STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, May 25, 2012

ZFA yaifungulia milango Yanga kutua Zenji

MSEMAJI WA ZFA, Munir Zakaria CHAMA cha Soka cha Zanzibar, ZFA, kimesema kipo tayari kuipokea klabu ya Yanga, iliyotishia kutaka kuhamia visiwani humo, mradi wafuate taratibu zinazokubalika. Wazee wa klabu ya Yanga walinukuliwa wiki iliyopita kwamba wanafanya mpango wa kuihamishia Yanga visiwani Zanzibar kutokana na kukerwa na maamuzi ya uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania, TFF 'kumbeba' Mwenyekiti wao, Llyod Nchunga. Wanachama hao wa Yanga wamekuwa na mgogoro na Nchunga kiasi cha kuitisha mkutano na kuung'oa uongozi huo, jambo lililopingwa na TFF kwa madai ya kutozingatia katiba inayoiongoza klabu hiyo. Jambo hilo lilionyesha kuwakewa wazee hao ambapo kupitia Katibu wake, Ibrahim Akilimali alinukuliwa akitishia kuihamisha Yanga Zanzibar kama njia ya kuikomoa TFF na Nchunga, kitu kilichoufanya uongozi wa ZFA kusema upo tayari kuwapokea. Msemaji wa ZFA, Munir Zakaria alinukuliwa na kituo kimoja cha redio alisema wao wanaisubiri Yanga kutua visiwani humo wakiamini itasaidia kuinua soka la Zanzibar. Zakaria, alisema pia kuhamia kwa Yanga visiwani humo kutaifanya Zanzibar itambe kimataifa na hivyo wanafungua milango kwa klabu hiyo, ila wakiitaka kuzingatia taratibu za kuweza kucheza ligi ya visiwani humo. "Tunawasubiri waje, hatuna vikwazo kwao kwa vile tunaamini watasaidia kuinua soka la visiwani humo, ila wafuate taratibu ikiwemo kama wanaweza wainunue klabu yoyote ya ligi kuu kisha waibadilishe jina kwa kuiita Yanga ili waweze kucheza ligi yetu," alisema. Msemaji huyo ambaye pioa ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya ZFA, alisema wao hawaoni tatizo kwa Yanga kujiunga katika ligi yao kwani ni moja ya timu yenye mashabiki wengi visiwani humo na ina jina kubwa katika anga la kimataifa. Hata hivyo, tishio hilo la wazee wa Yanga kutaka kuhamia Zanzibar linaonekana kama 'danganya toto' kwani baadhi ya wanachama wake wamewapuuza wazee hao wakiona kama wanaotapatapa katika kuubana uongozi wa Yanga. "Hatudhani kama hilo linaweza kufanyika, nadhani wazee wanatafuta njia ya kutaka kuungwa mkono katika kile walichokifanya ambacho kinaendana kinyume na katiba hata kama ni kweli viongozi wa Yanga wanakosa," alisema mmoja wa wanachama wa klabu hiyo aliyekataa kutajwa jina la kwa madai ya uhusiano wake wa karibu na wazee. Klabu ya Yanga imekuwa katika hali tete tangu walipopoteza taji lao la ubingwa wa Ligi Kuu kwa watani zao, na pia kupokea kichapo cha aibu cha mabao 5-0 mbele ya Simba katika mechi ya kufungia msimu wa ligi Tanzania Bara. Hata hivyo tayari Nchunga ameshatangaza kuachia ngazi mwenyewe kwa hiari yake, na hivyo suala au tisho la Yanga kuhamia Zenji huenda lisiwepo tena. TUSUBIRI TUONE!

No comments:

Post a Comment