STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, November 18, 2011

Mabondia 10 kuwasindikiza Nassib vs Kariuki


BINGWA wa zamani wa Dunia wa World Boxing Forum, Juma Fundi na Rashid Ally ni miongoni mwa mabondia watakaolisindikiza pambano la kimataifa kati ya Nassib Ramadhan 'Manny Pacquiao wa Tz' dhidi ya Anthony Kariuki kutoka Kenya.
Nassib anayeshikilia kwa sasa taji la dunia la World Boxing Forum baada ya kumvua Juma Fundi Mei mwaka huu, atapigana na Karikuki katika pambano litaklofanyika siku ya kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru, Desemba 9 kwenye ukumbi wa DDC Keko, jijini Dar es Salaam.
Mratibu wa pambano hilo, Pius Agathon, aliiambia MICHARAZO kwamba Fundi na Ally ni kati ya mabondia 10 watakaopanda ulingoni kusikindikiza pambano hilo la raundi 10 lisilo la ubingwa kati ya Nassib na Kariuki.
Agathon, alisema Fundi atapigana siku hiyo na Juma Seleman katika pambano la raundi sita la uzani wa kilo 51, Fred Sayuni dhidi ya Bakar Dunda na Ramadhani Kumbele ataonyeshana kazi na Shabaan Madilu.
"Mipambano mingine siku hiyo itakuwa ni kati ya Rashid Ally atakayepigana na Daud Mhunzi katika uzito wa kilo 57 na Faraji Sayuni ataumizana na Alfa George ndipo Nassib atakapopanda ulingoni kupigana na Kariuki katika uzani wa Fly," alisema.
Mratibu huyo alisema maandalizi ya jumla ya mapambano hayo yanaendelea vema ikiwemo kumalizana na mabondia wote ambao kwa sasa wanaendelea kujifua kwa mazoezi tayari kuonyeshana ubabe siku hiyo kwenye ukumbi huo wa DDC Keko.
Aliongeza lengo la michezo hiyo mbali na kuwaweka fiti mabondia hususani Nassib ambaye mwakani atalitetea taji lake la World Boxing Forum, pia ni maalum kwa ajili ya kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru.
"Tumeandaa michezo hii ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru sambamba na kumuandaa vema Nassib kabla ya kulitetea taji lake mwakani," alisema.

Mwisho

Niyonzima aikana Simba, awatroa hofu Jangwani



KIUNGO nyota wa kimataifa wa klabu ya Yanga, Haruna Niyonzima 'Fabregas' amewatoa hofu wanayanga kwa kuweka wazi kwamba hana mpango wa kujiunga na mahasimu wao Simba kwa kile alichodai anaridhika na maisha yake Jangwani.
Pia, kiungo huyo alisema kama ni kuondoka Yanga, basi sio kwa kujiunga na klabu nyingine ya Tanzania, bali ni kwenda kucheza soka la kulipwa Ulaya, ikiwa ni kati ya ndoto anazoota kila siku maishani mwake.
Akizungumza moja na kipindi cha michezo cha Radio One 'Spoti Leo', Niyonzima, amedai kushangazwa na taarifa kwamba Simba inamnyemelea wakati hajawahi kufanya mazungumzo yoyote na uongozi wa klabu hiyo au mtu yeyote.
Kiungo huyo aliyetua Jangwani akitokea klabu ya APR ya Rwanda, alisema mbali na kutowahi kuzungumza na mtu yeyote ili kujiunga Simba, lakini yeye binafsi hana mpango huo kwa vile anaridhika na maisha yake ndani ya klabu yake ya sasa.
"Aisee sina mpango wa kuihama Yanga na hivyo nawataka wanayanga wasiwe na hofu nadhani yanayosemwa yanatokana na kuvutiwa na soka langu, lakini sijawahi kuzungumza na mtu yeyote kujiunga Simba," alisema.
"Pia kwa namna mambo yangu yanayotekelezwa ndani ya Yanga na mie kuitumikia klabu hiyo kwa mafanikio, sioni sababu ya kutaka kuhama na kama ikitokea hivyo basi ni kwenda zaidi ya Tanzania, lakini sio kujiunga Simba," alinukuliwa Niyonzima.
Nyota huyo anayeichezea pia timu ya taifa ya nchi yake ya Rwanda 'Amavubi' alisema ingawa yeye ni mchezaji na lolote linaweza kutokea, lakini hadi wakati akizungumza hakuwa amewaza lolote juu ya kuiacha Yanga aliyosaini nayo mkataba wa miaka miwili.
Kwa wiki kadhaa sasa kumekuwa na taarifa kwamba Simba imekuwa ikimwinda kiungo huyo ambaye soka lake limewakuna wengi tangu atue Jangwani, ikiwa kama jibu la watani zao, Yanga kudaiwa kumnyatia mshambuliaji wao, Felix Sunzu.
Tetesi hizo za Yanga na Simba kubadilishana wachezaji zimekuja wakati mbio za usajili wa dirisha dogo nchini likizidi kupambana moto.

Mwisho

Mkwasa, Julio wambeep Poulsen kwa Boban



MAKOCHA wapya wa timu ya taifa ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, Charles Boniface Mkwasa na Jamhuri Kihwelu 'Julio' wamembeep, kocha mkuu wa timu ya taifa, Taifa Stars, Jan Poulsen bada ya kumuita kikosi kiungo wa wa Simba, Haruna Moshi 'Boban'.
Boban na mshambuliaji mpya wa Azam, Gaudence Mwaikimba, wameitwa katika kikosi cha Kilimanjaro Stars kitakachotetea ubingwa wake katika mashindano ya Kombe la Chalenji yatakayoanza Novemba 25 jijini Dar es Salaam.
Baada ya Boban kusajiliwa na Simba na kuanza kuitumikia kwenye fainali zilizopita na Kombe la Kagame mwaka huu, kocha wa Taifa Stars, Jan Poulsen, alimuita katika kikosi cha vijana wa umri chini ya miaka 23 kilichokuwa na mechi mbili za kirafiki na Shelisheli jijini Arusha lakini kiungo huyo alikacha wito huo na hivyo kuendelea kuwa nje ya timu hiyo kwa muda mrefu.
Akitangaza kikosi cha nyota 28 jana, kocha msaidizi wa Kili Stars, Jamhuri Kihwelu 'Julio' alisema kuwa kikosi chake kitaanza mazoezi leo kwenye Uwanja wa Karume na lengo la kuita wachezaji hao ni kuwapima zaidi na baadaye watachujwa na kubaki 20 kama kanuni za usajili wa mashindano hayo zinavyoeleza.
Julio alisema kuwa ameita wachezaji wengi chipukizi ili kuwapa nafasi zaidi ya kujifunza na kuitumikia nchi yao kwa bidii huku pia akiwaita wazoefu ili waweze kupambana na changamoto kutoka kwa timu pinzani kwenye michuano hiyo.
"Tunawaomba Watanzania wajue kuwa hii ni timu yao, watupe ushirikiano, waipende na kuishangilia ili sisi wazawa tuweze kulitetea kombe, tunaahidi kupambana na kukibakisha kikombe," alisema kocha huyo.
Alisema kuwa wanaahidi kupambana na wachezaji wasio na nidhamu ili wajirekebishe na hatimaye kuitumikia vyema nchi yao kutokana na uwezo wa kucheza soka walionao.
"Hii ni timu ya wote na kwa kuwa mpira hauchezwi chumbani, hata Saidi Maulidi (SMG) kama anaweza kuja aje katika mazoezi apambane na akionyesha anaweza tutamchukua katika kikosi cha watu 20," aliongeza Julio kuhusiana na uteuzi wa wachezaji wanaocheza nje ya nchi.
Kikosi kamili cha timu hiyo kilichoitwa jana ambacho nahodha wake atakuwa ni kipa Juma Kaseja kutoka Simba ni pamoja na Deo Munishi 'Dida' kutoka Mtibwa Sugar, Shabani Kado (Yanga), huku mabeki wa pembini wakiwa ni Shomari Kapombe (Simba), Godfrey Taita (Yanga), Juma Jabu (Simba) na Paul Ngelema (Ruvu Shooting).
Mabeki wa kati walioitwa ni Juma Nyoso (Simba), Said Murad (Azam), Erasto Nyoni (Azam) na Salum Telela (Moro United) huku viungo wakiwa ni Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), Ibrahim Mwaipopo (Azam), Nurdin Bakari (Yanga), Mwinyi Kazimoto (Simba), Boban, Ramadhan Chombo (Azam), Rashid Yusuf (Coastal Union), Jimmy Shogi (JKT Ruvu Stars) na Mohamed Soud (Toto Africans).
Washambuliaji walioitwa ni Mrisho Ngassa (Azam), Mbwana Samatta (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo), Mwaikimba (Moro United), John Bocco (Azam), Thomas Ulimwengu (TP Mazembe ), Hussein Javu (Mtibwa Sugar), Daniel Reuben (Coastal Union) na Nizar Khalfan wa Vancouver Whitecaps ya Canada.
Kilimanjaro Stars itaanza kampeni ya kutetea ubingwa wake siku moja baada ya kwanza ya michuano hiyo kwa kuumana na Rwanda 'Amavubi' kwenye Uwanja wa Taifa.

Jailan, Matimbwa kuonyeshana kazi Morogoro

BONDIA mahiri wa ngumi za kulipwa wa mkoa wa Morogoro, Mohamed Jeilani anatarajiwa kupanda ulingoni kuonyeshana ubabe na Mohammed Matimbwa wa Dar katika pambano lisilo la mkanda litakalofanyika siku ya Desemba 3, mjini Morogoro.
Pambano hilo la raundi nane litafanyika kwenye ukumbi wa Urafiki na litasindikizwa na michezo kadhaa ya utangulizi.
Mkurugenzi wa kampuni ya BS Promotion, waandaaji wa pambano hilo, Daudi Julian aliiambia MICHARAZO kwamba mchezo huo ni wa uzani wa kilo 60 na lengo lake ni kuhamamisha mchezo wa ngumi mkoani humo.
Julian, alisema maandalizi ya pambano hilo na michezo yote ya utangulizi yanaendelea vema na tayari mabondia wote watakaopigana siku hiyo wanaendelea kujifua kujiweka tayari kuonyeshana kazi ulingoni.
Aliwataja mabondia watakaowasindikiza Jailan na Matimbwa siku ya pambano lao ni pamoja na Maneno William ‘Chipolopolo’, Nassib Msafiri ‘Ngumi Nondo’ na Said Idd ‘Simple Boy’ watachapana na mabondia kutoka Dar es Salaam na Tanga.
"Kampuni yetu imeandaa pambano la ngumi la kirafiki kati ya Mohammed Jailan dhidi ya Mohammed Matimbwa litakalofanyika Desemba 3 mwaka huu na kusindikizwa na michezo mingine kati ya mabondia wa Moro dhidi ya wale wa Dar na Tanga," alisema.
Alisema mbali ya pambano hilo, kampuni hiyo pia inatarajia kuandaa mapambano mengine ya ngumi , siku ya kusherehekea sikukuu ya X-mass ambapo mabondia wa mkoa wa Morogoro, Dar es Salaam, Dodoma na Tanga wataonyeshana kazi.
Julian ametoa wito kwa wafadhili wa michezo kujitokeza na kudhamini mapambano mbalimbali yatakayoandaliwa na kampuni yake kwa lengo la kuhamasisha mchezo huo mkoani humo.

Mwisho

Banka afichua kilichompeleka JKT Ruvu



KIUNGO mahiri wa zamani wa klabu za Simba na Yanga, Mohammed Banka ametua JKT Ruvu akisema ni klabu aliyokuwa akiiota kwa muda mrefu kutokana na na kuwa na soka la kuvutia na lenye ushindani uwanjani.
Aidha amekanusha kuwahi kufanya mazungumzo na viongozi wa timu za Coastal Union na Moro United ili ajiunge navyo kama ilivyokuwa ikiripotiwa.
Akizungumza na MICHARAZO Banka, alisema tayari ameshamwaga wino wa kuichezea JKT kwa ajili ya duru la pili la Ligi Kuu Tanzania Bara na amefurahi mno.
Banka, alisema soka la JKT ndilo lililomsukuma kujiunga akiamini namna ya uchezaji wa klabu hiyo na aina ya wachezaji anaoungana nao itamsaidia kurejea upya katika soka la Tanzania baada ya nusu msimu kuwa nje ya dimba kutokana na mzozo wake na Simba.
"Nimemwaga wino wa kuichezea JKT Ruvu, kikubwa kilichonivutia kujiunga na timu hii ni aina ya soka inalocheza na wachezaji iliyonayo, ni kati ya klabu nilizokuwa naota kuzichezea kwa vile ni timu yenye malengo na ushindani wa kweli dimbani," alisema Banka.
Alipoulizwa imekuwaje amezitosa Coastal Union na Moro United ambazo zimekuwa
zikijinasibu kumnyemelea, Banka, alisema zaidi ya kusikia kwenye vyombo vya habari
hakuwahi kufuatwa na kiongozi yeyote wa timu hizo kuzungumza nao.
"Ndugu yangu sijawahi kufuatwa wala kuwasiliana japo kwa simu kuzungumza kuhusu
kujiunga na klabu hizo, zaidi ya kusikia kwenye vyombo vya habari kwamba natakiwa nazo, ila JKT Ruvu kabla ya kujiunga nilishafanya nao mazoezi weakati duru la kwanza likielekea ukingoni," alisema Banka.
Banka, aliyewahi kuichezea Moro United na aliyekuwa mchezaji wa Simba kabla ya kuigomea klabu hiyo kumtoa kwa mkopo kwa klabu ya Villa Squad ni miongoni mwa wachezaji watano wapya waliongezwa katika klabu hiyo ya JKT Ruvu.
Wengine waliotua JKT Ruvu ni George Mketo na Paul Ngahyoma toka Kagera, Said Hamis toka Polisi Morogoro na Bakar Kondo aliyerejeshwa kikosini.

Mwisho

Bondia Moro amtaka Miyeyusho

BONDIA machachari wa ngumi za kulipwa mkoani Morogoro, Maneno William 'Chipolopolo' ameibuka na kudai anamtaka bingwa wa UBO-Mabara, Francis Miyeyusho wa Dar es Salaam, ili apigane nae.
Chipolopolo aliyejipatia umaarufu mkubwa mkoani humo, kutokana na uwezo wake wa kurusha makonde makali ulingoni, hivi sasa yuko katika mazoezi makali chini ya mwalimu Boma Kilangi.
Akizungumza na blog hii kutoka Morogoro, bondia huyo alisema amejipanga vizuri kufanya maajabu katika mchezo wa ngumi huku kiu yake kubwa ikiwa ni kuchapana na Miyeyusho maarufu kama 'Chichi Mawe'.
Chipolpolo, alisema anamuona Miyeyusho ni bondia wa kawaida na kwamba atapigika kirahisi licha ya kufanya vizuri katika mchezo huo katika siku za hivi karibuni.
Alisema, ili kutimiza dhamira yake yupo tayari kupanda ulingoni wakati wowote kuzipiga na Miyeyusho kama atatokea promota wa kuwaandalia pambano hilo.
Bondia huyo wa Morogoro alisema licha ya Miyeyusho kumchapa Mbwana Matumla hivi karibuni katika ukumbi wa Diamond Jubilee Dar es Salaam, ni lakini kwake lazima apate kipigo.
"Nipo fiti, najiamini na nafikiri sasa ni wakati wa kuchapana na Miyeyusho na kizuri zaidi ni bondia wa uzito wangu," alisema.
Chipolopolo alisema hachagui mahali pa kupambana na bondia huyo na kwamba yupo tayari kuvaana naye hata jijini Dar es Salaam.
MIcharazo lilijaribu kumsaka Miyeyusho kwa njia ya simu kupata maoni yake juu ya tambo za bondia huyo wa Morogoro, lakini hakuweza kupatikana.

Mwisho

Saturday, November 12, 2011

Maugo kuweka kambi Mwanza kumwinda Mjerumani



BONDIA machachari wa ngumi za kulipwa nchini, Mada Maugo anatarajia kuingia kambini jijini Mwanza, kujiandaa na pambano lake la kimataifa la kuwania ubingwa wa IBF dhidi ya Mjerumani Rico Nicovic atakayepigana nae Desemba 26 jijini humo.
Maugo ameiambia MICHARAZO kuwa, anatarajia kuondoka jijini Dar es Salaam wiki ijayo kwenda kuweka kambi jijini Mwanza tayari kumkabili mpinzani wake huyo katika pambano litakalofanyika kwenye uwanja wa CCM Kirumba.
Bondia huyo alisema kambi na pambano hilo la kimataifa litakalosimamiwa na Shirikisho la Ngumi za Kulipwa nchini, vyote vimeandaliwa na kugharamiwa na Mbunge wa Jimbo la Rorya, Lameck Airo 'Obama'.
"Maandalizi ya pambano langu yanaendelea vema nikiwa nimeshanza kuzungumza na mabondia watakaosindikiza siku hiyo na wiki ijayo natarajia kuondoka Dar kuelekea Mwanza kuweka kambi kwa ajili ya pigano hilo," alisema Maugo.
Aliongeza pambano lake na Mjerumani huyo, litakuwa la raundi 12 katika uzani wa kilo 72.5 na watasindikizwa na michezo zaidi ya mitano itakayowahusisha pia mabondia wakongwe nchini akiwemo bingwa wa zamani wa dunia wa WBU, Rashid Matumla.
Maugo alisema Matumla atapigana na bondia kutoka Uganda, huku Emma Kichere na mabondi wengine wa kanda ya Ziwa watapanda ulingoni kuonyeshana kazi sambamba na kuhamasisha mchezo katika kanda hiyo.
"Mkongwe Matumla atakuwepo kunisindikiza siku ya pambano langu na Nicovic, kuba analofanya mfadhili wangu, yaani Mbunge wa Rorya ni kuhamasisha ngumi katika kanda ya ziwa," alisema Mada.
Maugo, hivi karibuni alipata ushindi wa KO kwa kumpiga Joseph Odhiambo katika pambano lisilo la ubingwa ikiwa ni baada ya kutoka kupokea kipigo toka kwa Francis Cheka katika pambano la kuwania taji la UBO-Inter Continental.

Mwisho

Miyeyusho aota ubingwa wa dunia



BONDIA machachari, Francis Miyeyusho anayeashikilia taji la UBO-Mabara baada ya kumvua aliyekuwa akilishikilia, Mbwana Matumla, aliyemtwanga hivi karibuni alisema kiu yake kubwa kwa sasa ni kuona anautwaa ubingwa wa dunia katika mchezo huo.
Miyeyusho anayefahamika zaidi kama 'Chichi Mawe', alisema kumvua taji Mbwana ni furaha kubwa, lakini hajaridhika hadi atakapotwaa ubingwa wa dunia katika mchezo huo kama wanavyofanya mabondia wengine duniani.
Bondia huyo, alisema haitakuwa na maana yoyote ya ushindi wake kwa Mbwana kama ataishia kwenye taji hilo la Mabara, ndio maana anasisitiza angependa kuona anafika mbali katika mchezo huo kwa kutwaa ubingwa wa dunia.
"Kiu yangu kubwa kwa sasa ni kuona natwaa ubingwa wa dunia, itakuwa furaha kubwa kuliko hii ya kumvua taji Golden Boy, ambaye ni mmoja kati ya mabondia ninaowaheshimu kwa mafanikio yao nchini kama ilivyo kwa kaka yake," alisema.
Miyeyusho alimtwanga Mbwana kwa pointi katika pambano lao lililofanyika Oktoba 30 kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam likiwa ni pambano la tatu kati yao kukutana katika mchezo huo.
Katika mapambano yao ya awali yaliyochezwa Februari 21, 2004 na Januari 17, 2009, Miyeyusho alichezea kichapo toka kwa Mbwana.
Wakati huo huo, bingwa anayeshikilia taji la dunia la World Boxing Forum, Nassib Ramadhan anatarajiwa kupanda ulingoni Desemba 9 kuzipiga na mkenya Anthony Kariuki katika pambano litakalofanyika kwenye ukumbi wa DDC Keko.
Mratibu wa pambano hilo, Pius Aghaton alisema pambano hilo la raundi 10 la uzito wa fly, litasindikizwa na michezo kadhaa ya utangulizi na lengo kubwa ni kumuandaa Nassib kwa pambano la kutetea taji lake hilo analoshikilia baada ya kumvua aliyekuwa bingwa wake, Juma Fundi, katika pambano lililofanyika nchini Mei mwaka huu.

Coastal yawafuata Banka, Chuji Dar




UONGOZI wa klabu ya soka ya Coastal Union ya Tanga, imewafuata viungo nyota wa zamani wa Simba na Yanga, Mohammed Banka na Athuman Idd 'Chuji', ikipuuza taarifa kwamba Chuji ameamua kurejea Yanga kwa duru lijalo la Ligi Kuu Tanzania.
Mwenyekiti wa timu hiyo, Ahmed Aurora, alisema wanaamini Chuji ataichezea timu yao kama itakavyokuwa kwa Mohammed Banka na Ally Ahmed Shiboli ambao imekuwa ikiwanyemelea kukiimarish kikosi chao kwa duru hilo lijalo.
Aurora, alisema alikuwa akijiandaa kuja Dar ili kuonana na wachezaji hao watatu inayotaka kuwasajili kwenye dirisha dogo linalotarajiwa kufungwa Novemba 30.
"Klabu yetu bado inawahitaji wachezaji hao ili kuisaidia katika duru la pili na najiandaa kuja huko, licha ya kwamba nimeshtusha kusikia Chuji ametua Yanga, wakati tayari tulishaanza mazungumzo nae," alisema.
Aurora alisema hata kama Chuji atakuwa ametua Yanga (ingawa Yanga imemruka kimanga) bado wao watamfuata kuzungumza nae kabla ya kumsainisha mkataba wa kuicheza Coastal katika duru la Pili litakaloanza Januari mwakani.
Mbali na kuwawinda wachezaji hao, timu hiyo pia imetangaza kuwarudisha kundi nyota wake wa kimataifa, Mkenya Edwin Mukenya na Wanigeria wawili, Felix Amechi na Felix Amechi na Samuel Temi ambao walikuwa kwenye orodha ya usajili wa timu hiyo kabla ya kukwamba kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wa pande mbili.
Coastal iliyorejea Ligi Kuu msimu huu ikitokea Daraja la Kwanza na timu nyingine tatu za Oljoro JKT, Moro United na Villa Squad, imemaliza duru la kwanza ikiwa katika nafasi tatu za kwanza toka mkiani baada ya kujikusanyia pointi 11 kwa michezo 13.

Taifa Stars yatakata Chad



Na Maulidi Kitenge, Chad
USHIRIKIANO wa wachezaji waliotokea benchi, Nurdin Bakari na Thomas Ulimwengu katika dakika za lala-salama uliipa Taifa Stars mwanzo mzuri wa mechi za hatua ya mchujo za kuelekea kwenye hatua ya makundi ya kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia 2014 kufuatia ushindi wa 2-1 ugenini kwa Chad jana.
Kiungo wa Yanga, Nurdin, aliyeingia katika kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Abdi Kassim anayecheza soka la kulipwa nchini Vietnam, aliifungia Stars goli la ushindi katika dakika ya 82 akitumia pasi ya mshambuliaji wa TP Mazembe ya DRC, Ulimwengu, ambaye pia aliingia katika kipindi cha pili kuchukua nafasi ya nyota mwenzake wa klabu hiyo ya Congo, Mbwana Samatta.
Katika mechi hiyo iliyofanyika kwenye Uwanja wa Idriss Mahamat Ouya mjini N'djamena, Stars walitangulia kupata bao la mapema katika dakika ya 11 kupitia kwa Ngassa aliyemalizia kiufundi pasi ya kiungo anayecheza soka la kulipwa nchini Canada, Nizar Khalfan.
Hata hivyo, wenyeji walihitaji dakika moja tu kusawazisha goli hilo walilopata kupitia kwa mshambuliaji wao anayecheza soka la kulipwa katika Ligi Daraja la Pili Ufaransa (Ligue 2) ya Club Laval B, Mahamat Labbo katika dakika ya 12 na kufanya matokeo ya 1-1 hadi wakati wa mapumziko.
Wakati mechi ikielekea ukingoni na wenyeji wakiamini kwamba wangeweza kupata angalau sare, Nurdin aliifungia Stars goli la pili na la ushindi katika dakika ya 80 lililoeafanya mashabiki wa Chad waliokuwa wamejaa uwanjani kuanza kuondoka kimyakimya.
Stars itarejea kifua mbele kesho kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere lakini itahitaji kutoruhusu kipigo katika mechi yao ya marudiano Jumanne kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kama Stars itasonga mbele, itatinga katika Kundi C la kuwania kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwaka 2014 nchini Brazil, ambapo watajumuika timu ngumu za Ivory Coast, Morocco na Gambia.
Kocha wa Stars, Jan Poulsen aliwapongeza wachezaji wake baada ya mechi hiyo lakini alisema kazi bado haijamalizika na wanahitaji umakini mkubwa ili kusonga mbele.
Kikosi cha Stars jana kiliundwa na Juma Kaseja, Shomari Kapombe, Idrisa Rajab, Agrey Morris, Juma Nyoso, Shaban Nditi, Henry Joseph, Abdi Kassim/ Nurdin Bakari, Nizar Khalfan, Mrisho Ngassa, Mbwana Samatta/ Thomas Ulimwengu.

BFT yapiga 'dochi' kozi ya makocha


KOZI ya ukocha wa ngumi ngazi ya kimataifa, iliyoandaliwa na Shirikisho la Ngumi za Ridhaa nchini, BFT ikishirikiana na Kamati ya Olimpiki Tanzania, TOC, imekwama kuanza leo Jumamosi kama ilivyopangwa badala yake sasa ifanyika Alhamisi ijayo.
Kozi hiyo itakayoshirikisha washiriki 30 watakaonolewa na Mkufunzi wa Kimataifa kutoka Algeria, ilikuwa imepangwa kuanza leo mjini Kibaha, lakini BFT imetoa taarifa kwamba imesogezwa mbele kutokana na kuchelewa kwa mkufunzi huyo.
Katibu Mkuu wa BFT, Makore Mashaga, alisema mkufunzi huyo, Azzedin Aggoune, aliwatumia taarifa za kupatwa na dharura na hivyo kutoweza kuwasili jana Ijumaa kama alivyokuwa amepanga ambapo sasa ameahidi kuwasili siku ya Jumatano..
Mashaga alisema kutoka na dharura hiyo iliyompata mkufunzi huyo wameona ni vema kuahirisha kozi hiyo na kutoa fursa kwa makocha walioteuliwa kushiriki kozi hiyo kushuhudia michuano ya ngumi ya Kova inayoendelea jijini Dar es Salaam.
"Ile kozi ya kimataifa ya ukocha wa ngumi iliyokuwa ianze Novemba 12-18 mjini Kibaha, imekwama kuanza kutokana na mkufunzi wa kimataifa toka Algeria kupatwa na dharura na kuchelewa kuja, sasa itaanza Novemba 17 huko huko Kibaha," alisema.
Mashaga alisema kozi hiyo inayotambuliwa na Shirikisho la Ngumi la Kimataifa, AIBA, itafungwa rasmi Novemba 25, ambapo washiriki watatunukiwa vyeti pamoja na wasifu wao kuwekwa kwenye database ya shirikisho hilo ili kuwaweza kutumika na kushiriki michuano yoyote ya kimataifa ya ngumi popote duniani.
Mmoja wa washiriki wa kozi hiyo, Rajab Mhamila 'Super D' alisema amefurahi kuteuliwa kushiriki kozi hiyo, akiamini itamsaidia kumpa ujuzi na kumjenga zaidi katika taaluma hiyo ya ukocha aayoifanya katika klabu za Ashanti na Amana zote za Ilala.

Mwisho

Matumla, Oswald kula X-mass ulingoni


MABONDIA wakongwe wa ngumi za kulipwa nchini, Rashid Matumla 'Snake Man' na Maneno Oswald 'Mtambo wa Gongo' wanatarajia kula Xmass wakiwa ulingoni watakapochapana katika pambano lisilo la ubingwa litakalochezwa jijini Dar es Salaam.
Wakongwe hao watapigana kwenye pambano la uzani wa Middle la raundi 10 litakalofanyika kwenye ukumbi wa Heinkein, Mtoni Kijichi na kusindikiwa na michezokadhaa ya utangulizi.
Kwa mujibu wa waratibu wa pambano hilo kampuni ya Adios Promotion kupitia afisa habari wao, Mao Lofombo ni kwamba kabla ya Matumla na Oswald kupanda ulingoni kuonyeshana kazi, mabondia Rashidi Ally na Hassan Sweet watapimana ubavu.
Lofombo alisema michezo mingine itawakutaniosha Kalulu Bakari dhidi ya Athuman Kalekwa na Shabani Kazinga ataonyeshana kazi na Kashinde.
Pambano la la nne kuwakutanisha mabondia mabingwa wa zamani, litafanyika huku kila mmoja akiwa na matokeo tofauti katika michezo yao ya mwisho ambapo Oswald alipigwa na Mada Maugo, wakati Matumla alimshinda Mkenya Ken Oyolo.
Katika michezo yao mitatu iliyopita, Matumla alimshinda Oswald mara mbili moja akimpiga kwa KO mnamo Oktoba 3, 2001 na jingine kwa pointi Oktoba 28, 2006 huku alikubali kichapo cha pointi mbele ya mpinzani wake Februari 4, 2001.
Tayari mabondia wote wameshaanza kutambiana juu ya pambano hilo, kila mmoja akijinasibu kutaka kuibuka na ushindi ili kulinda hadhi yake pamoja na kudhihirisha bado wamo katika mchezo huo licha ya umri kuwatupa mkono.
Matumla aliyewahi kuwa bingwa wa dunia wa WBU, kwa sasa ana umri wa miaka 43 miaka miwili zaidi ya mpinzani wake mwenye miaka 41 na mwenye rekodi ya kucheza mechi 64 akishinda 37, 26 kwa KO, akipigwa mara 24, 9 kwa KO na kupata sare tatu.
Mpinzani wake rekodi yake pia inaonyesha kapanda ulingoni mara 64 ameshinda mara 46 (33 kwa KO) amepoteza 16 (5 kwa KO) na kupata sare mbili.
Kwa kuangalia rekodi za mabondia hao ni wazi pambano lao lijalo litakuwa lenye mpinzani mkali kila mmoja akipenda kushinda ili kuendeleza rekodi aliyonayo katika mchezo huo wanaoendelea kuucheza karibu miaka 30 sasa.

Mwisho

Jumbe, atambia Shoka la Bucha

UONGOZI wa bendi ya Talent umedai kuwa, albamu yao mpya inayoendelea kuandaliwa itakuwa moto kuliko ile ya kwanza ya 'Subiri Kidogo' ambayo inaendelea kubamba sokoni.
Mkurugenzi wa bendi hiyo, Husseni Jumbe, alisema maandalizi wanayofanya kuipika albamu yao ya pili itakayofahamika kama 'Shoka la Bucha' ni ya aina yake kitu kinachompa jeuri kwamba itafunika kuliko ile ya awali.
Jumbe, alisema tayari wamesharekodi nyimbo nne kati ya sita za albamu hiyo katika studio za Sound Crafters na mara watakapomaliza mbili za mwisho wataanza kurekodi video kabla ya kufanya uzinduzi na kuziingiza sokoni mapema mwakani.
"Nadhani Shoka la Bucha itafunika zaidi kuliko Subiri Kidogo kwa namna tunavyoiandaa kwa sasa tukiwa tumesharekodi nyimbo nne kati ya sita," alisema.
Jumbe, alisema tayari baadhi ya nyimbo hizo zilizorekodiwa zimeshasambazwa kwenye vituo vya redio ili kurushwa hewani.
Alizitaja nyimbo zilizorekodiwa hadi sasa ni Kilio cha Swahiba, Shoka la Bucha, Kiapo Mara Tatu na Jipu la Moyo.
Aliongeza, wapo kwenye mipango ya kufanyta ziara mikoani kwa nia ya kujitangaza zaidi sambamba na kuitambulisha albamu zao mbili, ikiwemo hiyo inayomaliziwa kurekodiwa.

TMK waumwa kichwa videoni




KUNDI la muziki wa kizazi kipya la TMK Wanaume Family, limeachia mtaani video yake mpya ya 'Kichwa Kinauma', ikiwa ni maandalizi ya kupakuliwa albamu mpya ya kundi hilo.
Aidha, kundi la Tip Top Connection kesho linatarajia kuadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwake kwa wasanii waliowahi kupitia katika kundi hilo na waliopo sasa kujumuika pamoja katika onyesho litakalofanyika Maisha Club Masaki, jijini Dar es Salaam.
Meneja wa kundi la TMK Wanaume Family, Said Fella 'Mkubwa Fella', alisema video ya wimbo huo ulioimbwa na wasanii Mheshimiwa Temba na Said Chegge, ni kati ya maandalizi ya kundi lao.
Mkubwa Fella alisema kukamilika kwa video ya wimbo huo ni mwanzo wa maandalizi ya upigwaji video wa nyimbo nyingine zitakazokamilisha albamu yao itakayokuwa na vibao 10 ambayo hata hivyo, hakuweza kuitaja jina lake.
"Mkubwa tumekamilisha video ya wimbo wetu mpya wa 'Kichwa Kinauma' tukiwa mbioni kufyatua video za nyimbo zetu nyingine za kukamilisha albamu ijayo ya TMK," alisema.
Mkubwa aliongeza sambamba na hilo, upande wake albamu yake ya miondoko ya taarab ya 'Kunguni Kunguni', ipo katika hatua ya mwisho kuachiwa hadharani ikiwa na nyimbo sita.
Nyimbo za albamu hiyo ya Mkubwa Fella ni 'Kusonakusonona', 'Simuachi', 'Midomo Imewashuka', 'Mchakamchaka', 'Sijapopoa Dodo' na 'Kimodern Modern'.
Nalo kundi la Tip Top Connection, moja ya makundi yanayotamba nchini, kesho litafanya onyesho maalum la kuadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwake ambalo litapambwa na burudani mbalimbali ikiwemo soka na muziki utakaotumbuizwa na wasanii mbalimbali.
Onyesho hilo litawajumuisha wasanii wote waliowahi kupitia kundi hilo na wale waliopo sambamba na wengine walioalikwa kuwapiga tafu katika maadhimisho hayo yatakayofanyika kwenye ukumbi wa Maisha Club, Masaki jijini Dar es Salaam.

Young D, Aslay wote boda kwa boda




WASANII wanaokuja juu katika anga la muziki wa kizazi kipya nchini, Aslay Isiaka 'Dogo Aslay' na David Genz Mwanjela 'Young D' wanatarajia kuonyesha kazi watakapoungana na wakali wengine wa miondoko hiyo kwenye onyesho maalum litakalofanyika leo jijini Dar.
Dogo Aslay na Young D, wanaowatishia wakongwe wa muziki huo kwa namna ya kasi yao tangu walipoibuka, watashiriki tamasha lililopewa jina la 'Boda kwa Boda Beach Concert' ambalo litafanyikia kwenye ufukwe ya Mbalamwezi.
Mbali na wasanii hao wanaochuana kimuziki sambamba na chipukizi mwingine, Abdulaziz Chende 'Dogo Janja', pia tamasha hilo litawahusisha wakali kama msanii kutoka Kenya, Jaguar anayetamba na nyimbo za 'Kigeugeu' na 'Nimetoka Mbali' alioimba na nyota wa Tanzania, Ambwene Yesaya 'AY'.
Wengine watakaoshiriki tamasha hilo la 'Bodaboda' ni 'Mzee wa Hakunaga' Sumalee, Godzilla wa Salasala, Beca, Reycho, Country Boy & Stamina, na wengineo huku wakinakshiwa muziki huo na DJ Zero.
Kwa mujibu wa waratibu wa onyesho hilo, G5 Click, wakali hao watashirikiana pamoja kuangusha moja moja kuanzia saa moja jioni hadi 'kuchwee' ili kuwapa burudani mashabiki wa muziki wa kizazi kipya watakaoungana kwenye ufukwe huo.
"Ni tamasha la aina yake siku ya Jumamosi (leo) ambapo wasanii chipukizi na wakali wengine akiwemo Mkenya Jaguar watafanya vitu vyao katika ukumbi wa Mbalamwezi Beach Club."

Bundi wa Sikinde kupelekwa Studio

BENDI kongwe za muziki wa dansi nchini, Mlimani Park 'Sikinde' ipo mbioni kuingiza studio kibao kipya cha 'Bundi', ikiwa katika harakati za kufyatua albamu mpya itakayokuwa na nyimbo sita.
Kibao hicho kipya kimetungwa na Abdalla Hemba, mmoja wa waimbaji mahiri wa bendi hiyo ambayo kwa sasa inatamba na wimbo wa 'Jinamizi la Talaka', kinachodaiwa ni 'dongo' kwa mahasimu wao, Msondo Ngoma wanaotamba na kibao cha 'Suluhu'.
Mmoja wa viongozi wa Sikinde, Hamis Milambo, alisema kibao cha 'Bundi', kitarekodiwa wakati wowote kuanzia sasa sambamba na vingine vitakavyokuwa katika albamu yao mpya.
Milambo alisema mbali na Jinamizi la Talaka na Bundi, nyimbo nyingine za albamu hiyo zilizokamilika ni 'Asali na Shubiri' uliotungwa na Shukuru Majaliwa, 'Nitalipa Deni', uliotungwa na bendi mzima ya Sikinde, 'Kilio cha Kazi'-Hassani Bitchuka na 'Nisamehe'-Hemba.
Wakati Sikinde wakijiandaa kuhitimisha albamu yao hivyo, kwa upande wa mahasimu wao, Msondo Ngoma wameibuka na kibao kingine kipya kiitwacho 'La Kuvunda' utunzi wa mkali Shaaban Dede 'Mzee wa Loliondo' ambaye anatamba pia na kibao kiitwacho 'Suluhu'.
Msondo ambao wameanza kurekodi nyimbo zao mpya kwa ajili ya albamu yao mpya, imeachia kibao hicho kipya ikiwa ni maandalizi ya albamu ya mwaka ujao.
Albamu yao ya sasa wanaotarajia kuiingiza sokoni mara itakapokamilika kurekodiwa inatarajiwa kufahamika kwa jina la 'Nadhiri ya Mapenzi' ambayo ni jina la kibao kilichotungwa na Juma Katundu.
Nyimbo nyingine za albamu hiyo na watunzi wake kwenye mabao ni 'Kwa Mjomba Hakuna Urithi (Huruka Uvuruge), Dawa ya Deni (Is'haka Katima 'Papa Upanga), LIpi Jema na Baba Kibene za Edmund Sanga 'Eddo Sanga' na 'Suluhu' (Shaaban Dede).

Mwaikimba aahidi ubingwa Azam






SIKU moja tangu amwage wino wa kuichezea Azam kwa mechi za duru la pili la Ligi Kuu
Tanzania Bara, Mshambuliaji Gaudence Mwaikimba 'Andy Carroll' ameahidi kuipigania klabu hiyo ili iwe bingwa mpya wa soka nchini.
Mwaikimba aliyekuwa akiichezea Moro United, aliyotua mapema msimu huu akitokea Kagera Sugar, alisema anaamini ana deni kubwa la kulipa fadhila ya kuaminiwa na klabu ya Azam kiasi cha kumsajili, ila atakachofanya yeye ni kushirikiana na wenzake kuipa ubingwa msimu huu.
"Kwangu ni furaha kubwa kutua Azam, moja ya klabu zenye malengo na muono wa mbali
katika soka la Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Wajibu wangu kama mchezaji ni kuhakikisha naipigania ifanye vema ikiwemo kuwa mabingwa wapya nchini," alisema.
Mshambuliaji huyo anayeshikilia nafasi ya pili katika orodha ya wafungaji mabao msimu huu, alisema kwa vile karibu wachezaji anayeenda kukutana nao Azam amewahi kucheza nao katika klabu mbalimbali na timu ya taifa, Taifa Stars hana hofu ya kuelewana nao mapema.
"Kwa mfumo wa soka letu toka klabu moja hadi nyingine kufanana, naamini itanichukua
muda mfupi kuzoeana na wenzangu na kubwa nalopenda kuwaahidi mashabiki wa Azam
kwamba watarajie mambo makubwa katika duru lijalo," alisema.
Kuhusu suala la uhakika wa namba kwa nafasi anayocheza ambayo tayari ndani ya Azam
inayo wachezaji nyota kama John Bocco, Mwaikimba alisema hana tatizo lolote kwa vile
anajiamini yeye ni mchezaji mzuri na mwenye uwezo mkubwa ndio maana amesajiliwa Azam.
Nyota huyo aliyewahi kuwika na klabu za Tukuyu Stars, Yanga, Ashanti United na Prisons Mbeya ni mmoja wa wachezaji wapya waliotua Azam ambayo imewatema wachezaji wao wawili wa kimataifa kutoka Ghana, Wahabu Yahya na Nafiu Awudu.
Mwingine aliyesajiliwa Azam katika dirisha hilo dogo ni beki wa zamani wa kimataifa wa Simba, Joseph Owino na huku mshambuliaji Jerry Tegete wa Yanga ni miongoni mwa
wanaowindwa na klabu hiyo.