STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, September 11, 2014

BFT yasogeza mbele mashindano ya Taifa hadi Nov 3.

http://www.eatv.tv/sites/default/files/styles/detailpageimg/public/field/image/ngumilo.JPG?itok=lsVKoZrLMASHINDANO ya Taifa ya Ngumi za Ridhaa yaliyokuwa yafanyike mwezi ujao yameota mbawa baada ya Shirikisho la mchezo huo nchini (BFT) kutangaza kuyasogeza mbele hadi Novemba.
Katibu Mkuu wa BFT, Makore Mashaga aliiambia MICHARAZO kuwa,  michuano hiyo iliyokuwa ianze kutimua vumbi lake kati ya Oktoba 8-14 sasa yataanza Novemba 3-8 kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wao.
Mashaga alisema alisema wameamua kuahirisha michuano hiyo ili kupisha mashindano ya ngumi ya kimataifa yanayoandaliwa na Chama cha Ngumi cha wilaya ya Temeke (TABA) ambayo yatafanyika mwezi ujao.
Katibu huyo alisema wameona siyo busara kuendesha michuano ya taifa na mashindano hayo ya kimataifa ambayo yamedhaminiwa na kampuni ya mtandao wa simu za mkononi ya Zantel.
"Tumeamua kuahirisha mashindano ya taifa ya ngumi hadi Novemba kupisha michuano ya kimataifa iliyoandaliwa na wanachama wetu mkoa wa Temeke, kuahirishwa huko kwa mwezi mzima ni fursa nzuri kwa mikoa kujipanga vema kabla ya kuja jijini Dar," alisema.
Mashaga alisema BFT inawatakia kila la heri timu za mikoa ambazo wameshawajulisha juu ya kuahirishwa kwa mashindano ya taifa, pia wakiipongeza Zantel kwa kujitolea kudhamini mashindano hayo ya kimataifa ya Temeke  kwa kutoa Sh. Milioni 10.
"BFT inawapongeza wadhamini wao na kuhimiza makampuni mengine kuiga mfano huo kwa lengo la kusaidia kuinua mchezo huo wa ngumi ambao umekuwa ukipambana kurejesha heshima ya Tanzania katika mazingira magumu," alisema Mashaga.
Katibu huyo wa BFT alisisitiza kuwa taratibu nyingine za mashindano ya Taifa yanaendelea kama kawaida na kwamba michuano hiyo itafanyikia kwenye uwanja wa Ndani wa Taifa.

Chicharito amvulia kofia Ronaldo, adai ni bora kuliko Messi

http://www.lapatilla.com/site/wp-content/uploads/2011/10/balon-de-oro-2011_323x216.jpg
MSHAMBULIAJI mpya wa Real Madrid, Javier Hernandez 'Chicharito' amesema tayari ameshawishika kwamba Cristiano Ronaldo ni bora zaidi ya Lionel Messi.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Mexico amejiunga na mabingwa hao wa Ulaya kwa mkopo wa msimu mmoja akitokea Manchester United muda mfupi kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili.
Hata hivyo, Chicharito, ambaye alitua Old Trafford mwaka mmoja baada ya Ronaldo kutimkia Madrid, amesema tayari amedatishwa na mambo makubwa yanayofanywa na Mreno huyo mazoezini.
Bila ya shaka, Ronaldo ndiye bora," mshambuliaji huyo mwenye miaka 26 aliliambia gazeti la El Chiringuito.
"Katika muda mfupi niliokuwapo hapa, nimemuona yeye ndiye bora zaidi duniani.
"Si kwamba hufanya vyema sana katika mechi tu bali hata kila siku.
"Kwangu mimi, Cristiano ndiye bora zaidi. Messi yuko matawi hayo pia; baada ya Cristiano, anafuatia Muargentina yule."

Mama Mkwe wa Jennifer Mgendi kutolewa Sept 22

FILAMU mpya ya muimbaji nyota wa Nyimbo za Injili nchini, Jennifer Mgendi iitwayo 'Mama Mkwe' itatolewa rasmi Septemba 22 mwaka huu.
Akizungumza na MICHARAZO, Mgendi alisema filamu hiyo iliyokamilika hivi karibuni akiwa ameigiza na wakali wa filamu na miondoko ya Injili akiwamo Mussa Banzi na Bahati Bukuku itatoka mtaani siku hiyo.
Mgendi amewataka mashabiki wa filamu wasiikose filamu hiyo kutokana na kubeba ujumbe mwanana wenye mafunzo makubwa kwa jamii.
Alisema filamu hiyo iliyoongozwa na Mgeni Khamis na Chrissant Mhega wa Mega  Video Production imekamilika wiki iliyopita.
Mgendi anayetamba na albamu ya Hongera Yesu, alisema ndani ya filamu hiyo inayozungumzia mkasa wa mama mkwe anayemlilia mwanae wa kiume kumletea mjukuu na kuzua kizaazawa wamo pia Senga,Bi Bi Esther, Christine Matai, Husna Chobis. yeye (Mgendi)  na wengine ambao wameinoigesha vilivyo.
"Nimekamilisha filamu yangu mpya ya 'Mama Mkwe' ambayo nimeigiza mimi, Bahati (Bukuku) Christine Matai, Senga, Bi Esther, Mussa Banzi na wengine. Ni filamu yenye mafunzo makubwa kwa jamii na hasa mama wakwe wanaoingilia ndoa za watoto wao," alisema.
Kabla ya filamu hiyo, Jennifer amewahi kutamba na filamu kadhaa kama 'Chai ya Moto', 'Joto la Roho', 'Teke la Mama', na 'Pigo la Faraja'.

Ruvu Shooting kupimana ubavu na 94 KJ Lugalo leo jioni

TIMU ya maafande wa Ruvu Shooting inayojiandaa na Ligi Kuu Tanzania Bara jioni ya leo inatarajiwa kushuka dimba la Lugalo kuvaana na maafande wenzao wa 94 KJ katika mchezo wa kirafiki.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa muda mfupi uliopita na Afisa Habari wa timu hiyo, pambano hilo ni maalum kwa ajili ya kumpa nafasi kocha wao Mkenya Tom Olaba kuangalia mapunfugu wa kikosi chake dakika za mwisho mwisho kabla ya kujichimbia kuisubiri Ligi itakayoanza Septemba 20.
Timu hiyo ambayo ilimaliza katika nafasi ya sita msimu uliopita ikilingana pointi na Simba na Kagera Sugar kila moja ikiwa na 38, inasema wanaamini timu hiyo ya 94 KJ iliyopo Ligi Daraja la Kwanza itawapa mazoezi ya kutosha vijana wao katika pambano hilo la leo.
Ruvu iliyoingia kambini tangu Juni 9 imekuwa ikichgeza mechi kadhaa za kirafiki tayari kwa ajili ya Ligi Kuu ambapo watafungua dimba kwa kuumana na maafande wa Magereza, Prisons Mbeya katika pambano litakalochezwa kwenye uwanja wa Mabatini.
Msimu uliopita walifungua dimba na wapinzani wao hao na kuwanyuka mabao 3-0, kitu ambacho Bwire anaamini hata msimu huu mambo yatakuwa hivi hivyo katika pambano hilo la ufunguzi wa ligi Jumamosi ijayo.