STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, April 19, 2012

Rage awatuliza wana Simba kuhusu Ngassa

WAKATI klabu ya soka ya Azam ikikanusha taarifa kwamba winga wao nyota, Mrisho Ngassa kuwa na mipango ya kutua Simba, Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage, amewatoa hofu wanachama wa klabu hiyo kwa kuwaeleza 'SUBIRINI TUONE'. Rage, alisema kama Ngassa atatua Msimbazi au la, litafahamika baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu Tanzania Bara, ila kwa sasa ni mapema mno kulizungumzia hilo. "Kama wao wamekanusha kwamba huyo mchezaji atakuja Simba, basi subirini, ila kwa sasa ni vigumu kuanza kulisemea hilo wakati hatujui mkataba wa Ngassa na klabu yake ukoje," alisema Rage. Mwenyekiti huyo mwenye 'kismati' na klabu hiyo ya Simba, alisema kuanza kumzungumzia Ngassa kabla hawajawasiliana na uongozi wa Azam ni kwenda kinyume na sheria za FIFA, ila amesisitiza watu wasubiri kujua ukweli wa mambo. Juzi chombo kimoja cha habari kiliripoti taarifa kwamba Simba inakaribia kumnyakua Ngassa kwa ajili ya kuichezea timu hiyo kwenye michuano ya kimataifa, hiyo itafanyika iwapo Simba itafuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho-Afrika. Hata hivyo Azam kupitia msemaji wake, Jaffer Idd Maganga, alisema hakuna kitu kama hicho na wanashangaa uzushi huo. "Hakuna kitu kama hicho, Simba haijawahi kutufuata kutueleza jambo hilo, wala Ngassa, pia mchezaji huyu bado ana mkataba na klabu hiyo ni ajabu kusikia kwamba anataka kwenda Simba, kivipi?" alihoji msemaji huyo. Hata hivyo suala la Ngassa kutua Simba lilitajwa tangu mchezaji huyo alipoihama Yanga na kutua Azam, ambapo ilielezwa ilikuwa janja ya kumvuta mchezaji huyo kutua Msimbazi na hasa alipokuwa akitafutiwa nafasi ya kucheza soka la kulipwa.
Mrisho Ngassa (kushoto) akiwajibika uwanjani na timu yake ya Azam. Hapa alikuwa akichuana na aliyekuwa mshambuliaji wa Simba, Mussa Hassani Mgosi ambaye kwa sasa anacheza soka la kulipwa DR Congo.

No comments:

Post a Comment