STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, May 25, 2012

Jackson Chove ajipigia debe

KIPA wa timu iliyoshuka daraja ya Moro United, Jackson Chove, amesema yupo tayari kujiunga na timu yoyote itakayomhitaji kwa sababukiwango chake kipo juu licha ya timu yake kuporomoka. Chove, ambaye aliwahi kuzidakia Yanga, Prisons-Mbeya, JKT Ruvu na Azam kabla ya kutua Moro United, alisema kama mchezaji anatambua soka ndio ajira yake, hivyo kila siku anaendelea kujivua kujiweka fiti ili aendelee kutesa. Alisema, timu yoyote ambayo itaridhiana nae atakuwa tayari kujiunga nayo kwa ajili ya msimu ujao, ingawa alisisitiza kuwa yupo katika maandalizi ya kwenda Msumbiji kucheza soka la kulipwa. "Kwa kweli nipo tayari kutua timu yoyote baada ya timu yangu ya Moro Utd kushuka daraja, soka ndio kazi yangu hivyo kokote mie nacheza," alisema. Chove, aliyewahi kucheza soka la kulipwa nchini DR Congo na Rwanda kwa nyakati tofauti baada ya kutemwa Yanga, alisema anaamini yeye ni miongoni mwa makipa mahiri nchini, ila hajapata sehemu ya kuonyesha makali yake. Kipa huyo anayefahamika kama Mandanda, alisema kwa kuwa msimu mpya ndio unaanza sasa kwa klabu kusajili wachezaji wapya na kuacha wa zamani, naye anasubiri mahali atakapoangukia kwa ajili ya msimu ujao. Chove, alikuwa miongoni mwa makipa tegemeo wa Moro Utd iliyoshindwa kuhimili vishindo vya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu iliyoirejea toka daraja la kwanza na kuteremka pamoja na Polisi Dodoma na Villa Squad. Mwisho

TPBO yamlilia Mafisango, yaasa wachezaji Simba

OGANAIZESHENI ya Ngumi za Kulipwa nchini, TPBO, imetuma salamu za rambirambi kwa klabu ya soka ya Simba kutokana na msiba wa kiungo wao nyota, Patrick Mutesa Mafisango aliyefariki wiki iliyopita kwa ajali ya gari. Rais wa TPBO, Yasin 'Ustaadh' Abdallah, alisema wameshtushwa na kifo cha ghafla cha mchezaji huyo aliyekuwa kiigizo chema kwa wachezaji vijana nchini na kuungana na ndugu, jamaa na wadau wa klabu ya Simba kwa msiba huo. Ustaadh, alisema wadau wa ngumi hasa wanaopenda kuhudhuria michezo mbalimbali ya soka, wanajua namna gani Simba imepata pigo kwa kufiwa na kiungo huyo rais wa Rwanda ingawa mwenyeji wa DR Kongo. "TPBO tunaupa pole uongozi wa Simba na wadau wote wa klabu hiyo na soka kwa ujumla kwa kuondokewa na Patrick Mafisango, kama wadau tunaungana nao katika majonzi na kuwatakia moyo wa subira," Ustaadh alisema. Aliongeza kwa kuwataka wachezaji wenzake ambao anafahamu itawachukua muda mrefu kusahau kifo cha Mafisango kumuenzi mwenzao kwa kuiheshimu kazi yake aliyoifanya enzi za uhai wake kwa kuipa Simba mafanikio zaidi. "Najua ni vigumu wadau wa Simba kusahau msiba wa Mafisango, lakini TPBO tunaamini nnia pekee ni kumshukuru Mungu kwani kazi yake haina makosa na pia kumuenzi kwa kuipa Simba mafanikio zaidi," alisema. Patrick Mutesa Mafisango, aliyezikwa Jumapili iliyopita nyumbani kwao, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, alifariki usiku wa kuamkia Alhamisi iliyopita kwa kupata ajali ya gari akitokea Maisha Club 'kujirusha'. Kiungo huyo aliyewahi kung'ara na timu za TP Mazembe, APR, Azam kabla ya kutua Simba akiichezeapia timu ya taifa ya Rwanda 'Amavubi', amefariki akitokea kuisaidia Simba kutwaa taji la Ligi Kuu Tanzania Bara 2011-2012.

ZFA yaifungulia milango Yanga kutua Zenji

MSEMAJI WA ZFA, Munir Zakaria CHAMA cha Soka cha Zanzibar, ZFA, kimesema kipo tayari kuipokea klabu ya Yanga, iliyotishia kutaka kuhamia visiwani humo, mradi wafuate taratibu zinazokubalika. Wazee wa klabu ya Yanga walinukuliwa wiki iliyopita kwamba wanafanya mpango wa kuihamishia Yanga visiwani Zanzibar kutokana na kukerwa na maamuzi ya uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania, TFF 'kumbeba' Mwenyekiti wao, Llyod Nchunga. Wanachama hao wa Yanga wamekuwa na mgogoro na Nchunga kiasi cha kuitisha mkutano na kuung'oa uongozi huo, jambo lililopingwa na TFF kwa madai ya kutozingatia katiba inayoiongoza klabu hiyo. Jambo hilo lilionyesha kuwakewa wazee hao ambapo kupitia Katibu wake, Ibrahim Akilimali alinukuliwa akitishia kuihamisha Yanga Zanzibar kama njia ya kuikomoa TFF na Nchunga, kitu kilichoufanya uongozi wa ZFA kusema upo tayari kuwapokea. Msemaji wa ZFA, Munir Zakaria alinukuliwa na kituo kimoja cha redio alisema wao wanaisubiri Yanga kutua visiwani humo wakiamini itasaidia kuinua soka la Zanzibar. Zakaria, alisema pia kuhamia kwa Yanga visiwani humo kutaifanya Zanzibar itambe kimataifa na hivyo wanafungua milango kwa klabu hiyo, ila wakiitaka kuzingatia taratibu za kuweza kucheza ligi ya visiwani humo. "Tunawasubiri waje, hatuna vikwazo kwao kwa vile tunaamini watasaidia kuinua soka la visiwani humo, ila wafuate taratibu ikiwemo kama wanaweza wainunue klabu yoyote ya ligi kuu kisha waibadilishe jina kwa kuiita Yanga ili waweze kucheza ligi yetu," alisema. Msemaji huyo ambaye pioa ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya ZFA, alisema wao hawaoni tatizo kwa Yanga kujiunga katika ligi yao kwani ni moja ya timu yenye mashabiki wengi visiwani humo na ina jina kubwa katika anga la kimataifa. Hata hivyo, tishio hilo la wazee wa Yanga kutaka kuhamia Zanzibar linaonekana kama 'danganya toto' kwani baadhi ya wanachama wake wamewapuuza wazee hao wakiona kama wanaotapatapa katika kuubana uongozi wa Yanga. "Hatudhani kama hilo linaweza kufanyika, nadhani wazee wanatafuta njia ya kutaka kuungwa mkono katika kile walichokifanya ambacho kinaendana kinyume na katiba hata kama ni kweli viongozi wa Yanga wanakosa," alisema mmoja wa wanachama wa klabu hiyo aliyekataa kutajwa jina la kwa madai ya uhusiano wake wa karibu na wazee. Klabu ya Yanga imekuwa katika hali tete tangu walipopoteza taji lao la ubingwa wa Ligi Kuu kwa watani zao, na pia kupokea kichapo cha aibu cha mabao 5-0 mbele ya Simba katika mechi ya kufungia msimu wa ligi Tanzania Bara. Hata hivyo tayari Nchunga ameshatangaza kuachia ngazi mwenyewe kwa hiari yake, na hivyo suala au tisho la Yanga kuhamia Zenji huenda lisiwepo tena. TUSUBIRI TUONE!

Watanzania zidini kuniombea, tumaini la kupona lipo-Sajuki

NYOTA wa filamu ambaye yupo nchini India kwa matibabu, Juma Kilowoko 'Sajuki' amewataka Watanzania kuzidi kumuombea kwa Mungu ili aweze kupona matatizo yake, akisema wakati akituoa nchini humo kwa matibabu hali yake ilikuwa tete. Akizungumza toka India, Sajuki alisema hali yake ilikuwa mbaya alipofika nchini humo ambapo alipimwa na kukutwa hana damu na huku akiwa kadhoofika kiasi cha kushindwa kufanyiwa chochote. Alisema hata hivyo uangalizi aliopewa katika siku chache zilizopita hali yake imeimarika na sasa anasubiri kupimwa tena kuona kama anaweza kufanyiwa upasuaji kuondoa uvimbe ambao alidai umeongezeka sehemu nyingine ya tumbo lake. "kwa kweli mpaka nazungumza hivi ujue nimeimarika, nilikuwa na hali mbaya hasa baada ya kubainika kuwa kulikuwa na vivimbe vingine vilivyodhoofisha afya yangu na pia nilikuwa na upungufu wa damu, hivyo nikawa katika uangalizi maalum, ila nashukuru mno na ninawaomba Watanzania waniombee," alisema. Sajuki, alisema wakati wowote kuanzia sasa huenda akafanyiwa upasuaji ambao ndio unaoelezwa ni salama ya maisha yake. Wakati akiondoka nchini, Sajuki aliwaliza watu kutokana na kushindwa kutembea mwenyewe na pia alionekana kadhoofu maradufu tofauti na siku za nyuma kabla ya kusafiri kwenda kufanyiwa matibabu nchini humo. Msanii huyo anatibiwa katika hospitali ya Saifee iliyopo Mumbai na sio Apollo kama ilivyokuwa ikiripitiwa awali na vyombo vya habari.

Hili Dude la Kitale ni nouma!

MCHEKESHAJI maarufu nchini, Mussa Yusuf 'Kitale' ameachia wimbo mpya uitwao 'Hili Dude' ukiwa miongoni mwa nyimbo anazoziandaa kwa ajili ya albamu ya kwanza. Akizungumza na MICHARAZO, Kitale ambaye amepata umaarufu mkubwa kwa kuigiza kama 'teja', alisema tayari ameshausambaza wimbo huo mpya katika vituo vya radio huku video yake ikiwa katika hatua za mwisho kabla ya kuachiwa. Kitale alisema kibao hicho ni cha pili kwake baada ya awali kufyatua 'Chuma cha Reli' alichokiimba na Gondo Msambaa. "Nimekamilisha dude jipya, linaitwa 'Hili Dude' ambalo limeshaanza kurushwa hewani ikiwa ni utambulisho wa albamu yangu ambayo tayari nyimbo saba kati ya nane zimeshakamilika," alisema. Alisema katika wimbo huo mpya, ameimba kwa kushirikiana na Mide Zo na Corner ambaye pia ndiye prodyuza wa wimbo huo kutoka studio za Kwanza Records ya mjini Morogoro. Msanii huyo alizitaja nyimbo nyingine zitakazokuwa katika albamu hiyo kuwa ni 'Anajifanya Msela' alioimba na Juma Nature, 'Hili Toto' alioimba na Sharo Milionea na Mide Zo, ' Tulianzishe', 'Kinaunau' na 'Chuma cha Reli'. "Wimbo wa mwisho nimeshautunga, ila sijaurekodi kwa sababu bado naendelea kufanya mazungumzo na mmoja wa wasanii kwa ajili ya kuimba nae," alisema. Aliongeza, ameamua kutumbukia kwenye muziki baada ya kuona fani ya uchekeshaji ikiwa haimlipi kwa vile kazi nyingi hufanya chini ya watu ambao ndio hunufaika.

Dogo Aslay kupagawisha Dodoma

DKAMPUNI ya Ruhazi Promotion ya jijini Dar es Salaam, inatarajia kumtambulisha msanii chipukizi anayetamba hivi sasa katika muziki wa kizazi kipya nchini Aslahi Isihaka ‘Dogo Aslay’ kwa mashaki wa mjini Dodoma . Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jijini Dar es Salaam jana mratibu wa onesho hilo Jackline Masano, alisema kuwa onesho hilo litafanyika Jumamosi Juni 9 kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma . Alisema kuwa wasanii wengine kutoka kituo cha Mkubwa na Wanawe watamsindikiza na kuwa mazungumzo na wasanii wengine watakaopamba onesho hilo yanaendelea na kwamba watawatangaza pindi watakapomalizana nao. “Tumeamua kuwaletea wapenzi wa burudani wa Dodoma burudani ya uhakika Jumamosi ya Juni 9, litaanza saa 6:00 mchana na litamalizika saa 12:00 jioni ambapo Dogo Aslay akisindikizwa na wasanii kutoka mkubwa na Wanawe na wasanii nyota nchini ambao tutawatangaza majina yao tukishamaliza makubaliano nao,” alisema Jackline. Alisema pamoja na kwamba onesho hilo litapambwa na wasanii wengi lakini wameamua kiingilio kiwe cha shilingi 5,000 tu kwa wakubwa na shilingi 1000 kwa watoto ili kuwawezesha wapenzi wengi zaidi waweze kukimudu na kushuhudia burudani hiyo.

Steve Nyerere kusomesha yatima kwa miaka 7

MSANII wa filamu nchini ambaye pia huiga sauti za viongozi mbalimbali, Steve Mengele 'Steve Nyerere' jana amezindua filamu yake mpya inayojulikana kama 'Mwalimu Nyerere', huku akiahidi kuwasomesha watoto wawili yatima wa kituo cha Maunga Centre ulipofanyikia uzinduzi wa filamu hiyo. Akizungumza mara baada ya kuzindua filamu hiyo akiwa pamoja na watoto yatima wa kituo hicho, Steve Nyerere alisema ameamua kufanya hivyo kutokana na ukweli kwamba Baba wa Taifa Mwali Nyerere hakubagua watu. Alisema ujio wa filamu hiyo ni kama azma yake aliyoipanga tangu awali kuhakikisha anamuenzi Baba wa Taifa kwa kutoa filamu itakayokuwa inaonesha mambo mbalimbali aliyowahi kuyafanya Baba wa Taifa. "Jina lililonibeba zaidi katika tasnia hii ya filamu ni jina la Steve Nyerere kiasi ambacho hata jina la Baba yangu halijanizoea, hivyo kutokana na ukubwa wa jina hili limenifanya mimi kutambulika na jamii nzima ya Tanzania hivyo ili kulienzi jina hili nimeamua kutoa filamu hii ya Mwalim Nyerere,"alisema Steve. Alisema msaada alioutoa kwa watoto yatima hautaishia kwao bali ataendelea kutoa kile atakachokipata kupitia filamu hiyo kuwasaidia na wale wasiojiweza. Alisema filam ya Mwalimu Nyerere ameifanyia Butiama alipozaliwa Baba wa Taifa ili kujenga uhalisia wa kile alichodhamiria na kwamba ameitengeneza filamu hiyo kwa kipindi cha miezi mitatu huku akishirikiana vema na mke wa Hayati Baba wa Taifa Mama Maria Nyerere. Alisema jumla ya sh. milioni 25 ametumia katika kuikamilisha filam hiyo ambayo itaanza kuingia sokoni leo ikiwa chini ya usambazaji wa Steps Entertaiment. Kabla ya kutoa filam hiyo Steve Nyerere alitamba na filam ya 'Mr President' aliyoitunga kwa kuvaa uhusika wa Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Dkt.Jakaya Kikwete ambayo aliitaja kama zawadi kwa Rais Kikwete katika kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika

Twiga yapaa kuwafuata wahabeshi, wamwagiwa 'mihela'

TIMU ya taifa ya soka ya wanawake Tanzania, Twiga Stars imeondoka jana jioni kwa ndege ya Ethiopian Airlines kuelekea Ethiopia ikiwa imekabidhiwa Bendera ya Taifa na Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla. Twiga Stars yenye msafara wa watu 24 wakiwemo wachezaji, benchi la ufundi na viongozi itacheza na Ethiopia katika mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya michuano ya mchujo kwa ajili ya Fainali za Nane za Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) zitakazofanyika Novemba mwaka huu Equatorial Guinea. Mechi hiyo itafanyika Mei 27 mwaka huu kwenye Uwanja wa Addis Ababa wakati ile ya marudiano itachezwa Juni 16 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Twiga Stars ikifanikiwa kuitoa Ethiopia itakuwa imepeta tiketi ya kwenda Equatorial Guinea. Wachezaji walioondoka na kikosi hicho ni Amina Ally, Asha Rashid (nahodha), Ester Chabruma, Ettoe Mlenzi, Evelyn Sekikubo, Fadhila Hamad, Fatuma Bashiri, Fatuma Khatib, Fatuma Mustafa, Fatuma Omari, Maimuna Said, Mwajuma Abdallah, Mwanahamisi Omari, Mwanaidi Tamba, Mwapewa Mtumwa, Rukia Hamis, Semeni Abeid na Zena Khamis. Kwa upande wa Benchi la Ufundi ni Charles Mkwasa (Kocha Mkuu), Nasra Mohamed (Kocha Msaidizi), Furaha Francis (Meneja wa Timu), Mwanahamisi Abdallah (Mtunza Vifaa) na Christina Luambano (Daktari wa Timu). Twiga Stars ambayo msafara wake unaongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu kwa Wanawake Tanzania (TWFA) ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) itarejea nyumbani Mei 28 mwaka huu saa 6 mchana kwa ndege ya Ethiopian Airlines. Timu hiyo imeondoka ikiwa imemwagiwa posho toka serikalini na wadhamini wengine kama motisha ya kufanya vema katika mechio yao dhidi ya wahabeshi watakaoumana nao kesho Jumamosi. Katika hatua nyingine, Ligi ya Taifa inayoshirikisha mabingwa wa mikoa sasa itaanza Mei 27 mwaka huu badala ya Mei 26 mwaka huu kama ilivyokuwa imepangwa awali. Uamuzi wa kusogeza mbele kwa siku kuanza kwa ligi hiyo uliofanywa na Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana jana (Mei 23 mwaka huu). Timu 23 zitachuana katika kinyang’anyiro hicho kitakachofanyika katika vituo vya Kigoma (Uwanja wa Lake Tanganyika), Musoma (Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume) na Mtwara (Uwanja wa Umoja) ambapo kinatarajia kumalizika Juni 13 mwaka huu. Kituo cha Kigoma kina timu za Aston Villa ya Singida, Bandari (Kagera), CDA (Dodoma), JKT Kanembwa (Kigoma), Majimaji (Tabora), Mwadui (Shinyanga) na Pamba (Mwanza). Ashanti United ya Ilala, Flamingo (Arusha), Forest (Kilimanjaro), Korogwe United (Tanga), Nangwa VTC (Manyara), Polisi (Mara), Red Coast (Kinondoni) na Tessema ya Temeke ziko kituo cha Musoma. Kituo cha Mtwara kina timu za Kurugenzi ya Iringa, Lindi SC (Lindi), Mighty Elephant (Ruvuma), Mkamba Rangers (Morogoro), Mpanda Stars (Rukwa), Ndanda (Mtwara), Super Star (Pwani) na Tenende (Mbeya)

Nchunga aachia ngazi baada ya 'kutishwa'

Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga akisoma taarifa yake mbele ya waandishi wa Habari (hawapo pichani)jana jijini Dar, kutangaza kujiuzulu uongozi ndani ya klabu ya Yanga. MWENYEKITI wa Yanga, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga ametangaza kujiuzulu wadhifa wake jioni hii ofisini kwake, jengo la NSSF, barabara ya Bibi Biti, Dar es Salaam, siku moja baada ya kuvamiwa na kundi la watu nyumbani kwake, Mbezi, Jijini usiku wa wa manane. Hata hivyo, Nchunga amekataa kulihusisha tukio la kuvamiwa kwake usiku wa juzi na kujiuzulu kwake, akisema kwamba amefikia uamuzi huo kuinusuru Yanga, kwa sababu wapo watu wako tayari Yanga ife, lakini wamng'oe yeye madarakani, kitu ambacho yeye hapendi kitokee. Nchunga alisema kwamba majira ya saa nane usiku wa jana, alivamiwa na kundi la watu takribani 15, lakini hawakufanikiwa kufanya chochote kutokana na ulinzi mkali uliopo katika nnyumba hiyo. "Kwanza mbwa walianza kubweka, walinzi wakashituka wakaomba msaada kwa walinzi wenzao, nasi tukapuga simu polisi, wakaja haraka sana na kukuta watu hao wamekwishakimbia,"alisema ISOME TAARIFA RASMI YA KUJIUZULU KWA NCHUNGA: LLOYD NCHUNGA BIHARAGU C/O LLOYD ADVOCATES, Morogoro/Bibi TIti Mohamed Rd,7th Floor, J.K. Nyerere Pension towers P.BOX 75111, Dar-Es- Salaam,Tanzania. TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU KUJIUZULU NAFASI YA UENYEKITI WA KLAB YA YANGA. Ndugu wana Habari, najua kwamba taarifa hii itawafedhehesha wajumbe na wanayanga wanaotuunga mkono,hasa ukizingatia maamuzi ya pamoja ya vikao vyetu vya kamati ya utendaji vilivyopita kwamba hakuna wa kujiuzulu kati yetu mpaka tujue hatma ya mkutano mkuu ambao tulipanga ufanyike tarehe 15 Julai 2012, ukiachia mbali shinikizo la kujiuzulu linalotolewa na baadhi ya wazee na wanaojiita vijana wa klab, kwa wajumbe wa kamati ya utendaji, na hasa mimi kama mwenyekiti. Nawashukuru wajumbe kwamba tulifanya kazi kwa pamoja na kwa ushirikiano mzuri, na hata pale tulipotofautiana tulifanya hivyo kwa hoja na kufikia maazimio ambayo wote tulikuwa tunawajibika nayo. Tangu tumeingia madarakani tumeweza kushirikiana na kupata mataji matatu katika kipindi cha mwaka mmoja, yaani; Ngao ya Hisani 2010, Ubingwa wa ligi kuu ya Vodacom 2010/2011, na Ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup), 2011. Zaidi ni kwamba tuliuwa uteja kwa watani wetu wa jadi kila tulipokutana katika ligi ukiachia mbali mechi ya tarehe 6 Mei 2012, ambayo tulifungwa goli 5 bila, na kuleta mtafaruku mkubwa katika klab yetu. Hali kadhalika tumeshirikiana mpaka tumeweza kuboresha mkataba kati yetu na TBL kupitia Kilimanjaro Premium Lager, tumeingia mkataba na kampuni ya NEDCO kuendeleza mali zetu katika mtaa wa mafia na uwanja wetu wa KAUNDA baada ya kufikia hatua nzuri katika kupata hati miliki za maeneo yote mawili. Nafahamu kwamba kampuni hiyo iko katika hatua za mwisho za kumalizia michoro. Hali kadhalika tuliingia mkataba wa kuzalisha na kuuza bidhaa zenye nembo yetu na hasa baada ya kufanya marekebisho yatokanayo na matakwa ya sheria kule BRELA na pia mkataba na kampuni ya NEXUS LTD, ambayo itakuwa inatutafutia wadhamini wa nje na ndani, kufanya promosheni zetu na kampeni kwa njia ya electronic kupitia mitandao mbalimbali na kukusanya data za wanachama na kusajili wapya tukiwa na malengo ya kukusanya shilingi 300,000,000/= hadi 800,000,000/= kwa mwaka katika kipindi cha miaka mitatu. Haya yote tuliyafanya tukilenga kujitegemea kujazia mapengo yaliyokuwa yakitokana na kutegemea ufadhili wa mtu mmoja mmoja. Kwa ridhaa yenu tumekua tukiendelea na mazungumzo na makampuni mbali mbali kwa ajili ya udhamini na kwa sababu maalum, nitazitaja katika hati ya makabidhiano kwa kiongozi ajaye. Aidha, tumeshirikiana katika kufanya mambo mbali mbali ya kijamii, ikiwa ni pamoja na sikukuu ya kuadhimisha miaka 77 ya Yanga, sikukuu za pasaka, kuchangia jamii na waliokumbwa na maafa, na kongamano la vijana lililolenga kuwaamsha vijana kuitambua nafasi yao katika Yanga ikiwa ni pamoja na kupata azimio la kuanzisha SACCOSS ya Yanga, ambapo maombi yapo kwa msajili Manispaa ya Ilala. Haya yote nayataja ikiwa ni kuwashukuru kwa ushirikiano na ikiwezekana muweze kuyakamilisha yaliyobaki ambayo mtaona yalikuwa mazuri. Lakini pia tulipopata matatizo tulikuwa pamoja. Nichelee kusema tu kwamba tulisimama pamoja baada ya kujiuzulu Makamu Mwenyekiti wetu Ndugu Davis Mosha na mjumbe wetu ndugu Seif A. Seif, Ali Mayayi, na wengineo, kwani tulifungwa na katiba.Tulisimama pamoja pia katika suala la kujiuzulu ndugu Yusuf M. Manji, aliyekuwa mdhamini mteule na mfadhili mkuu ambaye sasa ameonyesha nia ya kurudi nanyi mkaridhia mkutane naye. Awali, tulitumia kila jitihada za kumrejesha lakini ikashindikana. Hata hivyo doa limetupata baada ya kufungwa na watani wetu goli 5 bila, ambapo kuna wanachama wanaoelewa na wasioelewa kabisa. Ninachokiona mimi ni usaliti wa hali ya juu uliombatana na matukio mbalimbali yaliyopita na yanayoendelea hadi kujaribu kupindua uongozi wa halali wa kidemokrasia. SIWATUHUMU WACHEZAJI MOJA KWA MOJA, isipokuwa mfululizo wa matukio wiki tatu kabla ya mchezo ule na sasa, inaonyesha kwamba kulikuwa na usaliti mkubwa ambao sisi hatukuweza kuubaini mapema. Sioni mantiki katika hoja kwamba wachezaji walikuwa wakidai mishahara, posho n.k. Au ati mtendaji wetu alishikiliwa Arusha kwa deni la hoteli, ndiyo tuvune bao 5! Kwa wanaoijua Yanga, imewahi kuwa na madeni makubwa katika Hoteli mbali mbali, mawakala wa ndege n.k, na baadhi tumeyakuta na sisi tumekuja tukayalipa. Hii imewahi kutokea kabla na wakati akiwepo mfadhili, sembuse sisi tulioachwa baki, na bado wachezaji walicheza kwa morali. Hata hivyo, utamaduni wa kutimuana baada ya matokeo mabaya ni dhambi ambayo itatula kama hatutaiacha, kwani wenye hila na uchu wa madaraka wataendelea kutumia mbinu hiyo ili kuuondoa uongozi wa kidemokrasia. Baada ya mapinduzi kushindikana na TFF kuonya kuhusu mapinduzi hayo, wazee kupitia msemaji wao , Mzee Akilimali wamesikika katika kipindi cha Michezo cha Redio moja maarufu hapa nchini wakidai kwamba ni bora Yanga ishushwe daraja au kufungiwa kuliko mimi kuendelea kuongoza! Hii imenikumbusha HEKMA ZA MFALME SELEMANI akiamulia ugomvi wa wanawake wawili waliokuwa wakigombea mtoto naye akaamuru wamgawane nusu kwa nusu. Yule mwenye mtoto kweli alimuomba Mfalme amuachie mwenzie kuliko kumkata nusu. Kwa hekma hiyo nimeamua kujiuzulu nafasi yangu katika Uenyekiti wa Yanga kwani ni klab ninayoipenda hata kama sio kiongozi kwa mujibu wa ibara ya 28 ya katiba yetu. Vile vile siko tayari kuona klab yangu ikisalitiwa au kuhujumiwa eti kwa sababu tu mimi ni kiongozi. Natumaini kamati ya utendaji kwa pamoja na wale tuliowateua chini ya ibara ya 29(3) ya katiba ya Yanga pamoja na bodi ya wadhamini, itawaongoza wanachama mpaka kufikia mkutano mkuu kwa mafanikio zaidi. Nitaendelea kuwa mwanachama mwadilifu na nitatoa mchango wangu wa hali na mali pale nitakapo hitajika na nikiwa na uwezo wa kufanya hivyo. YANGA DAIMA MBELE, NYUMA MWIKO. Wasalaam, LLOYD NCHUNGA BIHARAGU. Nakala kwa:- Mama Fatma Karume,Mdhamini Francis Kifukwe, Mdhamini Bwana Yusuf Manji – Kwa taarifa