STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, March 15, 2014

Chelsea yapigwa kidude na Aston Villa

John Terry akipambana dhidi ya mchezaji wa Villa

Karim El Ahmadi and Willian
Willian akiwa chini na mchezaji wa Aston Villa
VINARA wa Ligi Kuu ya England, Chelsea wamejikita wakiangukia pua ugenini baada ya kulambwa bao 1-0 na Aston Villa katia mfululizo wa mechi za ligi hiyo, huku wachezaji wake wawili wa Kibrazil na kocha wao wakilimwa kadi nyekundu.
Chelsea waliokuwa wakihitaji ushindi ili kuzidi kujiimarisha kileleni mwa msimamo na kuzikimbia timu zinazoifukuzia, walishindwa kuonyesha makeke yao kwa Villa kwa kumaliza dakika 45 za kwanza wakiwa nguvu sawa ya bila kufungana.
Kipindi cha pili kiliendelea kuwepo kwa kosa kosa za hapa na Willian kulitolewa nje baada ya kuonyesha kadi ya pili ya njano na kufuatiwa na nyekundu dakika ya 68 kabla ya wenyeji kujiandikia bao lao hilo la pekee lililofungwa na  Fabian Delph katika dakika ya 82 na kuwakata maini vijana wa Jose Mourinho waliokuwa wakisaka ushindi wa nne mfululizo katika EPL.
Dakika za nyongeza za mchezo huo Ramires alionyeshwa kadi ya pili ya njano na kutolewa nje kwa kadi nyekundu na wakati kocha wake akienda kuzungumza uwanjani akajikuta naye akitolewa nje kwa kadi kama hiyo nyekundu.
Kwa kipigo hicho Chelsea imesaliwa na pointi zake 66 na kutoa nafasi nzuri kwa wapinzani wake Liverpool na Arsenal ambazo kesho zitakuwa viwanja tofauti kupunguza pengo la pointi. Timu hizo zina pointi 59 kila moja moja pungufu na ilizonazo Manchester City waliopo nafasi ya pili kwa sasa.

News Alert! Mbunge wa CHADEMA anaswa na Polisi, kisa...!

  IKIWA imebaki siku moja kabla ya uchaguzi Mdogo wa Ubunge jimbo la Kalenga, Iringa Vijijini, Mbunge wa viti Maalum Mkoa wa Manyara kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mh.Rose Kamili amekamatwa jioni ya leo kwenye kijiji cha Kitayawa kata ya Luhota, Iringa Vijijini kwa tuhuma za kugawa Fedha kwa wanakijiji hao, akijua fika Wananchi hao wanatarajiwa kupiga kura kwa ajili ya kumpata Mbunge wa jimbo hilo kesho siku ya jumapili.
 
Pichani shoto ni Mbunge wa viti Maalum Mkoa wa Manyara kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mhe. Rose Kamili akielekezwa sehemu ya kupita wakati wakiondoka ofisi za makao makuu ya CCM mjini Iringa jioni ya leo,akituhumiwa kukutwa akigawa fedha kwa Wanakijiji wa Kitayawa kata ya Luhota,Iringa Vijijini,ambapo Wananchi hao wanatarajiwa kupiga kura kwa ajili ya kumpata Mbunge wa jimbo hilo kesho siku ya jumapili.
 Mbunge huyo wa Chadema akipakizwa kwenye gari tayari kupelekwa kituo cha Polisi kwa taratibu nyingine za kisheria.
Mbunge wa viti Maalum Mkoa wa Manyara kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mh.Rose Kamili akiwa ndani ya gari ya polisi mara baada ya kukakamatwa jioni ya leo kwenye kijiji cha Kitayawa kata ya Luhota,Iringa Vijijini akituhumiwa kugawa Fedha kwa wanakijiji 
Gari ya Polisi PT 1895 ikiondoka na mtuhumiwa huyo,mara baada ya kuchukuliwa kwenye makao Makuu ya chama cha CCM alikokuwa ameshikiliwa na uongozi wa chama hicho,kwa taratibu nyingine za kisheria.  PICHA NA MICHUZI JR

Kipre Tchetche bado amganda Amissi Tambwe


Kipre Tchetche wa Azam
Amissi Tambwe (kushoto) akishangilia moja ya mabao yake na Ramadhani Singano 'Messi'
MSHAMBULIAJI nyota wa Azam, Kipre Tchetche ameendelea kumfukuzia Amissi Tambwe katika mbio za kuwania kiatu cha dhahabu, jioni hii akipunguza pengo hadi kufikia mabao saba dhidi ya kinara huyo wa mabao kwenye Ligi Kuu msimu huu aliyefumania mara 19.
Tchetche aliyekuwa mfungaji bora wa msimu uliopita leo amefunga mabao mawili wakati akiiongoza Azam kuitoa nishai Coastal Union kwa kuwalaza mabao 4-0 na kumfanya afikie mabao 12.
Mchezaji huyo kutoka Ivory Coast hata hivyo bado ana kibarua kigumu cha kumfikia Tambwe ambaye kasi yake ya kufumania nyavu imewafanya baadhi ya washambuliaji machachari kusalimu amri katika kukiwania kiatu hicho cha dhahabu.
Miongoni mwa washambuliaji waliokuwa wakifukuzana na Tambwe ni Tchetche raia wa Ivory Coast pekee ambaye amendelea kwenda naye sambamba, huku wazawa kama Elias Maguli wa Ruvu Shooting na Juma Luizio 'Ndanda' wakishindwa kufumania nyavu katika mechi zote za duru la pili mpaka sasa.

Newcastle yadonyolewa, Everton, Stoke zatamba EPL

Ashkan Dejagar akishangilia bao lake pekee lililoipa ushindi Fulham leo
Marko Arnautovic wheels away after putting Stoke ahead
Wachezaji wa Stoke City wakishangilia bao dhidi ya West Ham
Morgan Schneiderlin
Kitu! mchezaji wa Southampton akifunga bao
Juan Cala
Vita ya Evertona dhidi ya Cardiff City
BAO pekee lililofungwa na Muiran, Ashkan Dejagar lilitosha kuiwezesha Fulham kuiangamiza Newcastle United ugenini katika mechi ya Ligi Kuu ya England, huku Everton ikiibuka na ushindi nyumbani wa mabao 2-1 dhidi ya Cardiff City bao la ushindi likipatikana 'jioni'.
Dejagar alifunga bao hilo lililoipa ushindi Fulham katika dakika ya , huku bao lililoibeba Everton dhidi ya Cardiff City likifungwa na 68 dakika tano tu tangu alingia dimbani akitokea benchi akimpokea Dan Burn.
Ushindi huo hata hivyo haujaisaidia Fulham kujitoa mkiani mwa msimamo, ingawa imefufua matumaini ya kuendelea kupambana ili iwemo kwa msimu ujao.
Katika mechi nyingine zilizomalizika hivi punde, Everton ilisubiri dakika za lala salama kuweza kujiandikishia ushindi wa 2-1 nyumbani dhidi ya Cardiff.
Seamus Coleman ndiye aliyefunga bao hilo dakika tatu za nyongezana kuifanya timu yake ilingane pointi na Manchester United ingawa inaendelea kusalia nafasi ya saba.
Everton ilikuwa ya kwanza kupata bao katika dakika 59 kupitia kwa Gerard Deulofeu akimalizia kazi za Osman kabla ya wageni kuchomoa dakika tisa baadaye kupitia kwa Juan Cala na kuonekana kama matokeo yangesalia hivyo yaani timu hizo kufungana bao 1-1 kabla ya Colemans kufunga bao hilo la ushindi.
Nayo timu ya West Bromwich iliyomtimua mshambuliaji wake, Nicolas Anelka ilipata ushindi wa mabao 2-1 ugenini dhidi ya SwanseaCity, huku Sunderland ikilazimishwa suluhu ya bila kufungana nyumbani dhidi ya Crystal Palace.
Nayo timu ya Southampton ikiwa nyumbani ilipata ushindi mnono wa mabao 4-2 dhidi ya Norwich City na Stoke City ikaibamiza West Ham Utd kwa mabao 3-1.
Hivi punde timu ya Aston Villa itakuwa nyumbani kuikaribisha Chelsea inayonolewa na Jose Mourinho ambayo imejizatiti kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.

Man City pungufu yaibutua Hull City kwao


MANCHESTER City ikicheza pungufu kwa muda mrefu imefanikiwa kuifyatua Hull City nyumbani kwao kwa kuilaza mabao 2-0 na kurejea kwenye nafasi ya pili ya msimamo wa Ligi Kuu ya England.
Nahodha Vincent Kompany alilimwa kadi nyekundu  dakika 10 ya mchezo kitendo ambacho hata hivyo haikuikatisha tamaa City kwani iliweza kujipatia bao la kuongoza dakika ya 14 kupitia kwa David Silva.
Bao hilo lilidumu hadi wakati wa mapumziko na Hull City kuonekana kukomaa kabla ya kuruhusu bao la ushindi kwa wageni wao lililotumbukiza 'jioni' kabisa ya mchezo huo na Edin Dzeko.
Kwa ushindi huo, City imefanikiwa kutimiza pointi 60 baada ya kucheza mechi 27 na kurejea nafasi ya pili, nyuma ya Chelsea yenye pointi 66 baada ya mechi 29, Liverpool yenyewe imerudi nafasi ya tatu ikiwa na pointi 59 na kesho itakuwa ugenini kumenyana na watani zao Manchester Utd.

Simba kuchaguana Mei 4


https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhs3YLOLABWqGLvolfiCNC6htMXFKSuU5hflMOHvDGc2-zA0l2CpuCOvJFrTwrPZkrTmbVZ2p6BZA-J-sqxwf-vQX1ph8hYQpIMmGQDHdD0EDsZA-gzHeTMW9y4K12kU_hCmDn8-mWN7SQ/s1600/simba-logo%255B1%255D.jpg
UCHAGUZI Mkuu wa klabu ya Simba umepangwa kufanyika Mei 4, huku Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo imeteua Kamati Mpya ya Uchaguzi itakayoongozwa na Mwenyekiti Damas Ndumbaro.
Kwa mujibu wa Afisa Habari wa Simba, Asha Muhaji Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo ya uchaguzi ni Salum Madenge. Wengine katika Kamati hiyo ni Issa Batenga ambaye ni Katibu, Khalid Kamguna Katibu Msaidizi na Wajumbe Kassim Dewji, Juma Simba na Amin Bakhresa.
na kusisitiza kuwa uchaguzi huo utafanyika Mei 4 na kesho wanachama watakutana kwenye mkutano wa wanachama kwa ajili ya kujadili marekebisho ya katiba ya klabu yao kwa maana ya kuwa na ajenda moja tu tofauti na kilio cha wanachama wengi wa klabu hiyo walioutaka uongozi kuongeza ajenda zaidi.
Mkutano huo utafanyika kesho saa 3 asubuhi kwenye ukumbi wa Officers Police Mass, Oysterbay.

Azam haishikiki, Yanga yabanwa Prisons hoi

Yanga waliobanwa na Mtibwa mjini Morogoro
Azam iliyouia Coastal kwa mabao 4-0
Kagera Sugar iliyoitibulia Prisons-Mbeya rekodi ya kutofungwa duru la pili
WAKATI 'jinamizi' la kung'olewa Ligi ya Mabingwa Afrika likiendelea kuisumbua Yanga, Azam waliong'oka Kombe la Shirikisho wameendelea kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuwacharaza Wazee wa Oman, Coastal Union kwa mabao 4-0.
Azam walipata ushindi huo kwenye uwanja wa Chamazi, jijini Dar es Salaam wakati Yanga ikilazimishwa suluhu na Mtibwa Sugar kwenye uwanja wa Jamhuri Morogoro na kuendelea kurejea nafasi ya pili ikiiengua Mbeya City.
Katika mechi ya Yanga na Mtibwa, timu zote zilishambuliana na wenyeji walionekana kuusaka ushindi kutokana na mashambulizi makali yaliyokuwa yakiongozwa na Abdallah Juma ambaye hata hivyo alikuja kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 56.
Azam wanaouwania ubingwa wa ligi kwa mara ya kwanza, iliisasambua Coastal kwa mabao 4-0, mawili yakifungwa na Kipre Tchetche na jingine likiwekwa kimiani na John Bocco na jingine chipukizi wao Kelvin Friday.
Mjini Bukoba, Kagera Sugar iliitibua rekodi ya Prisons-Mbeya ya kutopoteza mchezo wowote kwqenye duru la pili baada ya kuichapa mabao 2-1 kwenye uwanja wa Kaitaba.
Wenyeji walitanguliwa kufungwa bao katika dakika ya 37 kupitia Peter Michael lililodumu mpaka kipindi cha kwanza kilipomalizika.
Kipindi cha pili wenyeji walicharuka na kufanikiwa kusawazisha bao kwa mkwaju wa penati kupitia Salum Kanoni katika dakika ya 55.
Wakati mashabiki wakiamini kuwa mechi imeisha kwa sare Kagera iliongeza bao la ushindi lililofungwa dakika ya 88 na Benjamini Asukile na kuifanya timu yao kuvuna pointi tatu na kufikisha pointi 32 na kujiimarisha kwenye nafasi ya tano nyuma ya Simba.
Azam kwa ushindi wa leo imeendelea kujimarisha kileleni ikifikisha pointi 43, nne zaidi ya Yanga na Mbeya City ziliyo nafasi ya pili na tatu wakiwa na pointi 39 kila moja kabla ya kutofautiana uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Anelka atimuliwa West Bromwich Albion

http://i.telegraph.co.uk/multimedia/archive/02794/Nicolas_Anelka_2794916k.jpg
KLABU ya West Bromwich Albion ya England imetangaza kumtimua kikiosini nyota wake Nicolas Anelka kwa utovu wa nidhamu. 
Maamuzi ya klabu hiyo yamekuja baada ya Anelka kutangaza kupitia mtandao wa kijamii kuwa ana mpango wa kuondoka klabu hapo.
Anelka amesema kuwa anaondoka baada ya kukosekana muafaka wa tofauti zilizopo kati yake na klabu hiyo kutokana ishara yake yenye utata ambayo inasemekana kuwa ya kibaguzi dhidi ya wayahudi. 
Mshambuluaji huyo mwenye umri wa miaka 35, alipigwa marufuku kutocheza mechi tano na kutozwa faini ya pauni 80,000 na FA, kwa kufanya ishara hiyo ya kinazi, baada ya kufunga bao dhidi ya West Ham United Desemba mwaka jana. 
West Brom imechukua hatua ya kumfuta kazi Anelka kutokana na ishara hiyo na pia kwa sababu ya matamshi yake kwenye mtandao wa kijamii.

Sajenti ana nne na Tip Top Connection

KIMWANA aliyejipatia umaarufu katika shindano la Manywele 2007, Husna Idd 'Sajenti', anajiandaa kutoa na filamu nne tofauti chini ya Tip Top Connection anaofanya nao kazi kwa sasa.
Akizungumza na MICHARAZO  kisura huyo aliyewahi kutamba kwenye Miss Tanzania Mkoa wa Singida, alisema filamu hizo zitakuwa zikitoka kwa awamu na ameshirikiana na wakali watupu.
Sajenti alizitaja filamu hizo kuwa ni Adella, Ndoa, Mtawala na Bwege ikiwa ni mwanzo wa 'project' za Tip Top mbali na filamu nyingine alizoshirikishwa na wasanii wenzake.
"Kwa sasa nafanya kazi chini ya Tip Top Connection upande wa filamu na kuna kazi kama nne ambazo zimeshakamilika tayari kwa kuachiwa sokoni kuanzia mwezi huu wa tatu," alisema Sajenti.
Msanii huyo aliyetumbukia kwenye filamu tangu mwaka 2007 baada ya kung'ara kwenye urembo na shindano la Kimwana wa Manywele alisema ndani ya filamu hizo amefanya 'kufuru' na wenzake.
"Sijisifu, lakini ndani ya filamu hizo nimefanya makubwa na wenzangu na mashabiki wasubiri wapate uhondo," alisema kimwana huyo.

Japenese:Muimbaji anayetamba ughaibuni aliyetamani kuwa daktari

MASHABIKI wa muziki wanamfahamu kwa jina la Japanese, ingawa majina yake halisi ni Amina Kassim Ngaluma, mmoja wa waimbaji mahiri wa kike wa muziki wa dansi nchini anayefanya kazi ughaibuni.
Japanese, aliyewahi kuziimbia bendi mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa sasa anafanya shughuli zake za muziki akiwa na bendi ya Jambo Survivors iliyopo Thailand, Mashariki ya Mbali barani Asia.
Mwanadada huyo anakiri licha ya kipaji cha muziki cha kuzaliwa, lakini alijikuta akipenda kuwa mwanamuziki kwa kuvutiwa na muimbaji nyota wa zamani wa Kongo, Mbilia Bell.
Anasema sauti na uimbaji wa Mbilia ulikuwa ukimkuna na kutamani kuwa kama muimbaji huyo, hivyo kuja kuangukia mikononi mwa nyota wa taarab nchini, Bi. Shakila Said, aliyemnoa kwenye uimbaji.
"Siyo siri nilimzimia mno Mbilia Bell, nikatamani kuwa kama yeye na kwa bahati nikaangukia mikononi mwa Bi Shakila aliyeninoa na kuwa hivi nilivyo kupitia kundi la JKT Taarab," anasema.
Anasema hata hivyo alipata wakati mgumu kwa vile mama yake hakupenda awe mwanamuziki badala yake kutaka afanye kazi za ofisi, tofauti na baba yake aliyemuunga mkono hadi leo ukubwani.
Japanese anasema baada ya kuiva kwa Bi Shakila pale JKT Taarab alihamia katika muziki wa dansi akianzia Less Mwenge-Arusha kisha   kukimbilia Kenya alipojijengea jina akizipigia bendi mbalimbali.
"Niliizipigia bendi za Sayari iliyokuwa chini na Badi Bakule 'Mkandarasi', Sky Sound iliyoongozwa na Mwinjuma Muumin, kisha Mangelepa ya Evanee kabla ya kurejea Tanzania," anasema.
Anasema aliporejea nchini alijiunga na African Revolution 'Tamtam' iliyomjengea jina kabla ya kwenda Double M Sound kisha TOT-Plus kabla ya kuhamia Jambo Survivors alionao mpaka sasa.
Japanese anaitaja bendi ya African Revolution kama ilimtambulisha katika ulimwengu wa muziki, ila bendi ya mafanikio na maendeleo kwake ni Jambo Survivors iliyomuinua kiuchumi toka alipokuwapo.

MKALI
Japanese aliyekuwa mahiri kwa mchezo wa Netiboli alioucheza kwa mafanikio kabla ya kutumbukia kwenye muziki, pia ni mahiri kwa utunzi wa nyimbo baadhi ya tungo zake ziliwahi kutikisa muziki wa Tanzania.
Baadhi ya nyimbo alizotunga mwanadada huyo mwenye ndoto za kuja kumiliki bendi binafsi akishirikiana na mumewe ambaye pia ni mwanamuziki Rashid Sumuni ni; 'Mapendo', 'Manyanyaso Kazini', 'Ukewenza', 'Wajane' na Mwana Mnyonge'.
Pia alishawahi kupakua albamu binafsi iitwayo 'Jitulize' aliyoizindua mkoani Morogoro ikiwa na nyimbo sita baadhi ni 'Jitulize', 'Uombalo Hutopata', 'Pete ya Uchumba', 'Mapenzi ya Kweli' na 'Tulia Wangu'.
Japanese anayefurahia tukio la kufunga ndoa na mumewe Rashid Sumuni na kulizwa na kifo cha kaka yake, Mashaka Ngaluma aliyeuawa na majambazi kwa kupigwa risasi akiwa kazini kwake.
"Kwa kweli matukio haya ndiyo yasiyofutika kichwani mwangu, nilipofunga ndoa na mume wangu kipenzi, Rashid Sumuni na siku kaka yangu alipouawa kwa risasi akiwa kazini," anasema.
MAFANIKIO
Japanese asiyefuatilia soka aliota kuja kuwa Daktari ila muziki ukaja kumbeba jumla, ingawa hajutii kwa namna fani hiyo ilivyomsaidia kwa mambo mengi ya kujivunia.
Anasema mbali na kupata rafiki wengi, kutembea nchi mbalimbali duniani na kujifunza tamaduni tofauti, pia muziki umemwezesha yeye na mumewe kumiliki miradi kadhaa ya kiuchumi, nyumba na magari.
Hata hivyo anasema bado hajaridhika hadi atakapoanzisha bendi yao ya Skwensa hapa nchini itakayokuwa ikipiga mahotelini na kurekodi kazi zake katika studio yao binafsi.
Pia angependa kuwasaidia waimbaji wa kike ili kusaidia kuongeza idadi yao katika muziki wa dansi alikodai imekuwa ikizidi kupungua kwa sababu wengi wao hawapendi tabu wala kujifunza muziki.
"Waimbaji wa kike hawapendi dansi kwa ugumu wake hivyo huona bora wajikite kwenye muziki wa kizazi kipya, ila kujifunza muziki wa dansi hasa upigaji ala husaidia kujitangaza kimataifa," anasema.
JUMBE
Japanese alizaliwa Nov 29, mjini Morogoro akiwa ni mtoto wa tatu kati ya tisa wa Baba Kassim Ngaluma na Mama Khadija Abdallah, watatu kati yao wakiwa wameshatangulia mbele ya haki ya kubakia sita tu.
Mkali huyo yupo Jambo Survivors inayopiga muziki wake katika hoteli iitwayo Banthai Beach Resort & SPA akiwa na Hassan Shaw, Eshter Lazaro, Ramadhani Kinguti, Yuda Almasi na mwana BSS Edson Teri.
Mwanadada huyo anasema kwa hapa nchini anawazimia wanamuziki  Hussein Jumbe na Nyota Waziri.
"Hawa ndiyo wanaonikosha na umahiri wao katika muziki," anasema.
Japanese anayewataka wanamuziki wenzake kuwa wabunifu ili kwenda na mabadiliko ya dunia na kuiomba serikali kuutupia macho muziki wa dansi anamshukuru Mungu kwa kumsaidia kufika alipo.
Pia anawashukuru wazazi wake kwa sapoti kubwa anayompa, mumewe Rashid Sumuni pamoja na mwalimu wake Shakila Said bila kuwasahau wote walio bega kwa bega katika fani yake kwa ujumla.