STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, April 19, 2012

Yanga yatemeshwa taji, Simba kidogo kulibeba jumla




KIPIGO cha bao 1-0 ilichopewa na Kagera Sugar jana kwenye uwanja wa Kaitaba, umeifanya Yanga kulitema taji la ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Yanga iliyokuwa watetezi wa taji hilo ilikumbana na kipigo hicho ikiwa ni cha pili ndani ya siku tatu, baada ya awali kufungwa mabao 3-2 na Toto Afrika jijini Mwanza na kuwafanya wasalie na pointi 43 na michezo mitatu ambayo hata ikishinda yote haiwezi kuzifikia pointi za watani zao, Simba wanaojiandaa kulitwaa taji hilo.
Bao lililoizamisha Yanga lilitumbukizwa wavuni na Shija Mkina na kukatisha ndoto za Yanga ambao walikuwa wakisubiri pointi zao walizopokwa na Kamati ya Mashindano ya TFF kutokana na rufaa waliyokata ambayo imetupiliwa mbali na Kamti ya Nidhamu na Usuluhishi ya Alfred Tibaigana.
Wakati Yanga ikitota Kagera na kuweka rekodi na kupoteza pointi sita katika Kanda ya Ziwa kwa mara ya kwanza, watani zao Simba jana walitakata uwanja wa Taifa baada ya kuinyoa JKT Ruvu mabao 3-0.
Ushindi uliifanya Simba ifuzu kucheza michuano ya CAF msimu ujao baada ya kujihakikishia kumaliza katika moja ya nafasi mbili za juu kutokana na kufikisha pointi 56 ambazo haziwezi kufikiwa na Yanga.
Azam yenye pointi 50 huku ikiwa na mechi moja mkononi, itaikaribisha Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Chamazi Jumamosi.
Simba ilianza kuhesabu goli la kwanza katika dakika ya kwanza ya mchezo kupitia kwa kiungo Uhuru Selemani aliyefunga kwa kichwa akiunganisha krosi ya Mganda Emmanuel Okwi na kiungo kipenzi cha mashabiki wa Simba, Haruna Moshi 'Boban' akafunga moja ya mabao bora ya msimu wakati alipokimbia na mpira kutokea katikati ya uwanja na kupiga shuti lililomshinda kipa Amani Simba wa JKT katika dakika ya 17.
Kiungo wa timu ya taifa, Taifa Stars, Mwinyi Kazimoto alifunga goli la 'kideoni' katika dakika ya 64 na kuisogeza Simba jirani zaidi na ubingwa.
Matokeo mengine ya ligi hiyo kwa jana, Ruvu Shootingi ilishinda 1-0 dhidi ya Moro United, bao lililotumbukizwa wavuni na Saleh Kitala dakika ya 90, huku Toto wakiendeleza wimbi la ushindi kwa kuicharaza African Lyon mabao 2-0.
Nao watoto wa Julio, Coastal Union, ilizinduka baada ya kichapo cha aibu cha mabao 4-2 toka kwa Villa Squad kwa kuitandika Polisi Dodoma mabao 3-l.
Kipigo hicho kimezidi kuiweka pabaya Polisi Dodoma kwani sasa ni kudra za Mungu tu ndizo zinazoweza kuinusuru isishuke daraja kurejea Ligi Daraja la Kwanza.

No comments:

Post a Comment