STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, January 12, 2013

Mbio za uchaguzi mkuu wa TFF kuanza rasmi J'3

Deo Lyatto katika majukumu yake ya Uenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF

KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la soka nchini TFF, jana ilitangaza kuzindua rasmi mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa Shirikisho hilo na kutoa fulsa kwa wadau wa soka kuchukua fomu za kuomba kugombea uongozi ndani ya shirikisho hilo.
Uchaguzi mkuu wa TFF umepangwa kufanyika Februari 24 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa kamati hiyo Deogratias Lyatto, alisema kuwa fomu kwa ajili ya kuomba kuwania uongozi wa TFF zitaanza kutolewa Jumatatu, Januari 14 ambapo zitatakiwa kurudishwa kabla ya Januarui 18.
Lyatto alisema kuwa mbali na kuanza rasmi mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa TFF, pia kamati yake imezindua rasmi mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa bodi itakayoendesha ligi kuu Tanzania bara (TPL- Board).
Lyatto alisema kuwa katika uchaguzi wa TFF, nafasi zitakazogombewa ni pamoja na Rais wa TFF, Makamu wa Rais pamoja na nafasi 13 za wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho hilo ambazo zimepangwa katika kanda.
Pia alisema kuwa kwa upande wa Bodi ya TPL, nafasi zitakzogombewa ni Mwenyekiti wa Bodi, Makamu Mwenyekiti pamoja na wajumbe wawili wa bodi hiyo kutoka katika klabu za ligi daraja la kwanza.
Lyatto alisema kuwa kwa nafasi ya Mwenyekiti na makamu wake wa bodi ya ligi kuu ni lazima wawe wenye viti wa klabu za ligi kuu zilizoshika nafasi ya kwanza mpaka ya sita msimu uliopita.
"Kwa wajumbe wa bodi ni lazima wawe wenyeviti wa klabu za ligi daraja la kwanza ambao wote hao pamoja na mwenyekiti na makamu wake wa bodi lazima wapigiwe kura na vilabu," alisema Lyatto.
Alisema kuwa moja ya sifa za kugombea uongozi TFF na katika kamati ya ligi ni lazima mgombea awe na elimu isiyopungua kidato cha nne isipokuwa kwa nafasi ya Rais na Makamu wa Rais wa TFF ambapo atatakiwa kuwa na kiwango cha elimu kisichopungua Shahada ya Chuo Kikuu na awe na uwezo na haiba ya kuiwakilisha TFF ndani na nje ya nchi.
Pia sifa nyingine ni lazima mgombea awe na uzoefu wa uendeshaji wa mpira wa miguu uliothibitishwa kwa angalau miaka mitano na pia asiwe na hatia yoyote ya kosa la jinai na awe amewahi kua ama mchezaji wa mpira wa miguu, Kocha, mwamuzi au kushiriki katika uendeshaji wa mpira wa miguu katika ngazi ya mkoa.
Lyatto alisema kuwa ada ya uchukuaji fomu kwa upande wa Rais wa TFF ni Sh. 500,000, Makamu Rais ni Sh. 300,000 wakati wajumbe wa kamati ya utendaji ya TFF ni Sh. 200,000.
Kwa upande wa bodi ya ligi kuu Mwenyekiti na Makamu wake watachukua fomu kwa Sh. 200,000 wakati wajumbe wa bodi hiyo watachukua fomu kwa Sh. 100,000.
Lyatto alisema kuwa wadau wa soka wenye sifa wabnaruhusiwa kujitokeza kuchukua fomu kuwania uongozi katika chaguzi hizo.
Aidha, alisisitiza wadau wa soka kuwa makini katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi wa TFF.

Kitale azidi kumlilia Sharo Milionea

Kitale katika pozi zake matata

Kitale akiwa na Sharo Milionea katika moja ya kazi walizowahi kuzifanya pamoja
MSANII wa fani ya maigizo na muziki, Mussa Yusuf 'Kitale' amesema itamchukua muda mrefu kumsahau swahiba wake, Hussein Mkiety 'Sharo Milionea' kwa namna walivyokuwa wamezoeana na kufanya kazi pamoja.
Alisema namna rafikiye alivyofariki ghafla huku wakiwa wamejipanga kufanya mambo kadhaa ya kimaisha na kisanii ndiyo yanayomfanya kila mara kukumbwa na jinamizi la kumlilia Sharo, aliyefariki kwa ajali ya gari akielekea Tanga.
Alisema yeye na Sharo walikuwa zaidi ya marafiki, ndiyo maana analizwa na kifo cha msanii huyo aliyekuwa akizidi kupaa kwa umaarufu kwa 'swaga' zake za 'Ooh Mamaaaa', 'Kamata Mwizi Meen', 'Umebugi Meen' na nyingine.
"Ni vigumu kumsahau Sharo Milionea, alikuwa zaidi ya rafiki...kibaya zaidi tulikuwa na mambo mengi tumeyapanga kuyafanya ambayo baadhi tulishayaanza na mengine ndiyo hivyo yameishia njiani," alisema Kitale.
Kitale alisema kwa sasa anafanya mipango ya kuachia kazi mbili alizozifanya na Sharo filamu iitwayo 'Impossible' na wimbo uitwao 'Hili Toto'.

Rooney kuwakosa Liverpool kesho Uingereza

Mshambuliaji nyota wa Manchester United, Wayne RooneyLONDON, England
MFUMANIA nyavu mahiri wa Manchester United,  Wayne Rooney kesho ataukosa mchezo Ligi Kuu ya England dhidi ya Liverpool baada ya kushindwa kupona jeraha lake la kifundo cha mguu amesema kocha wa timu hiyo Alex Ferguson.
Rooney aliumia kwenye mazoezi na kukosa michezop yote ya kipindi cha sikukuu dhidi ya Newcastle United, West Bromwich Albion na Wigan Athletic pamoja na mchezo waliotoka sare wa kombe la FA dhidi ya West Ham United.
"Wayne Rooney bado ataendelea kuwa nje ya uwanja ," Ferguson aliwaambia waandishi wa habari. "Natumaini leo ataanza mazoezi mepesi kwa maana hiyo hatachukua muda mrefu kuanzia sasa kurejea uwanjani. Sidhani kama hilo ni tatizo lakini tutakiwa kimlinda.
"Nategemea atakuwa tayari kurejea uwanjani kwenye mchezo wetu wa Jumatano wa marudiano (Dhidi ya West Ham).
Winga Nani na kiungo  Anderson wote wanarejea kikosini kuwakabili Liverpool kwenye uwanja wa Old Trafford.
"Nani ameanza mazoezi na atajumuishwa kwenye kikosi kwa ajili ya mchezo wa Jimapili (kesho).
"Anderson amerejea mazoezini kwa siku kumi sasa hivyo atakuwepo kikosini kwa ajili ya mchezo wa Jumapili. Lakini yote kwa yote tupo katika hali nzuri na ni vizuri kuwa nao kikosini wote.
United wanaongoza ligi kwa tofauti ya pointi saba nyuma ya majirani zao Manchester City baada ya kucheza michezo 21 na wapo mbele kwa pointi 14 dhidi ya Liverpool wanaoshika nafasi ya nane.
Furgeson alisema kuwa upinzani na Liverpool aubadiliki na siku zote mchezo dhidi yao (Liverpool) ni muhimu kwa kuwa unavuta hisia za mashabiki.

Golden Bush Veterani, Wahenga hapatoshi leo TP Sinza


Kikosi cha Golden Bush Veterani

TIMU ya soka ya Golden Bush Veterani, leo inatarajiwa kushuka dimbani kupepetana na wapinzani wao, Wahenga Fc ikitaka kulipiza kisasi cha kipigo ilichopewa na wapinzani wao hao katika mechi ya kuuaga mwaka 2012.
Golden Bush, ilikumbana na kipigo cha aibu kwa kunyukwa mabao 4-3, licha ya kuchezesha nyota kadhaa wa zamani wa timu za Simba, Yanga na Mtibwa Sugar na waliomba mechi hiyo ya marudiano ichezwe leo kama mechi ya kuukaribisha mwaka mpya wa 2013 na kusherehekea miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Pambano hilo linalosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka wa maeneo ya Sinza na vitongoji vyake kutokana na vijembe vilivyokuwa vimetawala tangu baada ya mechi ya awali iliyochezwa wiki mbili zilizopita na Wahenga kuwazidi maarifa wenzao na kulipa kisasi cha kipigo walichowahi kupewa na wapinzani wao hao.
Wahenga walinyukwa mabao 4-2 katika pambano lililochezwa katikati ya Oktoba, wiki moja baada ya kutoka sare ya baoa 1-1 katika mechi zote zilizochezwa kwenye uwanja wao wa nyumbani wa TP Sinza.
Pande mbili za timu hizo wamekuwa wakitambiana kwamba leo ndio mwisho wa mzizi wa fitina, Golden Bush wakiapa lazima warejeshe kipigo hicho walichopewa na Wahenga walichokilalamikia kilichangiwa na maamuzi ya 'kimamluki' yaaliyokuwa yakifanywa na mwamuzi, Ally Mayay Tembele.
Mlezi wa Golden Bush, Onesmo Waziri 'Ticotico' alisema kuwa kikosi chao kimejiandaa vya kutosha kwa ajili ya mechi hiyo itakayochezwa majira ya jioni kwenye uwanja wa TP, huku akiwahimiza mashabiki wajitokeze kwa wingi kushuhudia watakavyoishindilia mabao Wahenga.
"Tutakachofanya leo ni kujumlisha idadi ya mabao tuliyofungana mechi iliyopita, yaani 4+3 na idadi yake ndiyo ambayo Wahenga watakavyobeba kipigo hicho, tupo fiti na mie mwenyewe natarajia kusaidia safu ya mashambulizi kwa sababu jamaa wamechonga sana baada ya kutuotea Desemba 31," alisema Ticotico.

Hatari katika lango la Wahenga, Golden Bush siku walipotoka sare ya bao 1-1. Je leo nani atakayecheka au kulia?

Azam bila Kipre Tchetche kuivaa Tusker leo Zanzibar

Kikosi cha mabingwa watetezi wa Kombe la Mapinduzi, Azam Fc
Kikosi cha mabingwa wa Kenya, Tusker

TIMU ya soka ya Azam inatarajiwa kuvaana na Tusker ya Kenya katika pambano la fainali za michuano ya Kombe la Mapinduzi bila ya mshambuliaji wake nyota, Kipre Tcheche, ingawa inafurahia kurejea kwa kiungo wao, Abdulhalim Humud 'Gaucho'.
Azam ambao ni mabingwa watetezi wa michuano hiyo, itaumana na Tusker katika pambano litakalofanyika kwenye uwanja wa Amaan, Zanzibar, huku uongozi wa klabu hiyo ukitamba umejipanga kutetea taji hilo licha ya kukiri itakuwa mechi itakuwa ngumu.
Mabingwa hao watetezi walipata nafasi hiyo kwa kuing'oa Simba katika mechi ya fainali kwa mikwaju ya penati 5-4 baada ya kutoka sare ya 2-2 katika muda wa dakika 120 wakati Tusker walifuzu juzi kwa kuilaza Miembeni kwa mabao 2-0.
Azam itashuka dimbani bila ya nyota wake Kipre Tchetche aliyeumia katika pambano dhidi yao ya Coastal Union, japo karibu kikosi chake chote kipo imara hasa baada ya kurejea kwa kiungo nyota, Abdulhalim Humud 'Gaucho'.
Afisa Habari wa Azam, Jafar Idd 'Mbunifu' alisema kurejea kwa Humud kumewapa faraja na matumaini makubwa ya kutetea ubingwa huo walioutwaa mwaka jana kwa kuilaza Jamhuri ya Pemba mabao 3-0.
Idd alisema licha ya kutarajia kupata upinzani mkubwa kutoka kwa Tusker aliokiri ni moja ya timu ngumu isiyotabirika, lakini wamejipanga kutetea ubingwa wao kwa mara ya pili mfululizo.
"Kwa kweli tumejipanga vema, japo hatutakuwa na Kipre Tchetche aliye majeruhi, lakini kocha John Stewart Hall amemuita Humud aliyepona ambaye ameshatua mjini hapa tayari kwa pambano hilo la kesho (leo) dhidi ya Tusker," alisema Idd.
Kwa mujibu wa rekodi za michuano hiyo ni Yanga pekee iliyowahi kutetea taji kwa kulitwaa mara mbili mfululizo, ilivyofanya hivyo mwaka 2004 na 2005, wakati miaka mingine yote kila anayetwaa taji hilo hushindwa kulitetea.
Mabingwa waliopita wa michuano hiyo ni;
2003-Mtibwa Sugar
2004-Yanga SC
2005-Yanga SC
2006-Simba SC
2007-Yanga SC
2008-Simba SC
2009-Miembeni FC
2010-Mtibwa Sugar
2011-Simba FC
2012-Azam FC
2013   ???

TAIFA STARS HOI ETHIOPIA YAPIGWA 2-1 NA WAHABESHI


Na Boniface Wambura, Addis Ababa
TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imepoteza mchezo wa kirafiki dhidi ya Ethiopia uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Addis Ababa hapa mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Mechi hiyo iliyochezeshwa na Bamlak Tesema wa Ethiopia ilikuwa ya kusisimua, hasa kutokana na timu zote kucheza kwa kasi kwa muda wote. Wenyeji Ethiopia ndiyo walioanza kupata bao dakika ya 13 lililofungwa na Fuad Ibrahim akiwa wastani wa hatua sita kutoka kwa mlinda mlango Juma Kaseja wa Taifa Stars.
Bao hilo liliweza kumudu hadi timu hizo zilipoenda mapumziko licha ya kuwepo kwa kosa kosa za hapa na pale.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kama kilivyokuwa cha kwanza, huku Ethiopia wakiwa wamefanya mabadiliko kwa wachezaji watano. Tanzania ilifanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 50 likifungwa na Mbwana Samata baada ya kumzidi maarifa beki mmoja wa Ethiopia.
Bao la ushindi kwa Ethiopia lilifungwa kwa kichwa dakika ya 69 na mshambuliaji Shemelis Bekele aliyeingia kipindi cha pili akiunganisha mpira wa krosi uliopigwa na winga Yossuf Sallah kutoka upande wa kushoto.
Taifa Stars inarejea nyumbani leo (Januari 12) ambapo itatua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 7 kamili mchana kwa ndege ya Ethiopian Airlines.
Katika pambano hilo Stars iliwakilishwa na kikosi kifuatacho;
Taifa Stars: Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Issa Rashid, Shomari Kapombe, Aggrey Morris, Amri Kiemba, Mrisho Ngasa, Salum Abubakar, Thomas Ulimwengu/Khamis Mcha, mwinyi Kazimoto na Mbwana Samata.

OMBAOMBA FEKI ATIMKA BAADA YA KUGUNDULIKA SIO MLEMAVU


Baada ya kugundua wananchi wamemshtukia baada ya kumhoji maswali na kushindwa kujibu aliamua kutimua mbio kukwepa kamera ya Francis Godwin isimpate picha yake, kama unavyomuona hapo mdau mguu gafla umetokea kimiujiza pamoja na mkono, yote hiyo alikuwa ameificha kwa kutumia koti lake na Suruali alizovaa. 
Baada ya hali kuwa tete alijikuta anazisaha umpaka kandambili zake, kama unavyoziona. 
Huyu ni omba omba anayeigiza kutokuwa na mkono mmoja na mguu Mmoja akiwa amekaa eneo la M.R Iringa mjini akisubiri kuomba chochote kutoka kwa wapita njia leo.

ULE usemi wa wahenga kuwa ukistaajabu ya Mussa utayaona ya Firauni, ulitimia katika eneo la M.R,  mjini Iringa baada ya wananchi waliokuwepo eneo hilo kupigwa na butwaa baada ya ombaomba marufu anayefahamika kama Mzee Janja anayeshinda katika eneo hilo akijifanya mlemavu aliyekuwa na mkono na mguu mmoja mmoja, kutimua mbio kukwepa kamera ya mapaparazi mjini humo.
Tukio hilo limetokea majira ya saa 8 mchana baada ya kamera ya mtandao wa Francis Godwin kufika eneo hilo la kushuhudia umati wa wananchi wakiendelea kumpa fedha Mzee Janja, ambaye walikuwa wakidhani ni mlemavu wa viungo, na anayeongea kwa tabu..
Hata hivyo baada ya mmoja kati ya wananchi kufika eneo hilo alionyesha kufichua mbinu hiyo chafu ya mzee huyo kujifanya ni mlemavu wakati asubuhi alikutana nae maeneo ya mjini akiwa mzima wa afya njema na katika kumhoji zaidi ndipo kamera ya mtandao huo ilipoamua kufanya kazi yake ya kunasa kituko hicho na ndipo mzee huyo alipoanza kuongea kwa sauti vizuri tofauti na alivyokuwa akijifanya kuwa hawezi kuongea kabisa (bubu)

Wakati mabishano yakiendelea eneo hilo ghafla mzee huyo alisimama kwa miguu yake yote miwili pamoja tofauti na  awali alivyokuwa akijifanya ni mlemavu asiye na mguu mmoja ila baada ya watu kutaka apigwe picha ndipo mzee huyo alipoanza kutimua mbio huku ulemavu aliokuwa nao akiusahau hapo pamoja na kandambili zake na hakuna mtu aliyeweza kumfukuza na kufanikiwa kumkuta.

Baadhi ya wananchi wameuomba uongozi wa Manispaa ya Iringa kuwabana omba omba hao ambao wamekuwa wakidanganya watu kuwa wao ni walemavu kumbe ni wazima na kutaka kuwepo kw

THOMAS MASHALI, MKENYA KUMALIZA UBISHI LEO JIJINI DAR


Bondia  Benard Mackoliech wa Kenya akipimwa afya na Dk Madorina
Mabondia Thomas Mashali na Bernad Mackoliech wa Kenya wakitunishiana misuli baada ya kupima uzito jana Dar es Salaam.


MABONDIA Thomas Mashali wa Tanzania na Mkenya Benard Mackoliech, leo wanatarajiwa kumaliza ubishi baina yao watakapopanda kwenye ulingoni kupigana kuwania ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati.
Mgeni rasmi katika pambano hilo la uzani wa kati litakalokuwa la raundi 10 anatarajiwa kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela pamoja na kuhudhuriwa pia na wabunge Idd Azan na John Mnyika.
Pambano hilo litafanyika kwenye ukumbi wa Friends Corner, Manzese Dar es Salaam na litasindikizwa na michezo minne ya utangulizi itakayowahusisha mabondia nane watakaoumana katika mapambano ya raundi nane nane.
Mratibu wa pambano hilo, Aisha Mbegu na Rais wa Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa nchini, TPBO, Yasin 'Ustaadh' Abdallah, walisema kuwa maandalizi ya mapambano hayo yamekamilika na kuwahimiza mashabiki wa mchezo huo kujitokeza kwa wingi kuungana na wazanzibar kuadhimisha miaka 49 ya Mapinduzi.
Mabondia hao wanakutana kwa mara ya kwanza na Mashali atakuwa akitetea taji lake alilolitwaa Oktoba 14 mwaka jana kwa kumshinda kwa pointi Mganda Med Sebyala.