STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, November 27, 2012

Sharo Milione: Nyota iliyozimika ghafla ikielekea kilele cha mafanikio

NAMNA ya uigizaji wake katika hali ya kitanashati na mikogo ya kipekee inayoendana  na lugha ya kisharobaro, imemfanya msanii Husseni Ramadhani Mkiety kulipoteza jina lake halisi.
Ilikuwa vigumu kumsaka msanii huyo kwa jina lake halisi na kumpata kirahisi tofauti na kama ungemtafuta kwa jina la Sharoi Milionea.
Msani huu alibadilisha jina lake la awali na Sharobaro na kuwa Sharo Milionea baada ya kuingia mzozo na msanii mwenzake, Bob Junior na kuhofua wasikosane aliamua kutumia jina hilo jipya lililomnganda kuliko maelezo.
Nakumbuka katika mahojiano baina yetu mwishoni mwa mwaka juzi, alisema alipenda kuigiza alivyoigiza kama brazameni, ili kujitofautisha na wasanii wengine nchini akiiga staili ya msanii aliyekuwa akimhusudu mno, Will Smith.
Sharo Milionea, aliyekuwa mahiri kwa kuigiza filamu na uimbaji wa muziki wa kizazi kipya, alikiri kwamba karibu kila jambo katika sanaa yake, ina chembe cha nyota huyo wa Kimarekani anayetamba kwenye muziki na filamu ulimwenguni.
Pia, alidai ndoto yake ni kuona siku moja anakuja kuwa kama msanii huyo, mbali na kuanzisha biashara binafsi za kumuingizia pato la kutosha litakalomsaidia maishani mwake.
"Sio siri mambo mengi nayaiga kwa Smith. Nampenda mno huyu mtu, natamani siku moja niwe kama yeye," aliniambia katika mahojiano hayo yaliyofanyika eneo la Magomeni Mikumi.
Mkali huyo aliyewahi kutamba na nyimbo kama 'Nahesabu Namba','Tusigombane', 'Chuki Bure', 'Hawataki', 'Sondela', 'Tembea Kisharobaro' na aliyekuwa mbioni kuachia kazi nyingine za 'Vululuvululu' na 'Changanyachanganya', hatunaye tena.
Msanii huyo amefariki usiku wa kuamkia jana katika ajali ya gari wakati akielekea mjini Muheza, mji aliozaliwa miaka 25 iliyopita.
Sharo, ambaye nilizungumza naye mara ya mwisho jioni ya siku ya Ijumaa na kunieleza mipango yake ya kufyatua video za nyimbo hizo mbili mpya alizoimba na Ally Kiba na Tundaman, aliwahi kudai pamoja na kipaji cha kuzaliwa, lakini kukunwa na Smith na King Majuto kumemfanya afike hapo alipokuwa amefikia.
"King Majuto niliyeigiza nae filamu kadhaa ikiwemo  'Back to New York' na Smith ni kati ya waliochangia mie kuingia kwenye sanaa, navutiwa nao kwa kila wanalofanya," alisema.
Sharo Milionea, alinidokeza kuwa yeye alizaliwa katika kijiji cha Lusanga, kilichopo Muheza mkoani Tanga, Machi 20, 1987 akiwa mtoto wa mwisho wa familia yenye watoto watatu, alisema licha ya mafanikio aliyokuwa nayo tangu atumbukie kwenye fani akisoma Shule ya Msingi Luisanga na baadae Sekondari Kabuta, alikuwa hajaridhika.
Mkali huyo alianza kung'ara kupitia kundi la Chanya na Hasi kabla ya kutua Dar na kuungana na wasanii wenzake katika kundi la Jamaa Arts lililoongozwa na mtayarishaji Gumbo Kihorota alipokuwa na Mac Regan, Masanja Mkandamizaji, Snura na wengine.
Filamu ya kwanza kuigiza ilikuwa ni Itunyama na baadae Zindua akiwa na kundi hilo kuangukia Jumba Arts lililoundwa na wasanii waliojiengua Fukuto Arts Professional wanaotamba na filamu ya Elikanza.
Kazi yake ya kwanza ya vichekesho kwake ni 'Mbwembwe', iliyofuatiwa na 'Vichwa Vitatu', 'Sharobaro', iliyokuwa kazi yake binafsi, pia amecheza 'Nazi Koroma', 'Kuku wa Kichina', 'Muuza Sura', 'Sharo Milionea'.
Mwaka 2009 alitua kundi la Bongo Super Stars Comedy chini ya kampuni ya Al Riyamy Production ambapo walifyatua filamu ya 'Sharo Milionea', 'Mtoto wa Mama' alipoibuka na maneno ya 'Kamata Mwizi Meeen' na kabla ya kufuatiwa na kazi nyingine kadhaa ikiwemo Back From New York'.
Hata hivyo mapema mwaka huu alinidokeza kwa simu kuwa alikuwa amejiondoa Al Riyamy na kufanya kazi chini ya usimamizi wa meneja Ustaadh Juma Namusoma.
Mwenyewe alikiri kwamba sanaa ilimmsaidia mengi ikiwemo kiuchumi na kufahamika, licha ya kutopenda mengi yaanikwe gazetini kwa madai ni mambo yake binafsi.
"Sanaa imenisaidia mambo mengi, ila sipendi kuyaanika gazetini," nilimnukuu.
Msanii huyo aliyekuwa akipenda kula hasa vyakula vinono kuliko kitu kingine maishani mwake na kunywa juisi ya Parachichi, alisema angekutana na Rais angemuomba asaidia kuinua uchumi na kuboresha huduma za kijamii ili kila Mtanzania aifurahie nchi yake.
"Pia ningemuomba asaidie fani za michezo na sanaa, ziwe na nguvu ya kulikomboa taifa hususan katika tatizo la ajira," alisema.
Ila , alidai kaka yeye angekuwa ni Rais, angetoa kipaumbele katika huduma za kijamii hasa elimu na afya, pia angepigania sanaa na michezo ziwe sehemu ya nguzo za uchumi nchini.
Sharo Milionea aliyetaja tukio la furaha ni siku alipofahamishwa kwamba kazi zake zinaonwa nje na kuwavutia wengi kiasi cha vijana wanazoziangalia kumuiga, alisema ili kutimiza ndoto za kung'ara kimataifa amekuwa akigeuka kuwa 'Kinyonga'.
"Ukinyonga wangu kuigiza vichekesho, filamu 'seriuos' na muziki," alisema.
Sharo Milionea, alikuwa shabiki wa klabu ya Real Madrid, ingawa alinidokeza hakuwa anamjua hata moja la nyota wa kikosi hicho, huku akidai katika matukio ya huzuni kwake ni kifo cha babu yake aliyekuwa mlezi baada ya kumlea tangu baba yake afe akiwa kinda.
"Alikuwa mlezi na muongozo wangu kimaisha, alinipenda na nilimpenda mno." aliniambia kwa huzuni
Mkali huyo aliyetamba na filamu ya 'Chumo' aliyoigiza na Yusuph Mlela na Jokate Mwegelo, alikuwa hajaoa wala kuwa na mtoto, ingawa alikuwa na mchumba aliyekuwa akidai angemuoa muda muafaka ungefika..
Sharo Milionea aliyekunwa na Joti na Kanumba kwa hapa nchini, alisema kama msanii nyota amekuwa akipata usumbufu toka kwa wanawake wanaomtaka kimapenzi, ila alidai hutumia busara kuwaepa akitambua kuwa sio wote wanampenda, pia kuwepo Ukimwi.
"Hili la Ukimwi, kila mtu analitambua, ni wajibu wa kila mtu ndani ya jamii kuepukana nao, ili kutimiza ndoto za maisha yao, kama ninavyofanya mimi," alisema.
Kuhusu wasanii nyota kujitumbukiza kwenye skondo na matendo maovu, Sharo Milionea, alisema ni vigumu kuwazuia wanaofanya, ila aliwataka watambue kuwa wao ni vioo vya jamii na wenye familia nyuma zao, hivyo wajiheshimu na wajithamini kusudi nao wathaminiwe na jamii.
"Kama mtu hajiheshimu au kujithamini ni vigumu kuheshimiwa na jamii, kitu hicho ndicho kinachochangia fani yetu kuonekana ya kihuni wakati sivyo ilivyo," alisema.
Wakati mauti yanamkumba msanii huyo alikuwa ametoka kuingia mkataba wa kutangaza huduma za simu za mkononi za Airtel na kuuza sura katika matangazo ya bidhaa za kampuni za Bakhresa hasa soda za Azam akishirikiana na King Majuto.
Sharo atakumbukwa daima kwa ucheshi wake na kujichanganya na watu licha ya umaarufu alionao, hakuwahi kunata au kujiona kama baadhi ya watu wa kariba yake.
Kifo cha Shario Milionea kimekuja wakati wadau wa sanaa wakiendelea kuomboleza vifo wa wakali wengine waliofariki hivi karibuni, kuanzia Steven Kanumba, Mlopelo, Mariam Khamis, John Maganga.
Kwa hakika tuliwapenda wenzetu, lakini Mwenyezi Mungu aliwapenda zaidi. Jina la Allah Lihimidiwe kwani kazi yake haina makosa.

No comments:

Post a Comment