STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, December 27, 2011

Kingwande 'aitabiria' mema Lyon duru la pili

KIUNGO Mshambuliaji nyota wa timu ya African Lyon, Adam Kingwande, amesema ana matumaini makubwa kwa timu yake kufanya vema katika duru lijalo la Ligi Kuu Tanzania Bara kutokana na kusajiliwa kwa wchezaji kadhaa wapya katika kikosi chao.
Akizungumza na MICHARAZO, Kingwande, aliyewahi kuzichezea timu za Ashanti Utd na Simba, alisema usajili uliofanywa kupitia dirisha dogo lililomalizika mwezi uliopita kwa namna moja utaisaidia timu yao kufanye vema kwenye duru hilo lijalo.
Kingwande, alisema awali kikosi chao kilikuwa na mapungufu makubwa ambayo yaliifanya Lyon iyumbe kwenye duru la kwanza, jambo ambalo lilionwa na kufanyiwa kazi na uongozi na benchi la ufundi lao la ufundi kwa kusajiliwa wachezaji hao wapya.
Alisema kwa namna usajili huo uliofanyika kwa kuchanganya wachezaji wa ndani na nje ya nchi ni wazi Lyon, itakuwa moto wa kuotea mbali katika duru lijalo, kitu alichotaka timu pinzani zikae chonjo dhidi yao.
"Binafsi naamini Lyon itakuwa moto duru lijalo kutokana na kuongezwa wachezaji wapya kupitia dirisha dogo, pia, nashukuru kwamba kwa sasa nipo fiti tukianza maandalizi ya duru hilo," alisema.
Lyon inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu wa tatu sasa, ilianza vema duru la kwanza kabla ya kutetereka ikimaliza duru hilo ikiwa nafasi ya tisa katika msimamo wa ligi hiyo kwa kujikusanyia jumla ya pointi 14.
Msimamo wa ligi hiyo unaongozwa na Simba yenye pointi 28 ikifuatiwa na Yanga yenye piinti 27 na Azam waliona pointi 23 sawa na JKT Oljoro wanaoshika nafasi ya nne.

Mwisho

Kocha Papic 'aivua' nguo Yanga, Niyonzima mh!




KOCHA Kostadian Papic wa Yanga amefichua ubabaishaji mkubwa uliopo katika klabu yake na kuonya kuwa kamwe asitafutwe mchawi pindi watakapoboronga kwani hadi sasa hakuna maandalizi yoyote ya maana waliyoanza kuyafanya kwa ajili ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Bara na pia kwa mechi yao ya kwanza ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Zamalek ya Misri.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Papic maarufu kama 'Clinton' alisema, hali ngumu ya maisha klabuni hapo ni tatizo kwani wachezaji wake hawahakikishiwi maslahi yao kwa wakati na hadi sasa wanashindwa hata kupata chakula cha uhakika.
Papic alisema kuwa kukosa fedha kumeifanya timu hiyo kushindwa kufanya mazoezi kwa siku saba sasa kwavile hawana hata fedha za kukodisha uwanja wa kufanyia mazoezi.
"Kwa hali hii ya ukata, siwezi kuahidi matokeo mazuri kwa mashabiki wetu... ukweli ni kwamba hivi sasa wachezaji wamepoteza morari ya mazoezi kwa kukosa fedha zao na chakula. Hali hii inasikitisha kwa sababu hivi sasa tunashindwa hata kwenda gym kwa kukosa fedha," alisema Papic.
"Wanayanga wasije wakawalaumu wachezaji au kocha wakati watakapoona timu inafanya vibaya. Pengine si habari nzuri, lakini hiyo ndio hali halisi klabuni," aliongeza Papic.
Papic alisema kuwa kutokana na hali mbaya waliyo nayo kifedha, sasa anakosa nguvu ya kuwabana wachezaji wake kufanya mazoezi kwa kuwa anafahamu hali ngumu wanayokabiliana nayo.
Ppic alianika zaidi udhaifu mwingine klabuni kwao kuwa ni wamawasiliano duni kati ya benchi la ufundi na uongozi wa klabu hiyo.
Kuhusiana na maslahi yake, Papic alisema kuwa mambo mengi waliyokubaliana awali na uongozi kwenye mkataba wao hayajatekelezwa na hivyo hata yeye anakabiliwa na wakati mgumu.
Katika hatua nyingine, Papic alisema kuwa pamoja na timu hiyo kuwa mbioni kushiriki mashindano ya Kombe la Mapinduzi (visiwani Zanzibar), hadi sasa bado hajapewa taarifa rasmi za kuandaa timu yake kwa ajili ya mashindano hayo.
"Sifahamu chochote kuhusu mashindano hayo... nasikia juu juu tu," alisema Papic.
Papic alisema kuwa wametuma majina ya wachezaji 28 kwa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) kwa ajili ya klabu bingwa Afrika, lakini amemtema kiungo Rashidi Gumbo kwa maelezo mafupi kuwa mchezaji huyo hayupo tayari kwa mashindano hayo.
Papic alisema vilevile kuwa baada ya ratiba iliyotolewa na CAF kuonyesha kuwa watacheza dhidi ya Zamalek, aliomba kupatiwa mikanda ya video ya timu hiyo ili iwasaidie katika maandalizi yao lakini hadi sasa hawajaipata kutokanan na sababu ileile ya uklata inayokwamisha pia harakati nyingine za maandalizi ya kikosi chake.
"Inatakiwa dola za Marekani 10,000 ili kuipata mikanda niliyokuwa nikiitaka... jambo hili hadi sasa limeshindikana," alisema Papic.
Kuhusiana na kiungo wao wa kimataifa kutoka Rwanda, Haruna Niyonzima, ambaye hajaripoti hadi sasa tangu alipomaliza mapumziko waliyopewa baada ya kumalizika kwa michuano ya Kombe la Chalenji, Papic alisema kuwa atamuadhibu ili fundisho kwa wengine.
"Mara kwa mara amekuwa akitoa visingizio kuwa ana matatizo ya hati yake ya kusafiria.. nitamwadhibu na kumkata mshahara wake ili iwe fundisho kwa wachezaji wengine," alisema Papic.
Hata hivyo uongozi wa Yanga ulipoulizwa juu ya madai hayo ya Papic, Afisa Habari wa klabu hiyo, Louis Sendeu, alisema kuwa hawezi kuzungumzia chochote kuhusiana na suala hilo kwa kuwa ni la kiutendaji.
“Hilo suala ni kubwa kwangu. Ni la kiutawala zaidi na hivyo naomba mumtafute katibu au mwenyekiti. Wao ndio wanaoweza kuwajibu,’ alisema Sendeu.
Pia Sendeu alidai kushangazwa na kocha wao kukimbilia kwenye vyombo vya habari wakati angeweza kutoa malalamiko yake kwa uongozi ili kumaliza tatizo.
Naye Katibu wa Yanga, Celestine Mwesigwa, alijibu kwa kifupi kuwa watatoa ufafanuzi juu ya taarifa za kocha wao, ambazo ni kama kuwavua nguo mbele ya wadau wa soka.

Villa kuchagua mwenyekiti Februari

UCHAGUZI mdogo wa klabu ya soka ya Villa Squad ya jijini Dar es Salaam kuziba nafasi ya Mwenyekiti na wajumbe wa Kamati ya Utendaji unatarajiwa kufanyika mwezi Februari.
Makamu Mwenyekiti wa Villa, Ramadhan Uledi, aliiambia MICHARAZO kuwa, uchaguzi huo mdogo utafanyika mwanzoni mwa Februari mara baada ya duru la pili la Ligi Kuu Tanzania Bara kuchanganya kasi.
Uledi, alisema mwezi ujao kupitia kamati yao ya uchaguzi itatangaza taratibu za uchaguzi huo, ili kufanyika kwake na kuikamilisha safu ya uongozi wa klabu yao.
"Uchaguzi mdogo wa kumpata mwenyekiti na wajumbe wawili wa kamati ya utendaji utafanyika mara baada ya duru la pili la ligi kuu kuanza, nadhani itakuwa mapema Februari mwakani," alisema Uledi.
Aliongeza, kwamba wangeweza kuitisha mapema uchaguzi huo hata sasa, lakini hali mbaya ya ukata waliyonayo na maandalizi ya ligi inayowakabili ndio maana wameona wavute muda hadi baadae huku akisisitiza ni lazima ufanyike katika muda huo.
Mbali na kuwahimiza wanachama wa klabu hiyo kuanza kukaa mkao wa kula kujitokeza kuwania nafasi hizo, ambazo zilishindwa kuwapata washindi wake kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika Juni, mwaka huu pia aliwataka wajitokeza kuichangia Villa.
"Wanachama na wadau wa Villa wasaidie kuichangia timu yao kwa ajili ya ushiriki wa duru lijalo, sambamba na kujiweka tayari kuziba nafasi hizo zilizo wazi kwenye uchaguzi huo mdogo," alisema.
Villa ilishindwa kumpata Mwenyekiti wakati wa uchaguzi wake mkuu, kufuatia Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, kumuengua aliyekuwa mgombea pekee wa nafasi hiyo, Abdallah Majura Bulembo kwa kilichoelezwa kukosa sifa stahiki.

Mwisho

Toto Afrika kuwavaa Wanigeria Mwanza na Shinyanga

TIMU ya soka ya Toto Afrika ya Mwanza jioni ya leo inatarajiwa kushuka dimba la CCM Kirumba, jijini humo kupepetana na wageni wao Abuja FC ya Nigeria katika pambano la kirafiki la kimataifa la kujiandaa na duru la pili la Ligi Kuu Tanzania Bara.
Pambano hilo la Mwanza ni kati ya mechi mbili zitakazochezwa baina ya timu hizo mbili ambazo zimeanzisha ushirikiano wa pamoja.
Kwa mujibu wa Katibu Mipango wa Toto, Hassani Kiraka, pambano jingine la timu hizo mbili litachezwa kesho kwenye dimba la Kambarage, mkoani Shinyanga.
Kiraka alisema, mbali na mechi hizo mbili kutumiwa na timu yao kukiandaa kikosi chao kwa ajili ya duru la pili litakaloanza Januari 21, pia zitatumiwa kukusanya fedha kwa za kuiwezesha Toto kushiriki vema ligi hiyo kutokana na kuwa na hali mbaya kiuchumi.
"Tunawahimiza mashabiki wa soka wa jijini Mwanza na Shinyanga ambao kwa muda mrefu hawajapata burudani ya kimataifa kujitokeza kwa wingi katika mechi hizo ikiwa sehemu yao ya kuichangia timu yetu, ili ishiriki vema katika duru lijalo," alisema Kiraka.
Alisema, uongozi wao umepania kuona Toto Afrika katika duru la pili, ikifanya vema tofauti na ilivyokuwa duru lililopita kwa nia ya kuiokoa timu yao isishuke daraja, ndio maana wameialika Abuja Fc ambayo wameanzisha ushirikiano wa pamoja baina yao.
Aliongeza, katika mechi hizo mbili benchi la ufundi la Toto lililopo chini ya John Tegete na msaidizi wake, Choki Abeid, watatafuta wachezaji wanne kutoka kikosi cha Abuja Fc, ili ikiwezekana mwakani wawasajili katika timu yao.
Toto iliyoanza duru la kwanza kwa makeke kabla ya kutetereka na kumaliza mzunguko huo ikiwa nafasi ya 11 katika msimamo wa ligi, katika kikosi chake inao nyota wawili wa Kinigeria, akiwemo kinara wao wa mabao, Enyima Darlington na Chika Chimaobi Chukwu.

Mwisho

Simba, Yanga zaumwa sikio



BEKI wa zamani wa timu za Ushirika-Moshi, Simba na Yanga, Willy Martin 'Gari Kubwa', amezitaka klabu za Simba na Yanga na kufanya maandalizi kwa vitendo badala ya maneno ili kujiandaa na mechi za kimataifa mwakani.
Aidha amelitaka Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, kumsaidia kocha Jan Poulsen wa Taifa Stars kuitafutia timu mechi za kutosha za kimataifa kabla ya kushiriki wa mechi za kuwania Fainali za Afrika za 2013 na Kombe la Dunia la 2014.
Akizungumza kwenye mahojiano maalum, Gari Kubwa, alisema ili Simba na Yanga ziweze kufanya vema katika mechi zake za Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho ni lazima zijipange vya kutosha badala ya kupiga 'blabla' huku muda ukienda.
Gari Kubwa, aliyewahi kuzichezea pia timu ya Majimaji-Songea, Bandari-Mtwara na Taifa Stars kwa nyakati tofauti, alisema maandalizi ya kutosha na kupata mechi nyingi za kirafiki za kimataifa zinaweza kuzibeba Simba na Yanga mwakani.
Alisema kinyume cha hapo ni kwamba timu hizo zisubiri kung'olewa mapema kama ilivyozoeleka na kuishia kutoa visingizio visivyo na maana.
"Naamini Simba na Yanga zikijipanga vema zinaweza kufanya vizuri katika uwakilishi wao, lakini zikiendelea kupiga blabla wakati muda ukizidi kwenda basi watarajie kuendelea kuwasononesha mashabiki wao kwa kung'olewa mapema," alisema.
Aidha, alilishauri Shirikisho la Soka nchini, TFF, kuanza maandalizi ya kuitafutia mechi za kirafiki za kimataifa, timu ya taifa, Taifa Stars, ili ijiweke vema kabla ya kukabiliana na wapinzani wao katika kuwania Fainali za Afrika na zile za Dunia.
Alisema amegundua Kocha Mkuu, Jan Poulsen amekuwa na wakati mgumu kwa matokeo mabaya ya timu yake kwa makosa yanayofanywa na TFF kwa kutoitafutia Stars mechi za kutosha kumpa nafasi kocha kurekebisha makosa.
"TFF lazima ibadilike na kuitafutia Stars mechi nyingi za kimataifa mapema, ili kumsaidia Poulsen, ni vigumu timu kufanya vema kama haipati mechi za maana za kujipima nguvu kabla ya kuingia kwenye ushindani," alisema.
Stars imepangwa kundi C katika makundi ya kuwania Fainali za Dunia zitakazofanyika Brazil, huku pia ikiwa na kibarua cha kuumana na Msumbiji katika mechi za mchujo za kuingia makundi ya kufuzu Fainali za Afrika 2013 zitakazochezwa nchini Afrika Kusini.

mwisho

Mchaki 'aula' VIlla Squad

KLABU ya soka ya Villa Squad, imemteua aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Soka wilaya ya Kinondoni, KIFA, Frank Mchaki kuwa Kaimu Katibu Mkuu baada ya Katibu Mkuu wao, Idd Godigodi kuwa mgonjwa.
Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ramadhani Uledi, aliiambia MICHARAZO kuwa, wamelazimika kumuomba Mchaki awashikie nafasi hiyo ya Ukatibu kuitokana na Katibu wao kuwa mgonjwa na huku wakikabiliwa na majukumu kabla ya kuanza kwa ligi.
Uledi, alisema kamati yao ya utendaji ililazimika kuhitisha kikao cha dharura na kufanya maamuzi hayo, kwa nia ya kuifanya Villa isitetereke wakati ikijiandaa na duru la pili la Ligi Kuu Tanzania bara litakaloanza Januari 21.
"Tumemundikia barua kumuomba akaimu ukatibu mkuu, kutokana na uzoefu alionao na ametukubalia kwani kabla ya uteuzi alikuwa ndiye Katibu wa Kamati ya Usajili ya klabu yetu ambayo alifanya kazi nzuri kwa kuimarisha kikosi," alisema Uledi.
MICHARAZO iliwasiliana na Mchaki, ambaye alikiri kuombwa na uongozi wa klabu hiyo kushikilia cheo hicho na kudai haoni sababu ya kuikataa ilihali ni mmoja wa wadau wakubwa wa klabu hiyo.
"Ni kweli kuhusu jambo hilo na nimeshawajibu kuafiki uteuzi huo na kuwahidi wana Villa wanipe ushirikiano kuiwezesha timu yetu ifanye vema kwenye ligi hiyo na kuondokanan na janga la kushuka daraja pamoja na ukata uliopitiliza," alisema.
Villa Squad iliyorejea Ligi Kuu msimu huu, ndiyo inayoshikilia mkia katika msimamo wa ligi hiyo yenye timu 14.

Mwisho

Maneno, Matumla washindwa kutambiana





MABONDIA wakongwe wa ngumi za kulipwa nchini, Maneno Oswald 'Mtambo wa Gongo' na Rashid Matumla 'Snake Man' juzi walishindwa kutambiana baada ya pambano lao la kumaliza ubishi kuisha kwa kutoka sare.
Hata hivyo Oswald, ameyakubali matokeo hayo kwa ushingo upande, akidai kwamba alistahili kutangazwa mshindi kutokana na kumzidi maarifa mpinzani wake aliyeteleza na kuanguka ulingoni mara sita na kujikuta akiumia mguu.
Pambano hilo lisilo la ubingwa lililokuwa na raundi 10 na uzani wa kati lililosimamiwa na Shirikisho la Ngumi za Kulipwa Nchini, PST, lilifanyika kwenye ukumbi wa Heinken Pub, Mtoni Kijichi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Katika pambano hilo lililochezeshwa na mwamuzi wa kimataifa wa mchezo huo nchini, Anthony Rutta, mabondia wote wawili walipewa pointi 99-99, kitu ambacho Maneno Oswald aliiambia MICHARAZO kuwa ni kama mpinzani wake 'alibebwa' tu.
"Kwa kweli nimeyakubali matokeo hayo kwa shingo upande kwa vile nilistahili kabisa ushindi, ila mpinzani wangu amelindwa, Matumla kaanguka mara sita ulingoni, utetezi wake ulingo ulikuwa unateleza mbona mie sikuteleza," alisema Maneno.
Aliongeza kuwa, licha ya kuambiwa kuna mipango inafanywa ili warudiane tena, yeye binafsi hana mpango wa kufanya hivyo na kudai anataka kupigana na Mada Maugo, aliyedai ndiye anayemuona mpinzani wake wa ukweli.
"Sitarudiana na Matumla hata iweje, nataka kupigana na Maugo kwani namuona ndiye bondia wa kweli kwa sasa nchini katika uzito wetu.," alisema.
MICHARAZO lilijaribu kumsaka Matumla kusikia kauli yake juu ya matokeo ya mchezo huo, lakini simu yake haikuwa hewani.
Hilo lilikuwa ni pambano la nne kwa Maneno na Matumla kuzipiga, kwani walishacheza mechi tatu na mara mbili Matumla aliibuka na ushindi dhidi ya moja la mpinzani wake.
Katika mechi nyingine za utangulizi zilizochezwa kabla ya pambano la wawili, Ubwa
Kabla ya pambano hilo kuchezwa kulifanyika mechi kadhaa za utangulizi, ambapo moja wao lilimkutanisha bondia Ubwa Salum aliyempiga kwa pointi Mustafa Dotto.