STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, May 1, 2014

Azam yazidi kuibomoa Yanga, yambeba Domayo

Kavumbagu na Domayo walitotua Azam baada ya mikataba yao Yanga kumalizika
BAADA ya kufanikiwa kumnyakua mshambuliaji wa kimataifa wa Yanga, Didier Kavumbagu, klabu ya Azam imeendelea kuibomoa Yanga kwa kumsajili kiungo wa klabu hiyo ya Jangwani, Frank Domayo.
Domayo ambaye pia ni kiungo wa timu ya Taifa (Taifa Stars) ameingia mkataba wa miaka miwili na mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Bara.
Kiungo huyo aliyejijengea umaarufu mkubwa klabuni hapo msimu huu akimuweka benchi nahodha wa timu ya taifa ya Rwanda, Haruna Niyonzima, amesajiliwa kutokana na kupendekezwa na kocha wa Azam, Mcameroon Joseph Omog.
"Domayo ameshasaini. Ni katika kukamilisha maelekezo ya kocha," alisema Katibu Mkuu wa Azam, Nasoro Idrisa.
Kusajiliwa kwa Domayo, kijana mdogo mwenye kipaji, kumekuwa ni pigo kubwa kwa Yanga, ambayo tayari msimu huu imevuliwa taji lake la ubingwa wa Tanzania Bara kwa matajiri hao wa Chamazi.
Azam ambao wametwaa ubingwa wa Bara kwa mara ya kwanza msimu huu wameanza usajili mapema ili kuunda kikosi cha kitakachoshiriki mashindano ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika mapema mwakani.
Wachezaji wengine wanaotajwa kutakiwa na Azam ni pamoja na washambuliaji wa Simba, Amissi Tambwe na Ramadhani Singano.
Hata hivyo, nyota hao wawili bado wana mikataba na klabu yao ambayo mwakani haitashiriki tena michuano ya kimataifa.
Katika hatua nyingine Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeanza uchunguzi juu ya kitendo cha viongozi wa Azam kuvamia kambi ya Stars mjini Mbeya na kumsainisha Domayo kwa kilichoelezwa ni kwenda kinyume na taratibu za usajili.
Hata hivyo Azam siyo ya kwanza kufanya hivyo kwani Yanga na Simba walishawahi kufanya misimu iliyopita na haikufanywa uchunguzi wowote kwa nia ya kuchukulia hatua waliohusisha na ukiukwaji huo.

No comments:

Post a Comment