STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, July 7, 2010

Forlan alicheza akiwa majeruhi-Kocha
CAPE TOWN, Afrika Kusini
NYOTA tegemeo wa timu ya taifa ya Uruguay, Diego Forlan, alicheza pambano la nusu fainali dhidi ya Uholanzi akiwa majeruhi na kumlazimisha kocha wake Oscar Tabarez, kumtoa nje kabla ya kumalizika kwa pambano hilo.
Forlan aliyekaririwa jumanne iliyopita kwamba katu hawezi kurejea tena katika Ligi Kuu ya Uingereza na kufuta ndoto za meneja wa Tottenham Hotspur, Harry Redknapp kumnyakua, alimua tangu mwanzo wa mchezo huo.
"Tangu dakika ya kwanza Forlan alikuwa na tatizo. Aliumia na hakuweza kuendelea kucheza,"
"Alikuwa na maumivu na wakati wa mchezo tuliamua kuchukua maamuzi ya kumjaribu kumbadili na mchezaji mwingine" aliongeza Tabarez.
Hata hivyo kocha huyo alisema tatizo la mshambuliaji huyo anayeichezea Atletico Madrid ya Hispania, sio kubwa na huenda kesho akacheza kuipigania nchi yake katika pambano la kusaka mshindi wa tatu kati yao na mshindi kati ya Ujerumani na Hispania.
"Sio tatizo lake halikuwa kubwa, lakini hakuwa fiti kwa asilimia 100 kucheza hadi mwisho," alisema kocha huyo.
Forlan, mshambuliaji wa Atletico Madrid ya Hispania, alifunga bao maridadi wakati timu yake iliposhindwa mabao 3-2 na Uholanzi.
Mshambuliaji huyo alifunga bao hilo dakika moja kabla ya mapumziko kwa shuti kali la umbali ya mita 30 lililomshinda nguvu kipa wa Uholanzi, Maarten Stekelenburg.
Huenda kesho mchezaji huyo aliyeifungia timu hiyo mabao manne katika fainali hizo za WOZA 2010 akawemo katika pambano la kusaka mshindi wa tatu litakalochezwa kwenye mjini wa Port Elizabeth.

Sajuki: Mkali wa filamu anayeulilia mguu wa mkewe


NDOTO zake enzi akiibukia kwenye sanaa ilikuwa ni kuja kuwa mchekeshaji kutokana na kumzimia mno, msanii Athuman Amir 'King Majuto'.
Hata hivyo kupenda kwake kuangalia filamu za Sylvester Stallone 'Rambo' zilimfanya abadili upepo na kujikita kwenye uigizaji wa kawaida na kisha kujitumbukiza kwenye tasnia hiyo, ambapo leo ni mmoja wa nyota wa fani hiyo nchini.
Sajuki, ambaye majina yake kamili ni Juma Juma Issa Kilowoko, alisema hamu yake ya kufika mbali katika sanaa ya uigizaji ndiyo iliyomfanya apite kundi moja hadi jingine hadi kuangukia Kaole Sanaa, lililomtangaza vema kupitia michezo iliyokuwa ikirushwa na kituo cha runinga cha ITV.
Alisema mchezo wake wa kwanza ndani ya kundi hilo lililotoa nyota kibao wa filamu nchini ni Baragumu wa mwaka 2005 na kufuatia na michezo mingine hadi mwaka 2008 alipojitoa kundini na kujikita zaidi katika filamu, kazi yake ya kwanza ikiwa ni Revenge.
"Baada ya kupita makundi kadhaa tangu nikiwa mjini Songea nilipozaliwa, hatimaye nilitua Kaole Sanaa, lililoniivisha kabla ya kuachana nao kusaka masilahi zaidi na kujikita katika filamu," alisema.
Mbali na Revenge filamu zingine alizocheza Sajuki ni pamoja na Dhambi, Mboni Yangu, Two Brothers, Behind the Scene, Round, Shetani wa Pesa, Hero of the Church na nyinginezo.
Kwa sasa yupo mbioni kuachia kazi mbili binafsi za Vita na Briefcase zilizowashirikisha nyota kadhaa nchini akiwemo mshindi wa pili wa BBA, Mwisho Mwampamba.
Sajuki alisema fani ya filamu imemnufaisha kwa mambo mengi ikiwemo kimaisha, lakini kubwa ni kufanikiwa kumuoa mke mrembo na muigizaji mwenzake, Wastara Juma.
"Kufanikiwa kumpata Wastara na kumuoa kwangu ni jambo kubwa na la kuvutia mno kati ya mafanikio kibao niliyoyapata katika fani hii ya filamu nchini," alisema.
Mkali huyo, ambaye hupenda kucheza na watoto na shabiki wa muziki wa 'Quito', alisema kama kuna kitu kinachomkera katika sanaa hiyo ni tabia za 'Wauza Sura' wanaojiingiza kwenye skendo chafu zinazowachafua wasanii wote wa tasnia hiyo mbele ya jamii.
Alisema wasanii wenye kusaka umaarufu kwa lazima wanamnyima raha kwa vile jamii inadhani wasanii wote wana silka na tabia kama za wauza sura hao wanaojirahisi na kujidhalilisha.
Kuhusu rushwa ya ngono, Sajuki mtoto wa nne kati ya watano wa Mzee Juma Issa Kilowoko, alisema wanaojihusisha nao wanafanya hivyo kwa kujitakia kwa sababu hakuna anayelazimishwa kutoa mwili wake iwapo ana uwezo na kipaji kikubwa katika sanaa hiyo.
"Rushwa ya ngono kwa watoto wakike ni kujitakia kwa vile wana akili na ufahamu wa kujua athari za kufanya hivyo na watayarishaji wanaolazimisha hawafai na wanapaswa kuchukuliwa hatua kali za kisheria," alisema Sajuki.
Sajuki, aliyelifafanua jina lake hilo kuwa ni muunganisho wa jina la kaka yake mkubwa Salum, lake la Juma na lile la ukoo wao la Kilowoko, alisema hakuna kitu kinachomtia simanzi na kumsikitisha kama tukio la ajali ya pikipiki iliyompata akiwa na mkewe, Wastara Juma enzi wakiwa wachumba.
Nyota huyo mwenye mtoto mmoja wa kiume na anayeishukuru famili yake na Vincent Kigosi 'Ray' kwa kumfikisha hapo alipo, alisema ajali hiyo sio inayomuuma, ila kitendo cha kulazimika kuidhinisha fomu hospitalini ili Wastara akatwe mguu wake uliokuwa umeharibika kwa ajali hiyo.
"Kwa kweli kile kitendo cha kuidhinisha kukatwa kwa mguu kwa Wastara kinaniuma hadi leo, lakini sikuwa na jinsi ila kufanya hivyo ili kumuokoa," alisema Sajuki.
Hata hivyo alisema anajisikia fahari mno kuuoana na kisura huyo ambaye kwa sasa anao mguu wa bandia, kwa vile wamesaidia kuanzisha kampuni yao binafsi ya Wajey Films Production.
Mkali huyo alizaliwa miaka zaidi ya 25 iliyopita huko Songea na kusoma hadi elimu ya sekondari katika shule za Songea na Luwiko, alikoanza kuonyesha kipaji chake cha sanaa katika matamasha mbalimbali ya shule kabla ya kujitosa kwenye makundi.
Kwa sasa, Sajuki anayeitaka filamu ya Mboni Yangu kama picha kali kuliko zote alizowahi kuigiza, yupo mbioni kuachia kazi zake mbili binafsi za Vita na Briefcase zilizowashiriki wakali kadhaa na matarajio yake ni kujiendeleza zaidi ili kuleta mapinduzi katika tasnia ya filamu nchini.
.
Mwisho

Bileku Mpasi: Dansa na Rapa wa Empire Bakuba anayekumbukwa * Alifunika na kumtia kiwewe Papy Tax, akamuibua Kokoriko Tz *
KWA wapenzi wa muziki wanaweza kukumbuka kuwa, bendi ya Empire Bakuba ilianzishwa na watu watatu, marehemu Joseph Kabasele Yampanya 'Pepe Kalle', Papy Tex na Dilu Dilumona miaka ya 1970.
Lakini pamoja na bendi hiyo kuasisiwa na watatu hao na baadae kupewa nguvu na Jojo Ikoma, ni vigumu kutaja mafanikio yake bila kumhusisha Djouna Mumbafu 'Bikelu Mpasi' a.k.a Big One.
Bileku aliyezaliwa na kupewa majina ya wazazi wake ya Bileku Jean-Pierre Matonet, aliweza kuifanya Bakuba ie juu kinoma.
Pamoja na ukweli kuwa alichukuliwa na Pepe Kalle kama dansa na rapu wa bendi hiyo, Bileku Mpasi aliweza kupanda haraka na kuwa maarufu pengine hata waasisi wenyewe.
Kupanda kwake kwa mafanikio kulitokana na umahiri wake wa kucheza, kurapu na baadae kuimba kiasi kwamba marehemu Pepe Kalle alifikiria kumpa nafasi ya hisa zake katika bendi hiyo.
Marehemu Pepe Kalle alitokea kumpenda na kumuamini Bileku Mpasi kama alivyofanya marehemu Franco kwa marehemu Madilu Systems enzi za uhai wao walipokuwa pamoja bendi ya T.P OK Jazz.
Jitu hilo la Miraba Minne hakumpenda bure kijana huyo, bali ni kutokana na ukweli alikuwa akijituma na kuifanya Empire Bakuba iliyoanzishwa kutokana na jina la moja ya makabila ya nchini Zaire (DR Congo ya sasa) kufunika kwa sana enzi za uhai wake.
Kasi yake ya kucheza na kurapu kwa wakati mmoja ndiyo kwa sasa imekuwa ikiigwa na marapa mbalimbali wa makundi ya muziki wa Lingala kuanzia DR Congo, Congo Brazaville hadi Bongo.
Enzi zake mkali huyo alikuwa akichuana na wakali kama Robert Ekokota Wenda wa Wenge Musica BCBG kabla ya kuibuka wengine kadhaa waliofuata nyayo zao.
Wapo wengine wanaodai kuwa Bileku Mpasi ndiye muasisi wa Ma-Atalaku walioibua nchini Congo na kufanya muziki wa Lingala ama Bolingo kuchangamka mno isivyo kawaida.
Ukali wake na ushirikiano aliokuwa nao na mbilikimo Emorro na baadae Djuma Fatembo na Jully Bebe, kulimfanya Bileku kuzidi kuwa juu na hasa kwa rafu zake matata katika albamu mbalimbali.
Ingawa hakuna taarifa kamili juu ya historia kamili ya mkali huyo ambaye kwa sasa ana kundi lake binafsi la Orchestra Big One, akitamba na albamu ya Tonnerre de Brest yenye kibao cha 6600 Volts, inadaiwa alizaliwa miaka zaidi ya 40 iliyopita.
Shughuli zake za muziki alizianza katika mji wa Kalemi kabla ya kuibukia Kishansa miaka ya mwishoni ya 1970.
Mwanzoni mwa miaka ya 1980 alikuwa akifanya shughuli zake katika bendi ndogondogo kama mnenguaji kabla ya kuchukuliwa na Pepe Kalle na kuwa dansa na rapa wao.
Hata hivyo kutokana na kuonyesha kipaji kikubwa katika uimbaji, Pepe Kalle akishirikiana na mtunzi mahiri wa Empire Bakuba enzi za uhai wake, Papy Tex walimpika kuwa muimbaji mkali.
Hata hivyo ukali wake na kuwafunika wawili kati ya waasisi wa kundi hilo, inaelezwa kuwa kulimsababishia rapa huyo 'kuunda' bifu kali na Papy Tex.
Ndio maana mara baada ya kifo cha marehemu Pepe Kalle Novemba mwaka 1998, kulitokea mtafaruku kama ule wa TP OK Jazz baada ya kifo cha Franco juu ya mustakabali wa bendi hiyo na Madilu.
Ilidaiwa kuwa wanamuziki waliosalia katika bendi hiyo walikuwa na nia ya kuiendeleza Empire Bakuba, ila waasisi na waliokuwa wamiliki wake, Dilumona na Papy walianzisha zengwe baada ya kufahamika Bileku amepewa usimamizi wa hisa za Pepe Kalle.
Yeye na Gode Lufombo waliamua kujiondoa na kuiacha Bakuba mikononi mwa mwenye nayo na kwenda kujiunga na kundi la Delta Force, ambalo lilikuwepo hata kabla ya kifo cha Pepe Kalle.
Delta Force alikaa nao kwa muda tngu mwaka 1999 hadi 2002 kabla ya kuamua kujiondoa na kuwa msanii wa kujitegemea na kufanikiwa kufyatua albamu yae ya kwanza ya Tonnerre de Brest.
Albamu hiyo ilikuwa na kibao matata cha 6600 Volts, ilitolewa mwaka 2004 na kumfikisha Bileku kwenye Fainali za Tuzo za Muziki za Afrika za Kora (Kora Music Award) za mwaka huo kupitia kibao hicho, ingawa hakufanikiwa kubeba tuzo yoyote.
Miongoni mwa vibao vya albamu hiyo iliyompa mafanikio makubwa kabla ya mkali huyo kujiundia Orchestra Big One inayotamba na albamu nyingine mpya ya mwaka jana ni pamoja na 100% TVA, 6600 Volts na Cupidon Brisé.
Vibao vingine ni pamoja na Fin Du Match, Karachiga, Nez a Nez, Mihona, Onze, Respect Pepe Kalle, Tatou na Tonnerre De Brest.
Bileku anayekumbukwa na Watanzania kwa kuchangia kuibua vipaji vya madansa wa Kitanzania kama akina Kokoriko aliyeshabihiana nae, Marehemu Maxi Prest, Mrisho Mpasi na wengine ndani ya bendi yake anaimba pamoja na mdogo wa marehemu Pepe Kalle.
Mdogo huyo wa marehemu Pepe Kalle, Ally Kale amefanana mno kisauti na marehemu kaka yake kiasi ukisikiliza nyimbo za kundi hilo unaweza kudhani 'Tembo wa Afrika' amefufuka.

Mr. Ebbo asita kuweka albamu sokoni
MSANII wa muziki wa kizazi kipya, 'Mr.Ebbo' amesema amesita kuingiza sokoni albamu yake mpya ambayo hajaipa jina kwa madai albamu ya sita bado inaendelea kufanya vema kwa sasa.
Mr. Ebbo ambaye jina lake halisi ni Abel Loshilaa Motika, aliambia Micharazo kwa njia ya simu toka Tanga kuwa albamu yake ya sita iitwayo 'Watoto Wangu' bado ina mashabiki wengi.
Alisema kuwa kutokana na hali hiyo, imeona ni vyema kuisitisha kwanza albamu ya saba ambayo nayo amesema nyimbo zake zimakamilika na zimesharekodiwa katika studio yake ya Motika Records.
"Nina albamu ya saba yenye nyimbo za Uzuri wa Kichina, Mama Rosa, Ninasaini, na Wazazi Wangu ambazo kwa kweli ni moto wa kuotea mbali, lakini siipeleki sokoni kwa sasa," alisema Mr. Ebbo.
Alisema kuwa nyimbo za albamu ya sita zinazoendelea kutesa sokoni ni 'Hajui Kupika', 'Kahamishwa', 'Kaka Hoza', 'Maisha Plastiki', 'Kunanuna', 'Mbado remix', 'Sikopi Tena', na 'Ulimi'.
Msanii huyo aliendelea kutaja nyimbo nyingine za albamu hiyo kuwa ni 'Bodaboda', 'Simu Feki', 'Tabia Mbaya' na 'Bado Naimba' ambazo alisema ameziachia nafasi ili ziendelee kumtangaza.
Mr. Ebbo aliyeibuka kwenye muziki wa kizazi kipya mwaka 2002, aliwahi kutamba na albamu yake ya kwanza ya 'Fahari Yako' na nyingine kama 'Bado Ijasungumiswa', 'Kazi Gani', 'Alibamu', 'Kamongo' na ndipo alipoachia hiyo ya 'Watoto Wangu' inayoendelea kutamba sokoni.