STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, January 15, 2013

UNAAMINI MAMBO YA UTABIRI? MSOME MAALIM HASSAN YAHYA 





MAALIM  Hassan Yahya Hussein, ameibuka na kupinga vikali utabiri uliotyolewa na Sheikh mmoja kwamba Rais wa mwaka 2015 lazima awe mwanamke akidai ana lengo la kuwakatisha wanaume wanaoota kuwania nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu ujao.
Pia ameweka bayana kwamba ndani ya mwaka huu kutakuwa na vifo vya kushtukiza na vibaya kwa waandishi wa habari, wasanii na watunzi wa vitabu kuliko ilivyokuwa mwaka uliopita.
Maalim Hassani Yahya Husseni mrithi wa aliyekuwa mtabiri maarufu nchini Sheikh Yahya Husseni, aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam majuzi na kudai kwamba  kwa kawaida utabiri uhusisha mwaka husika kwa kila mwaka hata kama mengine hutokea mbele zaidi.
 Alisema kwa mwaka 2013 utabiri utaanza rasmi Machi 21 na kudai kiutabiri huwezi kutoa utabiri katika matukio ya mwaka mmoja mbele, kama ilivyuofanywa na Sheikha Khalifa Khamisi na kudai kitendo chake ni sawa na kutaka kuwakatisha tamaa baadhi ya watu wenye nia ya kutaka kugombea nafasi hiyo  2015.
“Huwezi kutoa utabiri wa miaka miwili mbele hata Sheikh Yahya Hussein mtabiri aliyekuwa akikubalika hakuwahi kufanya hivyo, pia sikubaliani naye kuwa rais ajaye atakuwa mwanamke hata ukiangalia katika njia zetu za utabiri ambazo ni namba zinapingana na hilo”alisema.
Alisema matokeo ya utabiri kama huo ni sawa na uwamuzi wa kuwafungia milango kidemokrasia baadhi ya wanasiasa wenye nia ya kugombea urais mwaka 2015.
“Kuna baadhi ya viongozi wakiwemo Lowassa na Membe wanadaiwa kuwa huenda wakagombea nafasi hiyo, kwa kufanya hivyo itakuwa ni kuwakatisha tamaa”alisema.
Akizungumzia utabiri wa mwaka huu, alisema kuwa kuna viongozi wengi, wabunge, wakuu wa mikoa na wengine watatoa matamshi ya  utatanishi na kusababisha hofu na mitafaruku itakayowafanya watu kupigana.
 Vile vile alisema wapo wabunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wataungana katika masuala ya msingi yatakayohusu utaifa bila kujali itikadi zao za kivyama au kimajimbo.
Maalim Hussein alibainisha kuwa Rais Jakaya Kikwete ataunganisha nchi na kuwa moja yenye uimara wa utaifa kuliko watangulizi wake, akishirikiana zaidi na wanasiasa na viongozi wa dini kuondoa mtikisiko wa uvunjifu wa amani uliyojitokea mwaka jana.
Aidha, Chama kimoja cha siasa kitajitokeza na kitachochea kujitenga na kuunda Taifa lake hata hivyo, kusudio hilo halitafanikiwa kwani litapingwa na Watanzania wote kwa kauli moja na vitendo.
Maalim Hussein pia alisema kutatokea vifo vya ghafla kwa watunzi wa hadithi na vitabu, wandishi wa habari, wanasiasa na wasanii ambapo matukio hayo yatakuwa mabaya zaidi kuliko mwaka jana. 
Akigusia Uchaguzi Mkuu utakaofanyika hivi karibuni   nchini Kenya ambao ni majirani, alisema kuwa Muungano wa CORD, ukiongozwa na Raila Odinga utashinda uchaguzi huo, ambao ana amini utakuwa wa amani na tulivu.
“Ushindi huo utakuja baada ya kuushinda Muungano wa Jubilee ukiongozwa na akina Uhuru Kenyata na Ruto pamoja na ule wa Musalia Mudavadi unaoitwa AMANI”alisema.

ZAWADI ZA EXTRA BONGO KUANZA KUTOLEWA MEEDA CLUB

Ally Choki na Athanas Montanabe wakiwajibika jukwaani

MASHABIKI wa bendi ya Extra Bongo wanatarajiwa kuanza kuzoa zawadi katika shindano lao maalum lililopewa jina la 'Wiki 4 za Zawadi Extra Bongo' siku ya Jumamosi katika onyesho litakalofanyika kwenye ukumbi wa Meeda Club, Sinza Mori, Dar es Salaam.
Shabiki atakaayecheza vema katika onyesho hilo atazoa kitita cha Sh Laki Unusu (150,000) huku wa pili akizoa Laki Moja (100,000) na wa tatu yeye ataambulia Nusu Laki (50,000).
Mkurugenzi wa Extra Bongo, Ally Choki alisema utaratibu huo wa kutioa zawadi hizo kwa mashabiki wao utafanyika katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya jijini Dar es Salaam kwa muda wa mwezi mmoja kuanzia Januari 19.
Choki alisema mara watakapotoka Meeda Extra Bongo watapeleka zawadi kwa mashabiki wao wa Temeke kabla ya kuelekea Kibaha Pwani na mahali pengine watakapoona panafaa kwenda kumwaga zawadi hizo kama njia ya kurudisha shukrani kwa mashabiki wao waliowaunga mkono tangu bendi hiyo irejee upya 2010.
"Tunataka mashabiki wafurahie burudani na pia kuondoka ukumbini wakiwa na zawadi kama ambavyo walivyokuwa wanatuunga mkono tangu tuliporejea kwa awamu ya pili na sasa tukielekea miaka mitatu," alisema.
Choki alisema kila watakapokuwa wakikaribia kumaliza onyesho watawapigia sebene mashabiki wao na kuchuana wenyewe na watawapa fursa mashabiki watazamaji kuteua washindi ambao watapewa chao hapo hapo kabla ya kuelekea mahali pengine hadi watakaporidhika na kusitisha mchuano huo.
Naye kiongozi wa safu ya uenguaji ya Extra Bongo, Hassani Mussa 'Syper Nyamwela' alisema anadhani mchuano huo ni fursa nzuri ya mashabiki wao kuifurahia Extra Bongo sambamba na kutunisha mifuko yao kwa kuonyesha umahiri wao wa kucheza miondoko ya bendi hiyo.
"Badala ya kutozoea kwa muda mrefu kutuona wanenguaji na wana Extra Bongo kwa ujumla kuonyesha umahiri wa kunengua safari hii ni zamu yao kushindana wenyewe kwa wenyewe na kuzoa fedha taslim bila zengwe wala nini, na huu ni mwanzo tu tutarejesha fadhila kwa mashabiki kadri tutakavyojipanga," alisema.

Bendi hiyo ya Extra Bongo inayotamba na vibao matata kama 'Ufisadi wa Mapenzi', 'Mjini Mipango', 'Mgeni' na nyingine, itakuwa bendi ya kwanza kwa mwaka huu na siku za karibuni kufanya kitu kama hicho ili kuwafurahisha mashabiki ambao wamekuwa wakiwaunga mkono kwa kuhudhuria maonyesho wao kila mahali.

Extra Bongo waja na Wiki 4 za Kutoa Zawadi kwa Mashabiki

Mkurugenzi wa Extra Bongo Ally Choki akiwapagawisha mashabiki wa bendi hiyo katika moja ya maonyesho yao
BENDI ya dansi inayotisha nchini kwa sasa, Extra Bongo 'Wana Next Level' a.k.a Wazee wa Kizigo imeandaa wiki nne za kuwazawadiwa mashabiki wake katika shindano maalum litakalofahamika kwa jina la 'Wiki 4 za Zawadi za Extra Bongo'.
Shindano hilo litakaloshindanisha mashabiki wa bendi hiyo kwa kunengua miondoko ya bendi hiyo ya 'Kizigo' ndani ya wiki nne mfululizo ambapo kwa kuanzia watatoa zawadi hizo kwenye ukumbi wa Meeda Club, Sinza jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa bendi hiyo, Ally Choki alisema katika shindano hilo mashabiki watatu watakacheza vema muziki wa bendi hiyo watawazadiwa vitita vya fedha taslim ukumbini.
Choki alisema mshindi wa kwanza katika shindano hilo lililoandaliwa kwa nia ya kuongeza hamasa kwa mashabiki wao kupima kama nao ni wakali wa muziki atapewa Sh 150,000 wakati wa pili atazawadiwa Sh 100,000 na wa tatu ataambulia Sh 50,000.
"Extra Bongoi tunatarajia kuja na Wiki Nne ya Zawadi kwa Mashabiki ambayo rasmi itaanza Jumamosi kwenye ukumbi wa Meeda Club, Sinza kabla ya kuelekea TMK Ijumaa ya Januari 25 ksiha kuangalia kama tuhamie Bagamoyo au Kibaha," alisema Choki.
Choki alisema uzinduzi rasmi wa shindano hilo utasindikizwa na wakali wa muziki wa kizazi kipya, Amin, Linah na Ditto kutoka THT na Saynag wa Respect.
"Yaani ni burudani kwa kwenda mbele pamoja na kuwashuhudia mashabiki wakichuana kucheza Kizigo, pia watawashuhudia wakali wa muziki wa kizazi kipya ambao watatusindikiza katika wiki hizo nne za kutoa zawadi kwa mashabiki wetu," alisema.
Choki alisema japo mpambano huo wa mashabiki sio shindano haswa kwa sababu halitakuwa na majaji wala waamuzi, zaidi ya mashabiki lakini wamefanya hivyo ili kuonyesha namna gani wanavyowathamini mashabiki wao waliowaunga mkono karibu miaka mitatu ya kurejea kwao upya katika 'game'.

Zola D, P Funk wote wana Knockout

Msanii Zola D akiwa katika pozi


MSANII nyota wa muziki wa hip hop nchini, David Michael 'Zola D' ameuanza mwaka 2013 kwa  kishindo kwa kuachia wimbo wake mpya uitwao 'Knockout' aliomshirikisha mtayarishaji mahiri wa muziki, P. Funk 'Majani'.
Tayari wimbo huo uliotolewa katika 'audio' na video tayari umeshaanza kurushwa hewani katika vituo vya redio na runinga nchini, huku Zola D akidai hizo ni salamu zake kwa mashabiki kwamba mwaka 2013 amejipanga kuwapa raha mwanzo mwisho.
Zola D alisema kuwa, wimbo huo ameurekodia studio za Bongo Rocords kwa Majani na video ameifanya chini ya kampuni yake ya Uncle Films akishirikiana na kampuni ya Benjamini wa Mambo Jambo.
"Katika kuwapa raha mashabiki wangu, nimeachia hewani wimbo wangu mpya uitwao 'Knockout' ambao nimeimba na P Funk 'Majani' ambayo pia nimeitolea video yake na tayari imeshaanza kuchezwa na vituo vya redio na runinga," alisema Zola D.
Mkali huyo ambaye pia ni mwanamasumbwi wa uzito wa juu nchini, alisema wakati wimbo huo ukiendelea kutamba hewani, ameshaanza maandalizi ya kufyatua kazi nyingine mpya, japo hakupenda kuweka hadharani kwa madai ni mapema mno.
"Ndugu yangu unajua siku hizi wasanii wamekuwa wepesi kuiba 'idea' za wenzao, hivyo kutaja jina la 'project' yangu mpya ijayo inaweza kuwa mtaji kwa wachakachuaji, ila mashabiki wakae wakijua kuna burudani mpya nawaandalia," alisema Zola D.
Msanii huyo alisema kazi hiyo mpya huenda ikakamilika ndani ya wiki ijayo kabla ya kufanyiwa utaratibu ya kuachiwa hewani baada ya kukamilika kila kitu ikiwemo kurekodiwa kwa video yake.