STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, June 14, 2013

TFF yasisitiza 'kiama' cha mapro kipo pale pale

Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limeendelea kusisitiza matumizi ya kanuni ya kuzitaka klabu kutosajili wachezaji wa kigeni zaidi ya watatu katika msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Shirikisho hilo limesisitiza kwamba kanuni hiyo ni lazima iingizwe na kuzingatiwa na klabu zote 14 zitakazoshiriki ligi kuu ya Bara msimu ujao kwavile ni hoja iliyokubaliwa na wajumbe wengi waliohudhuria mkutano uliofanyika mwaka  2010 kupitisha mapendekezo mbalimbali ya Azimio la Bagamoyo.
Azimio hilo lilifikia makubaliano ya kupunguza idadi ya wachezaji wa kigeni kutoka watano wa sasa hadi watatu ili kutoa fursa zaidi kwa wachezaji wazawa kwa manufaa ya taifa.
Akizungumza na NIPASHE, Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema kuwa wataingiza kipengele cha kusajili wachezaji wasiozidi watatu kwenye kanuni za ligi kitakachoanza kutumika msimu ujao (2013/14), maamuzi ambayo yatazilazimu klabu zote, zikiwamo za Yanga na Azam zitakazoiwakilisha nchi katika michuano ya Afrika kupunguza idadi ya nyota wao wa kigeni.
Klabu hizo zilizomaliza katika nafasi ya pili na ya tatu pamoja na Simba ndizo ambazo kwa misimu kadhaa zimekuwa na wachezaji wa kigeni zaidi ya watatu.
Katika msimu uliopita, Yanga ilikuwa na Haruna Niyonzima 'Fabregas' (Rwanda), Didier Kavumbagu (Burundi), Hamis Kiiza (Uganda), Mbuyu Twite (Rwanda) na Yaw Berko (Ghana). Simba iliwatumia Daniel Akuffor (Ghana), Mussa Mude (Uganda), Felix Sunzu (Zambia), Emmanuel Okwi (Uganda) ambaye baadaye walimuuza katika klabu ya Etoile Du Sahel ya Tunisia, Abel Dhaira (Uganda), Komalbil Keita (Mali) na Mkenya Pascal Ochieng.
Nyota wa kigeni waliopo Azam ni Kipre Tchetche na Kipre Bolou (Ivory Coast), Brian Umony (Uganda) na nyota wa kimataifa kutoka Kenya, Joackins Atudo na Humphrey Mieno.
Wambura alisema kuwa katika mkutano huo ambao viongozi wa klabu zote za ligi kuu msimu wa 2010/11 walihudhuria, walikubalina kwamba kuanzia msimu wa 2013/14 klabu zisisajili zaidi ya wachezaji watatu wa kigeni ili kuwapa nafasi wachezaji wazawa.
"Kipengele hicho kilitakiwa kiingizwe msimu uliopita (2012/13) lakini baadhi ya klabu zikaomba kanuni hiyo ianze kutumika msimu wa 2013/14 kwa kuwa baadhi ya wachezaji wa kigeni zilizokuwa nao msimu wa 2010/11 walikuwa na mikataba iliyokuwa inamalizika msimu uliopita (2012/13)," alisema Wambura.
"Tunaamini kwamba klabu ambazo zinasajili wachezaji wa kigeni kwa sasa zinatambua kuanza kutumika kwa kipengele hicho kwa sababu zilikuwa na wawakilishi katika mkutano huo," aliongeza Wambura.

KLABU ZANENA
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti jana, viongozi wa klabu walikuwa na mitazamo tofauti kuhusu kuanzishwa kwa kanuni hiyo.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage aliponda jambo hilo, akisema litaziathiri klabu za Tanzania zikienda kwenye michuano ya kimataifa ambako hazijapata mafanikio ya muda mrefu.
"Maamuzi hayo yatazidhoofisha klabu zetu kwa sababu tutalazimika kusajili wachezaji wa ndani hata kama hawana uwezo. Matokeo yake timu zetu hazitafanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa. Kwa kuwa TFF ndiyo mama wa mpira nchini, sisi tutafuata walichoamua," alisema Rage.
Meneja wa Azam, Patrick Kahemele alikosoa pia kuingizwa kwa kanuni hiyo akisema kuwa imedhamiria kuwabeba wachezaji wa ndani pasipo kuzingatia athari zitakazozikumba klabu na ligi kwa ujumla.
Alisema kuwa kinachopaswa kufanywa na TFF kwa sasa ni kuangalia namna ya kuibua, kulea na kukuza vijana wenye vipaji vya soka ili baadaye wasajiliwe na klabu kubwa za nje ya nchi.
"Kinachoonekana hapa ni kwamba tumejipanga kuwabeba wachezaji wa Tanzania na kuwanyima nafasi wageni katika ligi yetu. Kuwa na wachezaji wa kigeni wachache katika ligi kuu si hoja katika kukuza viwango vya wachezaji wa ndani. Tunatakiwa tuwe na wachezaji wengi wa kigeni wenye uwezo mkubwa kisoka ili wachezaji wetu wajifunze kutoka kwao," alisema Kahemele.
"Huku kubebana hakutatufikisha kokote, tutakuwa na mpira wa kucheza sisi wenyewe usiokuwa na vionjo vya watu wa nje. Tutengeneze mfumo utakaowawezesha vijana wetu kwenda kucheza nje badala ya kukimbilia kuanziasha kanuni za kuzuia wageni kwenye ligi zetu. TP Mazembe ina wachezaji nyota kibao lakini Mtanzania Mbwana Samatta anapata namba kwa sababu ameandaliwa kushindana," alisema Kahemele.
Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako alisema kinachotakiwa zaidi ni kuangalia vigezo vya wachezaji wa kigeni wanaopaswa kucheza ligi kuu ya Tanzania Bara.
"Kanuni hiyo iweke taratibu zitakazoweka wazi sifa za mchezaji wa kigeni anayetakiwa kusajiliwa na klabu zetu. Kwa kufanya hivyo klabu zitakuwa na wachezaji wa kigeni ambao wataleta changamoto ya ligi yetu na vijana wetu wa ndani watajifunza kutoka kwao."

Chanzo:NIPASHE

No comments:

Post a Comment