STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, January 18, 2013

EMMANUEL OKWI KUIAGA RASMI SIMBA JAN 26

KLABU ya Simba imesema mshambuliaji wake, Emmanuel Okwi atawaaga mashabiki wa klabu hiyo katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya African Lyon utakaofanyika Januari 26, mwaka huu.

Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, Okwi ameamua kuwaaga mashabiki wa timu hiyo kutokana na kumpa ushirikiano mkubwa.

Hata hivyo, Mtawala alisema watalazimika kuomba ruhusa ya kumtumia mchezaji huyo kutoka katika klabu yake ya sasa ya Etoile Du Sahel ya Tunisia.

Simba imemuuza Okwi kwa Etoile Du Sahel kwa kitita cha dola 300,000 za Marekani (sawa na sh. milioni 480,000) baada ya kufuzu majaribio aliyofanyiwa.

Kwa mujibu wa Mtawala, kikosi cha Simba, ambacho kwa sasa kipo kambini nchini Oman, kinatarajiwa kurejea nchini Januari 23 mwaka huu kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya hatua ya pili ya ligi kuu ya Tanzania Bara.

Okwi ametia saini mkataba wa kuichezea Etoile Du Sahel kwa miaka miwili, ambapo atakuwa akilipwa mshahara wa dola 200,000 kwa mwaka. Pia amepewa nyumba ya kuishi na gari.

Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uganda, alijiunga na Simba miaka mitatu iliyopita akitokea SC Villa ya Uganda na kuiwezesha kufanya vizuri katika michuano ya ligi na kimataifa.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspope amesema hawana haraka ya kutafuta mchezaji wa kuziba nafasi ya Okwi.

Hanspope alisema jana kuwa, watalazimika kufanyakazi hiyo kwa umakini mkubwa ili waweze kumpata mchezaji mwenye kiwango kinachoshabihiana na Okwi.

Okwi amekuwa mchezaji wa tatu wa Simba kuuzwa nje kwa bei mbaya. Awali, Simba iliwauza mshambuliaji Mbwana Samatta na kiungo Patrick Ochan wa Ugand

WAGOMBEA 45 KUCHUANA UCHAGUZI MKUU WA TFF

Jamal Malinzi anayewania Urais TFFAthuman Nyamlani (kulia) anayewania Urais wa TFF


Na Boniface Wambura
WANAMICHEZO 45 wamechukua fomu kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) utakaofanyika Februari 24 mwaka huu. Nafasi zinazowaniwa ni Rais, Makamu wa Rais na wajumbe wa Kamati ya Utendaji kuwakilisha kanda 13 tofauti.
Waombaji wapya 11 waliojitokeza leo (Januari 18 mwaka huu) ni Richard Rukambura anayeomba urais wakati kwa upande wa ujumbe wa Kamati ya Utendaji ni Kaliro Samson, Jumbe Magati, Richard Rukambura, Omari Walii, Ahmed Mgoyi, John Kiteve, Stanley Lugenge, Francis Ndulane, Riziki Majara na Hassan Othuman Hassanoo.
Mwisho wa kuchukua fomu kwa waombaji wote ni leo (Januari 18 mwaka huu) saa 10 kamili alasiri. Fomu pia zinaweza kuchukuliwa katika tovuti ya TFF ambayo ni www.tff.or.tz na kurejeshwa kupitia email ya tfftz@yahoo.com Pia Kanuni za Uchaguzi za TFF zinapatikana katika tovuti hiyo.
Orodha kamili ya waombaji ni Athuman Nyamlani, Jamal Malinzi, Omari Nkwarulo na Richard Rukambura (Rais). Walioomba kuwania nafasi ya Makamu wa Rais ni Michael Wambura, Ramadhan Nassib na Wallace Karia.
Kwa upande wa ujumbe wa Kamati ya Utendaji ni Salum Chama na Kaliro Samson (Kagera na Geita), Jumbe Magati, Mugisha Galibona, Richard Rukambura, Samuel Nyalla, Titus Osoro na Vedastus Lufano (Mara na Mwanza).
Epaphra Swai na Mbasha Matutu (Shinyanga na Simiyu), Charles Mugondo, Elly Mbise na Omari Walii (Arusha na Manyara), Ahmed Mgoyi na Yusuph Kitumbo (Kigoma na Tabora), Ayubu Nyaulingo, Blassy Kiondo, Nazarius Kilungeja na Selemani Kameya (Katavi na Rukwa) na James Mhagama na Stanley Lugenge (Njombe na Ruvuma).
Athuman Kambi, Francis Ndulane na Zafarani Damoder (Lindi na Mtwara), Hussein Mwamba na Stewart Masima (Dodoma na Singida), Farid Nahdi, Geofrey Nyange, Hassan Othman Hassanoo, Riziki Majara na Twahili Njoki (Morogoro na Pwani), Elias Mwanjala, Eliud Mvella na John Kiteve (Iringa na Mbeya), Khalid Mohamed (Kilimanjaro na Tanga) na Muhsin Balhabou, Omari Abdulkadir na Shaffih Dauda (Dar es Salaam).

MAKALI YA UTURUKI YA YANGA KUONEKANA KESHO TAIFA

MABINGWA wa Kombe la Kagame, Yanga kesho inatarajiwa kushuka dimbani kuonyesha makali yao ya Uturuki kwa kuumana na timu ya Black Leopard ya Afrika Kusini katika pambano la kirafiki la kimataifa.
Kikosi cha Leopard ambacho kipo nafasi za mkiani mwa Ligi Kuu ya nchini mwao kinatarajiwa kutua nchini leo baada ya kukwama kufanya hivyo jana, tarayi kwa mtanange huo utakaochezwa kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Yanga iliyorejea wiki iliyopita kutoka Uturuki ilipoweka kambi ya mazoezi ya wiki mbili inasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka kuona walichojifunza ughaibuni katika mechi hiyo dhidi ya Leopard.
Hata hivyo kikosi hicho kinaweza kumkosa mshambuliaji wa kimataifa kutoka Uganda, Hamis Kiiza ambaye ametajwa kuwa mgonjwa.
Mbali na Kiiza pia mchezaji Juma Abdul naye pia ataikosa mechi hiyo kwa kuwa ni mgonjwa, japo wachezaji wengine wapo tayari kuvaana na 'Chui Mweusi' huyo.
Yanga ilikuwa Uturuki kwa wiki mbili kwa kambi ya mazoezi na ilirejea Jumapili alfajiri nchini. Katika ziara yake hiyo, ilicheza mechi tatu za kujipima nguvu na kufungwa mbili na kutoka sare moja.
Katika mchezo wake wa kwanza, ilitoka sare ya 1-1 Ariminia Bielefeld ya Daraja la Tatu (sawa na la nne) Ujerumani kabla ya kufungwa 2-1 na Denizlispor FC ya Daraja la Kwanza Uturuki na baadaye 2-0 na Emmen FC ya Ligi Daraja la Kwanza Uholanzi.
Hata hivyo rekodi ya wapinzani wao kutoka Afrika Kusini inatoa shaka kama itakuwa kipimo kizuri cha Yanga baada ya kuhimili mikiki mikiki ya Ulaya.

KOCHA ZAMBIA AANZA TAMBO MAPEMA AFCON 2013

Herve Renard
Herve Renard
Herve Renard

Wachezaji wakimbeba juu kocha Herve Renard baada ya kuwaongoza kutwaa ubingwa wa Afrika mwaka jana
 


KOCHA wa timu ya taifa ya Zambia, Herve Renard anaamini kwamba timu hiyo iko vizuri zaidi ya mwaka jana, wakati wakijiandaa kutetea ubingwa wao wa Mataifa ya Afrika nchini Afrika Kusini.

Wazambia wataanza kampeni zao Jumatatu Januari 21 dhidi ya Ethiopia, wakitokea kupokea vipigo vitatu mfululizo na sare mojka katika mechi zao nne za majaribio.

Lakini Renard, ambaye aliiongoza timu hiyo kutwaa taji lao la kwanza la Afrika mwaka jana, ana furaha na maandalizi ya kikosi chake.

"Nadhani tuko vizuri kuliko mwaka jana wakati kama huu," alisema.
"Kwa wakati kama huu (mwaka jana), nilikuwa na wasiwasi mkubwa sana. Mechi zote za kujiandaa tulicheza ovyo.

"Lakini angalia kilichotokea baadaye - hatukuwa na kingine cha kuonyesha bali kombe ya ubingwa.

"Nina bahati kuwa na kikosi kama hiki."

Zambia walitoka sare ya 0-0 dhidi ya washiriki wenzao wa AFCON 2013, Morocco katika mechi ya kirafiki wiki iliyopita mjini Johannesburg, iliyofuatia vipigo vitatu mfululizo kutoka kwa Angola, Saudi Arabia na Tanzania iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Goli la pekee la mechi dhidi ya Taifa Stars ya Tanzania lilifungwa na Mrisho Ngassa.
Renard, hata hivyo, amedai kwamba matokeo hayo mabovu katika mechi za kujiandaa hayampi presha.

Kocha huyo Mfaransa amesema licha ya kwamba wao ndiyo mabingwa watetezi, nafasi kubwa ya kutwaa taji hilo wanapewa Ivory Coast na Ghana.

"Hatuwezi kusema sisi ndiyo tunaopewa nafasi. Kila mtu atakucheka ukisema hivyo. Ivory Coast na Ghana ndiyo wanaopewa nafasi."

Zambia watakabiliana na Nigeria na Burkina Faso katika Kundi C, baada ya mechi yao ya ufunguzi dhidi ya Ethiopia.

RAIS ZUMA AWAPA UBINGWA BAFANA BAFANA

Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma akionyesha ufundi wa kuchezea mpira wakati alipoitembelea timu ya taifa ya nchi hiyo, Bafana Bafana, kwenye Uwanja wa Orlando mjini Soweto, Afrika Kusini Januari 15, 2013.
Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma akipozi na wachezaji wakati alipoitembelea timu ya taifa ya nchi hiyo, Bafana Bafana, kwenye Uwanja wa Orlando mjini Soweto, Afrika Kusini Januari 15, 2013.

Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma akizungumzana wachezaji wakati alipoitembelea timu ya taifa ya nchi hiyo, Bafana Bafana, kwenye Uwanja wa Orlando mjini Soweto, Afrika Kusini Januari 15, 2013.

Kama Dinho vile... Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma akionyesha ufundi wa kuchezea mpira wakati alipoitembelea timu ya taifa ya nchi hio, Bafana Bafana, kwenye Uwanja wa Orlando mjini Soweto, Afrika Kusini Januari 15, 2013.

RAIS wa Afrika Kusini, Jacob Zuma amesema anajiamini kwamba wenyeji watazima shutuma wanazoelekezewa na kubakisha nchini humo kombe la Mataifa ya Afrika 2013 kama walipolitwaa mara pekee mwaka 1996 wakati michuano ilipofanyika nchini humo.
nchini humu," alisema Rais Zuma. 
"Nilikuwa nawaeleza wachezaji kwamba (wale) wanaoshutumu hawajawahi hata kuugusa mpira. Hawaujui 'ladha' yake. 

"Tumeridhika kwamba timu imeandaliwa vyema kwa ajili ya michuano hii. 

"Ni lazima watulie, wasiwe katika presha, hawapaswi kusikiliza shutuma hizi. Ni lazima waweke akili katika kile walichojiandaa kukikafanya na watakifanya. 

"Najiamini sana wakati huu kuliko wakati mwingine wowote kwamba tutawaonyesha watu kuwa sisi ndiyo Wasauzi. 

"Nimewaambia wachezaji 'nataka kulishika kombe', na kuligusa inamaanisha kwamba tubaki nalo hapo. Na watalitwaa. Hatupaswi kuhofia chochote."

AZAM WATUA SALAMA KENYA KUCHEZA KUCHEZA MECHI KESHO

Kikosi cha Azam kilipokuwa kikishangilia taji lao la Mapinduzi iliyotwaa wiki iliyopita visiwani Zanzibar kwa kuilaza Tusker ya Kenya katika mechi ya fainali.
KIKOSI cha timu ya Azam kimetua salama jijini Nairobi jana na kesho wanatarajiwa kushuka dimbani kuumana na AFC Leopard kabla ya Jumapili kuivaa Sofapaka kisha kumalizia mechi yao ya tatu dhidi ya KCB.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mtandao wa klabu hiyo ukimnukuu kocha wao mkuu, Stewart John Hall, mechi zote hizo zitachezwa kwenye uwanja wa Nyayo ambapo leo walitarajiwa kuanza mazoezi katika uwanja huo kwa ajili ya mechi hizo za kujiandaa na mechi za duru la pili la Ligi Kuu Tanzania Bara itakayoanza Januari 26.
“Tutacheza michezo mitatu, michezo yetu itahusisha timu zenye viwango vizuri katika ligi ya Kenya ambazo ni A.F.C Leopard, Sofapaka na K.C.B, mechi hizo zitasaidia kuimarisha timu yangu” alisema Stewart.
Kocha Stewart alisema watafanya mazoezi na kucheza mechi katika viwanja aina mbili vyenye nyasi za kawaida na zenye nyasi bandia kwa kuwa katika michezo ya ligi viwanja hivyo vinaendana na mazingira ya Tanzania.
Azam FC itamaliza safari yake ya maandalizi na mechi za kirafiki siku ya Jumanne kwa kuvaana naK.C.B kwenye Uwanja wa City mchezo ambao utakamilisha safari hiyo ya siku saba.
Wachezaji walioko jijini ni Mwadini Ally, Aishi Manula, Jackson Wandwi, Himid Mao, Samih Haji Nuhu, David Mwantika, Luckson Kakolaki, Jockins Atudo, Michael Bolou, Humphrey Mieno, Khamis Mcha, Gaudence Mwaikimba, Uhuru Selemani, Brain Umony, Malika Ndeule, Omary Mtaki, Abdi Kassim ‘Babi’, Abdalah Seif, Jabir Aziz, Ibrahim Mwaipopo na Salum Abubakar ‘Sure Boy’.
Father alisema kuwa mechi yao ya awali itakuwa dhidi ya Sofapaka itakayochezwa kesho kwenye dimba la Nyayo, kabla ya kucheza mechi nyingine baadae japokuwa watawakosa Gor Mahia waliokuwa wamepania kucheza nao.

Zahoro Pazi aanza kujaribiwa Bondeni, akiri kazi nzito

Zahoro Pazi (kulia) hapa akiwa mazoezi ya Azam


MSHAMBULIAJI wa Azam aliyekuwa amesajiliwa kwa mkopo na JKT Ruvu, Zahoro Pazi aliyepo nchini Afrika Kusini kuwania kucheza soka la kulipwa ameanza majaribio yake katika klabu ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini, Bloemfotein Celtic.
Akizungumza na MICHARAZO jana usiku kutoka Afrika Kusini, Pazi alisema majaribio yake yalianza juzi katika uwanja wa klabu hiyo wa Seisa Ramabodu, uliopo mji wa Bloemfotein.
Pazi alisema mazoezi yake kwa siku ya kwanza yalikuwa ni ya mwili tu kwa ajili ya kuangaliwa stamina na pumzi na anashukuru aliyafanya mwanzo mwisho licha ya kwamba yalikuwa magumu kwake.
"Kaka nimeanza leo matizi hapa Bloemfotein but nimekutana na physic si mchezo ila nimekomaa hadi mwisho maana nilishatiwa upepo na Kilinda (kocha wa JKT Ruvu- Charles Kilinda)  hatujasuga mpira kabisa kwa leo," alisema Pazi.
Pazi aliongeza kuwa alitarajiwa kuendelea na majaribio yake leo na kuendelea kwa siku 10 kabla ya kurejea nchini kusubiri majibu yake iwapo amefuzu au la.
Mchezaji huyo aliyewahi kujaribiwa na klabu za Kaiserlauten ya Ujerumani na Nadi ya Oman, alisema anamuomba Mungu amsaidie kufuzu majaribio yake ili aweze kutimiza ndoto zake za kucheza soka la kulipwa aliloliota kwa muda mrefu.
Pazi, mtoto wa kipa wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Idd Pazi 'Father' aliivutia klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini iliyopo nafasi ya saba katika ligi hiyo iliyosimama kupisha Michuano ya Afrika, alipokuwa DR Congo na timu yake ya Azam.
Kabla ya hapo klabu hiyo ilimuona kinda huyo katika michuano ya Kombe la Kagame iliyokuwa ikichezwa nchini na kurushwa na kituo cha Supersport cha Afrika Kusini.

WAGOMBEA ZAIDI WAJITOKEZA TFF, PAZIA KUFUNGWA LEOWAKATI leo ndiyo mwisho wa kuchukua na kurejesha fomu za kuwania uongozi kwenye uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPL Board) waombaji 36 walikuwa wameshachukua na 18 kurejesha fomu hizo hadi jana.
Idadi hiyo ni kufikia jana mchana (Januari 17 mwaka huu). Pia Kamati ya Uchaguzi ya TFF inasisitiza kuwa wanaorejesha fomu hizo kwa email wanatakiwa kuzituma kwa Katibu Mkuu wa TFF kwa email ya tfftz@yahoo.comna si kwa email binafsi za wajumbe wa Kamati ya Uchaguzi au maofisa wa TFF.
Waombaji wanne walioongezeka katika orodha ni Blassy Kiondo kwa Kanda ya Katavi na Rukwa, Eliud Mvella (Mbeya na Iringa), Geofrey Nyange (Morogoro na Pwani), na Omari Abdulkadir kwa Kanda ya Dar es Salaam.
Orodha kamili ya waombaji ni Athuman Nyamlani, Jamal Malinzi na Omari Mussa Nkwarulo (urais) wakati waombaji wa umakamu wa rais mpaka sasa ni Michael Wambura, Ramadhan Nassib na Wallace Karia.
Kwa upande wa wajumbe wa Kamati ya Utendaji na kanda zao kwenye mabano ni Salum Chama (Kagera na Geita), Mugisha Galibona, Samuel Nyalla, Titus Osoro na Vedastus Lufano (Mara na Mwanza).
Epaphra Swai na Mbasha Matutu (Shinyanga na Simiyu), Charles Mugondo na Elly Mbise (Arusha na Manyara), Yusuph Kitumbo (Kigoma na Tabora), Ayubu Nyaulingo, Blassy Kiondo, Nazarius Kilungeja na Selemani Kameya (Katavi na Rukwa) na James Mhagama (Njombe na Ruvuma).
Athuman Kambi na Zafarani Damoder (Lindi na Mtwara), Hussein Mwamba na Stewart Masima (Dodoma na Singida), Farid Nahdi, Geofrey Nyange na Twahili Njoki (Morogoro na Pwani), Elias Mwanjala na Eliud Mvella (Iringa na Mbeya), Khalid Mohamed (Kilimanjaro na Tanga) na Muhsin Balhabou, Omari Abdulkadir na Shaffih Dauda (Dar es Salaam).
Kwa upande wa Bodi ya Ligi Kuu (TPL Board) waliochukua fomu mpaka sasa ni wawili tu. Yusuf Manji amechukua fomu ya uenyekiti wakati Said Mohamed amechukua fomu ya kuwania umakamu mwenyekiti.
SUPER WEEK TENA NDANI YA LIGI KUU YA VODACOM
Mzunguko wa pili ya Ligi Kuu ya Vodacom utaanza Januari 26 mwaka huu huku kukiwa na maombi ya televisheni ya SuperSport kuonesha mechi za Super Week kama ilivyokuwa katika mzunguko wa kwanza.
Raundi tano za awali katika ratiba ya mzunguko wa pili zinabaki kama zilivyo wakati nyingine zilizobaki zitatolewa baada ya kuingiza mechi za Super Week.
Wakati huo huo, mzunguko wa pili wa Ligi Daraja la Kwanza unatarajia kuanza Januari 26 mwaka huu. Ratiba ya ligi hiyo na tarehe rasmi ya kuanza itatangazwa baada ya kupitiwa na Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inayotarajiwa kukutana mwishoni mwa wiki.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

EXTRA BONGO KUANZA KUGAWA ZAWADI KWA MASHABIKI LEO

BENDI ya Extra Bongo 'Wana Next Level' chini ya Ally Choki leo inatarajiwa kuanza kugawa zawadi kwa mashabiki wao katika onyesho litakalofanyika kwenye ukumbi wa Meeda Club, Sinza Mori.
Extra Bongo imeanza wiki nne za kugawa zawadi kwa mashabiki wao, kama njia ya kurudisha shukrani zao kwa mashabiki hao ambapo washindi wa tatu watakaocheza vema miondoko ya bendi hiyo watazoa vitita vya fedha zipatazo 300,000.
Mgawanyo wa fedha hizo ni kwamba mshindi wa kwanza atazoa Sh 150,000 na wa pili kukamata kitita cha 100,000 na atakayekuwa wa tatu atambulia 50,000.
Choki alisema baada ya makamuzi hayo ya Meeda leo bendi yake itaelekea ukumbi wa Garden Breeze, Magomeni Mapipa kwa ajili ya bonanza lao kabla ya Ijumaa kugawa tena zawadi kwa mashabiki wa TMK.
Akizungumzia shoo ya Jumapili hii, Choki alisema, bendi yake imepania kuhakikisha inakonga nyoyo za mashabiki wao wa Magomeni na maeneo ya jirani na kwamba, kila atakayehudhuria atakubaliana na hilo.
“Kazi zetu zinatambulika, watakaokuja watashuhudia shoo kali kutoka kwa wanamuziki na wanenguaji mahiri wa dansi. Waje kwa wingi na kila atakayeingia Garden Breeze, hatojutia uamuzi wake wa kuja kujinafasi nasi wana wa ‘Next Level’ wikiendi hii,” alitamba Choki.
Aidha, mkongwe wa dansi Afrika Mashariki na Kati, Tshimanga Kalala Asosa, naye atafanya vitu adimu akiwa na bendi yake ya Bana Marquiz, watakapotumbuiza kwenye ‘kijiji hicho cha maraha’ cha Garden Breeze leo usiku.
Assosa maarufu kama ‘Mtoto Mzuri’, alisema, amejiandaa kukonga nyoyo za mashabiki kwa vibao vyake vipya na vya zamani, vikiwamo vile vilivyompa umaarufu mkubwa, kiasi cha kuitwa hapa nchini kuanzisha bendi kongwe ya Mlimani Park Orchestra ‘Sikinde Ngoma ya Ukae’ mwaka 1978.
“Nitawapa mashabiki vitu vipya na vile vyote nilivyopata kuimba katika bendi zangu tangu nikiwa Zaire (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo), hadi hapa Bongo,” alisisitiza Assosa bila kutaja nyimbo hizo na kuwataka mashabiki wa muziki wa dansi kufurika Garden Breeze.

SERIKALI YABARIKI FAINALI ZA TAIFA MISS UTALII TANZANIA 2012/13


Serikali ya Jamuhuri ya muungano wa Tanzania, kupitia Baraza la Sanaa la Taifa, limebariki kufanyika kwa Fainali za Taifa za Miss Utalii Tanzania 2012/13 baada ya kuridhishwa na maandalizi yaliyo fanywa na Miss Tourism Tanzania Organisation waandaaji wenye dhima ya kikomo ya kuandaa na kuendesha mashindano hayo kitaifa na kimataifa, pia kwa kuzingatia sheria za nchi, kanuni na Taratibu za mashindano.

Serikali pia imeridhishwa na jinsi Fainali za ngazi za mikoa na kanda zilivyofanyika kwa mafanikio,ambapo kila mkoa umepata washindi wenye sifa za kuwakilisha mkoa husika katika Fainali za Taifa mwaka huu,ambapo jumla ya warembo 60 waingia rasmi kambini kesho katika hoteli ya Ikondelelo Lodge Dar es Salaam, kuanza mbio za kuwania Taji
hilo la Taifa.

Washindi wa 1-5 wa Fainali za Taifa ,watawakilisha Tanzania katika mashindano mbalimbali ya Dunia yakiwemo ya International Miss Tourism World, Miss Tourism United Nation, Miss Heritage World, Miss Tourism University World, Miss Globe International n.k

Miss Utalii Tanzania ,hadi sasa tunashikilia Jumla ya mataji 5 ya Dunia na kimataifa, yakiwemo ya Miss Tourism World 2005-Africa,Miss Tourism World 2006-SADC,Miss Tourism World 2007-Africa, Miss Tourism Model Of The World 2008-Personality n.k

Fainali za Taifa mwaka huu zimepangwa kufanyika wiki ya kwanza ya Februari ,wilaya ya Temeke na mkoa wa Dar es Salaam ukiwa umepewa heshima ya kuwa wenyeji wa Fainali hizo.

Asante,
Erasto Gideon Chipungahelo
Rais