STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, May 1, 2014

Msajili airejesha katiba ya Simba irekebishwe

Mkurugenzi wa Michezo, Leonard Thadeo
Na: Genofeva Matemu – Afisa Mawasiliano Serikalini (WHVUM)
SERIKALI kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imemaliza kupitia Rasimu ya Katiba ya klabu ya Simba kwa ajili ya kuidhinisha katiba hiyo na kuifanya klabu hiyo kuendelea na taratibu za uchaguzi mkuu.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Michezo Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bw. Leonard Thadeo alipokutana na waandishi wa habari kujibu hoja mbalimbali za waandishi leo jijini Dar es Salaam.
Akijibu moja ya hoja iliyomtaka kufafanua Wizara imefikia wapi katika upatikanaji wa Katiba ya Klabu ya Simba Bw. Thadeo amesema kuwa upitiaji wa Katiba umemelizika na kuonekana kuwa na mapungufu machache yanayohitaji kurekebishwa ili Wizara iweze kuidhinisha katiba hiyo.
“Mchakato wa upitiaji wa Katiba ya klabu ya Simba umemalizika jana lakini kumekuwepo na mapungufu machache yanayohitaji kurekebishwa ili Wizara iweze kuidhinisha Katiba hiyo” amesema Bw. Thadeo.
Akifafanua zaidi Bw. Thadeo amesema kuwa mapungufu hayo yanalenga zaidi upande wa kisheria ambapo mtu anaweza kutafsiri neno vibaya hivyo kupata maana tofauti na Katiba ilivyokusudia hivyo kuitaka klabu hiyo kufanya marekebisho hayo mapema na kurejesha Katiba hiyo Wizarani kwa ajili ya kuidhinishwa.
Aidha Bw. Thadeo amewataka waandishi wa habari pamoja na wanachama wa klabu ya Simba kuwa na subira ili waweze kupata Katiba itakayokidhi malengo ya klabu yao kwani mchakato wa upitiaji wa Katiba ulihitaji umakini.

Azam yazidi kuibomoa Yanga, yambeba Domayo

Kavumbagu na Domayo walitotua Azam baada ya mikataba yao Yanga kumalizika
BAADA ya kufanikiwa kumnyakua mshambuliaji wa kimataifa wa Yanga, Didier Kavumbagu, klabu ya Azam imeendelea kuibomoa Yanga kwa kumsajili kiungo wa klabu hiyo ya Jangwani, Frank Domayo.
Domayo ambaye pia ni kiungo wa timu ya Taifa (Taifa Stars) ameingia mkataba wa miaka miwili na mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Bara.
Kiungo huyo aliyejijengea umaarufu mkubwa klabuni hapo msimu huu akimuweka benchi nahodha wa timu ya taifa ya Rwanda, Haruna Niyonzima, amesajiliwa kutokana na kupendekezwa na kocha wa Azam, Mcameroon Joseph Omog.
"Domayo ameshasaini. Ni katika kukamilisha maelekezo ya kocha," alisema Katibu Mkuu wa Azam, Nasoro Idrisa.
Kusajiliwa kwa Domayo, kijana mdogo mwenye kipaji, kumekuwa ni pigo kubwa kwa Yanga, ambayo tayari msimu huu imevuliwa taji lake la ubingwa wa Tanzania Bara kwa matajiri hao wa Chamazi.
Azam ambao wametwaa ubingwa wa Bara kwa mara ya kwanza msimu huu wameanza usajili mapema ili kuunda kikosi cha kitakachoshiriki mashindano ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika mapema mwakani.
Wachezaji wengine wanaotajwa kutakiwa na Azam ni pamoja na washambuliaji wa Simba, Amissi Tambwe na Ramadhani Singano.
Hata hivyo, nyota hao wawili bado wana mikataba na klabu yao ambayo mwakani haitashiriki tena michuano ya kimataifa.
Katika hatua nyingine Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeanza uchunguzi juu ya kitendo cha viongozi wa Azam kuvamia kambi ya Stars mjini Mbeya na kumsainisha Domayo kwa kilichoelezwa ni kwenda kinyume na taratibu za usajili.
Hata hivyo Azam siyo ya kwanza kufanya hivyo kwani Yanga na Simba walishawahi kufanya misimu iliyopita na haikufanywa uchunguzi wowote kwa nia ya kuchukulia hatua waliohusisha na ukiukwaji huo.

Atletico Madrid moto, yaiua Chelsea kwao yaifuata Real fainali Ulaya

Chelsea wakishangilia bao lao lililofungwa na Fernanndo Torres
Atletico wakipambana kuwania kutinga fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya
MEI 24 mjini Lisbon, Ureno itakuwa Fainali ya timu za jiji la Madrid, baada ya Atletico Madrid kuwafuata wapinzani wao wa jiji hilo Real Madrid kufuatia kutoa kipigo cha mabao 3-1 kwa Chelsea katika pambano la marudiano la Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Chelsea ikiwa kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Stanford Bridge ilishindwa kuhimili makali ya wapinzani wao na kukubali kuondolewa kwa mara ya kwanza na timu za Hispania katika hatua hiyo baada ya kutandikwa huku wakishuhudiwa na gwiji wa zamani wa Argentina, Diego Maradona.
Vijana wa Mourinho walitangulia kupata bao la kuongoza lililofugwa na nyota wa zamani wa Atletico, Fernando Torres katika dakika ya 36 kabla ya wageni kusawazisha kupitia kwa Adrian dakika moja kabla ya kwenda mapumziko.
Kipindi cha pili kilikuwa kibaya kwa Chelsea baada ya Atletico kupata bao la pili lililofungwa kwa penati na Diego Costa katika dakika ya 60 kabla ya Tuiran kuongeza bao la tatu dakika ya 72 na kuihakikishia Atletico kutinga fainali za michuano hiyo kwa mara ya kwanza baada ya miaka 20 iliyopita.
Timu hiyo sasa itakutana na mahasimu wao, Real Madrid iliyowavua taji Bayern Munich juzi kwa kuicharaza mabao 4-0 nyumbani kwao na kufuzu hatua hiyo kwa jumla ya mabao 5-0 baada ya mechi ya kwanza mjini Madrid kupata ushindi wa bao 1-0.