STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, November 27, 2012

Sharo Milione: Nyota iliyozimika ghafla ikielekea kilele cha mafanikio

NAMNA ya uigizaji wake katika hali ya kitanashati na mikogo ya kipekee inayoendana  na lugha ya kisharobaro, imemfanya msanii Husseni Ramadhani Mkiety kulipoteza jina lake halisi.
Ilikuwa vigumu kumsaka msanii huyo kwa jina lake halisi na kumpata kirahisi tofauti na kama ungemtafuta kwa jina la Sharoi Milionea.
Msani huu alibadilisha jina lake la awali na Sharobaro na kuwa Sharo Milionea baada ya kuingia mzozo na msanii mwenzake, Bob Junior na kuhofua wasikosane aliamua kutumia jina hilo jipya lililomnganda kuliko maelezo.
Nakumbuka katika mahojiano baina yetu mwishoni mwa mwaka juzi, alisema alipenda kuigiza alivyoigiza kama brazameni, ili kujitofautisha na wasanii wengine nchini akiiga staili ya msanii aliyekuwa akimhusudu mno, Will Smith.
Sharo Milionea, aliyekuwa mahiri kwa kuigiza filamu na uimbaji wa muziki wa kizazi kipya, alikiri kwamba karibu kila jambo katika sanaa yake, ina chembe cha nyota huyo wa Kimarekani anayetamba kwenye muziki na filamu ulimwenguni.
Pia, alidai ndoto yake ni kuona siku moja anakuja kuwa kama msanii huyo, mbali na kuanzisha biashara binafsi za kumuingizia pato la kutosha litakalomsaidia maishani mwake.
"Sio siri mambo mengi nayaiga kwa Smith. Nampenda mno huyu mtu, natamani siku moja niwe kama yeye," aliniambia katika mahojiano hayo yaliyofanyika eneo la Magomeni Mikumi.
Mkali huyo aliyewahi kutamba na nyimbo kama 'Nahesabu Namba','Tusigombane', 'Chuki Bure', 'Hawataki', 'Sondela', 'Tembea Kisharobaro' na aliyekuwa mbioni kuachia kazi nyingine za 'Vululuvululu' na 'Changanyachanganya', hatunaye tena.
Msanii huyo amefariki usiku wa kuamkia jana katika ajali ya gari wakati akielekea mjini Muheza, mji aliozaliwa miaka 25 iliyopita.
Sharo, ambaye nilizungumza naye mara ya mwisho jioni ya siku ya Ijumaa na kunieleza mipango yake ya kufyatua video za nyimbo hizo mbili mpya alizoimba na Ally Kiba na Tundaman, aliwahi kudai pamoja na kipaji cha kuzaliwa, lakini kukunwa na Smith na King Majuto kumemfanya afike hapo alipokuwa amefikia.
"King Majuto niliyeigiza nae filamu kadhaa ikiwemo  'Back to New York' na Smith ni kati ya waliochangia mie kuingia kwenye sanaa, navutiwa nao kwa kila wanalofanya," alisema.
Sharo Milionea, alinidokeza kuwa yeye alizaliwa katika kijiji cha Lusanga, kilichopo Muheza mkoani Tanga, Machi 20, 1987 akiwa mtoto wa mwisho wa familia yenye watoto watatu, alisema licha ya mafanikio aliyokuwa nayo tangu atumbukie kwenye fani akisoma Shule ya Msingi Luisanga na baadae Sekondari Kabuta, alikuwa hajaridhika.
Mkali huyo alianza kung'ara kupitia kundi la Chanya na Hasi kabla ya kutua Dar na kuungana na wasanii wenzake katika kundi la Jamaa Arts lililoongozwa na mtayarishaji Gumbo Kihorota alipokuwa na Mac Regan, Masanja Mkandamizaji, Snura na wengine.
Filamu ya kwanza kuigiza ilikuwa ni Itunyama na baadae Zindua akiwa na kundi hilo kuangukia Jumba Arts lililoundwa na wasanii waliojiengua Fukuto Arts Professional wanaotamba na filamu ya Elikanza.
Kazi yake ya kwanza ya vichekesho kwake ni 'Mbwembwe', iliyofuatiwa na 'Vichwa Vitatu', 'Sharobaro', iliyokuwa kazi yake binafsi, pia amecheza 'Nazi Koroma', 'Kuku wa Kichina', 'Muuza Sura', 'Sharo Milionea'.
Mwaka 2009 alitua kundi la Bongo Super Stars Comedy chini ya kampuni ya Al Riyamy Production ambapo walifyatua filamu ya 'Sharo Milionea', 'Mtoto wa Mama' alipoibuka na maneno ya 'Kamata Mwizi Meeen' na kabla ya kufuatiwa na kazi nyingine kadhaa ikiwemo Back From New York'.
Hata hivyo mapema mwaka huu alinidokeza kwa simu kuwa alikuwa amejiondoa Al Riyamy na kufanya kazi chini ya usimamizi wa meneja Ustaadh Juma Namusoma.
Mwenyewe alikiri kwamba sanaa ilimmsaidia mengi ikiwemo kiuchumi na kufahamika, licha ya kutopenda mengi yaanikwe gazetini kwa madai ni mambo yake binafsi.
"Sanaa imenisaidia mambo mengi, ila sipendi kuyaanika gazetini," nilimnukuu.
Msanii huyo aliyekuwa akipenda kula hasa vyakula vinono kuliko kitu kingine maishani mwake na kunywa juisi ya Parachichi, alisema angekutana na Rais angemuomba asaidia kuinua uchumi na kuboresha huduma za kijamii ili kila Mtanzania aifurahie nchi yake.
"Pia ningemuomba asaidie fani za michezo na sanaa, ziwe na nguvu ya kulikomboa taifa hususan katika tatizo la ajira," alisema.
Ila , alidai kaka yeye angekuwa ni Rais, angetoa kipaumbele katika huduma za kijamii hasa elimu na afya, pia angepigania sanaa na michezo ziwe sehemu ya nguzo za uchumi nchini.
Sharo Milionea aliyetaja tukio la furaha ni siku alipofahamishwa kwamba kazi zake zinaonwa nje na kuwavutia wengi kiasi cha vijana wanazoziangalia kumuiga, alisema ili kutimiza ndoto za kung'ara kimataifa amekuwa akigeuka kuwa 'Kinyonga'.
"Ukinyonga wangu kuigiza vichekesho, filamu 'seriuos' na muziki," alisema.
Sharo Milionea, alikuwa shabiki wa klabu ya Real Madrid, ingawa alinidokeza hakuwa anamjua hata moja la nyota wa kikosi hicho, huku akidai katika matukio ya huzuni kwake ni kifo cha babu yake aliyekuwa mlezi baada ya kumlea tangu baba yake afe akiwa kinda.
"Alikuwa mlezi na muongozo wangu kimaisha, alinipenda na nilimpenda mno." aliniambia kwa huzuni
Mkali huyo aliyetamba na filamu ya 'Chumo' aliyoigiza na Yusuph Mlela na Jokate Mwegelo, alikuwa hajaoa wala kuwa na mtoto, ingawa alikuwa na mchumba aliyekuwa akidai angemuoa muda muafaka ungefika..
Sharo Milionea aliyekunwa na Joti na Kanumba kwa hapa nchini, alisema kama msanii nyota amekuwa akipata usumbufu toka kwa wanawake wanaomtaka kimapenzi, ila alidai hutumia busara kuwaepa akitambua kuwa sio wote wanampenda, pia kuwepo Ukimwi.
"Hili la Ukimwi, kila mtu analitambua, ni wajibu wa kila mtu ndani ya jamii kuepukana nao, ili kutimiza ndoto za maisha yao, kama ninavyofanya mimi," alisema.
Kuhusu wasanii nyota kujitumbukiza kwenye skondo na matendo maovu, Sharo Milionea, alisema ni vigumu kuwazuia wanaofanya, ila aliwataka watambue kuwa wao ni vioo vya jamii na wenye familia nyuma zao, hivyo wajiheshimu na wajithamini kusudi nao wathaminiwe na jamii.
"Kama mtu hajiheshimu au kujithamini ni vigumu kuheshimiwa na jamii, kitu hicho ndicho kinachochangia fani yetu kuonekana ya kihuni wakati sivyo ilivyo," alisema.
Wakati mauti yanamkumba msanii huyo alikuwa ametoka kuingia mkataba wa kutangaza huduma za simu za mkononi za Airtel na kuuza sura katika matangazo ya bidhaa za kampuni za Bakhresa hasa soda za Azam akishirikiana na King Majuto.
Sharo atakumbukwa daima kwa ucheshi wake na kujichanganya na watu licha ya umaarufu alionao, hakuwahi kunata au kujiona kama baadhi ya watu wa kariba yake.
Kifo cha Shario Milionea kimekuja wakati wadau wa sanaa wakiendelea kuomboleza vifo wa wakali wengine waliofariki hivi karibuni, kuanzia Steven Kanumba, Mlopelo, Mariam Khamis, John Maganga.
Kwa hakika tuliwapenda wenzetu, lakini Mwenyezi Mungu aliwapenda zaidi. Jina la Allah Lihimidiwe kwani kazi yake haina makosa.

Wasanii, Airtel wamlilia Sharo Milionea

Meneja Uhusiano wa kampuni ya Airtel, Jackson Mbando

Sharo Milionea enzi za uhai wake
KAMPUNI ya simu za mkononi ya Airtel imeungana na watanzania wengine kumlilia msanii nyota wa filamu na mwanamuziki wa kizazi kipya, Husseni Ramadhani Mkiety 'Sharo Milionea' aliyefariki usiku wa kuamkia jana kwa ajali ya gari.
Meneja Uhusiano wa Airtel, Jackson Mbando, alisema wameshtushwa na kusikitishwa na kifo cha ghafla cha Sharo Milionea ambaye waliingia naye mkataba hivi karibuni ili kutangaza huduma za kampuni hiyo.
Alizungumza asubuhi hii na kituo cha Cloud FM, Mbando alisema kifo cha Sharo Milionea, kimewatia simanzi kutokana na ukweli kimekuja ghafla mno na huku akiwa bado anahitajika katika kuitangaza kampuni yao.
"Tunaungana na familia, ndugu na jamaa na wadau wote wa burudani kutokana na kifo cha Sharo Milionea, alikuwa kijana mdogo, mchangamfu na aliyekitumia vema kipaji chake cha sanaa, Airtel tumeguswa na msiba huu kwani tulikuwa bado tunamtegemea kutangaza huduma zetu," alisema Mbando.
Wasanii wengine waliowahi kufanya kazi na msanii huiyo aliyefariki jana saa mbili usiku baada ya gari alilokuwa akiliendesha kwenda kwao Muheza Tanga, kupinduka na kusababisha kifo chake wamedai wanashindwa kuamini kama amefariki.
Masai Nyota Mbofu, amedai itamchukua muda mrefu kumsahau Sharo aliyewahi kutamba naye keenye filamu na kipindi cha 'Vituko Show' wakati kampuni ya Al Riyamy.
Naye mtayarishaji wa filamu nchini Mustafa Wazir 'West' alisema atamkumbuka daima Sharo Milionea kwa kipaji alichokuwa nacho.
Mchekeshaji mwingine aliyekuwa akiigiza na Sharo, Ally Boffu 'Man Bizo', alidai mpaka sasa haamini kama Sharo Milionea amemtoka kwa jinsi ilivyokuwa ghafla.
Kifo cha Sharo Milione kimekuja huku wadau wa sanaa wakiendelea kuwaomboleza muimbaji wa TOT-Taarab Mariam Khamis 'Paka Mapepe' aliyefariki wiki mbili zilizopita na waigizaji Mlopero na John Maganga waliokufa wiki iliyopita.
Hussein Mkiety 'Sharo Milionea, aliyezaliwa Machi 20, 1987 Muheza, akiwa mtoto wa mwisho kati ya watoto watatu na amefariki akiwa mbioni kufyatua video za nyimbo zake mbili zilizokamilika hivi karibuni za 'Vululuvululu' alioimba na Tundaman na 'Changanya Changanya' alioimba na Ally Kiba.
Taarifa tulizozipata hivi tunde zinasema kwamba huenda marehemu Sharo Milionea akazikwa leo mjini Muheza, Tanga ingawa tunaendelea kufuatilia taarifa zaidi juu ya msiba huo.

Mashindano ya ngumi yaota mbawa mpaka mwakani

MASHINDANO ya ngumi za ridhaa ya klabu bingwa ya taifa yaliyopangwa kuanza kufanyika jana Novemba 26 hadi Novemba -30 mwaka huu yamesogezwa mbele hadi Januari 29 hadi Februari 3 mwakani.
Katiku Mkuu wa Shirikisho la Ngumi za Ridhaa nchini (BFT), Makore Mashaga alisema juzi kuwa, wamelazimika kusogeza mbele mashindano hayo hadi mwakani kutokana na sababu mbalimbali.
Alizitaja baadhi ya sababu hizo kuwa ni pamoja na timu shiriki kushindwa kukamilisha taratibu, ikiwa ni pamoja na kutothibitisha ushiriki wake katika tarehe iliyopangwa.
Kwa mujibu wa Mashaga, sababu zingine ni timu shiriki kushindwa kuwasilisha majina na picha za mabondia wake pamoja na kulipa ada ya ushiriki ya sh. 200,000.
"Hadi leo hakuna hata timu moja iliyokamilisha utaratibu huo kwa nia ya kupanga mashindano vizuri ili yawe na hadhi ya taifa kwa kuzingatia sheria za Chama cha Ngumi za Ridhaa cha Dunia (AIBA)," alisema.
"Sababu kama hizi mara nyingi zimesababisha mashindano mengi kuendeshwa kwa kiwango cha chini na lawama nyingi kuelekezwa kwa BFT bila ya kufahamu sababu za msingi," aliongeza.
Mashaga alisema pia kuwa, kozi ya waamuzi iliyopangwa kuanza Novemba 11-30 mwaka huu ilishindwa kufanyika kutokana na washiriki kushindwa kukamilisha taratibu za ushiriki ikiwa ni pamoja na kulipa ada kwa wakati.
Kutokana na BFT kuwa na majukumu mengine, Mashaga alisema kozi hiyo sasa imepangwa kufanyika Januari 15 hadi Februari 4 mwakani na mazoezi ya vitendo yatafanyika wakati wa mashindano ya klabu bingwa.
Mashaga alisema kwa sasa, BFT imeweka nguvu kubwa katika usajili wa makocha, waamuzi, mabondia na madaktari ili waweze kutambulika kwa ajili ya kujiunga na mashirikisho ya ngumi za kulipwa.

Uncle D kuziba pengo la Uncle JJ Bongo Movie?

Uncle JJ (kushoto) na Uncle D anayejaribu kuvaa viatu vyake
Uncle D

BADO mashabiki wa filamu nchini wanaendelea kuumizwa na kifo cha aliyekuwa nyota wa fani hiyo, Steven Kanumba 'Uncle JJ' ama lile maarufu la 'The Great Pioneer' aliyefariki ghafla Aprili mwaka huu.
Tangu alipofariki dunia, mashabiki wake wamekuwa wakisikilizia na kutaka kuona nani atakayeweza kuvaa viatu vya mkali huyo aliyekuwa na kiu kubwa ya maendeleo katika fani yake tangu alipokuwa Kaole Sanaa.
Wengi wamekuwa wakijiuliza ni msanii gani atakayeweza kuwaburudisha kwa kiwango alichokuwa akikifanya Kanumba hasa kupitia filamu zake mchanganyiko zikiwemo za kiutu uzima, watoto, kidini na masuala mengi ya kijamii.
Japo wapo wasanii kibao waliowahi kufanya kazi pamoja na Kanumba wamekuwa wakiaminiwa huenda wakasimama na kuziba pengo hilo la msanii huyo, hata hivyo hali inaonekana kuwa ngumu.
Hii inatokana na ukweli kwamba marehemu Kanumba, aliiteka mioyo ya mashabiki wengi kiasi imekuwa vigumu kwa mashabiki hao kuruhusu mioyo hiyo kutoa nafasi kwa mtu mwingine kuingia.
Ndio maana hata soko la filamu lilionekana kuyumba tangu Kanumba alipofariki kwa kazi za watu wengine kusahauliwa kwa muda na kukimbiliwa kazi za nyuma za mkali huyo, ingawa kwa sasa hali inaendelea kubadilika kwa watu kuzoea hali halisi iliyotokea.
Hata hivyo, huenda mashabiki wa filamu wakasuuzwa roho zao, baada ya Jacklyne Wolper kuamua kutengeneza filamu mpya iitwayo 'After Death' ambayo imemshirikisha msanii asiye na jina, lakini aliyeshabihiana na marehemu Kanumba.
Msanii huyo si mwingine bali ni Philemon Latwaza ambaye ndani ya filamu hiyo mpya atafahamika kwa jina la 'Uncle D'.
Uncle D, ameigiza na 'watoto wa Kanumba', Jennifer na Patrick, walioibuliwa na filamu za 'Uncle JJ' na 'This is It', sambamba na waigizaji wengine wenye majina waliowahi kucheza pamoja na marehemu Kanumba enzi za uhai wake.
Muongozaji wa filamu hiyo, Leah Richard Mwendamseke 'Lamata' alisema ujio wa Uncle D unaweza kuziba pengo la Kanumba kwa kiasi fulani na pengine kuwarudisha mashabiki wa marehemu huko katika 'sononi' mpya ya kumkumbuka.
Lamata, alisema wamefyatua filamu hiyo kama njia ya kumuenzi Kanumba na pia kuendelezaa juhudi zake za kuibua na kukuza vipaji vya akina Jennier na Patrick.
"Nadhani After Death, itawakumbusha mbali mashabiki wa filamu kwa namna Uncle D alivyomudu kumuigiza Kanumba na hasa kutokana na kufanana naye kwa sura kwa kiasi kikubwa," alisema.
Mbali na Uncle D na watoto Jennifer na Patrick katika filamu hiyo pia wameigiza akina Mainda, Mayasa Mrisho, Ben Blanco, Wolper mwenyewe, Irene Paul, Shamsa Ford na Patcho Mwamba.
Swali la kujiuliza je, Uncle D atamudu kuvaa viatu vya Kanumba kama Lamata anavyodai? Ni suala la kusubiri kuona mara filamu hiyo itakapoachiwa mtaani.


Golden Bush: Klabu ya 'mastaa' wa soka iliyopania makubwa nchini * Yajipanga kuuza wachezaji wao barani Afrika kwanza kabla ya Ulaya


Nembo ya klabu ya Golden Bush


Kocha wa Golden Bush, Shija Katina akiwaelekeza wachezaji wake katika mazoezi ya timu hiyo

Kikosi kamili cha Golden Bush (wa kwanza kulia) ni kocha Shija KatinaKIU kubwa ya kutaka kuinua na kuendeleza vipaji vya soka kwa vijana pamoja na kutoa ajira kwa vijana hao kupitia soka ndiko kulikofanya baadhi ya nyota wa zamani wa soka nchini kuungana na kuanzisha timu yao ya Golden Bush.
Nyota hao wa zamani wakiongozwa na Ally Mayay, Wazir Mahadhi 'Mandieta' , Abuu Ntiro, Said Swedi 'Panucci', Salum Swedi 'Kussi', chini ya makocha Shija Katina na Madaraka Selemani waliungana na kuiasisi timu hiyo mpya.
Wakiwa wamepeana majukumu ndani ya timu hiyo iliyo chini ya muasisi na

mlezi wao, Onesmo Wazir 'Ticotico', kiu yao kubwa ni kuifanya klabu hiyo kuwa ya mfano nchini kutokana na malengo na mikakati waliyoijiwekea.
Moja ya malengo ya timu hiyo inayojiandaa na ushiriki wa Ligi ya TFF wilaya ya Kinondoni ni kuendeleza vipaji na kuwawezesha vijana wenye uwezo wa kucheza soka la kulipwa nje ya nchi wakitimiza ndoto zao.
Uongozi wa timu hiyo yenye maskani yake Sinza, Dar es Salaam japo iliasisiwa

Mabibo, ulisema haitakimbilia kuwapeleka wachezaji wao kucheza soka Ulaya badala yake wataanzia kuwapeleka nchi za barani Afrika kwanza.
Meneja wa timu, Wazir Mahadhi alisema wanaamini kucheza soka la kulipwa

barani Afrika ni njia nzuri ya kuwapa nafasi wachezaji wao kupata uzoefu wa kuhimili mikikimikiki kabla ya kusonga mbele kwenye ushindani zaidi kisoka.
Mahadhi alisema ndiyo maana katika timu yao wamejumuisha wachezaji wa umri wa miaka 17-23 tu, kwa kuamini umri huo ni sahihi kwa wachezaji kupata nafasi ya kucheza soka la kulipwa.
Naye mlezi wa klabu hiyo, Onesmo Wazir 'Ticotico' alisema tayari wameanza mipango ya kujenga uhusiano na klabu kadhaa za barani Afrika ili kurahisisha mipango yao wakianzia na nchi ya Msumbiji.
"Tayari tumeshaanza kutekeleza mikakati yetu, tunatarajia kupeleka wachezaji wetu nchini Msumbiji, tunatarajia miezi sita ijayo tutapanua wigo zaidi katika mahusiano na klabu nyingine za nje," alisema Ticotico.
Ticotico, 'membaz' wa zamani wa Friends of Simba na mjumbe wa zamani wa Kamati ya Fedha na Uchumi ya Simba chini ya uongozi wa akina ismail Rage,

alisema wamepanga miaka miwili ijayo Golden Bush iwe mbali kimaendeleo.
"Tumelenga kuja kuanzisha 'academy' ya soka itakayohusisha vijana wenye umri kati ya miaka 14-17,  pia tuweze kuwalipa wachezaji wetu mishahara tofauti na posho tunazowapa kwa sasa," alisema.

KWA NINI?
Ticotico alisema saababu kuu ya kuasisiwa kwa timu hiyo ilitokana na yeye na wachezaji hao nyota wa zamani kukerwa kuona vipaji vya soka vya vijana vikipotea mitaani bila kutumiwa wala kunufaisha taifa na wachezaji wenyewe.
Japo alikiri wanatambua changamoto kubwa zilizopo mbele yao ili kuifikisha

Golden Bush mahali walikokusudia, bado anaamini timu yao itafika mbali kutokana na walivyojipanga hasa  kuifanya timu yao iwe yenye ushindani.
Ticotico, Mahadhi na kocha Shija Katina walisema kwa nyakati tofauti wakati ilipoanzishwa klabu hiyo ilikuwa kwa ajili ya kushiriki mabonanza, lakini kule kuona vijana wengi wakijitokeza kucheza pamoja nao iliwapa wazo la kuiboresha.
Walisema ilipoanzishwa timu hiyo ilikuwa na wachezaji wasiozidi 20, ila kwa sasa wamesajiliwa 28 kwa ajili ya Ligi ya TFF inayotarajiwa kuanza hivi karibuni.

MATARAJIO
Mbali na kuifanya iwe klabu ya mfano, Mahadhi alidai wanataka kuipandisha timu hiyo daraja sambamba na kutoa ajira kwa vijana kama alivyofafanua mlezi wao juu ya mipango ya kuanzisha 'chuo' na kuuza wachezaji nje ya nchi.
Hata hivyo, Mahadhi wenzake walisema kitu cha muhimu wanachoomba ni kupata sapoti kwa wadau wa soka nchini wakiwamo wafadhili kujitokeza kuwapiga tafu ili kutimiza malengo yao.
"Hatuwezi kufanikiwa kama hatutaungwa mkono na wadau kuanzia watu binafsi hadi makampuni kwa ajili ya udhamini," alisema.
Aliongeza kuwepo kwa wadhamini wa kutosha na sapoti toka kwa wadau wa

soka kutaiwezesha Golden Bush kutimiza ndoto za kuwa klabu ya mfano sawia na kuwapa faraja wachezaji wanaotegemea vipaji vya kuwanufaisha.

NIDHAMU
Katika moja ya vitu ambavyo uongozi na benchi la ufundi la timu hiyo inavyoviangalia ni suala la nidhamu ndani na nje ya uwanja.
Makocha, Shija Katina na Madaraka Seleman 'Mzee wa Kiminyio', walisema suala la nidhamu ndicho kipaumbele cha kuchukuliwa kwa vijana kuichezea timu hiyo na suala hilo linaendelea kuzingatiwa hata sasa timu ikiwa inazidi kuimarika.
Katina, alisema bahati nzuri wachezaji walionao ni waelewa na wenye malengo ya kweli ya kufika mbali kisoka na hivyo wanazingatia nidhamu na kujituma kwa moyo bila kusukumwa.
Alisema nidhamu hiyo ya wachezaji na ushirikiano uliopo baina yao na uongozi mzima wa Golden Bush ndiyo iliyowawezesha katika mechi 15 walizokwishacheza moja sasa kushinda mara saba ikiwamo kuzilaza Mtibwa Sugar, 94 KJ na kuisimamisha Kagera Sugar waliotoka nao sare miongoni mwa sare mbili walizopata.
"Tumecheza mechi 15 tuimeshinda saba na kupoteza sita na sare mbili baadhi ya timu tulizocheza nazo ni za Ligi Kuu na Daraja la Kwanza, na tuliweza kuzisimamisha kwa vile wachezaji wana nidhamu ndani na nje ya dimba hata kwa mechi za kirafiki."

SAFU YAKE
Klabu hiyo ya Golden Bush iliyoasisiwa April mwaka jana kabla ya kupata usajili kamili mwishoni mwa mwaka jana, ina safu kamili ya uongozi ambapo Mwenyekiti wake ni Ally Mayay akisaidiwa na Salum Swedi.
Katibu Mkuu wa klabu hiyo ni Majaliwa Mwaigaga akisaidiwa na Henry Morris, huku Meneja akiwa ni Wazir Mahadhi, na makocha wake ni Shija Katina na Madaraka Seleman.
Mlezi wa timu hiyo ambayo imekuwa ikifanya mazoezi yake kwenye uwanja wa Kinesi Ubungo na wakati mwingine Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ni Onesmo Wazir na ikipata sapoti kubwa na nyota wa zamani akina Abuu Ntiro, Yahya Issa, Said Swedi, Shaaban Kisiga na waasisi wengine baadhi wakiendelea kucheza soka ngazi ya ligi kuu na daraja la kwanza.
Add caption

Wolper amkumbuka marehemu Kanumba

Jacklyne Wolper alipoigiza na Kanumba katika filamu ya Ndoa Yangu


NYOTA wa filamu nchini, Jacklyne Wolper, amemkumbuka marehemu Steven Kanumba na kumtungia filamu iitwayo 'After Death' aliyowashirikisha baadhi ya wasanii chipukizi walioibuliwa na Kanumba enzi za uhai wake.
Muongozaji wa filamu hiyo, Leah Richard, aliiambia MICHARAZO kuwa  filamu hiyo ni maalum kwa ajili ya kuenzi mchango wa mkali huyo wa filamu aliyefariki ghafla na kuzikwa Aprili mwaka huu.
Leah alisema filamu hiyo imetungwa na Jacklyne Wolper aliyewahi kucheza na Kanumba filamu mbalimbali ikiwemo 'Ndoa Yangu' na imeongozwa na yeye.
"Imetungwa na Wolper na kuongozwa na mimi mwenyewe na mpaka sasa imekamilika na inasubiriwa kufanyiwa uzinduzi rasmi hapo baadae," alisema Leah.
Mwanadada huyo alisema anaamini filamu hiyo itakapoingia sokoni itawarejeshea kumbukumbu wapenzi wa filamu juu ya Kanumba na watoto wake kwa namna mtu aliyeigiza kama Kanumba kushabihiana naye kwa sura kwa kiasi kikubwa.
"Yaani ni kama Kanumba amerejea upya ulimwengu kupitia 'After Death' kwa namna aliyemuigiza kufanana naye na namna alivyoigiza na watoto hao wa Kanumba," alisema.
Kanumba, aliyekuwa akifahamika kama The Great', aliwaibua watoto wenye vipaji  na kuigiza nao katika filamu kadhaa kama 'Uncle JJ', 'This is It' na 'Big Daddy', alifariki dunia Aprili 6 mwaka huu.

Tutegemee vipaji sio miili yetu-Salha

Salha Abdallah katika pozi


MUIMBAJI wa kundi la taarab la Dar Modern 'Wana wa Jiji', Salha Abdallah, amewataka wasanii wenzake wa kike kujiheshimu, kujiamini na kutumia vipaji vyao kuwakomboa kiuchumi badala ya kuitegemea miili yao kujitajirisha.
Salha anayetamba kwa sasa na kibao alichokitunga na kukiimba cha 'Nauvua Ushoga', alisema msanii anayetegemea kipaji chake, kujiheshimu na kujiamini hawezi kukubali kukudhalilishwa na watu wachache wanaowaozunguka katika fani na ndani ya jamii.
Alisema wasiojiamini na siyo na vipaji vya kweli ndio wamekuwa wepesi kujidhalilisha kwa kuitegemea miili yao kuwapa mafanikio na mwishowe kuachwa wakiwa hawana thamani mbele ya watu waliowachezea na jamii kwa ujumla.
"Lazima niseme ukweli wapo baadhi ya wasanii wenzetu wanaitegemea miili yao kuwainua kisanii na kimaisha, ila hawatambui waavyojishushia hadhi, mwanamke wa kweli ni yule anayejiamini, kujiheshimu na kutegemea kipawa alichojaliwa," alisema.
Alisema kama msanii mrembo amekuwa akikutana na vishawishi vingi toka kwa wanaume wakware, ila amekuwa akiwakwepa kistaarabu huku akifichua wengi wa wanaume wa hivyo huandika namba zao za simu katika fedha wanaozoenda kuwatunza.
Muimbaji, aliyezaliwa pacha na mwenzake, alisema binafsi huwa anakerwa na wasanii wa kike wanaojihusisha na skendo na kukubali kutolewa picha za ovyo magazetini.

Ruvu Shooting wamsubiri MkwasaUONGOZI wa klabu ya soka ya Ruvu Shooting ya Pwani, umesema wiki hii utaweka hadharani mikakati yao kwa ajili ya maandalizi ya duru lijalo la Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kupokea taarifa na mapendekezo ya kocha wao.
Afisa Habari wa Ruvu, Masau Bwire aliiambia MICHARAZO kwamba panga pangua ya kikosi chao inatarajiwa kufahamika wiki hii baada ya kumaliza kucheza mechi zao za duru la kwanza kwa kuilaza Prisons-Mbeya mabao 2-0.
Bwire, alisema uongozi unasubiri ripoti ya bnchi lao la ufundi chini ya kocha Charles Boniface Mkwasa, ili kujua wapi pa kuanzia katika maandalizi ya duru hilo walilodai wamelipania ili wamalize msimu katika nafasi nzuri.
"Baada ya kumalizika kwa pambano letu na Prisons tukishukuru kushinda kwa mabao 2-0, kwa sasa tunasubiri taarifa na mapendekezo ya mwalimu wetu kwa ajili ya kujipanga kwa duru lijalo," alisema Bwire.
Bwire, alisema wangependa kuona duru lijalo wakifanya vizuri zaidi na duru lao la kwanza lililowaacha wakiwa nafasi ya saba wakijikusanyia jumla ya pointi 20 kutokana na mechi 13 ilizocheza katika duru hilo.
Afisa Habari huyo, alisema yapo baadhi ya mapungufu yaliyoonekana katika kikosi chao yanayohitajika kurekebishwa, lakini uongozi hauwezi kusema lolote mpaka waipate ripoti ya kocha Charles Boniface.
***

Kipa wa zamani Yanga kwenda Msumbiji


KIPA wa zamani wa timu za Yanga na Moro United, Steven Marashi, anatarajiwa kuondoka nchini mwishoni mwa wiki kwenda nchini Msumbiji kujaribu kucheza soka la kulipwa katika klabu ya Ligi Kuu nchini humo.
Akizungumza na MICHARAZO, Marashi, aliyeachwa kitatanishi misimu miwili iliyopita pamoja na akina Wisdom Ndhlovu na John Njoroge, alisema mipango ya safari yake inafanya mmoja wa mawakala waliopo nchini Msumbiji aliyewahi kumuona akicheza.
Marashi, alisema japo jina la timu anayoenda kufanyiwa majaribio haikumbuki kwa jina, lakini amedai ni ya Ligi Kuu ya Msumbiji na imani yake ni kufanya vema.
"Kaka nipo katika maandalizi ya safari ya kwenda Msumbiji kwa ajili ya kujaribu kucheza soka la kulipwa baada ya kupatiwa na nafasi na mmoja wa mawakala wa nchini humo aliyevutiwa nami wakati nikiwa Moro United," alisema.
Kipa huyo ambaye aliamua kujiengua Moro United mara baada ya kushuka daraja toka Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita, alisema kama mambo yataenda yalivyopangwa basi ataondoka nchini Jumamosi au Jumapili.

ZANZIBAR WAANZA NA SARE CHALLENJI - NIYONZIMA AKIING'ARISHA RWANDA

Beki wa timu ya Zanzibar Heroes, Said Chollo akimiliki mpira wakati wa
mchezo dhidi ya timu ya Eritrea wakati wa michuano ya Cecafa Challenge
2012 uliochezwa katika Uwanja wa Mandela nchini Uganda

Wachezaji wa timu za Zanzibar na Eritrea wakiwania mpira wakati wa
mchezo dhidi ya timu ya Eritrea wakati wa michuano ya Cecafa Challenge
2012 uliochezwa katika Uwanja wa Mandela nchini Uganda.Haruna Niyonzima akishangilia goli lake aliloifungia Rwanda dhidi ya Malawi na kufanya matokeo kuwa 2-0 mpaka kipenga cha mwisho kilipopulizwa - kufuatia goli la kwanza lilofungwa na Jean Baptiste Muginereza katika dakika ya 38 ya kipindi cha kwanza.   

SHARO MILIONEA ATUNAYE TENA!MCHEKESHAJI mahiri ambaye pia ni msanii wa muziki wa kizazi kipya nchini, Hussein Mkiety ‘Sharo Milionea’amefariki papo hapo usiku wa kuamkia leo baada ya kupatwa ajali akielekea nyumbani kwao Muheza, mkoani Tanga.

.

Hussein Mkiety
Msanii Husseni Mkiety 'Sharo Milionea'  enzi za uhai wake

Taarifa za awali ambazo MICHARAZO ilizipata jana usiku zilisema kuwa, marehemu alifariki wakati gari alililokuwa akiendeza kupinduka mara kadhaa na kumsababishiaa kifo chake ikiwa ni siku tatu tangu alipozungumza na mwandishi wa habari hizi akielezea mipango ya kupakua avideo zake mbili za nyimbo za 'Vululuvululu' na 'Changanya Changanya' alizoimba na Tundaman na Ally Kiba.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Tanga, Constantine Massawe alinukuliwa na kituo kimoja cha redio na kuthibutisha taariofa za kifo cha msanii huyo machachari.
“Leo majira ya saa mbili usiku kwenye barabara ya Segera Muheza Tanga mtu mmoja aliyetambulika kwa jina la Hussein Ramadhani au Sharo Milionea akiwa anaendesha gari namba T478 BVR Toyota Harrier akitokea Dar es salaam kwenda Muheza alipofika eneo hilo gari lake liliacha njia na kupinduka mara kadhaa na kusababisha kifo chake.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa kwenye hospitali Teule ya wilaya ya Muheza” Kamanda amesema hakuna kona kali sana wala ubovu wa barabara kwenye sehemu aliyopata ajali Sharo Milionea, katikati ya Segera na Muheza ambapo gari imehifadhiwa mahali salama kwa sababu haitembei.
Taarifa hii imetolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa Tanga Constantine Massawe,
Hadi mauti inamkuta alikuwa ni mwanamuziki wa muziki wa kizazi kipya wimbo wake wa Chuki Bure alioimba na Dully Sykes mbali na kibao chake cha 'Hawataki'.
taarifa zaidi kuhusu taratibu za mazishi tutaendelea kuwajulisha
ingawa inaelezwa msiba wake upo nyumbani kwao Muheza Tanga.
MICHARAZO inawapa pole  familia, ndugu, jamii na rafiki wote wa  msanii huyo Mungu aipokee Roho ya