STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, June 3, 2013

Mwili wa Ngwair waagwa rasmi, kutua nchini kesho mchana


Baadhi ya Watanzania waishio Afrika Kusini wakiuaga mwili wa Ngwair (Picha kwa hisani ya deejaydeo.blogspot.com)


Kinjekitile 'Kinje' Ngombale Mwiru (mbele) akiwa na watanzania wengine kufanya harakati za mwili wa Ngwair kurejeshwa nchini.

BAADA ya danadana ya siku kadhaa juu ya ratiba kamili ya kuwasili kwa mwili wa msanii Albert Mangwea 'Ngwair' aliyefariki Jumanne iliyopita nchini Afrika Kusini, sasa imethibitika kuwa atatua nchini kesho mchana kabla ya mwili huo kuagwa na watanzania kwenye viwanjavya Leaders, Kinondoni.
Taarifa zilizopatikana jioni hii zinasema kuwa mwili wa msanii huyo umeagwa rasmi na watanzania waliopo nchini humo na kwamba kila kitu kimekamilika kwa ajili ya kesho kurafirishwa kuletwa Tanzania tayari kwa mazishi yatakayofanyika Alhamis katika makaburi ya eneo la Kihonda, Morogoro.
Awali kulikuwa na sintofahamu juu ya siku halisi ya mwili wa mkali huyo wa (free Style) kutokana na taarifa ya kwanza kuelezwa angetua nchini Jumamosi, kisha kuelezwa Jumapili kabla ya ratiba hiyo kuutwa asubuhi ya siku hiyo na kuelezwa ingekuwa leo au kesho.
Hata hivyo uhakika kabisa ni kwamba mwili wa nyota huyo wa albamu ya a.k.a Mimi na Ng'e utatua kesho kabla ya kuagwa jijini na kusafirishwa kwenda kuzikwa mjini Morogoro ambapo matayarisho mengine yamekamilika kwa kuhifadhi mwili wa mkali huyo aliyeenda Afrika Kusini kufanya maonyesho ya muziki na msanii mwezake M to the P, anayeendelea vyema kiafya nchini humo baadaya awali kuwa mahututi.

Azam yaanika silaha zake kwa msimu wa 2013-2014

Kocha Stewart John Hall akionyesha makeke yake kwenye mazoezi

Wakali wa klabu ya Azam ambapo baadhi wa hawatakuwa kwenye kikosi cha msimu ujao akiwemo Gaucho (24)
 
KLABU ya soka ya Azama imeweka bayana kwamba haitaacha mchezaji iliyo na mkataba naye na wala haitaongeza mchezaji mwingine katika kikosi ilichonacho sasa. 
Kwa mujibu wa taarifa yake, Azam imesema kama ilivyokuwa wakati wa dirisha kubwa la usajili 2012/13 ambapo Azam  ilimuongeza George Odhiambo 'Blackberry' pekee, safari hii imepandisha twachezaji wawili wa U20, Mudathir Yahaya na golikipa Hamadi Juma Yahya Kadedi na kufunga zoezi la usajili.
Taarifa hiyo inanukuu ripoti toka kwa Kocha mkuu wa Azam Stewart Hall, kuwa hakuna sababu ya klabu kwenda nje kusajili wachezaji ambao viwango vyao havipishani na waliopo klabuni.
Mchezaji Abdulhalim Humoud amepata timu nchini Afrika ya Kusini, Abdi Kassim 'Babi' mkataba wake umekwisha kama ilivyo kwa Deogratius Munishi Dida huku Uhuru Selemani akirejeshwa Simba SC baada ya kumaliza msimu wa mkopo na Azam FC.
Wachezaji wengine wote waliosalia wanabaki klabuni na kocha mkuu amependekeza baadhi ya makinda wa Under 20 walioonesha viwango vya juu wapandishwe timu kubwa, wapewe mikataba na kisha wapelekwe kwa mkopo ili wakapate nafasi ya kucheza. Wachezaji hao ni Omary Mtaki na Kevin Friday.
Azam ambayo imemaliza ligi ikishika nafasi ya pili kwa msimu wa pili mfululizo itaanza kambi ya kujiandaa na msimu mpya hapo June 24 kwa mujibu wa ratiba ya mwalimu na baada ya kumaliza kipindi cha pre season, kikosi cha Azam kitasafiri nje ya nchi kucheza mechi za majaribio kama ilivyo kawaida yake.

Wachezaji wanaounda kikosi cha Azam FC ni;

Magolikipa; Mwadili Ally, Aishi Salum na Hamad Juma Yahya

Mabeki; Himid Mao, Erasto Nyoni, Waziri Salum, Samih Nuhu, Luckson Kakolaki, Aggrey Morris, Said Moradi, David Mwantika na Jockins Atudo

Viungo; Kipre Bolou, Salum Abubakar, Jabir Aziz, Ibrahim Mwaipopo, Humphrey Mieno na Mudathir Yahya

Washambuliaji; John Bocco, Gaudence Mwaikimba, Khamis Mcha, Kipre Tchetche, Brian Umony na Abdallah Seif Karihe

Sh Mil 32 zachangwa msiba wa Ngwair, mwili kutua kesho

Ngwair enzi za uhai wake


KAMATI ya Mazishi ya aliyekuwa Msanii wa Bongo Fleva, Albert Mangwea ‘Ngwea’, mpaka jana mchana ilikuwa imekusanya jumla ya Sh milioni 32 kutoka kwa wadau mbalimbali.

Kamati hiyo inahitaji Sh milioni 50 kwa ajili ya kusaidia kusafirisha mwili wa marehemu kutoka Afrika Kusini mpaka Morogoro kwa ajili ya mazishi. Fedha hizo pia zinahitajika kwa ajili ya kuratibu shughuli nzima ya mazishi.

Mangwea alifariki dunia Jumanne iliyopita nchini Afrika Kusini akiwa usingizini kwa madai ya kuzidisha matumizi ya madawa ya kulevya. 

Alitarajiwa kuwasili nchini jana lakini kushindwa kutoka kwa ripoti ya uchunguzi wa madaktari kwa wakati, kumesababisha isijulikane atatua lini, licha ya kudaiwa kuwa anaweza kutua leo.

Kamati ya Mazishi bado inaendelea na mchakato wa kuratibu shughuli hiyo jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na mwandishi wetu akiwa Mbezi Goig jijini Dar ambako ndiko kwenye msiba huo, mmoja wa waweka hazina wa kamati hiyo, Paul Matthysse ‘P-Funk’, alisema mpaka sasa kamati yake imefikisha Sh 32,259,000 ingawa wanatarajia kuendelea kupokea michango mbalimbali kutoka kwa wadau.

Miongoni mwa watu wa kwanza kutoa michango yao katika msiba huo ni P-Funk aliyetoa Sh milioni tano, Clouds Media Group (Sh milioni tano) na Push Mobile (Sh milioni tano). 

Juzi Kampuni ya Global Publishers ilitoa Sh milioni moja.
“Nawasisitiza Watanzania waendelee kutoa michango yao kwa ndugu yao ili kuonyesha umoja tulionao. Fedha zikiwa nyingi tunataka kumfanyia kitu mama yake ili kuendelea kumfariji kwani kipindi hiki ni kigumu kwake,” alisema P-Funk.
 

Wakati huohuo jana  taarifa zilisema mama mzazi wa Mangwea aishie Morogoro, Denisia Mangwea, alipandwa na presha baada ya jana kupata taarifa kuwa mwili wa mwanaye umezuiwa Afrika Kusini kutokana na uchunguzi wa madawa ya kulevya. Alikimbizwa hospitali na inadaiwa anaendelea vizuri.

Mangwea aliwahi kutamba na nyimbo kadhaa kali zikiwemo Gheto Langu, She Got a Gwan, Mikasi na Tupo Juu.

Chelsea yathibitisha Mourinho kutua darajani


Back in town: Jose Mourinho holds his Chelsea shirt after being confirmed as the new Chelsea manager
Kocha Jose Mourinho akiwa na uzi wa Chelsea baada ya kutambulishwa jioni hii

KLABU ya Chelsea imethibitisha  kumjeresha kikosi aliyekuwa kocha wao, Jose Mourinho kwa mkataba wa miaka minne akitokea klabu ya Real Madrid ya Hispania.
Kwa mujibu taarifa zilizotolewa na klabu hiyo jioni hii inasema kuwa wamemalizana na kocha huyo kutoka Ureno na kwamba Mourinho ataanza kazi wiki hii.
Klabu hiyo imemtambulisha rasmi kocha huyo na kukabidhiwa jezi ya klabu hiyo kuthibitisha kuwa sasa ni rasmi karejea nyumbani baada ya kuondoka kwa kuipa mafanikio makubwa ikiwamo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya England mara mbili na lile la Carling Cup mara mbili na Kombe la FA alipotua hapo kwa mara ya kwanza mwaka 2004 hadi 2007 alipoondoka kwenda Inter Milan kabla ya kuchukuliwa Real Madrid.
Hii itakuwa ni mara ya pili kwa Mourinho kuinoa Chelsea ambao wanashikilia taji la Ligi ndogo ya Ulaya baada ya kuinyoa Benfica katika pambano la Fainali lililofanyika Mei 15 mwaka huu, ikiwa ni miezi kadhaa tangu walipolitema taji la Ligi ya Ulaya walilotwaa mwaka jana kwa kuilaza Bayern Munich.

SITA WAPOTEZA MAISHA KTK AJALI MBEYA KADHAA WAJERUHIWA

 HIVI NDIVYO DALADALA HII ILIVYO HARIBIKA BAADA YA AJALI HIYO KUTOKEA 
 
 GARI LA ABIRIA AINA YA HIACE IKIWA IMEGONGANA USO KWA USO NA GARI AINA YA LAND CRUISER
HIZI NI BAADHI YA MAITI ZILIZO OKOLEWA PUNDE BAADA YA AJALI KUTOKEA  
MWILI WA DEREVA WA DALADALA ALIYE FARIKI PAPO HAPO UKIPELEKWA CHUMBA CHA KUHIFADHIA MAITI RUFAA
******************************

Watu sita wamefariki Dunia na wengine Sita kujeruhiwa katika ajali ya Barabarani iliyo tokea Nanenane Darajani eneo la Uyole Mbeya.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mbeya Barakael Masaki amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kuwataja marehemu hao kuwa ni pamoja na madereva wote wa magari hayo. 

Masaki amesema dereva wa Hiace amefahamika kwa jina la Meshack Hosea aliye kuwa anaendesha Gari nambali T178 AAV aina ya Toyota Hiace inayofanya kazi Sokomatola na Uyole ambapo muda huo ilikuwa ikitokea Sokomatola kuelekea uyole. Dereva wa pili aliyekuwa anaendesha Gari aina ya Toyota Land Cruiser iliyokuwa inatokea Uyole kwenda mjini yenye namba za usajili T 181 BHT iliyokuwa inaendeshwa na Dereva Abdalah Ndabagi .

Maiti nne hazijatambuliwa hadi sasa wakiwemo wanawake wanne waliokuwa abiria katika Daladala hiyo na miili yao imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa jijini Mbeya.

Aidha amesema majeruhi sita wamelazwa katika hospitali ya Rufaa wakiwemo wanawake watano na Mwanamke mmoja . Ambao mpaka sasa majina yao hayatambuliwa kutokana na kujeruhiwaa vibaya.

Chanzo cha ajali hiyo kimetajwa kuwa ni  mwendo kasi wa Magari hayo na wito ameutoa kwa Madereva kuwa makini na kufuata sheria za Barabarani ili kuepusha ajali ambazo zingeweza kutokea. Ikizingatiwa hilo ni eneo la Jiji.

Picha na Mbeya yetu Blog

JB, Irene Uwoya waja na Zawadi

Jacob Stephen 'JB'

MUIGIZAJI na mtayarishji hodari wa filamu nchini, Jacob Stephen 'JB' anatarajiwa kuibuka na filamu mpya iitwayo 'Zawadi Yangu'.

Filamu hiyo ambayo imekamilika hivi karibuni ikiwa kwenye foleni kabla ya kuachiwa mtaani ameicheza msanii huyo akiwashirikisha wakali wengine akiwamo mwanadada Irene Uwoya 'Mama Krish', Chuma Suleiman 'Bi Hindu' na Shamsa Ford.

JB anayefahamika pia kwa jina la 'Bonge la Bwana' alisema filamu hiyo ya kijamii inayoonyesha jinsi kinamama wanavyoweza kutawala sehemu kubwa ya ndoa za watoto zao na kudai ni moja ya kazi murua kutoka Jerusalem Films Production kwa namna simulizi lake lilivyo.

"Sijisifu, ila filamu hii mpya ya 'Zawadi Yangu' ni kati ya filamu ambazo nimeiandaa kwa umakini mkubwa na yenye ujumbe maridhawa kwa jamii," alisema JB.

Alisema filamu hiyo itatoka mapema mwezi huu akiwa tayari ameshaanza maandalizi ya 'kupika' kazi nyingine ambayo hata hivyo hakupenda kutaja jina kwa sasa akidai ni mapema mno.

JB aliyewahi kutamba na maigizo kupitia kituo cha ITV akiwa na makundi ya Mambo Hayo na Nyota Ensemble alisema kama ilivyo kwa 'Zawadi Yangu' hata kazi ijayo itakuwa kali na ikishirikisha nyota nchini.

Msondo Ngoma yajiandaa kuingioa studio kupakua albamu

 
Baadhi ya wanamuziki wa Msondo Ngoma 'Baba ya Muziki'
BENDI kongwe ya muziki wa dansi nchini, Msondo Ngoma inatarajiwa kuingia studio wiki chache zijazo kurekodi albamu ya kwanza tangu mwaka 2010.

Kwa muda mrefu mashabiki wa Msondo wamekuwa wakiililia albamu mpya tangu ilipotolewa 'Huna Shukrani' miaka mitatu iliyopita na kilio chao kimesikika kwa uongozi wa bendi kwa kuiingiza Msondo studio.

Mmoja wa watunzi wa bendi hiyo, Juma Katundu aliiambia MICHARAZO kuwa wataingia  studio Juni 12.

Katundu ambaye katika albamu hiyo ana wimbo uitwao 'Nadhiri ya Mapenzi', alisema kila kitu kimekaa vyema kwa ajili ya kuanza kazi hiyo ambayo imekuwa ikisubiriwa kwa hamu ya Wanamsondo kwa ujumla kuanzia wanamuziki hadi mashabiki wao.

"Tunatarajiwa kuingia studio Juni 12 kuanza kurekodi nyimbo za albamu yetu ambayo itakuwa na nyimbo sita, mmojawapo ikiwa ni utunzi wangu," alisema.

Alizitaja nyimbo nyingine zitakazorekidiwa kuwa ni 'Baba Kibene' na 'Lipi Jema' za Eddo Sanga, 'Kwa Mjomba Hakuna Mirathi' wa Huruka Uvuruge, 'Dawa ya Deni' na 'Suluhu' wa Shaaban Dede.

Msondo ilitoa albamu ya mwisho mwaka 2010 ambayo ni 'Huna Shukrani' baada ya kuzindua kwa kishindo mwaka mmoja uliotangulia albamu ya 'Kicheko kwa Jirani' iliyokuwa albamu ya kwanza tangu bendi hiyo iondokewe na nyota wake mkubwa, Tx Moshi William.

Vipimo halisi vya kifo cha Ngwair vyatoka



https://fbcdn-sphotos-e-a.akamaihd.net/hphotos-ak-ash3/p480x480/579293_526768957387103_1440212486_n.jpg
Albert Mangwea 'Ngwair' enzi za uhai wake

RIPOTI ya vipimo halisi vya kifo cha msanii wa Bongofleva, Albert Mangweha a.k.a Ngwair, imetolewa baada ya mwili wake kufanyiwa uchunguzi na madaktari wa hospitali ya St. Hellen Joseph mjini Johannesburg, Afrika Kusini.

Akizungumza na NIPASHE jana saa 9:50 jioni maeneo ya Mbezi Goig jijini Dar es Salaam ambako msiba wa msanii huyo upo, Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Radhia Msuya, ambaye alitembelea familia ya marehemu, alisema kuwa tayari madaktari wameshabaini chanzo cha kifo cha Ngwair na kwamba vipimo vitakabidhiwa kwa familia ya marehemu.

Msuya alisema kuwa ndugu wa marehemu ndiyo wenye mamlaka ya kuviweka wazi ama kutoiambia jamii kilichomo kwenye ripoti hiyo ya madaktari.

"Serikali imeshtushwa na kifo cha msanii huyu kwa sababu ni kijana. Tumepoteza mtu muhimu kwa sababu alikuwa balozi mzuri wa Tanzania anapokuwa nje ya nchi," alisema Msuya.

Alisema kuwa mwili wa marehemu umechelewa kuwasili nchini kwa sababu ya taratibu za vifo na mazishi nchini Afrika Kusini ambazo zinatofautina kwa kiasi kikubwa na taratibu za Tanzania.

"Mwili wa marehemu ungesafirishwa mapema lakini kilichochelewesha ni 'death certificate' (cheti cha kifo). Afrika Kusini mazishi hufanyika kwa siku za Jumamosi na Jumapili tu na sheria zao za vifo ni tofauti kabisa na za kwetu," alisema.

"Kinachoendelea kwa sasa ni 'booking' ya ndege. Kufikia kesho asubuhi zoezi hilo litakuwa limekamilika na mwili utawasili nchini kesho (leo) ama keshokutwa (kesho)," aliongeza balozi huyo.

Msuya alisema kuwa endapo mwili wa marehemu utasafirishwa kwa ndege ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini, utafika jijini Dar es Salaam leo saa moja jioni, lakini utafika kesho saa mbili asubuhi kama ukisafirishwa kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya.

Aidha, balozi huyo aliwapa pole ndugu, jamaa, marafiki na wasanii waliokuwa kwenye msiba wa marehemu kisha akazungumza na kamati ya mazishi inayoongozwa na Adam Juma.

Ngwair, aliyepata umaarufu mkubwa nchini kupitia tungo zake kali zikiwamo za 'Ghetto Langu' na 'Mikasi' alifariki Jumanne iliyopita nchini Afrika Kusini ambako alienda kwa ajili ya maonyesho ya muziki.

Mitandao ya kijamii na magazeti mbalimbali nchini (siyo NIPASHE) vilikurupuka kuchapisha ripoti 'feki' iliyozagaa kwenye internet ikidaiwa kuwa ndiyo chanzo cha kifo cha msanii huyo nyota ilhali hata vipimo vilikuwa havijafanyika.

Hadi kufikia jana hali ya msanii mwenzake Ngwair, M 2 The P ambaye naye amelazwa baada ya kuzidiwa pamoja na rapa huyo, ilikuwa ikiendelea vyema nchini Afrika Kusini.

Chanzo:NIPASHE