STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, May 10, 2013

WAHANGA WA MLIPUKO WA BOMU WAZIKWA KWA HUZUNI KUBWA


Misa ya Mazishi ya wahanga wa mlipuko wa bomu la Jumapili iliyopita kwenye parokia teule ya Olasiti ilianza katika eneo lile lile mlipuko ulipotokea.

Misa  hiyo  iliongozwa na Muadhama Polycarp Kardinal Pengo, Askofu Mkuu wa Dar es Salaam.


Maandamano yalianzia toka chumba cha kuhifadhia maiti, miili ikapelekwa makao makuu ya Asofu Mkuu, Burka  na  baadaye  ikawasilishwa kanisani
.....

Mahubiri ya Kardinali Pengo

Ndugu zangu,


Nafasi hii inaunganisha mawazo ya furaha na uchungu kutokana na kilichotukutanisha leo.

Mazingira haya yanaweka ugumu wa kupata cha kusema. Ila sisi ni watu wa imani. napenda kueleza imani yetu kama tunavyopaswa kuwa kwenye mazingira haya.

Tumejumuika ili kuwaweka kwenye nyumba ya milele hawa marehemu, lakini pia tunatumia nafasi hii kubariki Kanisa.

Kila mbatizwa ni kiungo cha mwili wa Kanisa. Kila kiungo cha mwili kinapaswa kuungana na kichwa cha Mwili ambae ni Yesu Mwenyewe

Kristo akipitia kwa mdomo wa mtume Paulo anatufundisha kuwa "Msijaribu kushindana na uovu kwa uovu, lakini shindeni uovu kwa wema".

Katika viongozi waanzilishi wa dini, ni Yesu peke yake aliyetolea uhai wake kujenga imani ya wafuasi wake. Viongozi wengine hawajikutoa sadaka wenyewe, na baadhi wametoa sadaka ya maisha ya watu wengine kwa ajili ya kueneza imani yao.

Sisi Wakristu
Imani yetu inajengwa juu ya mwanzilishi wetu ambaye alitoa uhai wake ili kujenga imani yetu, na hakutoa uhai wa mtu yeyote kwa ajili ya kujenga imani yetu.

Katika masomo tuliyosikia leo, Somo la plili limetupa neno la Mtume Paulo Rum:12:17 linasisitiza hilo: usishinde uovu kwa uovu, bali shinda uovu kwa wema.

Soma la Kwanza limeeleza kuwa Paulo na Sila wanateswa kwa ubaya mkubwa sana na kuwekwa gerezani kwa ubaya. Na baada ya kufunguliwa kwa muujiza, askari wa magereza alitaka kujiua, lakini Paulo na Sila wakatenda lililo jema kuokoa maisha yake. Ni baada ya wema huo wokovu ulifika kwa askari huyo na jamaa yake yote wakaweza kumwamini Mungu.

Nawauliza waumini: "
Wale waliotekeleza ubaya huu, akija mbele yetu akasema ni mimi ndiye, tungefanya nini kama waumini kwa kufuata mfano wa Yesu?"

Mimi nawaambia
"Tujifunze kutoka kwa Bwana wetu Yesu Kristo: 'Tusidiriki kulipia uovu kwa uovu, lakini tutende mema ili kushinda uovu'."

Lakini haya hayaondoi majukumu ya serikali, ambayo yanabaki, na si mimi ninayepaswa kuyasema, wenye mamlaka wanayajua majukumu yao. Mimi nawaambia ninyi waumini.

Uovu si kitu kinachopendeza. Warumi waliwatesa wakristo kwa karne tatu, na haikusaidia chochote Himaya ya Warumi, ambayo baadaye ilisambaratika. Lakini imani yetu imebaki.

Amemalizia kwa kusema:
Tukio hili na tukio la mauaji ya Padre Mushi, isiwe sababu ya kuacha amani ya nchi yetu isambaratike.

Lakini ni jukumu la wananchi wotte kuhakikisha nchi yetu haisambaratiki.

Wenye mamlaka watimize wajibu wao. Sisi wakristo tusamehe, tusijibu uovu, tudumishe amani na upendo katika taifa letu.

Tumsifu Yesu Kristu.

credit: jamiiforum

Wadhamini watangaza zawadi za Ligi Kuu 2012-2013



Meneja Uhusiano wa Mambo ya Nje wa Vodacom, Salum Mwalim (katikati) akizungumza katika mkutana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuhusu zawadi mbalimbali za Ligi Kuu ya Tanzania Bara. Kushoto ni Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura na kulia ni Meneja Mahusiano wa Vodacom, Matina Nkurlu.

WADHAMINI wa Ligi Kuu ya soka Tanzana Bara, Kampuni ya Vodacom imetangaza kutumia kiasi cha Sh. milioni 200 kwa ajili ya kutoa zawadi ya fedha taslimu katika ligi inayomalizika Mei 18 ambapo sasa mabingwa wa msimu huu, Yanga, watajinyakulia Sh. milioni 70, huku zawadi ya mfungaji bora inayotarajiwa kutua kwa Kipre Tcheche wa Azam ni Sh. milioni 5.

Mbali ya bingwa, Vodacom pia itatoa fedha kwa timu inayomaliza nafasi ya pili, ya tatu na  ya nne katika msimamo wa ligi ambazo ni Sh. milioni 35, Sh. milioni 25 na Sh. milioni 20 zote zikiwa na ongezeko ikilinganishwa na zawadi za fedha zilizotolewa katika msimu wa 2012 / 2013.

Zawadi hizo zimetangazwa kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kampuni hiyo kupitia Meneja Uhusiano wa Mambo ya Nje wa Vodacom, Salum Mwalim, ikiwa ni pamoja na kuainisha zawadi za washindi wa mchezaji mmoja mmoja pamoja na timu iliyoonyesha nidhamu kwa msimu huu.

"Mwaka huu tutatumia kiasi cha Sh. milioni 200 kwa ajili ya zawadi za fedha taslimu kwa washindi wa Ligi Kuu ya Vodacom huku bingwa akinyakua kitita cha Sh. milioni 70 ikilinganishwa na Sh. milioni 50 za msimu uliopita," alisema Mwalim.

Mwalimu amesema lengo la kuongeza zawadi ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya wadhamini wa ligi na wadau wengine wa soka na kwa pamoja kuwa na dhamira ya dhati katika kuendeleza soka nchini.

"Kila mmoja ni shahidi wa namna ambavyo soka letu limekua na namna ambavyo tunakabiliana hatua kwa hatua na changamoto zinazohusiana na ligi. Ni matumaini yetu kwamba tunapiga hatua na tuna matumaini ya kufikia kiwango cha juu zaidi cha maendeleo ya soka nchini yanaonekana," aliongeza Mwalim.

"Kwetu sisi kama wadhamini tutajitahidi kadri inavyowezekana kuhakiksha tunaleta mabadiliko katika soka la Tanzania, tunaangalia mpira wa miguu nchini kwa upana zaidi kama mchezo unaopendwa, unaotuleta pamoja kama taifa na kuitangaza nchi yetu. Falsafa yetu hii imechangia kwa kiasi kikubwa kuwapo kwa utulivu na ushirikiano mzuri miongoni mwa wadau na hivyo kutuletea mafanikio," alisema Mwalim.

Zawadi nyingine zilizotangazwa ni pamoja na zawadi ya Mchezaji Bora wa Mwaka, Kipa Bora na Mfugaji Bora, ambao kila mmoja  atajinyakulia Sh. milioni 5.

Mwamuzi Bora na Kocha Bora kila mmoja atajipatia Sh. milioni 7.5 wakati timu yenye nidhamu itazawadiwa fedha taslimu ya Sh. milioni 15.

"Tumekuwa na msimu mzuri uliojaa ushindani na hamasa, tunatarajia timu zitajipanga zaidi kwa ajili ya msimu ujao na hivyo kuendelea kuipa ubora ligi yetu," alisema Mwalim huku akiwashukuru wadau wa mpira wa miguu nchini ikiwamo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Bodi ya Ligi,  Kamati ya Ligi Kuu, Chama cha Waamuzi (FRAT), klabu shiriki, wachezaji na kipekee mashabiki.

Alisema bila ya ushirikiano wa wadau hao na wengine ikiwamo Serikali, ligi kuu ya Vodacom isingeweza kufikia maendeleo iliyoyafikia katika msimu unaomalizika ambao kwa kiasi kikubwa ulitawaliwa na mpira wa uwanjani na si vinginevyo
.

TFF lamchimba mkwara Shafii Dauda kisa barua ya FIFA

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgIcvtnmCBqRdmOdMhm1xSloe3lPbWzAf6TIuVarRn2iaYfjrLKFDRXaTZ6FP45x6Txkaxu0GTMf-wMLHf1HSRVsPASI__RtseGcbTrbiQW3z11FugVysqBPtfeQt7wvRCaNWIy1qsSQ6I/s1600/shafi+dauda.JPG
Shafii Dauda akiwa kwenye majukumu yake ya kuwapa wadau wa michezo taarifa kupitia tovuti yake ya www.shafiidauda.com


Na Boniface Wambura
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limemtaka Shaffih Dauda ambaye ni mmiliki wa tovuti ya www.shaffihdauda.com kutoa maelezo kuhusiana na barua ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) aliyoiweka kwenye mtandao wake huo.

FIFA ambayo ilisimamisha mchakato wa uchaguzi wa TFF baada ya baadhi ya wagombea kuulalamikia, baadaye ilitoa maelekezo kuhusu mchakato huo kwa barua ambayo iliituma kwa Rais wa TFF, Leodegar Lenga.

Rais wa TFF katika mkutano wake na waandishi wa habari ambao Dauda alihudhuria alibainisha kuwa barua hiyo ya FIFA hawezi kupewa kila mtu, na kuruhusu waandishi kuisoma kwa Ofisa Habari wa TFF bila kuondoka nayo.

Wakati Rais Tenga anazungumza na waandishi wa habari (Mei 2 mwaka huu), nakala ya barua hiyo ya FIFA ilikuwa kwa viongozi wakuu wa TFF pekee, na viongozi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo. Hivyo TFF imemtaka Dauda kutoa maelezo ya mahali alipoipata barua hiyo ndani ya siku saba.

Vita tupu Dar, Kagera katika Ligi Kuu kesho


Kagera Sugar Fc
Azam Fc
Mgambo JKT

Ruvu Shooting Stars
Na Boniface Wambura
Kagera Sugar inaikaribisha Ruvu Shooting ya Pwani katika mchezo pekee wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) utakaofanyika kesho (Mei 11 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kaitba mjini Bukoba.

Ingawa timu zote mbili hazipambani kutafuta ubingwa ambao tayari umetwaliwa na Yanga wala kukwepa kushuka daraja, mechi hiyo bado ni muhimu kwao katika mazingira matatu tofauti.

Kagera Sugar inayonolewa na kocha mkongwe kuliko wote katika VPL, Abdallah Kibaden na ikiwa na pointi 40 yenyewe inasaka moja kati ya nafasi nne za juu ambazo zina zawadi kutoka mdhamini wa ligi, lakini pia timu zinazoshika nafasi hizo za juu zinapata tiketi ya kucheza michuano ya BancABC Super 8.

Kwa upande wa Ruvu Shooting ya Kocha Charles Boniface Mkwasa yenye pointi 31 inasaka moja ya nafasi sita za juu ambazo ni fursa ya kuingia kwenye Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPL Board) ambayo inatarajiwa kuundwa baada ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Septemba 28 mwaka huu.

Wagombea nafasi za uenyekiti na makamu wake ni lazima watoke katika timu zilizoshika nafasi sita la juu katika VPL msimu uliopita. Uchaguzi wa TPL Board utafanyika siku moja kabla ya ule wa TFF uliopangwa kufanyika Septemba 29 mwaka huu.

Raundi ya 25 ya ligi hiyo itakamilika keshokutwa (Mei 12 mwaka huu) kwa mechi kati ya wenyeji Azam na Mgambo Shooting ya Tanga. Mechi hiyo namba 169 itachezwa katika Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Azam yenye pointi 48 inahitaji moja zaidi ili kutetea nafasi yake ya umakamu bingwa iliyoutwaa msimu wa 2011/2013 na kupata tiketi ya kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Wakati Azam ikisaka pointi hiyo moja, Mgambo Shooting inayofundishwa na wachezaji wa zamani wa mabingwa wa Tanzania Bara mwaka 1988, Mohamed Kampira akisaidiwa na Joseph Lazaro ni moja ya timu ziko katika hatari ya kurudi Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao.

Mgambo Shooting inahitaji pointi moja tu katika mechi mbili ilizobakiza kukwepa kurudi FDL, ikishindwa kupata pointi hiyo huku Polisi Morogoro na Toto Africans ya Mwanza zikishinda mechi zao za mwisho kwa uwiano mzuri wa mabao itakuwa imekwenda na maji.

Mechi ya Azam dhidi ya Mgambo Shooting itachezeshwa na refa Jacob Adongo kutoka Mara, na atasaidiwa na Abdallah Rashid wa Pwani na Charles Mbilinyi wa Mwanza. Mwamuzi wa mezani atakuwa Idd Lila wa Dar es Salaam wakati Kamishna ni Omari Walii wa Arusha.

Simba, Mgambo mapato kiduchu!


Na Boniface Wambura
Mechi namba 149 ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Simba na Mgambo Shooting iliyochezwa juzi (Mei 8 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa Simba kushinda bao 1-0 imeingiza sh. 16,651,000.

Watazamaji 3,006 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo ambayo viingilio vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 3,226,125 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 2,539,983.05.

Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 1,640,402.54, tiketi sh. 3,175,000, gharama za mechi sh. 984,241.53, Kamati ya Ligi sh. 984,241.53, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 492,120.76 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 382,760.60.

Kampira aionya Yanga kwa 'madogo' wa Simba

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgCwx6t_dBA2gr_eCQrTlNALtGAg97uXPt-4TMECmVo7k-QvGveoqvCHiMUxPf8_wW-xczLaqmoUf6Corg3SPn9CIIVhdY9DKMTQQ-KgAgTcrDLJog0Y3hySeSa7bSHScyXJ0uCK3wGThs/s1600/5.jpg
Ramadhani Kampira

 
Baadhi ya 'Yosso' wa Simba wanaomtisha Kampira pambano la Simba na Yanga Mei 18
WINGA wa zamani wa Yanga na TAMCO-Kibaha aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Wilaya ya Kinondoni (KIFA), Ramadhani Yusuph Mzimba 'Kampira', ameionya klabu ya Yanga kuwa inapaswa kuwa makini katika pambano lao na watani zao Simba ili wasiadhiriwe na 'Yosso' wa Msimbazi.
Kampira, ambaye ni mwanachama wa klabu ya Yanga alisema pamoja na kwamba Mabingwa hao wapya wa Ligi Kuu wanaonekana kuwa fiti na kukamilika kila idara, bado wanapaswa kuwa makini na chipukizi wa Simba ili wasiweze kuwatia machungu ya msimu uliopita walipochezea kipigo cha aibu cha mabao 5-0.
Alisema Yanga inapaswa kuingia kwenye pambano la Mei 18 wakiweka dharau kando na kucheza kwa tahadhari kubwa kutokana na ukweli kasi ya vijana wa Simba ambao wameisaidia 'Mnyama' kushinda mechi tatu mfululizo inatisha na kila anayefuatilia soka anaona Yanga itakuwa na wakati mgumu kwa vijana hao.
ke ya Jangwani kuwa makini na vijana wa Simba watakapoumana nao katika pambano la kufungia msimu "Licha ya kwamba Yanga imeshanyakua ubingwa na wanaonekana kuwa bora kuliko Simba msimu huu, bado nilikuwa natoa wito kwa kikosi cha Yanga kushuka dimbani Mei 18, wakiwa na tahadhari kubwa dhidi ya vijana chjipukizi wa Simba, wanaweza kurejesha machungu ya msimu uliopita," alisema Kampira.
Kampira alisema mbali na kuwachunga wachezaji chipukizi wa Simba hasa Haruna Chanongo, Ramadhan Messi, na  Edward Christopher, pia wawe makini na nyota wengine wa Msimbazi walioonyesha wapo juu msimu huu kama Shomar Kapombe, Amri Kiemba na Chollo anayepana na kushuka.
"Nimewaona vijana wa Simba, kwa hakika ni wazuri wanajituma na kujiamini dimbani, kama Yanga itafanya dharau basi yale ya msimu uliopita ya kupigwa mabao 5-0 yanaweza kujirudia, japo naamini msimu huu Yanga imetulia na wakichagiwa na taji walilotwaa kabla ligi haijaisha," alisema Kampira.
Simba na Yanga zitapambana katika pambano la kufungia msimu kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, huku Yanga wakiwa tayari mabingwa na Simba wakisubiri miujiza kuambulia nafasi ya pili ambayo inaonekana dhahiri inaenda kwa Azam ambayo hata msimu uliopita iliishika nafasi hiyo hiyo nyuma ya Simba.
yanga inaoongoza msimamo mpaka sasa ikiwa na pointi 57, ikifuatiwa na Azam itakayoshuka dimbani Jumamosi kuumana na Mgambo JKT ikiwa na pointi 47 na Simba ipo nafasi ya tatu na pointi zake 45.