STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, February 4, 2014

Mwakilishi wa Kiembe Samaki alivyoapishwa rasmi

Katibu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Yahya Khamis Hamad, akisalimiana na Mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki Mhe. Mahmoud Thabit Kombo alipowasili katika Ofisi ya Katibu wa Baraza kwa ajili kujitambulisha na kuhudhuria kuapishwa kwake kuingia katika Baraza la Wawakilishi baada ya kushinda kiti hicho katika Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Kiembesamaki uliofanyika wiki iliopita.
 Mhe. Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Pandu Ameir Kificho akiingia katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi kwa ajili ya kuaza kwa taratibu za shughuli za Kikao na kumapisha Mwakilishi Mpya wa Jimbo la Kiembesamaki Zanzibar Mhe. Mahmoud Thabit Kombo. wakati wa Kikao cha asubuhi leo.
Mhe. Spika Pandu Ameir Kificho akisoma Dua kabla ya kuaza kwa Kikao cha Baraza cha Asubuhi leo.
Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Wanawake wakimshindikiza Mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki Mhe. Mahmoud Thabit Kombo akiingia katika ukumbi wa Mkutano tayari kwa kuapishwa kwake kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa Jimbo la Kiembesamaki Zanzibar baada ya kushinda nafasi hiyo katika uchaguzi mdogo uliofanyika mwishoni mwa wiki.
 Mhe Mhmoud Thaib Kombo, akiapishwa na Spika wa Baraza la Wawakilishi kuwa Mwakilishi wa Jimbola Kiembesamaki, baada ya kushinda Jimbo hilo na kuwa Mwakilishi Mpya kuchukua nafasi ya aliyekuwa mwakilishi wa jimbo hilo Mhe. Mansoor Yussuf Himid.   
  Mhe. Mahmoud Thabit Kombo akitia saini baada ya kuapishwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Jimbo la Kiembesaki Zanzibar kwa kupata ushindi katika uchaguzi mdogo uliofanyika wiki iliopita.
Mhe. Spika wa Baraza la Mapinduzi Pandu Ameir Kificho akimkabidhi Vitendea Kazi vya Baraza la Wawakilishi Mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki Zanzibar Mhe. Mahmoud Thabit Kombo.baada ya kuapishwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi.
 Waheshimiwa Wawakilishi wa Chama cha Mapinduzi wakimshangilia Mwakilishi wao wa Jimbo la Kiembesamaki wakati akiapishwa katika ukumbi wa Mkutanona Mhe. Spika wa Baraza la Wawakilishi Pandu Ameir Kificho leo asubuhi.
 Wanafamilia ya Mhe. Mahmoud Thabit Kombo wakihudhuria sherehe za kuapishwa kwake leo asubuhi katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Wageni walioongozana na Mhe. Mahmoud Thabit Kombo wakisimama wakati wa kusomwa kwa Dua kabla ya kuaza kwa shughuli za Kikao cha Baraza leo asubuhi.
Mhe. Mahmoud Thabi Kombo akiwashukuru wananchi wa jimbo la kiembesamaki kwa mashirikiano yao tangu mwazo wa kampeni hadi kupiga kura na kumchagua kuwa mwakilishi wao.Picha Zote na Ramadhan Othman Mapara-Zanzibar

Mzee Kingunge aibuka, ashangaa wanamuandama Lowassa, ashtushwa Mawaziri kuitwa Mizigo

Mzee Kingunge Ngombale Mwiru akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na MICHARAZO nyumbani kwake jana jijini Dar es salaam.
WAKATI makada wa CCM wakilumbana juu ya kitendo cha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kujitokeza hadharani na kuonyesha nia ya kuwania Urais Uchaguzi wa 2015, mwanasiasa mkongwe Kingunge Ngombare Mwiru ameibuka na kusema haoni tatizo na kilichofanya na Mbunge huyo wa Monduli.
Aidha Kingunge amesema amesikitishwa na kitendo kilichofanywa na baadhi ya viongozi wakuu wa CCM kuwaumbua na kuwadhalilisha baadhi ya mawaziri wa serikali yao kwa kuwaita 'mizigo', akidai kama walikuwa na makosa katika utendaji wao walipaswa kukosolewa ndani ya vikao vya ndani vya chama chao badala ya kuvuana nguo hadharani na kukiaibisha chama.
Kwa wiki sasa kumekuwa na malumbano baina ya wanaCCM wakimnyooshea kidole Lowassa anayedaiwa kuanza kufanya kampeni zinazohisiwa ni harakati zake za kuwania urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwakani.
Miongoni mwa waliomshambulia Lowassa ni Katibu wa Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi-UVCCM, Paul Makonda na Waziri Mkuu Mstaafu, John Malecela.
Viongozi hao wameonyeshwa kukerwa na kitendo kinachofanywa na Lowassa kwa kudai anausaka urais kwa kutumia fedha na kutaka chama kimdhibiti, huku Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula naye akigusia suala hilo na kuwaonya wanachama walioanza kampeni kabla ya wakati.
Hata hivyo Kingunge, akizungumza na MICHARAZO jana nyumbani kwake jijini Dar es Salaam, alisema haoni tatizo kwa Lowassa na hata mwanachama yeyote ndani ya CCM kujitokeza na kuonyesha dhamira ya kutaka uongozi mapema.
Kingunge alisema kujitokeza mapema kwa mtu mwingine yeyote mwenye dhamira ya kutaka uongozi ni jambo litakalowasaidia wananchi kuwafahamu, kuwajadili na kuwapima kwa kina kuona kama wanafaa kuongoza au la.
Alisema  haoni sababu ya kuibuka malumbano baina ya wanaCCM au kusakamwa kwa Lowassa kwa kitendo chake akidai wengine wanaotaka kufanya hivyo wafanye ili kutoa nafasi kwa wanachama wenzao na wananchi kwa ujumla kuwafahamu na kuwajadili ili ukifika wa uchaguzi wajue la kufanya dhidi yao.
"Sipendi kuingia kwenye malumbano na wanachama wenzangu kwa sababu najua mwishowe watu tunaweza kuvuana nguo, ila kwa mtazamo wangu sioni kama ni kosa kwa wanachama na raia yeyote mwenye nia ya kutaka uongozi kujitokeza na kujionyesha mapema," alisema.
"Kujitokeza kwao mapema kutawafanya wananchi wawaone, wawafahamu, pia wawapime na kuwajadili kwa kina kama wanafaa kubeba majukumu ya uongozi au la, pia sidhani kama ni Lowassa pekee aliyefanya hivyo, vipi asakamwe yeye tu! Siyo dhambi watu wenye nia iwe katika ubunge, udiwani, uenyekiti wa serikali za mitaa na hata urais kuwangong'oneza rafiki na ndugu zao juu ya dhamira yao. Bora hao kuliko wanaofanya mambo yao kwa usiri," alisema.
Mwanasiasa huyo aliyewahi kwa waziri katika serikali za awamu zote nne nchini tangu enzi za Mwalimu Nyerere, alisema tangu enzi za TANU mpaka kuzaliwa kwa CCM upo msisitizo unaosema raia wote wana haki mbili kuu ya kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa, ingawa hawalazimishwi.
"Hakuna anayelazimishwa kuchagua au kuchaguliwa kwa maana ya kuwania uongozi, hivyo kujitokeza kwa wanasiasa na watu wengine kuonyesha nia yao yakutaka uongozi hawafanyi dhambi, hivyo sidhani kuna haja ya suala hili kuwa mjadala mkubwa wakati kuna mambo ya msingi ambayo CCM inapaswa kuyazungumza na kuyajadili kwa kina kwa manufaa ya wananchi," alisema.
Juu ya kitendo cha viongozi wakuu wa Sekretarieti ya CCM kufanya ziara mikoani kisha kutangaza majukwaani majina ya mawaziri walioitwa mizigo, Kingunge kwanza alipongeza ziara hiyo akidai itasaidia kukijenga na kuinua uhai wa CCM, lakini alidai hakubaliani na kilichofanywa na viongozi wao kuwavua nguo watendaji hao wa serikali yao.
Alihoji ina maana viongozi wa CCM hawajui mipaka ya uongozi iliyopo baina yao na serikali iliyopatikana kwa ridhaa ya wananchi.
"Zipo taratibu za kukosoana ndani ya chama, mawaziri ni wabunge, wanaCCM kama wamefanya makosa ilipaswa waitwe na kukosolewa katika vikao vya ndani ya chama badala ya kuwavua nguo hadharani kwa kisingizio wananachi ndiyo wanaowalalamikia. Haya hatukuwatuma," alisema.
alisema yapo mambo ya msingi viongozi wa CCM wanapaswa kuyazungumza na kuyajadili mbele ya wananchi ikiwemo mikakati ya kuwaletea maendeleo ili wafurahie uhuru, pia akidai kwa miaka mingi tangu enzi za TANU, CCM kilifahamika kuwa ni chama cha wanyonge, lakini kwa sasa hilo halipo na kuhoji viongozi hao wanapaswa kuliangalia hilo na kukirejesha chama katika mstari.
"Kama wameshindwa kazi ni vyema wakawapisha wengine wakiongoze, kuliko kukiyumbisha chama na kukifanya kipoteze mvuto mbele ya wananchi kwa kujadili mambo yasiyo na maana kwa wananchi hata kama wanapigiwa makofi, CCM ina sera na taratibu zake za kukosoana kupitia vikaoni, siyo kilichofanywa na viongozi wetu," alisema.
Alisema viongozi wa CCM kwa sasa ni kama wanaoanzisha vita baina yao na watendaji wa serikali kitu ambacho siyo tu kinaonyesha chama chao kuyumba, pia kinaonyesha namna gani wanavyofanya kazi ya kuwasaidia wapinzani badala ya kujijenga na kusaidia serikali yao ili waje kushinda katika chaguzi zijazo.
Kingunge alihoji viongozi waliowaita wanachama wenzao 'mizigo' ndani ya serikali  inayotokana na CCM wanatazamanaje na mawaziri hao kuliorejeshwa.
"Sidhani kama ni jambo zuri, watu waheshimu mipaka ya madaraka yao, wajikite katika kukijenga chama na serikali kwa ujumla badala ya vitu visivyo na tija kwa wananchi iliwayowapa ridhaa ya kuongoza," alisema Kingunge.

Makocha 40 waula TFF, kusaka vipaji Bara na Zenji

 
Fred Minziro mmoja wa makocha walioteuliwa na TFF
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limeteua kikosi cha makocha 40 kutoka sehemu mbalimbali, Tanzania Bara na Zanzibar ili kung’amua vipaji katika mpango wa kuboresha timu ya Taifa (Taifa Stars).

Makocha hao ambao watafanya kazi hiyo katika michuano maalumu ya mikoa wanatakiwa kuripoti katika ofisi za TFF siku ya Jumamosi (Februari 8 mwaka huu) saa 4 asubuhi kwa ajili ya kupewa maelekezo zaidi.

Walioteuliwa ni Abdallah Hussein (Kilimanjaro), Abdul Mingange (Dar es Salaam), Ali Bushiri (Zanzibar), Ali Mayay (Dar es Salaam), Ally Mtumwa (Arusha), Ayoub Selemani (Zanzibar), Boniface Pawasa (Dar es Salaam), Dan Korosso (Mbeya), Dk. Mshindo Msolla (Dar es Salaam) na Edward Hiza (Morogoro).

Elly Mzozo (Dar es Salaam), Fred Minziro (Dar es Salaam), George Komba (Dodoma), Hafidh Badru (Zanzibar), Hamimu Mawazo (Mtwara), Idd Simba (Mwanza), Jabir Seleman (Zanzibar), John Tegete (Mwanza), Juma Mgunda (Tanga) na Kanali mstaafu Idd Kipingu (Dar es Salaam).

Kenny Mwaisabula (Dar es Salaam), Khalid Abeid (Dar es Salaam), Madaraka Bendera (Arusha), Madaraka Selemani (Dar es Salaam), Mbarouk Nyenga (Pwani), Mohamed Mwameja (Dar es Salaam), Musa Kissoki (Dar es Salaam), Nicholas Mihayo (Dar es Salaam), Patrick Rweyemamu (Dar es Salaam) na Peter Magomba (Singida).

Peter Mhina (Songea), Salvatory Edward (Dar es Salaam), Salum Mayanga (Morogoro), Sebastian Nkoma (Dar es Salaam), Sekilojo Chambua (Dar es Salaam), Shaban Ramadhan (Zanzibar), Steven Nemes (Dar es Salaam), Sunday Manara (Dar es Salaam), Tiborowa Jonas (Dar es Salaam), Yusuf Macho (Dar es Salaam), Zamoyoni Mogela (Dar es Salaam).

Kivumbi cha Ligi Kuu kuendelea kesho, tiketi za Elekroniki zasitishwa kisa...!

LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, inaingia raundi ya 16 kesho (Februari 5 mwaka huu) kwa mechi tano huku Mtibwa Sugar ikiikaribisha Simba kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Kiingilio katika mechi hiyo ambayo itakuwa ya kwanza kuchezwa kwenye uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 10,000 tangu uanze mzunguko wa pili wa VPL kitakuwa sh. 5,000. Jonisia Rukyaa kutoka Bukoba ndiye atakayechezesha mechi hiyo.

Mechi nyingine za ligi hiyo ni Tanzania Prisons vs Coastal Union (Sokoine, Mbeya), Mgambo Shooting vs Ruvu Shooting (Mkwakwani, Tanga), Rhino Rangers vs Oljoro JKT (Ali Hassan Mwinyi, Tabora) na JKT Ruvu vs Ashanti United (Chamazi, Dar es Salaam).
Wakati huo huo: Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limesitisha matumizi ya tiketi za elektroniki kwenye viwanja vyote vyenye huduma hiyo ili kutoa fursa ya kufanyika tathmini ya kina kabla ya kuendelea tena.
Uamuzi huo umefikiwa kwa kuzingatia sababu mbalimbali baada ya kikao kati ya Sekretarieti ya TFF na maofisa wa benki ya CRDB kilichofanyika jana (Februari 3 mwaka huu) katika ofisi za Shirikisho.
Tathmini hiyo inafanyika ili kubaini changamoto zilizojitokeza na kuzitafutia ufumbuzi kabla ya kuendelea tena na matumizi hayo, kubwa ikiwa ni hadhari iliyotolewa na vyombo vya Usalama juu ya misongamano inayotokea uwanjani kutokana na kutokuwepo mtiririko mzuri wa uingiaji.
Tayari zipo changamoto za wazi ikiwemo uelewa wa washabiki wa jinsi ya kununua na kutumia tiketi hizo, milango michache ya kuingilia uwanjani na washabiki wengi kununua tiketi dakika za mwisho hivyo kuchangia misongamano.

Raia 12 wa kigeni wanaswa na dawa za kulevya


WATU 12, wanaodaiwa kuwa ni raia wa nchi za Iran na Pakistan wamekamatwa na shehena kubwa la madawa ya kulevya katika Bahari ya Hindi wakiwa wanaelekea Zanzibar kwa jahazi. 

Haikufahamika shehena waliyonaswa nayo ni dawa za aina gani na wala uzito wake.
Chanzo: RADIO ONE STEREO

ZITTO KABWE AMFUNIKA FREEMAN MBOWE KWA UMAARUFU TZ

Zitto Zuberi Kabwe
Mbunge huyu wa Kigoma Kaskazini Chadema ndiye alifungua milango kwa vijana wengi kujiingiza katika siasa mwaka 2005. Umahiri wake katika kujenga hoja zinazotikisa nchi, zilimpatia umaarufu mkubwa ndani na nje ya chama chake.

Anachukuliwa kama kijana aliyewapa wenzake uwezo wa kujiamini. Pamoja na misukosuko ya kisiasa inayomkabili lakibi bado ameng’ara kwa kuchaguliwa na watu 65,809, sawa na aslimia 15.
Kwa muda wa miezi miwili , magazeti ya Global Publishers Ltd yaliendesha zoezi la kuwashirikisha wasomaji wake juu ya mtu gani mwenye nguvu zaidi ya ushawishi katika jamii ya Watanzania.
Na kuwazidi umaafuru viongozi wa juu wa chama cha Demokrasi na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe na Dk Slaa. 

Rais Jakaya Kikwete.
Jumla ya Watanzania 438,726 walipiga kura kupendekeza majina mbalimbali. Watu 10 waling’ara zaidi kwa kugawana jumla ya kura asilimia 97.4, huku wengine ambao hawakuweza kuchomoza wakiambulia mgawo wa asilimia 2.6.
Katika hao 10 waliong’ara zaidi, mtiririko kulingana na wingi wa kura unagawanywa kama ifuatavyo.


Dk. Jakaya Mrisho Kikwete
RAIS Jakaya Mrisho Kikwete anashika nafasi ya kwanza. Kwa nafasi yake kama mkuu wa nchi, Amiri Jeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi na usalama, Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri na Mwenyekiti wa Chama Tawala CCM, ndiye aliyeongoza kwa kupata kura nyingi kwamba ana ushawishi mkubwa katika makundi yote. Watu 118,456 ambao ni sawa na asilimia 27 walimchagua.
Edward Ngoyai Lowassa
WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Ngoyai Lowassa anashika nafasi ya pili kwa nguvu ya ushawishi katika Tanzania. Ingawa hayumo kwenye Baraza la Mawaziri, ameonesha anakubalika sana kijamii kwa kuchaguliwa na watu 83,358 ambao ni sawa na asilimia 19.
Reginald Abraham Mengi
NI mfanyabiashara mkubwa mzawa, maarufu pengine kuliko wote Tanzania. Ndiye mtu anayemiliki vyombo vingi vya habari, vikiwemo televisheni, redio na magazeti. Ni mmoja wa matajiri wachache wenye utamaduni wa kuwasaidia wasiojiweza. Kutokana na mchango wake kijamii, naye ameng’ara. Watu 43,873 ambao ni sawa na asilimia 10 walimchagua.
Kadinali Polycarp Pengo
MUADHAMA Polycarp Kardinali Pengo ni kiongozi wa madhehebu ya Kikatoliki anayeheshimika katika jamii ya Kitanzania. Ni mtu makini na anayehubiri amani na upendo muda wote. Taswira yake kwenye jamii imemuwezesha kuchaguliwa na watu 35,098 (asilimia 8).
Dk. Willibroad Peter Slaa
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Alijipatia umaarufu mkubwa wakati alipokuwa mbunge wa kuchaguliwa Jimbo la Karatu. Uwezo wake wa kujenga hoja na kuitetea, msimamo mkali dhidi ya rasilimali za taifa kulimfanya kupendwa na wengi.

Jambo hili lilimfanya kuwa mpinzani mkubwa wa CCM wakati wa uchaguzi mkuu uliopita, ingawa baadaye alishindwa na Rais Kikwete. Mvuto wake kwa wananchi, ulichangia pia kuongezeka kwa idadi ya wabunge wa chama chake, kutoka 11 mwaka 2005 hadi 48. Watu 26,324 (6%) wamempigia kura.
Said Salim Bakhressa
MFANYABIASHARA maarufu nchini na mmoja wa watu wanaotajwa kuwa na fedha nyingi zaidi Tanzania. Anamiliki viwanda vya kutengeneza unga, juisi, matunda, biskuti, soda na koni. Pia ndiye msambazaji mkubwa wa unga kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Bakhressa ambaye ni Mzanzibari, pia anamiliki timu ya mpira wa miguu ya Azam FC ambayo ni ya kwanza nchini kuwa na uwanja wake wa kisasa. Ndiye mmiliki wa kituo cha televisheni cha Azam TV, vilevile ana vyombo vya usafiri wa majini. Watu 21,936 (5%) wamemchagua.
 
John Pombe Magufuri
MMOJA wa mawaziri wenye historia nzuri ya uchapa kazi kiasi cha kusifiwa sana na wananchi. Tokea alipoibuliwa kwa mara ya kwanza na kuwa waziri wakati wa utawala wa Awamu ya Tatu, kasi yake imezidi kung’aa na kumfanya kuwa kipenzi cha wananchi. Katika orodha hii amechaguliwa na watu 17,549 (4%).
 
Dk. Harrison George Mwakyembe
Makali yake yalidhihirika zaidi alipoongoza Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza kuhusu uwepo wa ufisadi katika kampuni ya kufua umeme ya Richmond mwaka 2007-2008, kazi ambayo ilimalizika kwa aliyekuwa Waziri Mkuu wakati huo, Edward Lowassa kuachia ngazi pamoja na Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi, waliokuwa mawaziri wakati huo.

Kazi yake nzuri akiwa mbunge, baadaye kuwa naibu waziri wa Uchukuzi na hata baada ya kuwa waziri kamili, imemfanya achaguliwe na watu 8,775 (2%) kuwa mmoja wale 10 wenye ushawishi.
 
Issa Ponda     
Ni Katibu wa Jumuiya za Kiislam Tanzania. Amekuwa akiendesha harakati nyingi kudai haki za Waislam, hivyo kumfanya awe akilumbana na serikali mara kwa mara.

Anachokifanya kinabeba maana kubwa kwa watu, ndiyo maana amechaguliwa kwa kura 6,142 (1.4%), hivyo kufunga orodha ya wale 10 wenye mvuto zaidi Tanzania kwa mwaka 2013-201.

Credit:

TAARIFA KUTOKA TFF

TFF YAADHIMISHA MIAKA 50 FIFA


SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) litaadhimisha miaka 50 tangu lipate uanachama wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (TFF) kwa shughuli mbalimbili ikiwemo michezo na makongamano. Kamati maalumu itaundwa kwa ajili ya kupanga na kuratibu shughuli hiyo ambayo TFF imepanga kuadhimisha nchini nzima kwa kutumia wanachama wake. 


TFF wakati huo ikiitwa Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (FAT) ilijiunga na FIFA Oktoba 8, 1964.
MSHABIKI mmoja anashikiliwa na Jeshi la Polisi akidaiwa kukutwa na tiketi bandia kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya Yanga na Mbeya City iliyochezwa jana (Februari 2 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Matei Cosmas (28) ambaye ni mkazi wa Buza Njiapanda Kitunda, Dar es Salaam amefunguliwa jalada namba CHA/IR/900/2014 kwenye Kituo cha Polisi Chang’ombe akidaiwa kupatikana na tiketi bandia. Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) leo asubuhi (Februari 3 mwaka huu) limeamkia Kituo cha Polisi Chang’ombe kusaini hati ya maelezo dhidi ya mtuhumiwa. 


Na tff ianaimani kuwa mtuhumiwa atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria za nchini. 


Witoumetolewa  kwa washabiki wa mpira wa miguu kuepuka kununua tiketi kutoka mikononi mwa watu, kwani kufanya hivyo ni kosa.

RAIS WA TFF ATEMBELEA RUANGWA
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ametembelea Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi. Katika ziara hiyo aliyoifanya jana (Februari 2 mwaka huu), pia alikuwa mgeni rasmi mechi ya kugombea Kombe la Majaliwa kati ya Hull City na Mbagala City, na kuahidi kuwa TFF itaandaa kozi za awali za ukocha na uamuzi kwa Wilaya ya Ruangwa.


TFF YAPATA HATI YA KIWANJA TANGA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepata hati ya kiwanja chake kilichopo eneo la Mnyanjani katika Jiji la Tanga. Hati hiyo ya miaka 99 ya kiwanja hicho namba 75 Block D chenye ukubwa wa ekari 7.6 ilikabidhiwa kwa TFF, Januari 13 mwaka huu. Kiwanja hicho kitaendelezwa kwa matumizi mbalimbali, kubwa ikiwa ni uwanja wa mpira wa miguu.
RAMBIRAMBI MSIBA WA OMARI CHANGA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha aliyekuwa mchezaji wa Vijana, Moro United na Yanga, Omari Changa kilichotokea juzi (Februari 1 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.
Msiba huo ni mkubwa katika familia ya mpira wa miguu kwani Changa wakati wake uwanjani akichezea timu mbalimbali alitoa mchango mkubwa ambao tutaukumbuka daima.
TFF tunatoa pole kwa familia ya marehemu Changa, klabu ya Moro United na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Katika maziko TFF itawakilishwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Kidao Wilfred, na imetoa rambirambi ya sh. 200,000.

Chelsea yaipa nafuu Arsenal, yaitungua Man City kwao

BAO pekee lililofungwa dakika ya 32 na Ivanovic usiku wa jana limeisaidia Chelsea kuibuka na ushindi ugenini mbele ya Manchester City na kuipa nafuu Arsenal waliopo kileleni.
Man City ambayo ipo kwenye kiwango cha hali ya juu na iliyokuwa ikigawa dozi nene kwa wapinzani wao, ilishindwa kuamini kama imelala kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Etihad baada ya pambano hilo kumalizika.
Hata hivyo katika mchezo wa jana ilidhibitiwa na vijana wa Jose Mourinho na kuambulia kipigo cha kwanza baada ya mechi  20 mfululizo bila kupoteza na cha kwanza tangu walipofungwa Novemba mwaka jana na Sunderland.
Kwa ushindi huo wa jana Chelsea wamefikisha pointi 53 sawa na Man City na kutofautishwa na uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Kileleni ameendelea kusalia Arsenal ambayo ni wazi jana ilikuwa ikiangusha dua mbaya kwa City ili wasishindi mchezo huo na kuwatoa kwenye uongozi, dua lililojibu kwa Chelsea kuwaziba mdomo vijana wa Etihad.