STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, February 9, 2014

Manchester Utd yazidi kuchechemea yabanwa nyumbani na Fulham

Darren Bent scores Fulham's equaliser
Darren Bent akiisawazishia Fulham bao dakika za lala salama
BAO la dakika ya 94 lililofungwa na Darren Bent liliiokoa Fulham dhidi ya kipigo toka kwa Mashetani Wekundu, Manchester United waliokuwa nyumbani kwao na kutoka sare ya 2-2.
Manchester United walioonekana kama wamevuna pointo zote tatu baada ya Robin van Persie na Michael Carrick kufunga mabao mawili na kuinyamazisha Fulham waliotangulia kupata bao la mapema la dakika 19 lililofngwa na Steve Sidwell.
Juan Mata alimtengenezea nafasi nzuri van Persie aliyefunga bao la kusawazisha dakika ya  78 kabla ya Carrick kuongeza la pili dakika mbili baadaye.
Hata hivyo mashabiki wa Old Trafford wakiamini wapata ushindi nyumbani, Bent alifunga bao la kusawazisha dakika nne za nyongeza za mchezo huo na kuipa pointi moja Fulham ugenini.
Matokeo hayo yameendelea kuiacha Manchester ambayo Jumatano itaifuata Arsenal iliyonyukwa jana na Liverpool kwa mabao 5-1, ikibaki nafasi ya saba ikiwa na pointi 41.

KMKM yawa Urojo Ethiopia kama Chuoni Zimbabwe

KMKM ya Zanzibar
KLABU za Zanzibar zimeendelea kuwa urojo baada ya jioni hii KMKM kutandikwa mabao 3-0 na Dedebit ya Ethiopia katika Ligi ya Mabingwa Afrika kama ilivyokuwa 'ndugu' Chuoni nchini Zimbabwe jana kwenye Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya wenyeji wao How Mine.
Kwa mujibu wa matokeo kutoka Addis Ababa, wenyeji walipata mabao yao katika vipindi vyote viwili, hadi mapumziko waliongoza kwa bao 1-0 lililoifungwa na Dawit Fekadu dakika ya 16.
Kipindi cha pili kilikuwa kigumu kwa KMKM baada ya kuongezwa mabao mengine mawili yaliyofungwa na Shimekit Gugsa dakika ya 52 kabla ya Micahel George kumalizia kazi dakika sita kabla ya pambano hilo kuisha.
Kwa matokeo hayo klabu za Zenji zimeendelea kuwa wasindikizaji katika michuano ya kimataifa kwani KMKM italazimika kupata ushindi wa mabao 4-0 ili kusonga mbele, kazi ambayo pia inayo Chuoni iliyopigwa 4-0 na How Mine ya Zimbabwe jana na kuonekana ni ndoto kushinda nyumbani 5-0.

Adebayor aipaisha Spurs, waishusha Everton

Emmanuel Adebayor
Adebayor akipongezwa na Paulinho baada ya kufunga bao pekee dhidi ya Everton

Tottenham 1-0 EvertonMSHAMBULIAJI kutoka Togo Emmanuel Adebayor jioni hii ameiwezesha Tottenham Hotspur baada ya kufunga bao pekee lililoiwezesha kuizima Everton na kurejea kwenye nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu ya England.
Adebayor alifunga bao hilo lililokuwa la tano kwake msimu huu kwenye ligi hiyo katika dakika ya 65 akimalizia kazi nzuri ya Kyle Walker na kumtungua Tim Howard na kuifanya Spurs kufikisha pointi 47 na kuwa nyuma ya Liverpool yenye pointi 50.
Everton waliokuwa wakishika nafasi ya tano kabla ya mchezo huo, imeshuka hadi nafasi ya sita ikisaliwa na pointi zake 44.
Muda mchache ujao, Manchester United wanaokamata nafasi ya saba watakuwa uwanja wake wa nyumbani wa Old Trafford kupepetana na Fulham katika pambano jingine la ligi hiyo.

Azam yatamba Afrika, yawapiga Wamakonde kidude

AZAM FC imepata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Ferroviario de Beira ya Msumbiji katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Awali Kombe la Shirikisho Afrika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam jioni hii.
Shukrani kwake mshambuliaji kutoka Ivory Coast, Kipre Herman Tchetche aliyefunga bao hilo pekee dakika ya 41 baada ya kutengewa pasi nzuri ya kichwa na Mganda Brian Umony na kufumua shuti kali.
Mchezo ulikuwa mkali dakika zote 90 na mashambulizi yalikuwa ya pande zote mbili.
Wachezaji wa Azam wakimpongeza Kipre Tchetche leo Chamazi

Mshambuliaji wa Ivory Coast, Kipre Tchetche na Mganda Umony kwa pamoja na Mzanzibari Khamis Mcha ‘Vialli’ walikuwa mwiba kwa safu ya ulinzi ya Ferroviario.  
Kipindi cha pili, Ferroviario walicharuka zaidi na Azam nao walipoteza nafasi kama tatu za kufunga mabao mwanzoni. 
Refa Mutaz Abdelbasit Khairalla na wasaidizi wake Waleed Ahmed Ali na Aarif Hassan Eltom wote kutoka Sudan walionekana kabisa kuwapendelea wageni katika maamuzi yao. 
Dakika ya 70 beki mmoja wa Ferroviario aliunawa mpira wazi wazi kwenye eneo la hatari kufuatia shuti la Kipre Tchetche mbele ya refa, lakini akapeta. 
Kiungo mkabaji wa Ferroviario, de Beira akipiga tik tak dhidi ya mshambuliaji wa Azam FC, Brian Umony leo Chamazi
Kipre Tchetche akimtoka beki wa kushoto wa Ferroviario, Emidio Matsinhe leo

Matokeo hayo yanamaanisha Azam itakuwa na kazi ngumu katika mchezo wa marudiano wiki mbili zijazo nchini Msumbiji, wakitakiwa kulazimisha sare ili kusonga mbele.
Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Mwadini Ali, Erasto Nyoni, Malika Ndeule, Aggrey Morris, Said Mourad, Kipre Balou, Salum Abubakar, Himid Mao, Khamis Mcha/John Bocco dk61, Kipre Tchetche na Brian Umony/Jabir Aziz dk81.
Ferroviarrio; William Manyatera, Zefanis Matsinhe, Emidio Matsinhe, Abrao Cura/Kiki Simao, Edson Morais, Reinildo Mandava, Valter Mandava/Hery Antony, Antonio Machava, Manuel Fernandes, Mario Sinamunda na Manuel Correia/Dje Buzana.

BIN ZUBEIRY

Simba ya Logarusic yafa Tanga, Mbeya yainyuka Mtibwa, Coastal yatamba Tabora, Oljoro yanabwa na Kagera

Mgambo JKT
Mbeya City
Coastal Union iliyoshinda ugenini mjini Tabora dhidi ya Rhino Rangers
Mtibwa Sugar iliyokufa jijini Mbeya kwa mabao 2-1
BAO pekee la dakika ya 28 lililofungwa na Full Maganga limetosha kuiua 'Mnyama' Simba inayonolewa na kocha mwenye mbwembwe, Zdravko Logarusic mbele ya Mgambo JKT katika pambano la Ligi Kuu Tanzania Bara lililochezwa Mkwakwani Tanga.
Simba ambayo iliitafuna Mgambo iliyokuwa ikifundishwa na King Abdallah Kibadeni kwa mabao 6-0 licha ya juhudi za kutaka kurejesha bao hilo ilishindwa kabisa kuwapa raha mashabiki wake kwa kukubali kipigo cha pili kwa msimu huu na cha kwanza chini ya Logarusic tena kwa timu kibonde ya Mgambo.
Huo ni ushindi wa pili mfululizo kwa Mgambo JKT ambayo ilikuwa ikiburuza mkia kwa kipindi kirefu baada ya wiki iliyopita kuicharaza Ashanti United uwanja wa cha Chamazi.
Ushindi huo umeifanya timu hiyo inayonolewa na kocha mpya Bakar Shime imefikisha pointi 12 huku Simba ikisaliwa na 31 na kushuka nafasi ya nne iliyokuwa awali baada ya Mbeya City kushinda mabao 2-1 dhidi ya Mtibwa Sugar mjini Mbeya.
Bao la Mtibwa lilifungwa na Jamal Mnyate kabla ya Mbeya kurudisha bao kupitia na Peter Mapunda kwa kichwa na bao la ushindi  lilifungwa na Amani Kibokile. Dakika mbili kabla ya kumalizika mchezo Mtibwa ilipata bao la kusawazisha ambalo hata hivyo lilikataliwa na mwamuzi Israel Mkongo.
Mechi nyingine zimeshuhudia Coastal Union ikipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji wao Rhino Rangers ya Tabora kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, huku Oljoro JKT ilibanwa nyumbani na Kagera Sugar na kutoka nao sare ya 1-1.

DAVID NAFTALI: Kiungo anayetaka viongozi wa soka kuacha mambo ya mwaka '47
David Naftali katia picha tofauti akiwa nchini Kenya
WAKATI wachezaji wenzake wanaocheza nje ya nchi wakirejea nyumbani, kiungo mkabaji David Naftal anasema hana mpango huo kwa sababu havutiwi na mfumo wa soka uliopo nchini.
Nyota huyo wa zamani wa timu za AFC ya Arusha na Simba anayeichezea Bandari ya Mombasa inayoshiriki ligi kuu ya Kenya anasema mfumo wa soka nchini hauthamini na kuwajali wachezaji kama ilivyo Kenya.
Anasema tangu atue nchini humo miaka mitatu iliyopita, hajawahi kusikia viongozi wa klabu wakiwatuhumu wachezaji kuzihujumu timu zao au kuuza mechi kama ilivyozoeleka hapa, hasa kwa Simba na Yanga.
"Huku matokeo ya aina yoyote yanachukuliwa sehemu ya mchezo," anasema. "Tanzania timu ikifungwa tu anatafutwa mchawi na watu wa kwanza huwa wachezaji bila kujali wanavyovuja jasho uwanjani kupigania timu."
Anasema vitendo vya kuwatuhumu wachezaji ni mambo ya kizamani yanayowavunjia heshima na kuwakatisha tamaa.
Naftal anayemudu nafasi nyingi uwanjani, anasema lazima viongozi wa soka wa Tanzania wabadilike na kutambua mchezo huo una matokeo matatu: kushinda, kufungwa na sare. Aidha, anasema, wasiamini timu zao ni bora kiasi cha kutofungika.
Mkali huyo anayefurahia kucheza Kenya na kuaminiwa na klabu yake ya Bandari, anasema kuwapo kwake nchini humo kumemfundisha mambo mengi ikiwamo tofauti iliyopo baina ya soka la Tanzania na nchi hiyo jirani.
Anasema Tanzania ina wachezaji wengi wenye vipaji lakini wasimamizi wa soka wamejisahau na kuelekeza  macho mijini. Pia anadai mfumo wa soka wa Kenya na Tanzania kwa ngazi za klabu umetofautiana sana, Kenya klabu zikiendeshwa 'kisomi' kulinganisha na Tanzania licha ya kwamba mchezo huo unaingiza fedha nyingi zaidi nchini.
"Kenya klabu zake zipo kiprofesheno zaidi kulinganisha na Tanzania, ila kifedha Tanzania ipo juu ndiyo maana wachezaji wa kigeni wanamininika huko."
Naftal anasema ndoto zake ni kuzidi kusonga mbele na ndiyo maana hana mpango wa kurudi nyumbani.
Anasema kwa sasa anafanyiwa mipango na wakala wake kwa ajili ya kwenda kucheza nchini Afrika Kusini wakati mkataba wake ukielekea kugota ukingoni Septemba.
Naftal ambaye ni shabiki mkubwa wa klabu ya Manchester United lakini anayemzimia kiungo Yaya Toure wa Manchester City, na ambaye wakati akiwa Simba alianza kucheza kama mshambuliaji, anasema anafurahishwa na changamoto zinazotolewa na klabu za Mbeya City na Azam katika ligi kuu ya Bara kwa sababu "itasaidia kuvunja ligi ya timu mbili za Simba na Yanga."
Anasema kuibuka kwa Mbeya City ni dalili za wazi kwamba mikoani kuna wachezaji wenye vipaji na kama kutakuwa na wawekezaji wanaweza kuleta mapinduzi katika soka la Tanzania.
"Ni lazima TFF na serikali kutupia macho soka la mikoani, kule ndiko kunakoweza kupatikana akina Samuel Et'oo na Didier Drogba wa Tanzania,Mbeya City ni mfano halisi."
" anasema.
NIPASHE JUMAPILI

Simba, Mbeya City kuombeana mabaya leo VPL?

Mbeya City
Simba
LICHA ya kwamba zitakuwa kwenye viwanja tofauti, lakini timu za Simba na Mbeya City zitakuwa zikiombeana mabaya watakapokuwa wakiumana kuwania pointi tatu ili kujiweka pazuri kwenye msimamo.
Simba watakuwa ugenini kuuamana na Mgambo JKT, wakati Mbeya itakuwa nyumbani uwanja wa Sokoine kuumana na Mtibwa Sugar.
Mechi hizo mbili kati ya nne zinazochezwa leo zinafuatiliwa kwa karibu kutokana na timu hizo kulingana pointi na zikifukuzana kwenye msimamo unaoongozwa na Azam ambayo leo itakuwa na majukumu ya kimataifa katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Ferroviario de Beira ya Msumbiji.
Timu hizo zina pointi 31 kila mmoja na zinatofautiana uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa na kila mmoja watakuwa wakiwaombea wenzao wateleze ili kukalia nafasi ya tatu na kuwasogelea Yanga waliopo nafasi ya pili na pointi zao 35.
Kocha msaidizi wa Simba Seleman Matola amesema timu yake imepania kupata ushindi katika mchezo wa leo wa ligi kuu ya soka ya Bara dhidi ya Mgambo JKT kwenye Uwanja wa Mkwakwani, hasa baada ya kupata sare kwenye mechi iliyopita dhidi ya Mtibwa Sugar.
"Ile sare ilimuuma kila mtu kuanzia wachezaji mpaka benchi la ufundi," alisema Matola.
Aidha, alisema kuwa hakuna majeruhi kwenye kikosi chake na kila mchezaji amepewa majukumu kuhakikisha wanapata pointi tatu. Mgambo inashika mkia katika msimamo wa ligi kuu ikiwa imeshinda mara mbili katika michezo 16 mpaka sasa.
Matola alisema kupoteza mchezo au kutoka sare wakati wapinzani wao wakipata ushindi kutawaweka katika mazingira magumu.
"Mbio za ubingwa ni ngumu hivyo hatutakiwi kupoteza mchezo sasa hivi... tunajua Mgambo wanacheza mpira wa nguvu lakini tumejiandaa kuwakabili."
Mbeya wenyewe watrakuwa na kibarua kigumu kwa Mtibwa Sugar na kocha wake, JUma Mwambusi amenukuliwa akisema wamejiandaa kushinda nyumbani baada ya kuteleza ugenini mvele ta Yanga.
Mbeya City, 'ilitenguliwa udhu' na Yanga kwa kufungwa kwa mara ya kwanza kwenye ligi hiyo iliyoipanda msimu huu baada ya kunyukwa bao 1-0 kwenye uwanja wa Taifa wiki iliyopita na kutibua rekodi yao waliyokuwa wanachuana na Azam ambayo ndiyo pekee sasa haijapoteza mchezo wowote katika ligi hiyo.
Mbali na mechi hizo mbili zinzofuatiliwa, leo pia kutakuwa ni michezo mingine miwili Oljoro JKT kuikaribisha Kagera Sugar uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha na Rhino Rangers kuikaribisha Coastal Union mjini Tabora katika pambano litakalochezwa uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.

MASHINDANO YA NGUMI YA NELSONI MANDELA OPEN CHAMPIONSHIP YAMALIZIKA KAWE

Bondia Rudia Mashala kushoto akioneshana umwamba wa kutupiana makonde na Ratifa Khalidi wakati wa mashindano ya Nelson Mandela Open Champion Ship yaliyo malizika katika viwanja vya Kawe Dar es salaam Ratifa alishinda kwa point Picha na www.superdboxingcoach.blogspot.com

Bondia Ezira Paur wa Kigoma akipambana na Hafidhi Kassimu wa Ngome wakati wa mashindano ya Nelson Mandela Open CHampion Ship yaliyomalizika kawe Dar es salaam Paur alishinda kwa point Picha na www.superdboxingcoach.blogspot.com

Baadhi ya watu waliofulika kuangalia michuano hiyo

Meya wa Kinondoni akizungumza wakati wa kufunga mashindano hayo

Mjumbe wa maendeleo ya wanawake katika mchezo wa masumbwi nchini Aisha Vonialis katikati akiwa na mabondia wa kike waliopigana na kunyakuwa zawadi mbalimbali

Meya wa Manspaa ya Kinondoni Yussuph Mwenda akimkabizi  Mwenyekiti wa timu ya Mkoa wa Kigoma  Eddie Kikwesha  baada ya kuibuka timu yenye Nidhamu katika mchezo wa masumbwi katikati ni Mjumbe wa maendeleo ya wanawake katika mchezo wa masumbwi nchini Aisha Vonialis

Katika picha ya pamoja
Rais wa Shilikisho la ngumi za Ridhaa Nchini BFT Mutta Rwakatare akimzawadia kocha wa timu ya kawe baada ya kuibuka washindi wa tatu katika mashindano hayo

Real Madrid bila Ronaldo yaua nyumbani, Gale atupia moja na kusaidia jingine

Gareth Bale akifunga bao la kwanza la Madrid ikiwa nyumbani jana
BILA ya nyota wake Cristiano Ronaldo anayetumikia adhabu ya kadi nyekundu, Real Madrid usiku wa kuamkia leo wamezidi kujiimarisha kileleni kwa La Liga baada ya kuishindilia Villareal kwa mabao 4-2.
Pambano hilo lililochezwa kwenye uwanja wa Santiago Bernabeu, wenyeji Madrid walianza mapema kuonyesha dhamira yao ya kupata ushindi kwa kuandika bao la kwanza lililofungwa na Gareth Bale katika dakikia ya 7 tu ya mchezo.
Mfaransa Karim Benzema aliiongezea Madrid bao la pili dakika ya 25 akimalizia kazi nzuri iliyofanywa na Bale na dakika mbili kabla ya mapumziko, Mario aliifungia wageni bao la kufutia machozi.
Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kushambuliana na kufanya mabadiliko kadhaa yaliyozisaidia timu hizo, japo wenyeji walinufaika zaidi kwa kuongeza mabao mengine mawili yaliyofungwa na Jesé Rodríguez dakika ya 64 baada ya kazi nzuri ya Angel di Maria na Benzema kuongeza jingine dakika ya 76 japo wageni alitangulia kupata bao lao la pili la kufutia machozi lililowekwa kimiani na Giovan dos Santos dakika ya 69.
Ushindi huo umeifanya Madrid kufikisha pointi 57 sawa na Atletico Madrid ambayo yenyewe iulinyukwa ugenini mabapo 2-0 na Almeria na kumpoteza kipa wake aliyeoonyeshwa kadi nyekundu.
Katika mechi nyingine za ligi juzi Espanyol ilishinda bao 1-0 nyubani dhidi ya Granada huku Valencia jana iliishindilia bila huruma Real Betis kwa mabao 5-0 na Rayo Vallecano kuichapa Malaga mabao 4-1.
Leo kutakuwa na mechi nyingine kadhaa ya ligi hiyo ambapo Osasuna itaumana na Getafe, Real Valladolid kuvaana na Elche, huku Real Sociedad itaonyeshana kazi na Levante, Sevilla itaikaribisha mabingwa watetezi Barcelona na keshokutwa Celta Vigo itaialika Athletic Club nyumbani kwake.

AC Milan Mwaka wa Majanga, Napoli yainyoa 3-1