STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, March 16, 2013

Wanachama wasisitiza mkutano kesho palepale

Kaimu Mwenyekiti wa Simba, Joseph Itang'are 'Mzee Kinesi'


WAKATI uongozi ukiupinga mkutano wa wanachama uliopangwa kufanyika kesho ukidai sio halali, wanachama waliouandaa mkutano huo wamesisitiza kesho piga ua lazima wakutane kwani wala kila baraka za kufanyika kwake.
Mratibu wa mkutano huo wa dharura, Mohammed Wandi amesisitiza kuwa kauli za uongozi kuupinga uongozi huo ni kutaka kuwayumbisha wanachama kwani ukweli mkutano huo utafanyika kama ulivyopangwa na tayari wanachama mbalimbali toka ndani na nje ya Dar wameshawasili jijini.
Wandi alisema wamepata baraka zote za kufanyika kwa mkutano huo ikiwemo vibali toka Manispaa ya Ilala na Jeshi la Polisi na kwamba mkutano huo ni wa amani na utulivu na kushangaa uongozi wa Simba kupitia Kaimu Makamu Mwenyekiti, Joseph Itang'are 'Kinesi' kuukana.
"Mkutano upo kama kawaida kesho na wanachama wa Simba wajitokeze kwa wingi kwenye Hoteli ya Starlight, wasisikie propaganda kwa vile tumezingatia katiba," alisema Wandi.
Wandi alisema kuwa mkutano wao wameuitisha kwa kuzingatia katiba na hivyo hawaoni sababu ya uongozi kuwa na presha wakati wenyewe waliridhia ombi lao la kutaka mkutano kwa lengo la kuinusuru timu yao.
Alisema kabla ya kuamua kuitisha mkutano huo, Mzee Kinesi na Mwenyekiti wa Kamati ya ushindi Simba, Rahma Al Kharoos 'Malkia ya Nyuki' walikutana nao na kuwaeleza wamemaliza tofauti zao hasa baada ya kuamua kulifungua Tawi la Mpira Pesa lililokuwa limefungiwa na kuruhusu mkutano.
"Mkutano huu sio wa kufukuza viongozi, tutawasilisha hoja mezani na viongozi wakishindwa kuzijibu basi ndiyo itakuwa kwaheri yao," alisema.
Pia alisisitiza kuwa mkutano wao haukuitishwa na tawi lao la Mpira Pesa, bali umeitishwa na wanachama wa Simba na wamewaalika viongozi wahudhurie na kujibu maswali ya wanachama hao.

Arsenal yang'ara ugenini, Liverpool hoi EPL




WAKATI Arsenal ikitakata ugenini kwa kuilaza Swansea City mabao 2-0, Liverpool yenyewe imekiona cha moto baada ya kutandikwa mabao 3-1 na Southampton katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu ya England zilizomalizika hivi punde.
Arsenal ilipata ushindi huo kupitia magoli ya Nacho Monrel aliyefunga katika dakika ya 74 na jingine la Gervinho dakika za lala salama na kuipa ushindi muhimu vijana hao wa Arsene Wenger.
Katika mechi nyingine, 'vijogoo' vya England Liverpool wenyewe wamekiona chamoto kwa kunyukwa ugenini mabao 3-1 na Southampton na kuzidi kuwaweka pabaya mabingwa hao wa zamani wa Ulaya.
katika ligi hiyo msimu huu.
Wageni hao walishtukizwa kwa bao la mapema la dakika ya 6 lililofungwa na Morgan Schneiderlin na jingine la dakika ya 33 kupitia kwa Rickie Lambert. kabla ya Phillippe Coutinho kuifungia Liverpool bao dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza na kufanya hadi mapumziko matokeo yawe 2-1.
Bao la dakika 80 lililofungwa na Jay Rodriguez liliikatisha tamaa Liverpool ambayo imeswaliwa na pointi zake 45 ikishika nafasi ya saba.
Nayo Aston Villa ikiwa nyumbani ilipata ushindi wa mabao 3-2 QPR, huku timu za West Ham na Stoke City zilishindwa kutambiana katika pambano jingine lililochezwa jioni hii, huku vinara Manchester United inatarajiwa kuikaribisha Reading katika mechi ya kufungia dimba kwa leo katika ligi hiyo ya England.
Kesho kutakuwa na kivumbi cha mechi nne ambapo Tottenham Hotspurs itakuwa nyumbani Kaskazini mwa London kuikaribisha Fulham, huku Chelsea watakuwa pia nyumbani kuilika West Ham, huku Sunderland     itakwaruzana na Norwich City na Wigan Athletic itakuwa dimba la nyumbani kuumana na Newcastle United.

Yanga yazidi kujichimbia kileleni, Toto yazinduka

Beki wa Yanga, Nadir Haroub 'Cannavaro' akihamisha mpira langoni mwake jioni ya leo

BAO la dakika za mwanzoni mwa kipindi cha pili lililofungwa na Hamis Kiiza 'Diego' limeweza kuipa Yanga ushindi muhimu jioni hii katikia mbio zake za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuwalaza maafande wa Ruvu Shooting kwa bao 1-0.
Ushindi huo uliopatikana katika pambano lililokuwa kali lililochezwa kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam umeifanya Yanga kufikisha pointi 48 na kuzidi kuziacha mbali timu zinazoifukuza katika msimamo wa ligi hiyo iliyosaliwa na mechi sita kwa kabla ya kumaliza msimu.
Vinara hao wameshashua dimbani mara 20 na kusaliwa mechi sita, huku Ruvu Shooting Stars imesaliwa na 
pointi 29 ikishuka uwanjani mara 19.
Matokeo mengine ya mechi zilizochezwa leo katika viwanja vya CCM Kirumba, Mwanza Toto African ilzinduka baada ya kuilaza Mgambo JKT kwa mabao 2-1 na pambano kati ya Mtibwa Sugar iliyoikaribisha Coastal Union ya Tanga liliisha kwa sare ya bao 1-1 wenyeji wakilazimisha kusawazisha bao kupitia Vincent Barnabas.

Man City yaweka rehani taji lake, Everton yaichinja




MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya England, Manchester City jioni hii imejikuta ikiuweka rehani taji lake baada ya kunyukwa mabao 2-0 na Everton.
Everton waliokuwa kwenye Uwanja wao wa nyumbani wa Goodson Park jijini Liverpool, wamefanikiwa kupata ushindi huo licha ya kumaliza mchezo ikiwa pungufu kwa zaidi ya dakika 25,
Nyota wao, Steven Pienaar alitolewa kwa nyekundu baada ya kuonyesha kadi ya pili ya njano katika mchezo huo ulioshuhudia hadi mapumziko wenyeji wakiwa mbele kwa bao 1-0.
Bao hilo lililokuwa la kiufundi liliwekwa kimiani na Osman kwa shuti kali la umbali wa mita 30 kwenye dakika ya 32.
Kipindi cha pili Everton iliingia na moto kabla ya Pienaar kutolewa nje ya uwanja na ilikuja kujipatia bao la pili dakika za lala salama kupitia Jelavic.

Kwa kipigo hicho, City wameipa nafasi Man Utd kuongeza pengo la kileleni hadi kufikia 15 huku zikiwa zimebaki mechi nane kumaliza msimu.

Uongozi Simba waupinga mkutano wa wanachama kesho, kisa...!

Msemaji wa klabu ya Simba, Ezekiel Kamwaga


UONGOZI wa klabu ya soka ya Simba umesema kwamba Mkutano Mkuu wa Wanachama wa Simba uliopangwa kufanyika Kesho katika ukumbi wa Star Light Hotel mjini Dar es Salaam kujadili mustakabali wa klabu ni batili.
Taarifa ya Ofisa Habari wa Simba SC, Ezekiel Kamwaga imesema kwamba ikumbukwe kwamba Mkutano Mkuu wa Wanachama ndiyo chombo cha juu kabisa cha maamuzi kwa klabu yetu. 
Katiba ya Simba SC imeupa Mkutano Mkuu hadhi ya juu mno na ndiyo maana imeweka utaratibu wa kufanyika kwake.
Taarifa hiyo imesema miongoni mwa utaratibu ni kwamba ni lazima uitishwe na Mwenyekiti aliye madarakani wa klabu. Kwa kushirikiana na Kamati ya Utendaji, ndiye atakayepanga ajenda, mahali na wakati wa kufanyika kwa mkutano wenyewe. 
Imeongeza kuwa katika miaka ya nyuma, zilikuwepo nyakati ambapo klabu ilikaa hadi miaka mitatu pasipo kuitishwa kwa Mkutano Mkuu wowote wa wanachama.   
Imesistiza hakuna mwanachama au kikundi chochote kilichojitokeza kudai mkutano wa dharura wakati huo ingawa ilikuwa ikifahamika kwamba huo ulikuwa ni ukiukwaji mkubwa wa katiba ya klabu.
Imesema tangu uongozi huu uingie madarakani takribani miaka mitatu iliyopita, mikutano mikuu miwili ya wanachama imefanyika kwa mujibu wa KATIBA na kwamba Mungu akijaalia, uongozi huu utafanya mkutano mwingine wa kawaida wa wanachama baadaye mwaka huu.
Hata hivyo, taarifa hiyo imesema kwa kuzingatia hali halisi ya klabu, Mwenyekiti wa Simba, Alhaji Ismail Aden Rage (Mb), mwezi uliopita alitangaza dhamira yake ya kuitisha Mkutano Mkuu wa Dharura wakati wowote kuanzia sasa.  
Taarifa imesema Rage alisema mkutano huo ungekuwa na ajenda moja tu; Kujadili Mwenendo wa Klabu kwenye mashindano inayoshiriki msimu huu. Imeendelea kusema kwamba kwa bahati mbaya, Mwenyekiti alishikwa na maradhi na akapelekwa India kwa matibabu na yuko huko hadi Mola atakapomjalia afya njema na kurejea. Kuna uwezekano mkubwa, Inshallah, akarejea mwishoni mwa wiki ijayo.
“Hii maana yake ni kwamba uongozi umeridhia kufanyika kwa Mkutano wa wanachama. Kimsingi, kama uongozi umeridhia, hakuna mwanachama mwingine anayeweza kuitisha mkutano mkuu mwingine,”.
 “Mwenyekiti ameruhusiwa kuitisha Mkutano Mkuu kwa sababu alichaguliwa na wanachama na hivyo ana nguvu ya kisheria (locus standi) kufanya hivyo. Hawa wengine wanaoitisha mkutano wana nguvu gani ya kisheria kufanya hivyo? Walichaguliwa na nani kuwakilisha wanachama? Lini na wapi?”  
“Uongozi pia unaweza kuitisha mkutano kwa vile wenyewe ndiyo wenye leja ya wanachama. Klabu sasa ina database yake ya kompyuta inayotambua wanachama walio hai na wasio hai,”. 
“Kwa kutumia database hiyo, uongozi huu unatambua wanachama walio hai na wasio hai. Hakuna mtu mwingine yeyote, aliye nje ya uongozi huu anayefahamu wanachama walio hai na wasio hai. Hao wanachama wanaoitana kufanya mkutano, wamehakikiwa na nani kubaini uhalali wao huo?” “Uongozi wa Simba SC unaona kwamba wanaolazimisha kufanyika kwa Mkutano Mkuu wana ajenda binafsi na si za maslahi ya klabu. Kama kweli wangekuwa na nia njema na klabu wangesubiri mkutano ambao utaitishwa punde,”. “Kwani, kuna uharaka gani wa kufanyika mkutano kesho? Kwanini hawataki Mwenyekiti, ambaye wanachama walimpa mamlaka ya kuongoza klabu kwa kipindi cha miaka minne, awepo kwenye mkutano huo?”
“Kwanini hawataki kuungana na wana Simba wengine kumwombea Mwenyekiti kwa Mungu ili amwepushe na ugonjwa na kumrejesha salama hapa nyumbani? Kwanini mikutano hii iitishwe katika kipindi ambacho uongozi umefungua mikono yake na kukaribisha kila mmoja mwenye mapenzi mema na klabu kuja kuchangia?”
“Kwenye macho ya Katiba ya Simba na sheria za Tanzania, huu mkutano wa kesho ni batili na una lengo la kuleta vurugu na mifarakano kwenye jamii na michezo kwa ujumla wake. Michezo ni amani na furaha na michezo si vurugu,”. “Tayari uongozi wa Simba umetoa taarifa kwa Jeshi la Polisi na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuhusiana na ubatili wa mkutano huo. Tunapenda kuwaomba wanachama wetu wasiopenda fujo na vurugu kwenye michezo kukaa mbali na mkutano huo kwa vile vyombo vya dola vitaufuatilia,”.  
“Uongozi hautajiingiza katika kutoa dhamana au msaada wa namna yoyote kwa yeyote ambaye atachukuliwa hatua na vyombo vya dola kutokana na kujihusisha na mkutano huo,”. “Pia, Simba SC inatoa wito kwa vyombo vya habari kuwa makini wakati vinaporipoti matukio ya vurugu kwenye michezo. Kabla mtu hajahojiwa kujieleza kama mwanachama wa Simba, ni vema kwanza akaonyesha kadi yake ya uanachama na risiti za malipo yake,”.
“Wakati mwingine, waandishi huwa tunawapa nafasi kwenye vyombo vyetu vya habari watu ambao hawana mchango wowote kwenye kukuza michezo bali kuleta vurugu. Kwanini, tungejiuliza, ni watu wale wale ambao kila mwaka huonekana wakati wa vurugu na wakati wa amani huwa hawaonekani?”
“Kwanini, vyombo vyetu vinatoa nafasi kwa watu ambao lengo lao ni kuhakikisha vilabu vyetu vinazidi kubaki nyuma, vinakuwa na vurugu kila wakati na michezo inaonekana kama ni sehemu ya wahuni na watu wasio na utaratibu?” “Mpira bado haujaleta tija kubwa kwenye uchumi wa Tanzania na kunufaisha wachezaji kwa sababu baadhi ya watu makini na makampuni makubwa yanaogopa kujiingiza kwenye michezo kwa sababu ya tabia kama hizi,”.
“Ni vema vyombo vya habari vikafanya jitihada kubwa katika kuwatambua waleta vurugu, si katika klabu ya Simba pekee, bali kwenye sekta ya michezo kwa ujumla, ili visiwape nafasi ya kuharibu na badala yake vitoe nafasi kwa wale wenye lengo la kujenga,”.  
“Tunasisitiza, uongozi huu utaitisha Mkutano Mkuu wa Wanachama Wote mara baada ya kurejea kwa Mwenyekiti,”.

Semina ya Copa Coca Cola yapigwa 'dochi'



Na Boniface Wambura 
SEMINA elekezi kwa ajili ya michuano ya Copa Coca-Cola 2013 iliyokuwa ifanyike Jumanne (Machi 19 mwaka huu) jijini Dar es Salaam sasa imesogezwa mbele hadi Machi 26 mwaka huu.

Uamuzi wa kusogeza mbele semina hiyo umetokana na maombi ya wadhamini, Coca-Cola ambao katika tarehe ya awali watakuwa na shughuli nyingine za kampuni hiyo.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linawaomba radhi wajumbe kwa usumbufu wowote utakaokuwa umejitokeza kutokana na semina hiyo kusogezwa mbele.

Hivyo, washiriki wa semina hiyo wanatakiwa kuripoti Dar es Salaam (TFF) siku moja kabla (Machi 25 mwaka huu).

Washiriki hao ni makatibu wa vyama vya mpira wa miguu vya mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar. Pia waratibu wa mikoa wa mashindano ya Umoja wa Michezo wa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA).

Barua za mwaliko kwa ajili ya semina hiyo tayari zimetumwa kwa vyama vya mpira wa miguu vya mikoa.

Yanga bila Yondani kuivaa Ruvu Shooting leo

Wachezaji wa Yanga wataendelea kushangilia mabao leo kwa Ruvu kama hivi?

VINARA wa Ligi Kuu nchini Yanga chini ya Kocha wake, Ernst Brandts wanatarajiwa kushuka dimbani jioni ya leo kuvaana na Ruvu Shooting, bila beki wake mahiri wa kati, Kelvin Yondani.
 Hata hivyo Brandts amesema licha ya kumkosa beki huyo, bado anaamini Yanga itaibuka na ushindi katika mechi hiyo itakayochezwa kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam. Yanga wanaongoza msimamo wa ligi hiyo wakiwa na pointi 45 baada ya mechi 19 wakifuatwa na mabingwa wa Kombe la Mapinduzi, Azam (37) na mabingwa watetezi wa Simba walio katika nafasi ya tatu (34).
Akizungumza jana baada ya kumalizika kwa mazoezi ya timu yake kwenye uwanja wa Bora wa Kijitonyama, jijini Dar es Salaam jana, Brandts alisema atawatumia mabeki waliopo kuziba pengo la beki huyo tegemeo kwa Yanga na timu ya taifa, 'Taifa Stars'.
Hata hivyo, ni wazi kwamba safu ya ulinzi ya Yanga haipo vizuri kwa sasa kutokana na kukosekana kwa mabeki watatu.
Ladislaus Mbogo ni mgonjwa baada ya kufanyiwa upasuaji wa uvimbe shavuni, Yondani anasumbuliwa na tatizo la uvimbe wa kidole gumba cha mguu na Stephano Mwasika ana maumivu ya misuli ya mguu.
“Naamini tutacheza vizuri licha ya kuwakosa mabeki wetu hao kwa sababu wachezaji wengine wako safi kiafya, kiakili na wana morali ya hali ya juu katika kuhakikisha timu inapata ushindi katika mechi ya Jumamosi (leo),” alisema Brandts.
Ruvu Shooting inayonolewa na Boniface Mkwasa inakamata nafasi ya saba katika msimamo wa ligi hiyo baada ya kucheza mechi 18, na imekuwa na historia ya kuikamia Yanga katika mechi baina yao.
Katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo, Yanga waliokuwa nyuma kwa magoli mawili hadi mapumziko, walizinduka na kuibuka na ushindi wa 3-2 katika kipindi cha pili.
Tangu kuanza kwa mzunguko wa pili wa ligi kuu Januari 26, Yanga ambao ni mabingwa wa soka Afrika Mashariki na Kati, wameshacheza mechi sita wakishinda tano na kutoka sare moja.
Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa Sh. 5,000, Sh. 8,000, Sh. 15,000 na Sh. 20,000, kwa mujibu wa taarifa ya shirikisho la soka (TFF).