STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, November 18, 2011

Mkwasa, Julio wambeep Poulsen kwa Boban



MAKOCHA wapya wa timu ya taifa ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, Charles Boniface Mkwasa na Jamhuri Kihwelu 'Julio' wamembeep, kocha mkuu wa timu ya taifa, Taifa Stars, Jan Poulsen bada ya kumuita kikosi kiungo wa wa Simba, Haruna Moshi 'Boban'.
Boban na mshambuliaji mpya wa Azam, Gaudence Mwaikimba, wameitwa katika kikosi cha Kilimanjaro Stars kitakachotetea ubingwa wake katika mashindano ya Kombe la Chalenji yatakayoanza Novemba 25 jijini Dar es Salaam.
Baada ya Boban kusajiliwa na Simba na kuanza kuitumikia kwenye fainali zilizopita na Kombe la Kagame mwaka huu, kocha wa Taifa Stars, Jan Poulsen, alimuita katika kikosi cha vijana wa umri chini ya miaka 23 kilichokuwa na mechi mbili za kirafiki na Shelisheli jijini Arusha lakini kiungo huyo alikacha wito huo na hivyo kuendelea kuwa nje ya timu hiyo kwa muda mrefu.
Akitangaza kikosi cha nyota 28 jana, kocha msaidizi wa Kili Stars, Jamhuri Kihwelu 'Julio' alisema kuwa kikosi chake kitaanza mazoezi leo kwenye Uwanja wa Karume na lengo la kuita wachezaji hao ni kuwapima zaidi na baadaye watachujwa na kubaki 20 kama kanuni za usajili wa mashindano hayo zinavyoeleza.
Julio alisema kuwa ameita wachezaji wengi chipukizi ili kuwapa nafasi zaidi ya kujifunza na kuitumikia nchi yao kwa bidii huku pia akiwaita wazoefu ili waweze kupambana na changamoto kutoka kwa timu pinzani kwenye michuano hiyo.
"Tunawaomba Watanzania wajue kuwa hii ni timu yao, watupe ushirikiano, waipende na kuishangilia ili sisi wazawa tuweze kulitetea kombe, tunaahidi kupambana na kukibakisha kikombe," alisema kocha huyo.
Alisema kuwa wanaahidi kupambana na wachezaji wasio na nidhamu ili wajirekebishe na hatimaye kuitumikia vyema nchi yao kutokana na uwezo wa kucheza soka walionao.
"Hii ni timu ya wote na kwa kuwa mpira hauchezwi chumbani, hata Saidi Maulidi (SMG) kama anaweza kuja aje katika mazoezi apambane na akionyesha anaweza tutamchukua katika kikosi cha watu 20," aliongeza Julio kuhusiana na uteuzi wa wachezaji wanaocheza nje ya nchi.
Kikosi kamili cha timu hiyo kilichoitwa jana ambacho nahodha wake atakuwa ni kipa Juma Kaseja kutoka Simba ni pamoja na Deo Munishi 'Dida' kutoka Mtibwa Sugar, Shabani Kado (Yanga), huku mabeki wa pembini wakiwa ni Shomari Kapombe (Simba), Godfrey Taita (Yanga), Juma Jabu (Simba) na Paul Ngelema (Ruvu Shooting).
Mabeki wa kati walioitwa ni Juma Nyoso (Simba), Said Murad (Azam), Erasto Nyoni (Azam) na Salum Telela (Moro United) huku viungo wakiwa ni Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), Ibrahim Mwaipopo (Azam), Nurdin Bakari (Yanga), Mwinyi Kazimoto (Simba), Boban, Ramadhan Chombo (Azam), Rashid Yusuf (Coastal Union), Jimmy Shogi (JKT Ruvu Stars) na Mohamed Soud (Toto Africans).
Washambuliaji walioitwa ni Mrisho Ngassa (Azam), Mbwana Samatta (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo), Mwaikimba (Moro United), John Bocco (Azam), Thomas Ulimwengu (TP Mazembe ), Hussein Javu (Mtibwa Sugar), Daniel Reuben (Coastal Union) na Nizar Khalfan wa Vancouver Whitecaps ya Canada.
Kilimanjaro Stars itaanza kampeni ya kutetea ubingwa wake siku moja baada ya kwanza ya michuano hiyo kwa kuumana na Rwanda 'Amavubi' kwenye Uwanja wa Taifa.

No comments:

Post a Comment