STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, October 12, 2013

Simba, Yanga vitani Ligi Kuu Tanzania Bara

* Yanga yaapa kisasi Kaitaba, Prisons kuishusha Simba kileleni?

Simba itakayokuwa Taifa kuilika Prisons Mbeya
Yanga watakaokuwepo Kagera ili kulipa kisasi kwa Kagera Sugar
Kagera Sugar watakubali 'kufa' nyumbani Kaitaba?
 Na Boniface Wambura
LIGI Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inakamilisha raundi ya nane kesho (Oktoba 12 mwaka huu) kwa mechi tatu zitakazochezwa Dar es Salaam na Bukoba mkoani Kagera.

Simba ina fursa ya kuendelea kukamata usukani wa ligi hiyo iwapo itaishinda Tanzania Prisons ya Mbeya katika mechi itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni. Tanzania Prisons inayofundishwa na Jumanne Chale inashika nafasi ya kumi na moja katika msimamo wa ligi hiyo.

Ili iendelee kupanda katika nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi hiyo iliyoanza Agosti 24 mwaka huu, Tanzania Prisons ambayo katika mechi yake iliyopita ugenini ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mgambo Shooting inalazimika kuifunga Simba.

Licha ya sare ya bao 1-1 katika mechi yake iliyopita dhidi ya Ruvu Shooting, Simba inayoongoza kwa tofauti ya pointi moja dhidi ya Azam na Mbeya City matokeo mazuri katika mchezo huo ni muhimu kwao kama ilivyo kwa wapinzani wao Tanzania Prisons.

Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 ambapo tiketi zitauzwa uwanjani kwenye magari maalumu kuanzia saa 4 kamili asubuhi.

Mabingwa watetezi Yanga wao watakuwa mjini Bukoba kwenye Uwanja wa Kaitaba kuwakabili wenyeji Kagera Sugar wanaofundishwa na Mganda Jackson Mayanja akisaidiwa na Mrage Kabage.

Kagera ambayo inapishana na Yanga kwa tofauti ya pointi moja ilipoteza mechi iliyopita dhidi ya JKT Ruvu baada ya kulala kwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Azam Complex. Wakati Yanga ikiwa katika nafasi ya nne kwa pointi 12, Kagera Sugar ni ya sita kwa pointi kumi na moja.

Iwapo Kocha Ernst Brandts atawaongoza vijana wake wa Yanga kuibuka na ushindi katika mechi hiyo na Simba kufanya vibaya kwenye mechi dhidi ya Tanzania Prisons huenda akakamata uongozi wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 14.

Mwamuzi Zakaria Jacob wa Pwani ndiye atakayechezesha mechi kati ya Ashanti United na Coastal Union itakayopigwa Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam.

Raundi ya tisa ya ligi hiyo inaanza keshokutwa Jumapili (Oktoba 13 mwaka huu) kwa mechi kati ya Ruvu Shooting na Rhino Rangers (Mabatini, Mlandizi), Mgambo Shooting na Mbeya City (Mkwakwani, Tanga), Azam na JKT Ruvu (Azam Complex, Dar es Salaam) na Mtibwa Sugar na Oljoro JKT (Manungu, Turiani).

Mechi zitakazooneshwa moja kwa moja (live) na Azam TV kupitia TBC1 wikiendi hii ni kati ya Simba na Tanzania Prisons itakayochezwa Jumamosi katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na ile kati ya Azam na JKT Ruvu itakayofanyika Jumapili kwenye Uwanja wa Azam Complex.

No comments:

Post a Comment