STRIKA
USILIKOSE
Thursday, April 19, 2012
Villa Squad mambo bado magumu
LICHA ya kufurahia ushindi wa mabao 4-2 iliyopata timu yao dhidi ya Coastal Union ya Tanga, iliyofufua matumaini ya kusalia Ligi Kuu Tanzania msimu ujao, uongozi wa klabu ya Villa Squad umedai mambo bado magumu kwao na kuomba msaada zaidi.
Katibu Mkuu wa Villa, Frank Mchaki, alisema bado wanahitaji msaada wa hali na mali ili kuisaidia timu yao katika maandalizi ya mechi zake zilizosalia ili kuweza kujihakikishia nafasi ya kusalia ligi kuu msimu ujao.
Mchaki, alisema japo ushindi wao wa mwishoni mwa wiki umewaongezea tumaini jipya la kujinusuru kushuka daraja, lakini ni vigumu kujihakikishia jambo hilo kulingana na ukaribu wa pointi uliopo baina ya timu zilizopo chini katika msimamo wa ligi hiyo.
"Tunashukuru kupata ushindi ambao umefufua matumaini yetu ya kusalia ligi kuu, ila bado tuna kazi ngumu na tunahitaji wadau wa soka watusaidie kwani kiuchumi tuna hali mbaya huku tukikabiliwa na mechi ngumu za kumalizia msimu," alisema Mchaki.
Mchaki alisema anaamini timu yao ikisaidiwa kwa hali na mali itajiandaa vema kwa mechi tatu zilizosalia ambazo kama wakizishinda zote zitawafanya wasalie kwenye ligi hiyo.
Villa, iliyorejea ligi kuu msimu huu ikitokea Ligi Daraja la Kwanza kwa ushindi iliyopata dhidi ya Coastal imewafanya wafikishe pointi 22 ikiwa nafasi ya 12 huku ikisaliwa mechi dhidi ya timu za African Lyon itakayocheza nao keshokutwa jijini Dar, kishaa kuvaana na JKT Oljoro kisha Ruvu Shooting watakaofunga nao dimba la msimu huu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment