STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, April 19, 2012

Rage awatuliza wana Simba kuhusu Ngassa

WAKATI klabu ya soka ya Azam ikikanusha taarifa kwamba winga wao nyota, Mrisho Ngassa kuwa na mipango ya kutua Simba, Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage, amewatoa hofu wanachama wa klabu hiyo kwa kuwaeleza 'SUBIRINI TUONE'. Rage, alisema kama Ngassa atatua Msimbazi au la, litafahamika baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu Tanzania Bara, ila kwa sasa ni mapema mno kulizungumzia hilo. "Kama wao wamekanusha kwamba huyo mchezaji atakuja Simba, basi subirini, ila kwa sasa ni vigumu kuanza kulisemea hilo wakati hatujui mkataba wa Ngassa na klabu yake ukoje," alisema Rage. Mwenyekiti huyo mwenye 'kismati' na klabu hiyo ya Simba, alisema kuanza kumzungumzia Ngassa kabla hawajawasiliana na uongozi wa Azam ni kwenda kinyume na sheria za FIFA, ila amesisitiza watu wasubiri kujua ukweli wa mambo. Juzi chombo kimoja cha habari kiliripoti taarifa kwamba Simba inakaribia kumnyakua Ngassa kwa ajili ya kuichezea timu hiyo kwenye michuano ya kimataifa, hiyo itafanyika iwapo Simba itafuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho-Afrika. Hata hivyo Azam kupitia msemaji wake, Jaffer Idd Maganga, alisema hakuna kitu kama hicho na wanashangaa uzushi huo. "Hakuna kitu kama hicho, Simba haijawahi kutufuata kutueleza jambo hilo, wala Ngassa, pia mchezaji huyu bado ana mkataba na klabu hiyo ni ajabu kusikia kwamba anataka kwenda Simba, kivipi?" alihoji msemaji huyo. Hata hivyo suala la Ngassa kutua Simba lilitajwa tangu mchezaji huyo alipoihama Yanga na kutua Azam, ambapo ilielezwa ilikuwa janja ya kumvuta mchezaji huyo kutua Msimbazi na hasa alipokuwa akitafutiwa nafasi ya kucheza soka la kulipwa.
Mrisho Ngassa (kushoto) akiwajibika uwanjani na timu yake ya Azam. Hapa alikuwa akichuana na aliyekuwa mshambuliaji wa Simba, Mussa Hassani Mgosi ambaye kwa sasa anacheza soka la kulipwa DR Congo.

Villa Squad mambo bado magumu

LICHA ya kufurahia ushindi wa mabao 4-2 iliyopata timu yao dhidi ya Coastal Union ya Tanga, iliyofufua matumaini ya kusalia Ligi Kuu Tanzania msimu ujao, uongozi wa klabu ya Villa Squad umedai mambo bado magumu kwao na kuomba msaada zaidi. Katibu Mkuu wa Villa, Frank Mchaki, alisema bado wanahitaji msaada wa hali na mali ili kuisaidia timu yao katika maandalizi ya mechi zake zilizosalia ili kuweza kujihakikishia nafasi ya kusalia ligi kuu msimu ujao. Mchaki, alisema japo ushindi wao wa mwishoni mwa wiki umewaongezea tumaini jipya la kujinusuru kushuka daraja, lakini ni vigumu kujihakikishia jambo hilo kulingana na ukaribu wa pointi uliopo baina ya timu zilizopo chini katika msimamo wa ligi hiyo. "Tunashukuru kupata ushindi ambao umefufua matumaini yetu ya kusalia ligi kuu, ila bado tuna kazi ngumu na tunahitaji wadau wa soka watusaidie kwani kiuchumi tuna hali mbaya huku tukikabiliwa na mechi ngumu za kumalizia msimu," alisema Mchaki. Mchaki alisema anaamini timu yao ikisaidiwa kwa hali na mali itajiandaa vema kwa mechi tatu zilizosalia ambazo kama wakizishinda zote zitawafanya wasalie kwenye ligi hiyo. Villa, iliyorejea ligi kuu msimu huu ikitokea Ligi Daraja la Kwanza kwa ushindi iliyopata dhidi ya Coastal imewafanya wafikishe pointi 22 ikiwa nafasi ya 12 huku ikisaliwa mechi dhidi ya timu za African Lyon itakayocheza nao keshokutwa jijini Dar, kishaa kuvaana na JKT Oljoro kisha Ruvu Shooting watakaofunga nao dimba la msimu huu.

Kinyogoli aandaa tamasha la ngumi

NYOTA wa kimataifa wa zamani wa ngumi nchini, Habib Kinyogoli kupitia taasisi yake ya Kinyogoli Foundation, inatarajiwa kuendesha michuano maalum ya ngumi iitwayo 'Top Ten Boxing Festival-2012' litakaloanza rasmi Mei 4, jijini Dar es Salaam. Michuano hiyo itakayoshirikisha mabondia wa ngumi za aina zote yaani za ridhaa na kulipwa itafanyika kwenye ukumbi wa Panandi Panandi kwa ajili ya kuibua na kuendeleza vipaji vya mchezo huo kwa kusaka wakali 10 wa kila uzito katika ngumi hizo. Akizungumza na MICHARAZO, Msaidizi wa Kinyogoli, Rajabu Mhamila 'Super D' alisema mabondia na klabu zinazotaka kushiriki michuano hiyo wanatakiwa kujiandikisha mapema kabla ya kuanza kwake akidai itakuwa ikichezwa hadi kupatikana wakali hao. Super D, alisema ameamua kubuni 'ligi' hiyo kwa lengo la kuleta mabadiliko katika mchezo wa ngumi kwa kuibua vijana watakaoisaidia taifa kwa michuano ya kimataifa. Naye Kinyogoli maarufu kama Master, alisema ameamua kuanzisha michuano hiyo katika kuendeleza juhudi zake za kukuza ngumi ambazo zilikwama miaka ya nyuma. "Japo michuano hii itaonekana kama mipya, lakini ni kama wazo nililolibuni miaka 30 iliyopita niliposaidia kuibua vipaji vilivyokuja kutanza nchini kama akina Matumla na wengine," alisema Kinyogoli. Alisema, anaamini michuano hiyo itakapokamilika itasaidia kuibua nyota wapya na kuvihimiza vyama na wadau wa ngumi kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kushuhudia mchuano sambamba na kuwapiga tafu wale watakaofanya vema kwa faida ya taifa.
Kocha wa ngumi, Rajabu Mhamila 'Super D' msaidizi wa nyota wa zamani wa ngumi nchini, Habib Kinyogoli 'Master' wanaoandaa ligi maalum ya mchezo huo itakayoanza Mei 4.

Mashale awataka Maugo, Cheka

BAADA ya kutwaa ubingwa wa taifa wa TPBO, bondia Thomas Mashale amesema sasa yupo tayari kupigana ama Mada Maugo au Francis Cheka kwa nia ya kuanza kusaka mataji yanayotambuliwa kimataifa. Akizungumza na MICHARAZO, Mashale alisema kwa kuwa mabondia hao wawili ndio walio kwenye viwango vya hali ya juu kwa sasa katika uzani wa kati ni vema akapata fursa ya kupigana ili kuanza mbio zake za kusaka ubingwa wa Dunia. "Kwa sasa natamani kupigana na bondia yeyote kati ya Cheka au Maugo ambao wanatarajiwa kupigana hivi karibuni, lengo ni kutaka kuanza mchakato wa kusaka mataji ya kimataifa," alisema. Alisema kati ya mabondia hao haoni wa kumtisha hasa baada ya kupata uzoefu wa kutosha katika michezo yake mbalimbali aliyocheza tangu aingie kwenye mchezo huo. Mashale, alisema cha muhimu anachoombea kwa sasa ni kupatikana promota wa kumuandalia pambano kati ya mmoja wa mabondia hao ambao wanacheza wote kwenye uzani mmoja wa Middle. Kuhusu ushindi wake alioupata wiki iliyopita dhidi ya Seleman Said 'Galile' Mashale, alisema ulitokana na kufanya vema katika raundi saba za awali na kukiri kwamba mpinzani wake ni mzuri na alimpa usumbufu mkubwa. Alipoulizwa kama yupo tayari kurudiana na Galile, Mashale alisem yu radhi iwapo mpinzani wake huyo atakuwa hajaridhika na matokeo ya ushindi wake uliokuwa wa pointi baada ya kuonyeshana umwamba katika pambano la raundi 10.
Bondia Thomas Mashale 'Simba wa Teranga', akiwa na taji lake la TPBO, mara baada ya kumpiga kwa pointi Seleman Said Galile. Kwa sasa bondia huyo anamtaka kati ya Mada Maugo au Francis Cheka ili apigane nao.

Barcelona yaleteza darajani, yadungwa 1-0

Didier Drogba akishangilia bao lake la pekee lililoisaidia Chelsea kuizima Barcelona kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya mechi iliyochezwa usiku wa kuamkia leo.
BAO lililoifungwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Ivory Coast, Didier Drogba dakika za lala salama kabla ya mapumziko ilitosha kuisaidia Chelsea kuizima Barcelona ya Hispania katika pambano la kwanza la nusu fainali baina yao lililochezwa Uingereza.
Drogba alifunga bao hilo pekee dakika ya pili ya dakika za majeruhi baada ya kutimu dakika 45 za kipindi cha kwanza kwenye Uwanja wa Stamford Bridge, London, England Licha ya Barcelona ambao ndio mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa sasa kucharuka katika kipindi cha pili, ilijikuta ikishindwa kurejesha bao hilo hadi pambano lilipomalizika.
Kwa ushindi huo, Chelsea sasa inahitaji sare yoyote kwenye mechi ya marudiano ugenini, Uwanja wa Camop Nou ili kutinga fainali, ambako itacheza na mshindi kati ya Bayern Munich ya Ujerumani na Real Madrid ya Hispania.
Mechi ya kwanza ya kwanza baina ya timu hizo mbili wenyeji Bayern Munich waliitungua Real Madrid mabao 2-1, hivyo Real inahitaji ushindi wa bao 1-0 kama inataka kutinga fainali.

Mgambo Shooting yatinga Ligi Kuu Tanzania Bara, Prisons, Polisi Moro zanusa

TIMU ya soka ya maafande wa Mgambo Shooting ya Tanga imekuwa timu ya kwanza kutinga Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya jana kuisasambua Transit Campo ya Dar kwa mabao 3-0.
Mgambo inayomilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa, ilipata ushindi huo uliowaingiza Ligi Kuu ikiifuata Coastal Union kwenye pambano lililochezwa kwenye uwanja wa Jamhuri, Mjini Morogoro kunakofanyika fainali za 9 Bora ya Ligi Daraja la Kwanza.
Katika mchezo huo Mgambo ilipata mabao yake kupitia kwa washambuliaji wake, Juma Mwinyimvua aliyefunga mabao mawili katika dakika za 16 na 37 na Nassoro Gumbo aliyefunga kwenye muda wa nyongeza za mchezo huo.
Kwa ushindi huo Mgambo imefikisha jumla ya pointi 15 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine ukiondoa Polisi Moro ambao nao wanainyemelea nafasi ya kucheza ligi hiyo msimu ujao.
Katika pambano jingine lililochezwa jioni kwenye uwanja huo, mabingwa wa zamani wa Tanzania, Prisons-Mbeya ilinusa kufuzu ligi kuu msimu ujao baada ya kuicharaza Polisi-Tabora mabao 3-0
Mabao ya Prisons waliofikisha pointi 11 kwa ushindi huo wa jana, yalifungwa na John Mtai aliyefunga mawili na jingine kutumbukizwa kimiani na Peter Michael katika dakika ya nne ya mchezo huo uliochezeshwa vizuri na Shabaan Shata wa Kigoma.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena mchana wa leo kwa mechi kati ya Polisi Moro dhidi ya Mbeya City kabla ya JKT Mlale ya Songea kuumana na Polisi Dar.

Msimamo kamili wa Ligi hiyo ya 9 Bora hadi sasa ni kama ifuatavyo;


MSIMAMO WA 9 BORA LIGI DARAJA LA KWANZA

P W D L F A Pts
1. Mgambo Shooting 7 4 3 - 12 3 15
2. Polisi-Moro 6 4 2 - 12 4 14
3. Prisons-Mbeya 6 3 2 1 8 5 11
4. Mbeya City 6 2 2 2 7 6 8
5. Rhino Rangers 7 2 2 3 4 6 8
6. Polisi Dar 6 1 4 1 6 4 7
7. Mlale JKT 6 1 2 3 5 10 5
8. Polisi-Tabora 6 1 2 3 5 11 5
9. Transit Camp 6 - 1 5 2 12 1

Mwisho

Yanga yatemeshwa taji, Simba kidogo kulibeba jumla
KIPIGO cha bao 1-0 ilichopewa na Kagera Sugar jana kwenye uwanja wa Kaitaba, umeifanya Yanga kulitema taji la ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Yanga iliyokuwa watetezi wa taji hilo ilikumbana na kipigo hicho ikiwa ni cha pili ndani ya siku tatu, baada ya awali kufungwa mabao 3-2 na Toto Afrika jijini Mwanza na kuwafanya wasalie na pointi 43 na michezo mitatu ambayo hata ikishinda yote haiwezi kuzifikia pointi za watani zao, Simba wanaojiandaa kulitwaa taji hilo.
Bao lililoizamisha Yanga lilitumbukizwa wavuni na Shija Mkina na kukatisha ndoto za Yanga ambao walikuwa wakisubiri pointi zao walizopokwa na Kamati ya Mashindano ya TFF kutokana na rufaa waliyokata ambayo imetupiliwa mbali na Kamti ya Nidhamu na Usuluhishi ya Alfred Tibaigana.
Wakati Yanga ikitota Kagera na kuweka rekodi na kupoteza pointi sita katika Kanda ya Ziwa kwa mara ya kwanza, watani zao Simba jana walitakata uwanja wa Taifa baada ya kuinyoa JKT Ruvu mabao 3-0.
Ushindi uliifanya Simba ifuzu kucheza michuano ya CAF msimu ujao baada ya kujihakikishia kumaliza katika moja ya nafasi mbili za juu kutokana na kufikisha pointi 56 ambazo haziwezi kufikiwa na Yanga.
Azam yenye pointi 50 huku ikiwa na mechi moja mkononi, itaikaribisha Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Chamazi Jumamosi.
Simba ilianza kuhesabu goli la kwanza katika dakika ya kwanza ya mchezo kupitia kwa kiungo Uhuru Selemani aliyefunga kwa kichwa akiunganisha krosi ya Mganda Emmanuel Okwi na kiungo kipenzi cha mashabiki wa Simba, Haruna Moshi 'Boban' akafunga moja ya mabao bora ya msimu wakati alipokimbia na mpira kutokea katikati ya uwanja na kupiga shuti lililomshinda kipa Amani Simba wa JKT katika dakika ya 17.
Kiungo wa timu ya taifa, Taifa Stars, Mwinyi Kazimoto alifunga goli la 'kideoni' katika dakika ya 64 na kuisogeza Simba jirani zaidi na ubingwa.
Matokeo mengine ya ligi hiyo kwa jana, Ruvu Shootingi ilishinda 1-0 dhidi ya Moro United, bao lililotumbukizwa wavuni na Saleh Kitala dakika ya 90, huku Toto wakiendeleza wimbi la ushindi kwa kuicharaza African Lyon mabao 2-0.
Nao watoto wa Julio, Coastal Union, ilizinduka baada ya kichapo cha aibu cha mabao 4-2 toka kwa Villa Squad kwa kuitandika Polisi Dodoma mabao 3-l.
Kipigo hicho kimezidi kuiweka pabaya Polisi Dodoma kwani sasa ni kudra za Mungu tu ndizo zinazoweza kuinusuru isishuke daraja kurejea Ligi Daraja la Kwanza.

TIBAIGANA AICHINJA YANGAKamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana jana (Aprili 17 mwaka huu) imetupa rufani ya Yanga iliyowasilishwa mbele yake kupinga uamuzi wa kupokwa pointi tatu kwa kumchezesha mchezaji asiyestahili.
Aprili 2 mwaka huu Kamati ya Ligi ya TFF iliipa Coastal Union ushindi wa pointi tatu na mabao matatu baada ya Yanga kumchezesha beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya timu hizo iliyofanyika Machi 31 mwaka huu wakati akiwa na adhabu ya kukosa mechi tatu.
Yanga katika rufani hiyo iliwasilisha sababu nane za kupinga kupokwa pointi hizo, kubwa zikiwa Cannavaro hakustahili kutumikia adhabu ya kukosa mechi tatu, si aliyempiga refa Israel Nkongo, ripoti za refa na kamishna wa mechi yao dhidi ya Azam zilionesha dalili ya njama (conspiracy) kwani zilifanana.
Pia Cannavaro alikuwa miongoni mwa wachezaji ambao adhabu zao zilisimamishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu, Kamishna mstaafu wa Polisi, Alfred Tibaigana.
Katika uamuzi wake, Kamati imesema adhabu ya Cannavaro ya kukosa mechi tatu kwa mujibu wa Kanuni ya 25(c) ya Ligi Kuu ya Vodacom ilitolewa na refa na si Kamati ya Ligi kama ambavyo inalalamikiwa na Yanga, na kanuni hiyo haikatiwi rufani.
Pia barua ambayo TFF iliiandikia Yanga kuhusu adhabu ya mchezaji huyo ilikuwa wazi kwani ilikariri kanuni ya 25(c), hivyo kitendo cha klabu hiyo kumtumia mchezaji huyo ulikuwa ni uzembe wa kutoheshimu kanuni. Kama Yanga haikufahamu vizuri kanuni hiyo ilikuwa na fursa ya kuiandikia TFF kwa mujibu wa Kanuni ya 25(f) ili kupata ufafanuzi kabla ya kuamua kumtumia mchezaji huyo.
Vilevile adhabu zilizokuwa zimesimamishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu ni zile ambazo zilikuwa zimetolewa na Kamati ya Ligi, na si zile zilizotolewa uwanjani na refa.
Kuhusu madai ya conspiracy kwa ripoti za kamishna wa mchezo huo na refa, Kamati imebaini kuwa hazifanani, na suala lililokuwa likibishaniwa (contentious issue) lilikuwa ni kunyang’anywa pointi tatu.
Pia Kamati ilikariri Ibara ya 50 ya Kanuni za Nidhamu za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kuwa mchezaji anayembughudhi refa kwa njia yoyote ile anastahili kufungiwa kwa angalau mechi sita.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)