STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, January 15, 2014

Nigeria yaifumua Msumbiji 4-2, Uganda kesho

 http://2.bp.blogspot.com/-nPswb25dhrg/UfJo0MzLqUI/AAAAAAAABXs/XLm5N-1eZ5o/s640/Nigeria%2BCHAN%2Bmatch.jpg
NIGERIA imezinduka kwenye michuano ya CHAN baada ya kuikandika Msumbiji mabao 4-2 ktika pambano la raundi ya pili kwa timu za kundi A lililochezwa usiku huu.
Msumbiji waliofungwa mabao 3-1 na wenyeji Afrika Kusini, walianza kupata bao dakika ya 10 ya mchezo huo kupitia kwa Dario Khan, lililodumu kwa dakika moja kabla ya Ede kurejesha akimaliza kazi ya Egwuekwe.
Nigeria iliongeza bao la pili dakika ya 13 kupitia kwa Rabiu Ali kabla ya Msumbiji kuchomoa dakika saba baadaye kupitia Diogo na kufanya hadi mapumziko matokeo kuwa 2-2.
Kipindi cha pili kilianza kwa Nigeria kujipatai bao la tatu kwa mkwaju wa penati kupitia kwa Ali tena kwenye dakika ya 54 na dakika mbili kabla ya pambano hilo kumalizika Imenger aliiongezea Nigeria bao la nne lililowapa ushindi wao wa kwanza kwenye mchuano hiyo.
Michuano hiyo inaendelea tena kwa michezo ya kundi B ambapo Uganda itaumana na Zimbabwe mapema kabla ya Burkina Faso kuumana na Morocco usiku. Katika mechi za awali Uganda iliichapa Burkinabe mabao 2-1 na Morocco na Zimbabwe zilitoshana nguvu kwa kutofunagana.

Bafana Bafana yabanwa na Mali CHAN 2014

http://www.citypress.co.za/wp-content/uploads/2013/06/bafana-bafana.jpg
WENYEJI Afrika Kusini pamoja na kutangulia kupata bao la mapema kwenye kipindi cha kwanza kwa mkwaju wa penati, imeshindwa kuendeleza wimbi lake la ushindi baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Mali.
Bafana Bafana ilipata bao lake kwenye dakika ya 25 kupitia kwa mshambuliaji wake nyota Benard Parkers ambalo lilikuwa la tatu katika mashindano hayo baada ya Mali kucheza madhambi langoni mwao.
Bao hilo lilidumu hadi mapumziko kabla ya kipindi cha pili kuanza na Mali kuonyesha uhai kwa kushambulia lango la Bafana Bafana na kufanikiwa kupata bao la kusawazisha kupitia kwa Ibourahima Sidide katika dakika ya 51.
Kwa matokeo hayo Afrika Kusini wameendelea kuongoza kundi hilo ikiwa na pointi nne sawa na Mali ila zinatofautiana kwa idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa, Bafana Bafana wakiwa na mabao manne na kufungwa mawili, huku Mali ikiwa na matatu ikiruhusu mawili.
Mechi nyingine ya kundi hilo inatarajiwa kuchezwa muda mchache baadaye kwa Nigeria kuumana na 'Mambaz' ya Msumbiji katika pambano linalotarajiwa kuwa kali kutokana na ukweli timu zote zilipokea vipigo katika mechi zao za fungua dimba ya CHAN 2014.

Kocha John Simkoko aula TAFCA-Moro

John Simkoko
 CHAMA cha makocha wa mpira wa miguu Tanzania (TAFCA) mkoa wa Morogoro kimepata viongozi wake wapya kufuatia uchaguzi uliofanyika hivi karibuni katika uwanja wa Jamhuri, mjini humo.
Katika uchaguzi huo uliovuta hisia za makocha wa soka mkoani Morogoro, John Simkoko alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho wakati nafasi ya katibu mkuu imekwenda kwa Ahmed Mumba.
Waliochaguliwa katika nafasi tatu za wajumbe wa kamati ya utendaji ya chama hicho ni John Tamba, Rashid Amri na Nyamtimba Muga wakati Jonas Mhango akichaguliwa katika nafasi ya mweka hazina na Charles Mwakambaya akiibuka mshindi katika nafasi ya mjumbe wa mkutano mkuu.
Awali, akizungumza kabla ya uchaguzi huo, mwenyekiti wa chama cha soka mkoa wa Morogoro (MRFA), Pascal Kihanga ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi aliwataka makocha mkoani Morogoro kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwao kwa lengo la kuhakikisha mchezo wa soka unapiga hatua kubwa mkoani hapa.
Naye, Simkoko akizungumza baada ya uchaguzi, alisema amejipanga vizuri kukiongoza chama hicho na kwamba watatekeleza majukumu yao kwa mujibu wa katiba ya chama hicho.

Mwalala, Matola kuongoza makocha kuivaa TASWA FC

http://4.bp.blogspot.com/-ELlQfM1Udqo/UbZbS3iqpjI/AAAAAAAAIIk/W6ipuIots0M/s1600/DSC_0013%2B(2).JPG
Baadhi ya makocha ambao wanatarajiwa kuivaa TASWA, Bakar Idd (kushoto)  Seleman Matola watatu toka kushoto, anayemfuata ni Mwalala wakiwa na Shafii Dauda 'Fundi' (wa pili kushoto)

MSHAMBULIAJI wa zamani wa Yanga, Benard Mwalala na makocha wasaidizi wa Simba na Azam, Kally Ongalla na Seleman Matola ni baadhi ya wachezaji wanaotarajiwa kuunda timu ya Makocha itakayocheza mchezo wa kirafiki na TASWA FC katika kusindikiza tuzo za Makocha wa Soka Tanzania inayotarajiwa kutolewa Machi 8, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na MICHARAZO jijini, afisa mtendaji wa tuzo hiyo, Fredrick Luunga alisema mchezo huo pia utatumika kumuenzi aliyekuwa mweka hazina na mchezaji wa Taswa FC, Sultan Sikilo na aliyekuwa kocha wa makipa wa Simba SC, James Kisaka, waliofariki dunia hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Luunga alisema maandalizi kwa ajili ya tuzo hiyo yanakwenda vizuri na kwamba anaamini mchezo huo utakuwa chachu kwa kuwa pia utawakutanisha makocha na waandishi wa habari za michezo na kupata fursa ya kubadilishana mawazo.
“Hili ni wazo jipya ambalo tumelipata tumeona ni vema kuandaa mchezo wa kirafiki kati ya timu ya makocha na Waandishi wa habari za michezo nchini kabla ya utoaji wa tuzo ili kuleta changamoto zaidi”, alisema.
Afisa huyo alisema mchezo huo unatarajiwa kuchezwa mapema siku hiyo ya utoaji wa tuzo katika uwanja utakaopangwa baadaye.
Mbali ya Mwalala, Matola na Ongala, makocha wengine wanaotarajiwa kuunda kikosi cha timu hiyo ni Juma Pondamali ‘Mensah’, Idd Pazi ‘Father’, Patrick Mwangata, Charles Boniface Mkwasa, Fred Felix Minziro, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, Charles Kilinda, Amri Said, Adolf Rishard, Mecky Maxime, Joseph Lazaro, Bakari Shime, John Tamba, Jackson Mayanja, Mrage Kabange na Ken Mwaisabula.
Wakati huo huo, luunga alisema zoezi la kuwapigia kura makocha ili waweze kushinda tuzo hizo limeshaanza na kwamba wadau wa soka wanatakiwa kuwachagua makocha wanaoona wanastahili kupata tuzo.
Luunga alisema namna ya kupiga kura, mdau wa michezo anatakiwa kuandika katika simu yake neno sokafasta acha nafasi kisha jina la kocha yeyote na tuzo anayostahili kupata kisha itumwe kwenda 15678.
Tuzo zinazotarajiwa kutolewa siku hiyo ni kocha bora wa mwaka, kocha bora wa makipa, kocha mkongwe mwenye mafanikio, kocha bora chipukizi, kocha bora wa kike, kocha bora wa kigeni, kocha wa kigeni aliyewahi kupata mafanikio makubwa na kocha bora Mtanzania anayefundisha nje ya nchi.

Cheka aumia mkono mazoezini, pambano lake na Mrusi hatihati

Francis Cheka
Bondia Francis Cheka

BINGWA wa Ngumi za Kulipwa anayeshikilia taji la IBF-Afrika, Francis Cheka yupo katika hati hati ya kuvaana na mpinzani wake kutoka Russia Valery Brudov, baada ya kujiumiza mkono akiwa kwenye mazoezi kujiandaa na pambano hilo lililopangwa kufanyika Februari 8, jijini Dar es Salaam.
Pambano hilo limepangwa kuchezwa kwenye uikumbi wa PTA na litakuwa la uzito wa Light Heavy raundi 12 likiwa limeandaliwa na promota Juma 'Jay' Msangi.
Akizungumza naMICHARAZO mapema leo, Cheka alisema amejiumiza mkono wa kulia akiwa kwenye mazoezi na amekimbilia hospitali kuchunguzwa kutokana na anachodai kusikia maumivu makali.
Bondia huyo aliyekuwa akishikilia taji la Dunia la WBF kabla ya kunyukwa kwenye pambano la kimataifa nchini Russia Desemba 21 mwaka jana, alisema mkono huo umekuwa ukimsumbua kwa muda mrefu na alishautibia ukapona, ila juzi ni kama ameutonesha na kumfanya ashindwe kufanya chochote kwa maumivu.
"Nipo hospitalini kwa sasa nimekuja kuucheki mkono wangu wa kulia ambao umekuwa ukinisumbua kitambo kirefu na kupona, ila juzi nikiwa kwenye mazoezi nilijitonesha na ninasikia maumivu makali na pia nashindwa kufanya lolote," alisema.
Alipouliuzwa anadhani itakuwaje wakati pambano lake la kimataifa dhidi ya Mrusi likiwa linakaribia, Cheka alisema atatoa maamuzi baada ya kujua hali ya mkono wake, kwani alidai saa nane alitakiwa kuingia katika kliniki maalum hospitalini.
"Sijajua mpaka sasa kuhusu mustakabali wa mchezo wangu, nataka kujua kwanza hali ya mkono wangu kwa sababu bila kuwa fiti ni vigumu kupanda ulingoni," alisema Cheka ambaye pia anashikilia mataji ya ICB, UBO na WB-C.

Burundi waanza kwa sare pacha CHAN, Nigeria kuvuna nini leo?

http://4.bp.blogspot.com/-s5_o31A7lqs/UfaAXRqeFxI/AAAAAAAAAtc/M-lfGHcmhzc/s1600/1070055_335448843254701_2023923399_n.jpg
Kikosi cha timu ya taifa ya Burundi, japo baadhi ya wachezaji hawakwenda Afrika Kusini
http://ewn.co.za/-/media/Images/2013/11/28/17/06/131128BafanaBafana%20jpg.ashx
Wenyeji Afrika Kusini wanaotarajiwa kuwavaa Mali jioni hii


MAJIRANI wa Tanzania na wawakilishi wengine wa ukanda wa CECAFA, Burundi jana ilianza michuano ya CHAN 2014 kwa kulazimishwa suluhu na Gabon katika mechi ya kundi D.
Suluhu imeifanya Burundi kuvuna pointi moja na kukamata nafasi ya pili nyuma ya DR Congo ambayo mapema jana iliitambia Mauritania kwa kuilaza bao 1-0 kwa mkwaju wa penati ambayo ilimponza beki wa Mauritania kutolewa nje kwa kadi nyekundu.
Michuano hiyo inatarajiwa kuendelea muda mchache ujao kwa wenyeji Afrika Kusini kuvaana na Mali huku timu zote zikiwa zimetoka kushinda mechi zao za kwanza dhidi Nigeria na Msumbiji ambazo zitaumana baadaye usiku huku zote zikiwa majeruhi.
Afrika Kusini iliifumua Msumbiji kwa mabao 3-1 wakati Nigeria ilijikwaa kwa majirani zao Mali kwa mabao 2-1, hivyo kufanya mechi za leo kutoa taswira ya timu zipi zitakazokuwa zikijitengenezea mazingira mazuri ya kusonga mbele au kuaga mapema michuano hiyo.
Nigeria ambayo ni Mabingwa wa Afrika (AFCON) huenda leo isikubali kufanywa asusa tena na Msumbiji ambayo itakuwa ikisaka pointi za kuwafanya waendelee kujipa matumaini ya kuvuka salama kwenye kudni la ambalo linaoonekana lina ushindani kama lilivyo kundi C lenye timu za Libya, Ghana, Ethiopia na Jamhuri ya Kongo.

Yanga yaendelea kugawa dozi Uturuki

MABINGWA wa soka nchini, Yanga imeendelea kufanya vyema kwenye mazoezi yake nchini Uturuki baada ya leo kuikwanyua Altay SK kwa mabao 2-0 ikiwa ni ushindi wa pili tangu itue nchini humo kujiandaa na duru la pili la Ligi Kuu.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Uturuki kupitia akaunti ya FB ya klabu hiyo maboa ya Yanga yaliwekwa kimiani katika kipindi cha pili kupitia kwa Didier Kavumbagu katika dakika ya 46 na Emmanuel Okwi kwenye dakika ya 57.
Klabu hiyo ya Antay SK inaashiriki Ligi daraja la Pili nchini humo na imekumbana na kipigo hicho baada ya ndugu zao wa Ankara Sekerspor kuchezea kipigo cha mabao 3-0 katika mechi ya kwanza kwa mabingwa hao wa Tanzania ikiwa nchini humo.
Mara baada ya mchezo huo wa leo Yanga itakamilisha ziara yake ya mafunzo wiki ijayo kwa kucheza na timu ya Simurq Zaqatala FC ya nchini Azberbaijan iliyopo katika Ligi Kuu ya nchi hiyo na msimu uliopita ikiwa imekamata nafasi ya nne kwenye msimamo wa Azerbaijan Premier League.

Simba kuvaana na Mtibwa kirafiki Jmosi

http://1.bp.blogspot.com/-bJYlCzY5xEo/UjMtGxqZGSI/AAAAAAAAmFk/7aK7ZjxjwgI/s640/simba%2Bvs%2Bmtibwa.JPG 
MABINGWA wa Mtani Jembe na washindi wa pili wa michuano ya Kombe la Mapinduzi, Simba inatarajiwa kushuka dimbani siku ya  Jumamosi kuumana na Mtibwa Sugar.
Mchezo huo wa kirafiki utakaochezwa kwenye uwanja wa Taifa utakuwa wa mwisho kwa Simba, kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kocha msaidizi wa Simba, Suleiman Matola, alisema wameamua kupata mechi moja katika uwanja wa taifa kabla ya kuanza kwa ligi.
Matola alisema sababu kuu ya kuamua kucheza mchezo huo ni moja ya sehemu yao ya kuipa timu yao mazoezi katika uwanja wa Taifa, ambao itachezea mechi zake za nyumbani.
Alisema wameamua kucheza mechi na timu ya Mtibwa, kwa sababu wanaitambua bora wake, hivyo wakicheza nayo inawapa maandalizi mazuri.
Matola alisema kuwa mchezo huo utafanyika majira ya saa 10.jioni, ikiwa ni moja ya sehemu ya kocha wao Zdravko Lugarusic, kutaka timu ngumu, ya kucheza na Simba.
"Haya ni maamuzi ya kocha mkuu Logarusic, anataka kuichezesha timu yake na timu ngumu, ambayo itaipa mazoezi mazuri timu yake, kabla ya kuanza kwaa ligi kuu" alisema Matola.
Simba iliyorejea juzi jijini Dar es Salaam, ikirtokea Zanzibar katika michuano ya Mapinduzi, ambapo ilifika hatua ya fainali na kupataushindi wa pili wa michuano hiyo.
SHAFII