STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, October 12, 2013

Simba yaendelea kung'ang'ania kileleni, Yanga yalipa kisasi Kaitaba


Simba walioshinda jijini Dar
Yanga iliyotakata mjini Bukoba kwa kuilaza Kagera Sugar
BAO la kipindi cha pili lililofungwa na kiungo mkabaji, Jonas Mkude limeiwezesha Simba kuendelea kung'ang'ania kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara iliyomaliza raundi ya nane.
Simba ilipata ushindi wa bao 1-0 katika pambano kali lililochezwa kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam dhidi ya maafande wa Magereza, Prisons-Mbeya na kufikisha jumla ya pointi 18.
Kiti cha Simba kilikuwa hatarini siku ya leo iwapo kama ingeteleza na matokeo iliyopata watani zao wa jadi mjini Bukoba, baada ya kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya wenyeji wao Kagera Sugar.
Mkude alifunga bao hilo katika dakika ya 61 na kuiokoa timu yake kugawana pointi na Prisons iliyoonyesha upinzani mkubwa katika pambano hilo.
Bao hilo ambalo ni la tatu kwa Mkude katika orodha ya wafungaji mabao, lilikuwa likusubiriwa kwa hamu na mashabiki wa Simba ambao dakika 45 za kwanza walikuwa wanyonge na hasa walipokuwa wakipata matokeo ya pambano la mjini Bukoba.
Kwa ushindi huo Simba imesalia kileleni na kufuatiwa na Yanga ambao walipata mabao yake kupitia kwa Mrisho Ngassa aliyefunga kwa kichwa  dakika moja tu baada ya pambano hilo kuanza bao lilidumu hadi mapumziko.
Kipindi cha kilianza kwa wenyeji Kagera Sugar kusawazisha bao dakika mbili baada ya kuanza kwa kipindi hicho, lakini Yanga ilidhihirisha kuwa ilipania kuilipa kisasi na kufuta unyonge wake mbele ya Kagera kila wanapokutana Kaitaba kwa kuongeza bao la pili.
Mganda Hamis Kiiza 'Diego' alifunga bao hilo katika dakika ya 57, goli linalomfanya afikishe jumla ya mabao matatu mpaka sasa katika ligi ya msimu huu, ikiwa ni wiki moja kabla ya timu yake ya Yanga kukabiliana na Simba katika pambano la watani wa jadi litakalochezwa Okt. 20.
Ushindi huo wa Yanga umeifanya mabingwa watetezi hao kufikisha pointi 15, tatu nyuma ya Simba na iwapo itafanikiwa kushinda katika mechi yao ya Jumapili ijayo, huenda vijana hao wa Jangwani wakakikalia kiti cha uongozi baada ya kuenguliwa walipoyumba katika ligi hiyo.

Golden Bush, Pugu Veterani kuvaana kesho Kinesi

Ticotico (kushoto) katika moja ya mechi zao za maveterani

WAKALI wa soka la maveterani jijini Dar es Salaam, Golden Bush Veterani kesho asubuhi inatarajiwa kuvaana na Pugu Veterani katika pambano la kukata na shoka la kirafiki litakalochezwa kwenye uwanja wa Kinesi, Ubungo jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa ya uongozi wa Golden Bush inayoundwa na wakali za zamani wa Simba na Yanga, mechi hiyo ni ya kumaliza mzizi wa fitina baada ya tambo za muda mrefu, huku wakali hao wa soka la jiji wakiwatisha Pugu kwamba wajiandae kupokea kipigo kikali hiyo kesho.
Taarifa ya Golden Bush kupitia Msemaji na mlezi wa klabu hiyo, Onesmo Waziri 'Ticotico' inasomeka hivi:

Wadau,
 
Kutokana na vipigo vya mfululizo kutoka kwa wapinzani wetu wakiwepo Pugu Veterans, na tambo nyingi kutoka kwa wapinzani wetu hapa jijini, Golden bush tumelazimika kuomba mechi ya kirafiki ya marudiano na Pugu Veterans, game itapigwa uwanja wa Kinesi maarufu kama St James Park siku ya jumapili asubuhi.  Kwakutambua umuhimu ya game hii, uongozi wetu umeitisha kikao cha dharula kesho baada ya mazoezi asubuhi ili kuweka mikakati kabambe ya kurudisha heshima ya timu yetu ambayo mpaka sasa inatambulika kama mabingwa wa jiji la Dar es Salaam. Timu yetu imekamilika kabisa hakuna majeruhi hakuna mgonjwa hakuna mgogoro, uwanja uko sawa kamati ya ufundi inamaalizia kazi yake kwa kushirikiana na Walimu wetu. Tumejiwekea lengo la kufunga magoli mengi iwezekanavyo ili kuvunja rekodi ya kufunga magoli.
 
Aidha ningependa kutoa taarifa kwamba timu yetu imeimarika zaidi  mara baada ya Juma Kaseja, Said Swedi ,Mwarami Mohamed na Shadrack Nsajigwa  kurejea kwenye timu yetu.  karibuni mje muone soka la hali ya juu sana huku likihanikizwa na ufundi wa vijana wa zamani chini ya kocha wetu Madaraka Selemani “Mzee wa kiminyio”
 
Baada ya game ya jumapili, timu itakuwa kwenye maandalizi ya mwisho kabisa kwenda kucheza mechi za kirafiki visiwani Zanzibar.
 
Asanteni kwa kunisikiliza.
Onesmo Waziri “Ticotico” Mchezaji Mwandamizi

Mimi ndiye niyeyaruhusu Rai, Mwananchi-Waziri Makalla

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Mhe. Amos Makalla 'Mtu wa Watu'
 SIKU moja tu baada ya serikali kuyaonya magazeti ya Mwananchi kwa kukiuka adhabu ya kufungiwa na kuamua kutoa habari kwa njia ya mtandao huku gazeti la Mtanzania, kutumia gazeti la wiki la Rai kuchapishwa kila siku , Naibu Waziri Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Amosi Makala ameibuka na kusema ndiye aliyeyaruhusu kufanya hivyo.

Katika habari iliyochapishwa jana na gazeti moja la kila siku (siyo NIPASHE), lilinukuu agizo la serikali likionya mmiliki wa Mtanzania kuzingatia ratiba ya kutoa gazeti lao kila siku ya Alhamisi, la Rai na mmiliki wa Mwananchi, kuacha kuchapisha gazeti lao katika mtandao kama amri ya kufungiwa ilivyoainishwa.

Hata hivyo, wakati kauli za Waziri na Naibu wake, Makala, zikitofautiana, gazeti la Mwananchi limemaliza adhabu yake jana ya kufungiwa kwa siku 14.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Naibu waziri Makala, alisema yeye ndiye aliruhusu Gazeti la Mwananchi kuendelea na utoaji wa taarifa/habari kwenye tovuti yake, pia Gazeti la Rai kutoka kila siku.

“Ninalazimika kutoa ufafanuzi kwa njia ya maandishi kutokana na kupigiwa simu nyingi na waandishi wa habari kuhusiana na tamko jipya la Mkurugenzi wa Habari – Maelezo, Assah Mwambene kuhoji uhalali wa Gazeti la Mwananchi kuwa online na Gazeti la Rai kutoka kila siku, badala ya mara moja kwa wiki (Alhamisi),” alisema.

Makala alisema Oktoba 4, alifanya mazungumzo na viongozi wa Kampuni ya Mwananchi Communication Ltd (MCL) na New Habari Corporation (2006) Ltd kwa upande mmoja na msajili wa magazeti kwa upande mwingine.

Alisema katika kikao hicho cha pamoja na viongozi wa Magazeti ya Mwananchi na Mtanzania waliomba waziri apitie upya adhabu iliyotolewa kwa magazeti hayo, ambapo yeye (Makala) aliwaambia kwamba mwenye mamlaka juu ya suala hilo ni waziri mwenye dhamana na masuala ya habari pekee.

Kuhusu ombi la Mwananchi kuwa online na Gazeti la Rai kutoka kila siku badala ya kutoka siku ya Alhamisi, alisema New Habari walieleza kuwa siku zilizopita waliwahi kuomba kwa maandishi kwamba gazeti la Rai litoke kila siku. Maelezo ya Naibu Msajili wa Magazeti katika kikao hicho yalikuwa kwamba, kulikuwa na tatizo la kiufundi katika kurejea maombi hayo na akakiri kuwa hakuna kinachozuia gazeti la Rai kutoka kila siku. Kutokana na maelezo hayo mimi niliridhia gazeti hilo sasa liruhusiwe kutoka kila siku.

Aidha, alisema kuhusu gazeti la Mwananchi kuwa online, Naibu Msajili alisema hakuna sheria yoyote inayoweza kuzuia gazeti hilo kuwa online ila aliwataka lisionekane gazeti zima kama lilivyo, pia wabadili nembo (Master Head) kwa kuweka ya MCL na siyo ya gazeti husika ambalo limefungiwa. “Pia baada ya maelezo hayo niliridhia gazeti hilo liwe mtandaoni kwa kuzingatia angalizo lililotolewa na Naibu Msajili wa Magazeti,” alisema.

Alisema hoja ya tatu ilikuwa ni ile ya Serikali kupitia Idara ya Habari - Maelezo kuwa na uhusiano mzuri na vyombo vya habari, ili kuepuka misuguano isiyo ya lazima, ambapo pendekezo hilo alilipokea na kuliwasilisha kwa Waziri wa Habari kwa hatua zaidi, likiwamo suala la kupitia upya adhabu na ushauri wa kujenga uhusiano na vyombo vya habari.

Aliongeza kuwa masuala ya gazeti la Mwananchi kuwa online na Rai kutoka kila siku, alilitolea uamuzi siku hiyo hiyo. “Na uamuzi ni kwamba niliwaruhusu baada ya kuridhika kwamba hakukuwa na ukiukwaji wa sheria yoyote uliofanywa na waombaji.”

“Nimeamua kuweka sawa jambo hili kutokana na taarifa ya Mkurugenzi wa Maelezo ambayo ninaamini kwamba kutolewa na kusambazwa kwake ni kukosekana kwa mawasiliano kati yake kwa upande mmoja na Mhe. Waziri, Naibu waziri na Naibu Msajili wa Magazeti kwa upande mwingine.

“Hivyo aliyeruhusu Gazeti la Mwananchi kuwa online na Rai ni mimi na ndiyo maana kuanzia tarehe 5/10/2013 Gazeti la Rai lilianza kuchapwa kila siku na kusambazwa, na Gazeti la Mwananchi likaanza kuwa mtandaoni kwa kuzingatia maelekezo ya Naibu Msajili wa Magazeti,” alisema katika taarifa hiyo.

CHANZO: NIPASHE

Kivumbi cha FDL kuendelea wikiendi hii


KIVUMBI cha Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kwa makundi yote matatu kinatarajiwa kuendelea wikiendi hii ambapo kundi B litakuwa na mechi moja tu kati ya Lipuli na Mlale JKT itakayochezwa kesho (Oktoba 12 mwaka huu) katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora mjini Iringa.

Transit Camp itakwaruzana na Tessema katika Uwanja wa Mabatini mjini Mlandizi wakati Polisi Dar itaumana na African Lyon kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam katika mechi za kundi A zitakazochezwa kesho (Oktoba 12 mwaka huu).

Mechi nyingine ya kundi hilo itachezwa keshokutwa (Oktoba 13 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam kwa kuzikutanisha Friends Rangers na Villa Squad.

Timu zote nane za kundi C zinashuka viwanjani kesho (Oktoba 12 mwaka huu) kusaka pointi tatu. Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Polisi Dodoma na JKT Kanembwa ya Kigoma.

Pamba na Mwadui zitacheza katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, Polisi Tabora itaikaribisha Toto Africans kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora wakati uga wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma utatumika kwa mechi kati ya Polisi Mara na Stand United ya Shinyanga.

Simba, Yanga vitani Ligi Kuu Tanzania Bara

* Yanga yaapa kisasi Kaitaba, Prisons kuishusha Simba kileleni?

Simba itakayokuwa Taifa kuilika Prisons Mbeya
Yanga watakaokuwepo Kagera ili kulipa kisasi kwa Kagera Sugar
Kagera Sugar watakubali 'kufa' nyumbani Kaitaba?
 Na Boniface Wambura
LIGI Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inakamilisha raundi ya nane kesho (Oktoba 12 mwaka huu) kwa mechi tatu zitakazochezwa Dar es Salaam na Bukoba mkoani Kagera.

Simba ina fursa ya kuendelea kukamata usukani wa ligi hiyo iwapo itaishinda Tanzania Prisons ya Mbeya katika mechi itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni. Tanzania Prisons inayofundishwa na Jumanne Chale inashika nafasi ya kumi na moja katika msimamo wa ligi hiyo.

Ili iendelee kupanda katika nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi hiyo iliyoanza Agosti 24 mwaka huu, Tanzania Prisons ambayo katika mechi yake iliyopita ugenini ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mgambo Shooting inalazimika kuifunga Simba.

Licha ya sare ya bao 1-1 katika mechi yake iliyopita dhidi ya Ruvu Shooting, Simba inayoongoza kwa tofauti ya pointi moja dhidi ya Azam na Mbeya City matokeo mazuri katika mchezo huo ni muhimu kwao kama ilivyo kwa wapinzani wao Tanzania Prisons.

Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 ambapo tiketi zitauzwa uwanjani kwenye magari maalumu kuanzia saa 4 kamili asubuhi.

Mabingwa watetezi Yanga wao watakuwa mjini Bukoba kwenye Uwanja wa Kaitaba kuwakabili wenyeji Kagera Sugar wanaofundishwa na Mganda Jackson Mayanja akisaidiwa na Mrage Kabage.

Kagera ambayo inapishana na Yanga kwa tofauti ya pointi moja ilipoteza mechi iliyopita dhidi ya JKT Ruvu baada ya kulala kwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Azam Complex. Wakati Yanga ikiwa katika nafasi ya nne kwa pointi 12, Kagera Sugar ni ya sita kwa pointi kumi na moja.

Iwapo Kocha Ernst Brandts atawaongoza vijana wake wa Yanga kuibuka na ushindi katika mechi hiyo na Simba kufanya vibaya kwenye mechi dhidi ya Tanzania Prisons huenda akakamata uongozi wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 14.

Mwamuzi Zakaria Jacob wa Pwani ndiye atakayechezesha mechi kati ya Ashanti United na Coastal Union itakayopigwa Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam.

Raundi ya tisa ya ligi hiyo inaanza keshokutwa Jumapili (Oktoba 13 mwaka huu) kwa mechi kati ya Ruvu Shooting na Rhino Rangers (Mabatini, Mlandizi), Mgambo Shooting na Mbeya City (Mkwakwani, Tanga), Azam na JKT Ruvu (Azam Complex, Dar es Salaam) na Mtibwa Sugar na Oljoro JKT (Manungu, Turiani).

Mechi zitakazooneshwa moja kwa moja (live) na Azam TV kupitia TBC1 wikiendi hii ni kati ya Simba na Tanzania Prisons itakayochezwa Jumamosi katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na ile kati ya Azam na JKT Ruvu itakayofanyika Jumapili kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Nyalla wenzake wapeta TFF, washinda rufaa zao

KAMATI ya Rufani ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imewarejesha warufani wote watatu katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wa Kamati mpya ya Utendaji ya TFF utakaofanyika Oktoba 27 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Samwel Nyalla, Ayubu Nyaulingo na Ayoub Nyenzi walikata rufani mbele ya Kamati hiyo inayoongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Bernard Luanda kupinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF kuwaondoa katika uchaguzi huo ambapo wote wanagombea ujumbe wa Kamati ya Utendaji kuwakilisha kanda mbalimbali.

Akisoma uamuzi wao leo (Oktoba 11 mwaka huu) mbele ya Waandishi wa Habari kwenye ofisi za TFF, Jaji Luanda amesema baada ya kusikiliza hoja za Mrufani Nyalla walipitia Kanuni za Uchaguzi za TFF na kugundua yafuatayo;

Ibara ya 10(3) imeweka masharti makuu mawili ya ujazaji wa fomu za kugombea uongozi. Fomu hiyo ni lazima iwe na saini ya mgombea na ni lazima ithibitishwe na viongozi wa shirikisho.

Kamati imepitia Kanuni za Uchaguzi haijaona sehemu fomu hiyo ya uongozi imeambatanishwa ili kuifanya kuwa Kanuni ya Uchaguzi. Ni maoni ya Kamati kuwa ni vizuri fomu za kugombea zikawa ni sehemu ya Kanuni za Uchaguzi.

Kwa vile Kanuni za Uchaguzi za TFF za 2013 pia hazijaainisha nini adhabu kwa mgombea aliyekosea kujaza Fomu namba 1 ya kugombea uongozi, Kamati inaona itakuwa si haki kumnyima mgombea nafasi ya kushiriki katika uchaguzi kwa vile tu fomu yake haijajazwa vipengele vyote.

Nyalla aliondolewa kwenye uchaguzi na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa maelezo kuwa si mtu makini anayeweza kutekeleza majukumu yake kikamilifu baada ya kushindwa kujaza Fomu namba 1 kipengele cha 15 kinachohusu malengo ya mgombea uongozi.

Kwa upande wa Nyaulingo ambaye aliondolewa kwa kukosa uzoefu uliothibitika kulingana na Ibara ya 29(3) ya Katiba ya TFF na Kanuni ya 9(3) ya Kanuni za Uchaguzi za TFF, Kamati ya Rufani imeamua ifuatavyo;

Kamati ya Rufani ya Uchaguzi imepokea sababu za rufani na imepata fursa ya kusikiliza hoja na maelezo kutoka kwa Mrufani juu ya sababu zake alizozitoa kupinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi.

Mrufani alifafanua historia yake katika masuala ya michezo kuanzia alipokuwa anasema Chuo Kikuu kuanzia 2005-2009 na pia ushiriki wake kama mchezaji wa Rukwa United iliyowahi kushiriki Ligi ya Mkoa wa Rukwa na ligi nyingine za kitaifa.

Kwa kusoma maana ya ‘Familia ya TFF’ iliyoko kwenye utangulizi wa Katiba ya TFF, pamoja na Ibara ya 29(3) na 29(6) ya Katiba hiyo, Kamati imejiridhisha kuwa Mrufani ana sifa za kugombea uongozi wa Shirikisho na amekidhi kigezo cha sifa za ugombea.

Ameshiriki kwenye mchezo wa mpira wa miguu kama mchezaji na mtawala, hivyo kutimiza kigezo kilichohitajika cha ushiriki katika uongozi na utawala wa mchezo wa mpira wa miguu kwa muda usiopungua miaka mitano.

Kwa kuzingatia hayo, Kamati ya Rufani ya Uchaguzi inaruhusu rufani ya Mrufani. Uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi umetenguliwa na Mrufani anapewa nafasi ya kushiriki katika uchaguzi.

Kuhusu Ayubu Nyenzi aliyeondolewa kwa kukosa uzoefu kwa mujibu wa Ibara ya 29(3) ya Katiba ya TFF na Kanuni ya 9(3) ya Kanuni za Uchaguzi za TFF, na pia kushindwa kuthibitisha uraia wake mbele ya Kamati ya Uchaguzi, Kamati ya Rufani katika uamuzi wake imesema;

Imepokea sababu za rufani na imepata fursa ya kusikiliza hoja na maelezo kutoka kwa Mrufani juu ya sababu zake alizozitoa kupinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi.

Baada ya uchambuzi wa kina, Kamati imeona kuwa kulingana na maelezo yaliyotolewa na Mrufani na viambatanisho vilivyowasilishwa, Kamati haina shaka kuhusu uraia wake. Uthibitisho wa uraia unapaswa kufanywa kwa umakini na taasisi yenye mamlaka ya kiserikali kufanya hivyo.

Kamati pia imejiridhisha kupitia Fomu namba 1 iliyojazwa na kusainiwa na Mrufani kuwa kuanzia mwaka 2004 mpaka 2010, Nyenzi ameshika nyadhifa za utawala wa mpira wa miguu na hasa katika klabu ya Yanga, uzoefu unaomfanya kuwa na sifa ya kugombea nafasi ya uongozi katika TFF kulingana na Ibara ya 29(3) ikisomwa pamoja na Ibara ya 29(6).

Kwa kuzingatia hayo, Kamati ya Rufani ya Uchaguzi inaruhusu rufani ya Mrufani. Uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi umetenguliwa na Mrufani atashiriki katika uchaguzi wa TFF kwa nafasi anayogombea.

Wakati huo huo, Kamati ya Rufani ya Maadili ya TFF inakutana keshokutwa (Oktoba 13 mwaka huu), kufanyia mapitio (revision) ya uamuzi wa Kamati ya Maadili kwa waombaji uongozi wanane kama ilivyoombwa na Sekretarieti ili kutoa mwongozo wa utekelezaji wa uamuzi huo.

Wanahabari wakumbushwa kuomba vitambulisho WC 2014

http://www.cambury.edu.br/blog/marketingepp/files/2011/11/logo-copa-2014.jpg
MAOMBI ya vitambulisho kwa waandishi wa habari (Accreditation) wanaotaka kuripoti Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani nchini Brazil kwa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) yataanza kupokelewa kwa mtandao Desemba 7 mwaka huu kupitia akaunti ya FIFA Media Channel.

Mwisho wa kupokea maombi hayo itakuwa Januari 31 mwakani, hivyo kwa waandishi wanaotaka kupata vitambulisho hivyo ni lazima wawe na akaunti ya FIFA Media Channel pamoja na utambulisho wa mtumiaji wa akaunti hiyo (user ID).

Kwa mujibu wa FIFA, kila nchi itapewa idadi maalumu ya nafasi kwa waandishi (waandishi wa kawaida pamoja na wapiga picha) baada ya mechi za mchujo za Kombe la Dunia kumalizika ambapo vigezo mbalimbali vitazingatiwa ikiwemo nchi kufuzu kwa fainali hizo.

Hivyo, nchi ambayo itakuwa imefuzu itakuwa na nafasi zaidi kulinganisha na zile ambazo hazitakuwa na timu katika fainali hizo za Brazil.

Mgawanyo wa nafasi zitakazotolewa kwa Tanzania utapangwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kulingana na maombi yatakayokuwa yamewasilishwa FIFA kupitia FIFA Media Channel.

TFF inatoa mwito kwa waandishi wa habari za mpira wa miguu ambao hawana akaunti FIFA Media Channel kuhakikisha wanakuwa nayo mapema ili waweze kutuma maombi yao.

Filama ya Dasmila karibuni kutoka hadharani

FILAMU  mpya ya Dasmila inatarajia kuingia sokoni mwishoni mwa mwezi huu. Akizungumza jijini Dar, Mkurugenzi wa  DJ Marketing & Promotion ambao ndio wasambazaji wa kazi hiyo, Haulle Daniel amesema kazi hiyo ime kamilika kwa asilimia zote hivyo wapenzi wa filamu wakae mkao wa kula kwani imewashirikisha wasanii wengi akiwemo Shamsa Frod,Jack Pentzel, Elias Mkali, Shaban Dicosta na wasanii wengine wanaotamba katika anga za filamu nchini. Filamu hiyo ya mapenzi ambayo kuna mambo mbalimbali ya kuelimisha jamii ya kitanzania ambapo Dasmila aliyeuawa kipindi cha nyuma kidogo, arudi tena kama mzimu, na mengi yanatokea. Fuatilia.. Familia, vichekesho na vimbwanga, mapenzi, kukosa uaminifu, visa na mikasa kibao  ambayo yatapatikana katika filamu hiyo, ambayo imetengenezwa kwa ubora wa ali ya juu na itakayokuwa ikisambazwa na kampuni ya kizalendo ya DJ Marketing ya jijini Dar es salaam.