STRIKA
USILIKOSE
Friday, May 25, 2012
Jackson Chove ajipigia debe
KIPA wa timu iliyoshuka daraja ya Moro United, Jackson Chove, amesema yupo tayari kujiunga na timu yoyote itakayomhitaji kwa sababukiwango chake kipo juu licha ya timu yake kuporomoka.
Chove, ambaye aliwahi kuzidakia Yanga, Prisons-Mbeya, JKT Ruvu na Azam kabla ya kutua Moro United, alisema kama mchezaji anatambua soka ndio ajira yake, hivyo kila siku anaendelea kujivua kujiweka fiti ili aendelee kutesa.
Alisema, timu yoyote ambayo itaridhiana nae atakuwa tayari kujiunga nayo kwa ajili ya msimu ujao, ingawa alisisitiza kuwa yupo katika maandalizi ya kwenda Msumbiji kucheza soka la kulipwa.
"Kwa kweli nipo tayari kutua timu yoyote baada ya timu yangu ya Moro Utd kushuka daraja, soka ndio kazi yangu hivyo kokote mie nacheza," alisema.
Chove, aliyewahi kucheza soka la kulipwa nchini DR Congo na Rwanda kwa nyakati tofauti baada ya kutemwa Yanga, alisema anaamini yeye ni miongoni mwa makipa mahiri nchini, ila hajapata sehemu ya kuonyesha makali yake.
Kipa huyo anayefahamika kama Mandanda, alisema kwa kuwa msimu mpya ndio unaanza sasa kwa klabu kusajili wachezaji wapya na kuacha wa zamani, naye anasubiri mahali atakapoangukia kwa ajili ya msimu ujao.
Chove, alikuwa miongoni mwa makipa tegemeo wa Moro Utd iliyoshindwa kuhimili vishindo vya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu iliyoirejea toka daraja la kwanza na kuteremka pamoja na Polisi Dodoma na Villa Squad.
Mwisho
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment