi ya nne.

Dk Kigwangwala anusurika kufa kwa risasi

http://2.bp.blogspot.com/-kfBD1UB1y9c/Urbf2kmgkwI/AAAAAAACks8/WYl-4rT9G8w/s640/317924_417505948326261_1390417981_n.jpgkupitia ukurasa wake wa Facebook Hamisi kaandika "Nimenusurika kuuawa muda si mrefu. Mungu mkubwa. Askari kwenye gari ananiambia na bahati yako nimekukosa, nililenga kichwa....kijana mmoja alikaa mbele yangu amepigwa risasi kwenye paji la uso, sijui kama amenusurika! Vijana wamenilinda kwa ujasiri bila hofu. Leo askari wamenikamata kwa staha. Siwezi kukubali kamwe dhulma ya mabepari dhidi ya wanyonge! Niliwaahidi na niliapa kuwatetea..."
Mourinho adai PSG wna furaha kukutana nao

 http://www.mwebantu.com/wp-content/uploads/2012/12/Jose-Mourinho-Wallpaper-HD-2.jpg
KOCHA asiyeisha vituko na anayependa kucheza na akili za wapinzani wake, Jose Mourinho wa Chelsea amedai anaamini PSG wana furaha kubwa ya kupangiwa kukutana nao kwenye mechi ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mabingwa hao wa Ligue 1 nchini Ufaransa, ilipangwa Ijumaa kukutana na Chelsea katika mechi ya mkondo huo wa 8 Bora na itaanzia nyumbani April 2 kabla ya kuwafuata 'the Blues' kwenye uwanja wao wa Stanford Bridge siku sita baadaye.
Akizungumza mara baada ya pambano lao la jana la Ligi Kuu ya England dhidi ya Arsenal na kuibuka na ushindi wa kishindo wa mabao 6-0, Mourinho alisema wapinzani wao hao wa Ufaransa ni wazuri na imani mechi yao itakuwa ngumu wakikutana mwezi ujao.

Kocha Man City atabiri nne zitakazotwaa taji EPL

 http://i.dailymail.co.uk/i/pix/2013/05/15/article-2325090-19C218DE000005DC-373_634x413.jpg
MENEJA wa klabu ya Manchester City,  Manuel Pellegrini amesema ubingwa wa Ligi Kuu ya England kwa sasa unaweza kunyakuliwa na timu nne za ligi hiyo.
Pellegrini amesema ukiondoa timu yake na Chelsea inayoongoza msimamo wa ligi hiyo  nyingine zenye nafasi ya kutwaa taji hilo ni Liverpool na Arsenal ambayo jana ilichezea kipigo cha aibu toka kwa Chelsea.
Kocha huyo anayekabiliwa na pambano dhidi ya mahasimu wao wa Manchester, Mashetani Wekundi siku ya Jumanne alisema kwa mwenendo wa Liverpool na hata Arsenal bado zina nafasi licha ya wengi kuzipa nafasi Manchester City au Chelsea kubeba taji hilo msimu huu.
Chelsea inaoongoza msimamo ikiwa na pointi 69 wakati Liverpool inafuatia ikiwa na pointi 65 kisha City yenye pointi sita pungufu dhidi ya vinara hao, ingaw aina michezo mitatu mkononi ikiwa imecheza mechi 28 na Chelsea 3-1.

Thomas Mourice arudi nyumbani kujipanga upya kimataifa

Thomas Mourice (wa pili toka kushoto) akiwa na wachezaji wenzake wa Bandari Kenya enzi akiichezea klabu hiyo
MSHAMBULIAJI nyota wa zamani wa Moro Utd na Yanga, Thomas Mourice amerejea nyumbani baada ya kumaliza mkataba wake na klabu ya Bandari-Kenya, huku akisema anafanya mipango ya kuondoka tena kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.
Akizungumza na MICHARAZO, Mourice aliyewahi kucheza pia katika Ligi Kuu ya Zanzibar, alisema badala ya kuongeza mkataba na klabu yake ya Bandari inayoshiriki Ligi Kuu ya Kenya ameona ni bora aje nyumbani kupumzika kabla ya kujipanga tena kutoka nje ya nchi.
"Nimerejea hivi karfibuni baada ya kumaliza mkataba na Bandari-Kenya, napumzika kidogo kabla ya kuondoka tena kwenda kucheza soka la kulipwa," alisema Mourice.
Mfumania nyavu huyo mahiri, alisema bado hajawa na uhakika ataelekea wapi safari katika mipango yake ya kucheza soka la kulipwa, lakini alidokeza huenda akaibukia Arabuni au barani Ulaya.
"Mimi kokote naweza kwenda kucheza, lakini katika mipango yangu huenda nikaenda Arabuni au Ulaya kulingana na wakala wangu anayeendelea kunisakia timu wakati napumziko hapa nyumbani," alisema.
Mshambuliaji huyo alijiunga na Bandari misimi mitatu iliyopita pamoja na wachezaji wenzake wa Kitanzania akiwamo Mohammed Banka aliyerejea na kujiunga Asdhanti Utd, Meshack Abel na David Naftal wanaoendelea kucheza mpaka sasa na kuisaidia kumaliza nafasi ya 6 msimu uliopita katika ligi ya nchi hiyo ambayo bingwa wake alikuwa Gor Mahia.

Wawili wauwawa Kanisani

mombasa 
VITENDO vinavyoonyesha binadamu hana ujanja mbele ya shetani vimeendelea baada ya leo jumapili tarehe 23/3 watu kadhaa ambao wanasadikika kuwa ni magaidi wamevamia kanisa moja linalojulikana kwa jina la Joy Jesus Church huko Mombasa na kuanza kupiga risasi kanisani hapo.
Mashuhuda wa tukio hilo wanasema baada ya watu hao kutekeleza tukio hilo walikimbia kwa miguu kuelekea pasipo julikana.
Afisa wa polisi wa eneo hilo amesema hadi sasa wamefariki watu wawili na wengine kumi wamepata majeraha ya risasi nakukimbizwa hospitali.
Kikundi cha Al Shabaab kiliwahi kuhusishwa na tukio kama hili huko Nairobi lakini hivi sasa limetokea Mombasa.
Maafisa wa polisi wamesema wanaendelea kufanya uchunguzi wa kuwakamata watu hao japokuwa hadi sasa bado hawajapata tetesi yoyote juu ya watuhumiwa hao