STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, December 27, 2011

Simba, Yanga zaumwa sikio



BEKI wa zamani wa timu za Ushirika-Moshi, Simba na Yanga, Willy Martin 'Gari Kubwa', amezitaka klabu za Simba na Yanga na kufanya maandalizi kwa vitendo badala ya maneno ili kujiandaa na mechi za kimataifa mwakani.
Aidha amelitaka Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, kumsaidia kocha Jan Poulsen wa Taifa Stars kuitafutia timu mechi za kutosha za kimataifa kabla ya kushiriki wa mechi za kuwania Fainali za Afrika za 2013 na Kombe la Dunia la 2014.
Akizungumza kwenye mahojiano maalum, Gari Kubwa, alisema ili Simba na Yanga ziweze kufanya vema katika mechi zake za Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho ni lazima zijipange vya kutosha badala ya kupiga 'blabla' huku muda ukienda.
Gari Kubwa, aliyewahi kuzichezea pia timu ya Majimaji-Songea, Bandari-Mtwara na Taifa Stars kwa nyakati tofauti, alisema maandalizi ya kutosha na kupata mechi nyingi za kirafiki za kimataifa zinaweza kuzibeba Simba na Yanga mwakani.
Alisema kinyume cha hapo ni kwamba timu hizo zisubiri kung'olewa mapema kama ilivyozoeleka na kuishia kutoa visingizio visivyo na maana.
"Naamini Simba na Yanga zikijipanga vema zinaweza kufanya vizuri katika uwakilishi wao, lakini zikiendelea kupiga blabla wakati muda ukizidi kwenda basi watarajie kuendelea kuwasononesha mashabiki wao kwa kung'olewa mapema," alisema.
Aidha, alilishauri Shirikisho la Soka nchini, TFF, kuanza maandalizi ya kuitafutia mechi za kirafiki za kimataifa, timu ya taifa, Taifa Stars, ili ijiweke vema kabla ya kukabiliana na wapinzani wao katika kuwania Fainali za Afrika na zile za Dunia.
Alisema amegundua Kocha Mkuu, Jan Poulsen amekuwa na wakati mgumu kwa matokeo mabaya ya timu yake kwa makosa yanayofanywa na TFF kwa kutoitafutia Stars mechi za kutosha kumpa nafasi kocha kurekebisha makosa.
"TFF lazima ibadilike na kuitafutia Stars mechi nyingi za kimataifa mapema, ili kumsaidia Poulsen, ni vigumu timu kufanya vema kama haipati mechi za maana za kujipima nguvu kabla ya kuingia kwenye ushindani," alisema.
Stars imepangwa kundi C katika makundi ya kuwania Fainali za Dunia zitakazofanyika Brazil, huku pia ikiwa na kibarua cha kuumana na Msumbiji katika mechi za mchujo za kuingia makundi ya kufuzu Fainali za Afrika 2013 zitakazochezwa nchini Afrika Kusini.

mwisho

No comments:

Post a Comment