STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, June 14, 2013

Serikali yaziruhusu Simba, Yanga kwenda Darfur kushiriki Kagame

Mh Amos Makalla kushoto akiwa na Ofisa wa Executive Solutions, Waratibu wa Udhamini wa Simba na Yanga kutoka TBL, Michael Mukunza kulia  
Na Mahmoud Zubeiry
SERIKALI imeziruhusu klabu za Simba SC, Yanga SC za Dar es Salaam na Super Falcons ya Zanzibar kwenda Sudan kushiriki michuano ya Klabu Buingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
Naibu Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo, Amos Makalla amefanya Mkutano na Waandishi wa Habari mjini Dodoma asubuhi ya leo kusema wameruhusu klabu hizo ziende Sudan baada ya kuhakikishiwa na Serikali ya nchi hiyo kwamba itatoa ulinzi wa kutosha dhidi ya timu za Tanzania.
Makalla amesema wameandikiwa barua na Serikali ya Sudan ikiwahakikishia kwamba timu za Tanzania zitapewa ulinzi mkubwa zisiathirike na machafuko yanayoedelea Sudan.
Kufuatia tamko la Serikali kuziruhusu klabu hizo sasa ziende Sudan, sasa ni juu yao ya klabu hizo kuamua kwenda au kutokwenda.
Lakini Katibu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Mkenya Nicholas Musonye amekwshatishia atazichukulia hatua kali klabu hizo zisipokwenda.
Juzi Serikali kupitia Makalla ilitoa tamko la kuzuia klabu za Tanzania kutokwenda Sudan kutokana na machafuko yanayoendelea nchini humo. 
Kufuatia tamko hilo, jana Yanga, ambao ni mabingwa watetezi kwa miaka miwili mfululizo, walitangaza kuvunja kambi yao hadi wiki mbili baadaye, wakati Kombe la Kagame linaanza kutimua vumbi Juni 18, mwaka huu.
Yanga wamepangwa Kundi C katika michuano hiyo pamoja na Ports ya Djibouti, Express ya Uganda na Vital 'O' ya Burundi, wakati wapinzani wao wa jadi, Simba SC wamepangwa Kundi A pamoja na wenyeji El-Mereikh, Elman  ya Somalia na APR ya Rwanda.
Katika michuano hiyo inayotarajiwa kufikia tamati Julai 2, mwaka huu mjini Khartoum, Sudan, mabingwa wa Kenya, Tusker wamepangwa Kundi B pamoja na wenyeji wengine, Al-Hilal, Falcons ya Zanzibar, Al Ahly Shandy ya Sudan na Al-Nasir Juba ya Sudan Kusini.
Yanga wataanza kampeni zao za kutetea taji hilo Juni 20 kwa kumenyana na Express, wakati Simba SC itashuka dimbani Juni 21 kufungua dimba na El-Mereikh, na mechi zote zitachezwa Elfashar.

Simba, Golden Bush kupimana ubavu kesho Dar

 
Kikosi cha Golden Bush Fc
Baadhi ya wachezaji vijana wa Simba
KLABU ya soka ya Simba ambayo imekuwa ikijifua kwenye uwanja wa Kinesi kwa ajili ya ushiriki wa Kombe la Kagame, japo kulikuwa na tishio la kutokwenda kutokana na kutishwa na hali ya usalama mjini Darfur, Sudan kesho jioni itashuka dimbani kuumana na Golden Bush Fc katika pambano la kirafiki.
Pambano hilo litachezwa kwenye uwanja wa Kinesi, ambapo Golden Bush inayonolewa na nyota wa zamani wa Kagera Sugar, Shija Katina, imepania kutoa upinzani mkali kwa 'Mnyama' inayonolewa na kocha Abdallah Kibadeni 'King Mputa'.
Kwa mujibu wa Mlezi wa klabu ya Golden Bush, Onesmo Wazir 'Ticotico', ametoa taarifa kwamba kikosi chao kipo imara kwa pambano hilo la timu yao ya vijana kabla ya Jumapili asubuhi timu yao wa Veterani , Golden Bus veterans kushuka dimbani kupambana na Mburahati Veterani uwanja wa Chuo Kikuu.
Taarifa rasmi ya Ticotico inasomeka kama ifuatavyo:

Wadau,
 
Naomba nitoe taarifa kwamba weekend hii, Golden Bush FC wazee na vijana tutakuwa na ratiba kama ifuatavyo:
 
Kesho Jumamosi (Uwanja Kinesi jioni)

Vijana wataingia uwanjani kumenyana na Wekundu wa Msimbazi (Simba sports Club). Maandalizi ya game yamekamilika na Simba hatimaye wamekubali kukabiliana na goldeb bush katika Uwanja wa Kinesi, timu imeandaliwa vizuri kabisa na tunataka kutoa upinzani wa kufa mtu dhidi ya Simba ili kuwakomesha na mpira wao wa magazetini. Game itaanza saa kumi na nusu alasiri/jioni
 
Keshokutwa Jumapili (Uwanja wa chuo Kikuu asubuhi)

Wazee wa kazi, wazee wa kuleta migogoro kwenye timu pinzani, wazee wanaotisha dar es salaam watakuwa na game ya kirafiki dhidi ya Mburahati veterans. Game hii itachezwa viwanja vya Chuo kikuu cha Dar es salaam, tumepeleka hii game pale kwa maksudi ili Mwenyekiti wa chuo apime mwenyewe kama timu yake inaweza kucheza na sisi au afuate utaratibu wa Survey Veterans (yaani kugomea mchezo).
 
Baada ya kusema hayo naomba sasa Mwenyekiti wa chuo ukubali ombi letu la kucheza na Chuo veterans siku ya weekend inayofuata tarehe 22/06/2013.
 
Naomba kutoa hoja
 
Onesmo

Makocha Stars, Ivory Coast uso kwa uso kesho kabla ya kuvaana Jumapili


Kocha wa Ivory Coast, Sabri Lamouchi
Kocha wa Stars, Kim Poulsen

Na Boniface Wambura
WAKATI timu ya Ivory Coast imewasili nchini jana usiku (Juni 13 mwaka huu) kwa ndege maalum, kocha wa timu hiyo Sabri Lamouchi na mwenzake wa Taifa Stars, Kim Poulsen watakutana na waandishi wa habari kuzungumzia mechi yao.

Mkutano huo utafanyika kesho (Juni 15 mwaka huu) saa 4 kamili asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Mkutano huo pia utajumuisha makocha wa timu zote mbili. Ivory Coast inafanya mazoezi yake ya kwanza leo (Juni 14 mwaka huu) saa 9 alasiri kwenye viwanja vya Gymkhana.

Timu zote kesho (Juni 15 mwaka huu) zitafanya mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Ivory Coast watafanya mazoezi saa 9 kabla ya kuwapisha Stars saa 10 kamili. Maandalizi yanaendelea vizuri ikiwemo kuwasili kwa maofisa wote wa mechi itakayochezwa Jumapili saa 9 kamili alasiri.

Wakati huo huo, mauzo ya tiketi kwa ajili ya mechi hiyo yameanza leo mchana (Juni 14 mwaka huu) katika vituo vya Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni, City Sports Lounge iliyoko Mtaa wa Samora na Azikiwe, Dar Live Mbagala, BMM Salon iliyoko Sinza Madukani na Uwanja wa Taifa.

Mauzo yataendelea kesho katika vituo hivyo, wakati siku ya mchezo yatafanyika Uwanja wa Taifa. Viingilio katika mechi hiyo ya mchujo ya Kombe la Dunia, Kanda ya Afrika katika kundi C ni sh. 5,000, sh. 7,000, sh. 10,000, sh. 15,000 VIP C, sh. 20,000 VIP B na VIP A sh. 30,000. Pia kuna kadi maalumu 100 kwa viti vya Wageni Maalumu (VVIP) zinazopatikana kwa sh. 50,000 katika ofisi za TFF.

TFF YATOA NOTISI YA MKUTANO MKUU

 
Rais wa TFF, Leodger Tenga na Katibu Mkuu, Angetile Osiah
Na Boniface Wambura
RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga ametoa notisi kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa Shirikisho utakaofanyika Julai 13 mwaka huu kwenye ukumbi wa NSSF Waterfront jijini Dar es Salaam ukiwa na ajenda moja ya marekebisho ya Katiba.

Notisi hiyo imetolewa juzi (Juni 12 mwaka huu). Rais ameitisha Mkutano huo kwa mujibu wa Ibara ya 25(1) ya Katiba ya TFF baada ya kupata maagizo kutoka Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kwa barua yake ya Aprili 29 mwaka huu.

Ajenda rasmi na taarifa nyingine zitatumwa kwa wajumbe siku 15 kabla ya Mkutano huo kwa mujibu wa Ibara ya 25(4) ya Katiba ya TFF. Wanachama wa TFF ambao ni vyama vya mikoa, vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu wanatakiwa kutuma majina ya wajumbe halali.

TFF inapenda kuwakumbusha wanachama wake kutuma majina ya wajumbe halali ili kufanikisha maandalizi ya Mkutano huo. Ni vizuri kuhakikisha kuwa jina linalotumwa ni la mjumbe halali wa Mkutano Mkuu kwa mujibu wa Katiba ya TFF.

Kivumbi cha RCL kuendelea kesho


Na Boniface Wambura
MECHI za kwanza za hatua ya tatu ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) kuwania nafasi tatu za kupanda Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao zinachezwa wikiendi hii kwenye viwanja vinne tofauti.

Mechi za kesho (Jumamosi) ni kati ya Kariakoo ya Lindi na Friends Rangers ya Dar es Salaam utakaochezwa katika Uwanja wa Ilulu mjini Lindi wakati Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya wenyeji Kimondo SC na Njombe Mji.

Timu za Machava FC ya Kilimanjaro na Stand United FC ya Shinyanga, Polisi Jamii ya Mara na Katavi Warriors ya Katavi zilizokuwa zipambane kesho mechi zao zimesogezwa mbele hadi keshokutwa (Jumapili). Mechi hizo zimesogezwa kutokana na viwanja vya Ushirika mjini Moshi na Karume mjini Musoma kuwa na shughuli nyingine za kijamii.

Hata hivyo, TFF imesisitiza kuwa ikibainika kuwa viwanja hivyo havikutumika kwa shughuli za kijamii siku hiyo ya Jumamosi, hatua kali zitachukuliwa kwa wanachama wake (vyama vya mpira wa miguu vya mikoa husika).

Mechi za marudiano za hatua hiyo ya tatu zitachezwa Juni 19 mwaka huu. Hatua ya nne ya RCL itachezwa kati ya Juni 23 na 23 mwaka huu wakati mechi za marudiano zitachezwa kati ya Juni 29 na 30 mwaka huu.

TFF yamlilia Abdallah Msamba

Abdallah Msamba (wa nne toka kulia) enzi za uhai wake

Na Boniface Wambura
Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mchezaji wa zamani wa timu za Pan Africans, Simba na Taifa Stars, Abdallah Msamba kilichotokea juzi usiku (Juni 12 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.

Msiba huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kwani kwa nyakati tofauti Msamba akiwa mchezaji, na baadaye kocha wa timu kadhaa alitoa mchango mkubwa kwa timu mbalimbali alizochezea na kufundisha ikiwemo Villa Squad, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.

TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Msamba, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Kinondoni (KIFA) na klabu ya Villa Squad na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.

Maziko ya mchezaji huyo yamefanyika leo (Juni 14 mwaka huu) katika makaburi ya Ndugumbi mkoani Dar es Salaam na kuhudhuriwa na mamia ya waombolezaji wakiwemo wachezaji wa zamani na viongozi mpira wa miguu nchini. Mungu aiweke roho ya marehemu Msamba mahali pema peponi. Amina


United yapania rekodi ya uhamisho kwa Ronaldo au Bale

Bale (kushoto) na Ronaldo (kulia)
KLABU ya Manchester United imepania kuweka rekodi ya dunia ya uhamisho wa wachezaji ikianza maisha bila ya Sir Alex Ferguson.
Wamiliki wa klabu hiyo ukoo wa Glazers wakiwa chini ya meneja mpya, David Moyes na fedha za kutosha imepania kuweka rekodi yta kumsajili ama Cristiano Ronaldo au Garreth Bale.
Ronadlo alifunguka jana kuwa milango i wazi kwake kurejea Old Trafford kwa kuwa alikuwa bado hajasaini mkataba wowote wa kusalia Real Madrid kama ilivyovumishwa awali.
Iwapo winga huyo wa Ureno ataamua kusaini mkataba mpya wa kusalia Bernabeu, basi Moyes atatupia macho yake kwa mchezaji bora wa EPL Bale anayeuzwa na klabu yake kwa kitita cha pauni Mil 85.
Wamiliki hao kutoka Marekani anataka kuifanya klabu yao iendelee kutamba Ulaya hata baada ya Ferguson kustaafu baada ya kuipa mataji lukuki ikiwa chini yake.
Ronaldo, 28, anaendelea kuwa chaguo la kwanza la United linalotupiwa macho na jana Mreno huyo aliandika kwenye akaunti yake ya Twitter kukanusha taarifa kwamba alikuwa anajiandaa kusaini mkataba mpya.
"Taarifa zote zilizoandikwa juu yangu kuhusu kusaini mkataba mpya ni uongo," aliandika Ronaldo.
Hata hivyo Rais wa Real Madrid, Florentino Perez  ameapa kumbakisha mreno huyo, hali inayoweza kutoa nafasi kwa Bale, 23 kuweka rekodi ya uhamisho iliyowekwa na Ronaldo aliposajiliwa na Real kutoka United miaka miwili iliyopita.
United ilimuuza Ronaldo kwa Real kwa kitita cha pauni Mil 80, lakini kama United itamnyakua Bale anayewindwa pia na Real Madrid na PSG atavunja rekodi ya dunia ya uhamisho.

Stars yaapa kuiduwaza Ivory Coast j'2

Kocha Kim Poulsen
WAKATI kikosi cha timu ya taifa ya Ivory Coast kikiwa kimetua salama nchini jana usiku tayari kuvaana na Taifa Stars, kocha mkuu wa Tanzania, Kim Poulsen ameapa kuwaduwaza wapinzani wao Jumapili katika pambano lao la kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2014.
Msafara wa timu ya Ivory Coast ulitua jana ukitokea Ghana ilipocheza mechi ya kirafiki ya kimataifa na kulala mabao 2-1 ikiwa njiani na walitatarajiwa kuanza kujifua leo tayari kwa pambano hilo, huku benchi la ufundi la Stars likiweka bayana kwamba iwe isiwe ni lazima tembo hao kuuwawa Jumapili uwanja wa Taifa.

Poulsen alinukuliwa jana akisema kuwa vijana wake wameiva na kwamba anaamini watawaduwaza mabingwa hao wa zamani wa Afrika (1992) na vinara wa viwango vya ubora wa soka barani.
Alisema kuwa wachezaji wake wanao uwezo na wanajua umuhimu wa kushinda mechi hiyo ambayo itaamua hatma ya Tanzania katika kampeni za kuwania kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani nchini Brazil.
"Wachezaji wako katika hali nzuri kuelekea kwenye mechi hiyo, asubuhi (jana) tulifanya mazoezi na tutarejea tena jioni kujiandaa zaidi. Kesho (leo) tutapumzika hadi Jumamosi jioni (kesho) tutakapofanya mazoezi ya mwisho," alisema Poulsen.
"Tunajua mechi itakuwa ngumu kutokana na wapinzani wetu kuwa na uwezo mkubwa, lakini tunaamini tutawafunga kama tulivyofanya dhidi ya timu nyingine ngumu kama Zambia na Cameroon. Tunatambua umuhimu wa kupata ushindi katika mechi hiyo na hivyo tutapambana kufa na kupona," aliongeza Poulsen.
Tanzania na Ivory Coast zimepangwa Kundi C ambalo pia lina timu za Morocco na Gambia. Ivory Coast ambao wanashika nafasi ya 13 katika orodha ya viwango vya ubora wa soka duniani, wanaongoza kundi hilo wakiwa na pointi 10, nne zaidi ya Stars inayoshika nafasi ya pili. Morocco wanaifuatia Stars wakiwa na pointi tano huku Gambia wakiwa mkiani mwa kundi hilo baada ya kuambulia pointi moja tu baada ya kushuka dimbani mara nne.
Taifa Stars, ambayo Jumamosi iliyopita ilikumbana na kipigo cha 2-1 dhidi ya mabingwa Afrika 1976, Morocco, itaingia uwanjani Jumapili ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa ugenini 2-0 dhidi ya Ivory Coast katika mechi yao ya kwanza iliyochezwa Juni 2 mwaka jana kwenye Uwanja wa Félix Houphouët-Boigny mjini Abidjan.
Stars pia watahitaji kulipiza kisasi na kuendeleza ubabe kwa timu 'vigogo' barani Afrika zinazokuja kucheza nao kwenye Uwanja wa Taifa. Desemba 22 mwaka jana waliifunga Zambia 1-0, kisha wakaipa kipigo kama hicho Cameroon Februari 6 kabla ya kuiadhibu Morocco 3-1 katika mechi yao ya kwanza ya Kundi C la Kombe la Dunia iliyochezwa Machi 24 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Langa Kileo kuagwa, kuzikwa Jumatatu

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgWGDLQAyXnDjIl54AOfwLOs9GWpx_kuFG4f29mB9PBbQjxKZjvccWU9K8Cq7w-AUdhQdWHuRv5exQJDSPhVY6yrhWNX3yGJjktqAA4RXy7VcT9j55-G2nYKoCMGsdG9eksuyDvsYiVDN5Q/s1600/LANGA+(1).jpg
Langa enzi za uhai wake
MWILI wa msanii Langa Kileo aliyefariki jana jioni unatarajiwa kuagwa siku ya Jumatatu kabla ya kuzikwa siku hiyo kwenye makaburi ya Kinondoni.
Taarifa kutoka kwa familia ya marehemu aliyefia hospitali ya Muhimbili, inasema kuwamwili huo utaagwa rasmi saa 7 ya Juni 17 na jioni yake kuzikwa kwenye makaburi ya Kinondoni na kwamba msiba kwa sasa upo nyumbani kwa wazazi wa marehemu, Mikocheni nyuma ya Hospitali ya AAR.
Langa, aliyeibuliwa na shindano la Coca Cola Pop Stars, akiunda kundi la WAKILISHA sambamba na wasanii Witness na Shaa, alifariki jana baada ya kuumwa ghafla kwa kilichoelezwa malaria ikiwa ni siku chache tangu atambulishe video ya wimbo wake wa 'Rafiki wa Kweli'.
Kifo hicho kimekuja wiki chache pia tangu tasnia ya sanaa nchini hasa muziki kumpoteza mkali mwingine wa hip hop, Albert Mangweha 'Ngwair' aliyefariki Mei 28 akiwa Afrika Kusini.
Mkali huyo anakumbukwa na ngoma zake kali akiwa na kundi la Wakilisha kabla ya kujiengua na kutoa kazi zake binafsi ikiwemo iliyomtangaza vyema ya Kimbia.

Simba yaamua kumtosa Ssenkoomi

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEh_TiroleOvZDZONKYHK37wThvZ5Uc3cunEt-Jl1CDD3w3ngrOkvo0xDy_j_U5vgSAPSPaJBk9ksk7arJU6Jc4H2G-95XTkqFP2UoMq1F2SX-9RQV2CxK8NM0BSbrDLNXYPfDL8Xk04-o5g/s1600/DSC_0738.jpg
Ssenkoomi (kulia)

KLABU ya soka ya Simba imeamua kuachana na beki Mganda Samuel Ssenkoomi baada ya kutoridhishwa na kiwango chake tangu ajiunge na timu hiyo Juni 4 mwaka huu kwa ajili ya majaribio. 
Habari za uhakika kutoka Simba  zinasema kuwa tayari uongozi umeshamkatia tiketi ya bus la  tayari kumrejesha kwao nchini Uganda.
Kiongozi mmoja wa Simba amesema kwamba Ssenkoomi anatarajiwa kuondoka nchini wakati wowote kuanzia sasa baada ya kushindwa kuonesha kiwango cha kuridhisha tangu atue nchini kwa majaribio. 
Ssenkoomi aliyeanza  kujinoa na wenzake Juni 5 kupitia mazoezi yanayoendelea kwenye uwanja wa Kinesi, ameshindwa kuonesha makali kama ilivyotarajiwa huku kocha mkuu wa Simba Abdallah ‘King’ Kibaden kwa nyakati tofauti alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa haridhishwi na kiwango cha Mganda huyo ambaye alikuwa nakipiga katika klabu ya URA.

Tamasha la filamu la Grand Malt kufanyika Mwanza




 Msanii wa Filam, nchini, Jaqueline Wolper, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Tamasha hilo, wakati wa mkutano huo uliofanyika jijini Dar es Salaam




Meneja Habari na Mawasiliano wa TBL, Edith Mushi (katikati) akizungumza na waandishi wa habari, wakati wa mkutano huo (kushoto) ni Mkurugenzi wa Sophia Records walio waandaaji na waasisi wa tamasha hilo, Musa Kissoky.

**************************************

Na Mwandishi Wetu

TAMASHA la Wazi la Filamu Tanzania maarufu kama ‘Grand Malt Tanzania Open Film Festival’ mwaka huu linatarajiwa kufanyika katika Viwanja vya Sahara jijini Mwanza.



 Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa tamasha hilo uliofanyika jijini Dar es Salaam jana, Meneja wa kinywaji cha Grand Malt, Consolata Adam alisema, wanaamini litafanikiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na mikakati waliyoiweka.



Consolata alisema, tamasha hilo linatarajiwa kufanyika katika viwanja hivyo kuanzia Julai 1-7, mwaka huu huku kukiwa na filamu mbalimbali zitakazoonyeshwa katika kipindi hicho.


“Tumejipanga kufanya uhamasishaji wa kutosha ili kuwawezesha wakazi wa Mwanza na maeneo ya jirani kuweza kuhudhuria tamasha hili. Tunawakaribisha watu wote wenye mapenzi na filamu zetu za Tanzania kufika na kushuhudia tamasha hili ambalo mwaka huu limeboreshwa zaidi,” alisema Consolata.


Naye Meneja Habari na Mawasiliano wa TBL, Edith Mushi alisema kwa ushirikiano na kampuni ya Sophia Records, ambao ndio waandaaji na waasisi wa tamasha hilo, wanaamini litafana na kufanikiwa zaidi mwaka huu.



“Tumeona jinsi wananchi wanavyozipenda filamu za Tanzania maarufu kama ‘Bongo Movies’ na jinsi walivyo na kiu ya kuwaona wasanii wa filamu ana kwa ana,” alisema.



Edith alisema waliingia mkataba wa miaka mitatu wa kudhamini tamasha hilo na kwa sasa wanalipeleka mikoa mingine kama walivyofanya kwa kulipeleka Mwanza kutoka Tanga lilikofanyika mwaka jana.



 “Tunawaahidi Watanzania wote kwa ujumla, kuwa tamasha hili litakuwa na mvuto wa aina yake na hatimae kutumika kulitangaza Taifa letu kupitia tasnia hii ya filamu ambayo kwa sasa inakua kwa kasi kubwa,” alisema Edith na kutaka kampuni au taasisi nyingine kujitokeza ili kuwa wadhamini wenza.



Naye Mkurugenzi wa Sophia Records walio waandaaji na waasisi wa tamasha hilo, Musa Kissoky alitoa shukrani kwa Grand Malt kulidhamini hivyo kuliboresha kwa kiasi kikubwa.



“Tunawashukuru sana Grand Malt na wasanii wa Bongo Movie, hususan uongozi wao, kwa ushirikiana mkubwa wanaotupatia katika kuhakikisha tamasha hili linafanikiwa.”

 

 Tamasha hilo litakuwa likianza asubuhi hadi usiku na kutakuwepo na burudaniu mbalimbali zitakazosindikiza na hakutakuwa na kiingilio, huku akisema bendi ya Extra Bongo watakuwepo siku ya uzinduzi.



Wasanii wote maarufu wa filamu wanatarajia kutua Mwanza Juni 29, ambapo siku hiyo watajumuika na wakazi wa Mwanza ndani ya Club Lips na siku inayofuata watashiriki katika shughuli za kijamii katika hospitali ya Mkoa wa Mwanza ya Sekou Toure, ambapo watatoa vyandarua zaidi ya 1000.



Akizungumzia tamasha hilo, mwigizaji Jacqueline Wiolper alisema, wana furaha kubwa na wanaamini watapata mengi zaidi wakati wote wa tamasha hilo.



Tamasha hilo linadhaminiwa kwa mwaka wa tatu sasa na kinywaji kisicho na kilevi cha Grand Malt kinachozalishwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).

TFF yasisitiza 'kiama' cha mapro kipo pale pale

Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limeendelea kusisitiza matumizi ya kanuni ya kuzitaka klabu kutosajili wachezaji wa kigeni zaidi ya watatu katika msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Shirikisho hilo limesisitiza kwamba kanuni hiyo ni lazima iingizwe na kuzingatiwa na klabu zote 14 zitakazoshiriki ligi kuu ya Bara msimu ujao kwavile ni hoja iliyokubaliwa na wajumbe wengi waliohudhuria mkutano uliofanyika mwaka  2010 kupitisha mapendekezo mbalimbali ya Azimio la Bagamoyo.
Azimio hilo lilifikia makubaliano ya kupunguza idadi ya wachezaji wa kigeni kutoka watano wa sasa hadi watatu ili kutoa fursa zaidi kwa wachezaji wazawa kwa manufaa ya taifa.
Akizungumza na NIPASHE, Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema kuwa wataingiza kipengele cha kusajili wachezaji wasiozidi watatu kwenye kanuni za ligi kitakachoanza kutumika msimu ujao (2013/14), maamuzi ambayo yatazilazimu klabu zote, zikiwamo za Yanga na Azam zitakazoiwakilisha nchi katika michuano ya Afrika kupunguza idadi ya nyota wao wa kigeni.
Klabu hizo zilizomaliza katika nafasi ya pili na ya tatu pamoja na Simba ndizo ambazo kwa misimu kadhaa zimekuwa na wachezaji wa kigeni zaidi ya watatu.
Katika msimu uliopita, Yanga ilikuwa na Haruna Niyonzima 'Fabregas' (Rwanda), Didier Kavumbagu (Burundi), Hamis Kiiza (Uganda), Mbuyu Twite (Rwanda) na Yaw Berko (Ghana). Simba iliwatumia Daniel Akuffor (Ghana), Mussa Mude (Uganda), Felix Sunzu (Zambia), Emmanuel Okwi (Uganda) ambaye baadaye walimuuza katika klabu ya Etoile Du Sahel ya Tunisia, Abel Dhaira (Uganda), Komalbil Keita (Mali) na Mkenya Pascal Ochieng.
Nyota wa kigeni waliopo Azam ni Kipre Tchetche na Kipre Bolou (Ivory Coast), Brian Umony (Uganda) na nyota wa kimataifa kutoka Kenya, Joackins Atudo na Humphrey Mieno.
Wambura alisema kuwa katika mkutano huo ambao viongozi wa klabu zote za ligi kuu msimu wa 2010/11 walihudhuria, walikubalina kwamba kuanzia msimu wa 2013/14 klabu zisisajili zaidi ya wachezaji watatu wa kigeni ili kuwapa nafasi wachezaji wazawa.
"Kipengele hicho kilitakiwa kiingizwe msimu uliopita (2012/13) lakini baadhi ya klabu zikaomba kanuni hiyo ianze kutumika msimu wa 2013/14 kwa kuwa baadhi ya wachezaji wa kigeni zilizokuwa nao msimu wa 2010/11 walikuwa na mikataba iliyokuwa inamalizika msimu uliopita (2012/13)," alisema Wambura.
"Tunaamini kwamba klabu ambazo zinasajili wachezaji wa kigeni kwa sasa zinatambua kuanza kutumika kwa kipengele hicho kwa sababu zilikuwa na wawakilishi katika mkutano huo," aliongeza Wambura.

KLABU ZANENA
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti jana, viongozi wa klabu walikuwa na mitazamo tofauti kuhusu kuanzishwa kwa kanuni hiyo.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage aliponda jambo hilo, akisema litaziathiri klabu za Tanzania zikienda kwenye michuano ya kimataifa ambako hazijapata mafanikio ya muda mrefu.
"Maamuzi hayo yatazidhoofisha klabu zetu kwa sababu tutalazimika kusajili wachezaji wa ndani hata kama hawana uwezo. Matokeo yake timu zetu hazitafanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa. Kwa kuwa TFF ndiyo mama wa mpira nchini, sisi tutafuata walichoamua," alisema Rage.
Meneja wa Azam, Patrick Kahemele alikosoa pia kuingizwa kwa kanuni hiyo akisema kuwa imedhamiria kuwabeba wachezaji wa ndani pasipo kuzingatia athari zitakazozikumba klabu na ligi kwa ujumla.
Alisema kuwa kinachopaswa kufanywa na TFF kwa sasa ni kuangalia namna ya kuibua, kulea na kukuza vijana wenye vipaji vya soka ili baadaye wasajiliwe na klabu kubwa za nje ya nchi.
"Kinachoonekana hapa ni kwamba tumejipanga kuwabeba wachezaji wa Tanzania na kuwanyima nafasi wageni katika ligi yetu. Kuwa na wachezaji wa kigeni wachache katika ligi kuu si hoja katika kukuza viwango vya wachezaji wa ndani. Tunatakiwa tuwe na wachezaji wengi wa kigeni wenye uwezo mkubwa kisoka ili wachezaji wetu wajifunze kutoka kwao," alisema Kahemele.
"Huku kubebana hakutatufikisha kokote, tutakuwa na mpira wa kucheza sisi wenyewe usiokuwa na vionjo vya watu wa nje. Tutengeneze mfumo utakaowawezesha vijana wetu kwenda kucheza nje badala ya kukimbilia kuanziasha kanuni za kuzuia wageni kwenye ligi zetu. TP Mazembe ina wachezaji nyota kibao lakini Mtanzania Mbwana Samatta anapata namba kwa sababu ameandaliwa kushindana," alisema Kahemele.
Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako alisema kinachotakiwa zaidi ni kuangalia vigezo vya wachezaji wa kigeni wanaopaswa kucheza ligi kuu ya Tanzania Bara.
"Kanuni hiyo iweke taratibu zitakazoweka wazi sifa za mchezaji wa kigeni anayetakiwa kusajiliwa na klabu zetu. Kwa kufanya hivyo klabu zitakuwa na wachezaji wa kigeni ambao wataleta changamoto ya ligi yetu na vijana wetu wa ndani watajifunza kutoka kwao."

Chanzo:NIPASHE