STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, December 2, 2013

Coastal Union mabingwa wapya Uhai Cup

 
MABAO mawili yaliyofungwa kipindi cha pili yalitosha kuiwezesha Coastal Union ya Tanga kunyakua taji la Uhai Cup ikiwa ni mara yao ya kwanza baada ya kuifunga Yanga katika pambano la Fainali la michuano hiyo.
Pambano la kuhitimisha michuano hiyo inayoshirikisha timu za vijana U20 lilichezwa kwenye uwanja wa Chamazi, lilishuhudia timu hizo zikienda mapumziko zikiwa hazijafungana.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na Coastal kuonyesha dhamira ya kulipa kisasi cha kufungwa 2-1 na Yanga katika mechi ya makundi kwa kujipatia bao la kuongoza lililofungwa dakika ya 52 na Ally Nassor.
Dakika moja kabla ya kumalizika kwa pambano hilo, Mahadhi Juma aliongeza bao la pili kutokana na pasi za videoni zilizopigwa na wachezaji wa Coastal ndani ya lango la Yanga kabla ya mfungaji kutumbukiza wavuni.
Kwa kutwaa ubingwa huo, Coastal wamezawadiwa Sh. Milioni 2 na wadhamini wa michuano hiyo, Maji ya Uhai wakati washindi wa pili Yanga wamezawadiwa Sh. Milioni 1.5 na Azam FC walioshika nafasi ya tatu wamepewa Sh. Milioni.
Mtoto wa beki wa zamani wa kimataifa Tanzania, Salum Kabunda ‘Ninja Msudan’ (sasa marehemu) aitwaye Ally Salum Kabunda wa Ashanti United ameibuka mfungaji bora wa mashindano kwa mabao yake tisa, ingawa timu yake iliishia Robo Fainali na kutolewa na Yanga.   
Azam walipata nafasi ya tatu baada ya kuifunga Mtibwa katika pambano lililotangulia fainali hiyo kwa mikwaju ya penati 3-1 baada ya timu hizo kumaliza dakika 120 zikiwa sare ya 3-3.
Dakika 90 za awali timu hizo zilifungana mabao 2-2 na katika muda wa nyongeza za dakika 30 timu hizo zilifungana tena bao 1-1 na kufanya matokeo kuwa 3-3 kabla ya kupigiana penati. Azam ndiyo waliokuwa mabingwa watetezi wa taji hilo.

No comments:

Post a Comment