STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, December 2, 2013

Tangulia Tabu Ley Rochereau, tutakukumbuka daima

Tabu :ley akiwa na Mbilia Bel
BRUSSELS, Ubelgiji
MWANAMUZIKI mkongwe wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Pascal Tabu Ley Rochereau, amefariki katika hospitali moja ya mjini Brussels.

Tabu Ley, alifariki juzi saa mbili usiku baada ya kuugua kwa muda mrefu ugonjwa wa kiharusi. Alianza kuugua ugonjwa huo tangu 2008.

Meneja wa zamani wa mwanamuziki huyo, Mekansi Modero, ambaye kwa sasa anaishi nchini Marekani, amethibitisha taarifa za kifo cha Tabu Ley, baada ya kuthibitishiwa na ndugu wa karibu wa mkongwe huyo.

Mwanamuziki Nyboma Mwandido, anayeishi mjini Paris, Ufaransa pia amethibitisha taarifa za kifo cha mwanamuziki huyo mkongwe.

Tabu Ley alikuwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa huo kwa muda mrefu na alikuwa akitembea kwa kutumia baiskeli maalumu kutokana na kushindwa kutembea kwa miguu.

Kifo cha Tabu Ley kimewapa simanzi kubwa mashabiki wa muziki barani Afrika, kutokana na kuwa mmoja wa watu mahiri, ambaye nyimbo zake zilikuwa na mvuto wa aina yake.

Katika miaka ya hivi karibuni, Tabu Ley aliamua kuachana na muziki na kujitosa katika masuala ya siasa, baada ya kuteuliwa kuwa waziri katika serikali ya Rais wa zamani wa DRC, Laurent Kabila mwaka 1997

Awali, Tabu Ley alilazimika kuikimbia DRC na kwenda kuishi uhamishoni nchini Ubelgiji kutokana na kutoelewana na rais wa zamani wa nchi hiyo, marehemu Mobutu Sese Seko.

Kabla ya kwenda Ubelgiji, Tabu Ley aliishi kwa muda nchini Ufaransa akipatiwa matibabu ya ugonjwa huo. Baada ya hali kuanza kuwa mbaya, alihamishiwa Ubelgiji kwa ajili ya kupatiwa matibabu maalumu.

Enza za uhai wake, Tabu Ley alikuwa akichuana vikali na wakati nyota wa DRC wa wakati huo kama vile Joseph Kabasele, Nicolas Kasanda na Rwambo Lwanzo Makiadi 'Franco'.

Alianza kujihusisha na muziki 1959 akiwa mtunzi, mwimbaji na mcheza shoo akiwa katika bendi ya African azz, iliyokuwa ikiongozwa na Kabasele. Mkongwe huyo amerekodi na kuimba nyimbo zaidi ya 2,000 na kutoa albamu 250.

Alizaliwa 1940 katika mji wa Bandundu nchini DRC. Alianza maisha akiitwa Pascal Tabu. Akiwa na umri wa miaka 14, aliandika wimbo wake wa kwanza Bessama Muchacha,  ambao aliurekodi na kundi maarufu la African Jazz, lililokuwa chini ya Kasebele, (asichanganywe na Pepe Kalle).

Aliendelea na shule na hatimae alipomaliza sekondari 1959, ndipo alipojiunga rasmi na African Jazz.

Alikuwa mmoja wa wanamuziki walioimba wimbo Independence Cha Cha, wa Grande Kalle, uliotikisa anga la Afrika miaka ya 1960. Wimbo huo ukawa rasmi wa kusherehekea uhuru wa DRC.

Baada ya miaka minne, alijiengua katika kundi la African Jazz. Akiwa na mpiga gita mahiri, Nicholaus Kassanda, wakaanzisha kundi la African Fiesta, ambalo alidumu nalo hadi 1965.

Wakati DRC ikiwaka moto kimuziki na ushindani kuwa mkali, aliamua kuachana na  Nico na kuanzisha kundi lake la African Fiesta National au mara nyingine ikiitwa Africa Fiesta Flash na kurekodi kibao maarufu cha Afrika Mokili Mobimba, ambacho kilivuka mauzo ya nakala milioni moja miaka ya 1970 na kuiingiza bendi hiyo kuwa kati ya bendi zilizopata mafanikio ya juu katika Afrika kwa wakati huo.

Wanamuziki kama Papa Wemba na Sam Mangwana ni miongoni mwa wakongwe waliowahi kupitia katika kundi hili tishio.

Mwaka 1970, Tabu Ley alianzisha bendi ya Orchestre Afrisa International. Wakati huo Afrisa na TPOK Jazz, ndizo zilizokuwa bendi maarufu zaidi Afrika. Afrisa waliteremsha vibao kama Sorozo, Kaful Mayay, Aon Aon na Mose Konzo.

Kutokana na umahiri wake, Tabu Ley aliweza kupata tuzo kutoka serikali za nchi kama Chad, iliyompa heshima ya 'Officer of The National Order' wakati Senegal ilimpa heshima ya 'Knight of Senegal' na akawa sasa anaitwa Siegneur Rochereau.

Katikati ya miaka ya 1980, Tabu Ley aligundua kipaji cha mwanamama aliyekuja kutikisa anga za Afrika, Mbilia Bel. Baadae Tabu Ley alimuoa Mbilia, wakapata mtoto mmoja.

Nyimbo kama Nadina, Nakei Nairobi zinaonyesha kipaji gani alikuwa nacho mwanamama huyo, aliyekuwa mzuri kwa sura, aliyejua pia kucheza na kutawala jukwaa vizuri.

Mwaka 1988, Tabu Ley akagundua kipaji cha mwimbaji mwingine wa kike, Faya Tess. Hapo Mbilia akaacha bendi na kuendelea na maisha yake ya muziki peke yake. Katika kipindi hicho, mtindo wa Soukus uliokuwa na mapigo yenye mwendokasi zaidi ya ile ya rumba ya Afrisa na TP OK Jazz, ulianza kuzishika nyoyo za vijana, bendi hizi kubwa zikaanza kufifia.

Mwanzoni mwa miaka ya 1990, Tabu Ley, alihamia Marekani, akawa anaishi Kusini mwa California na kubadili  muziki wake katika kujaribu kujikita zaidi katika soko la kimataifa.Akatunga nyimbo kama Muzina, Exil Ley na Babeti Soukous.

Mwaka 1996, Tabu Ley, alishiriki katika album ya kundi la Africando, akiimba wimbo wa Paquita, ambao aliurekodi miaka ya 1960, akiwa na African Fiesta.

Tabu Ley alipata cheo cha uwaziri katika utawala wa Kabila baada ya kuondolewa kwa Mobutu. Hata baada ya kifo cha Kabila, 2005, alipewa cheo cha gavana.

Mwaka 2006,  Tabu Ley,  alishirikiana na rafiki yake wa  muda mrefu, Maika Munah na kurekodi album yake ya mwisho, iliyoitwa Tempelo. Katika albumu hiyo, binti yake, Melodie aliimba nyimbo kadhaa.

Inaelezwa kuwa mkongwe huyo ameacha zaidi 54 kutoka kwa wanawake 36 aliozaa nao kwa nyakati tofauti.