STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, June 2, 2013

Makocha Ilala wainyuka Kinyerezi Veterani


TIMU ya makocha wa soka wilayani Ilala, Ilala Coaches Fc, imeinyuka Kinyerezi Veterani kwa bao 1-0 katika mfululizo wa mechi zao za kila mwezi, mchezo uliochezwa uwanja wa Shule ya Sekondari Benjamini Mkapa, Ilala Dar es Salaam.
Bao pekee la makocha hao, lilitumbukizwa kimiani na Hashim Gadiola na kuendeleza ubabe wa kikosi chao kinachojumuisha makocha mbalimbali wa Ilala.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Chama cha Makocha Ilala, TAFCA-Ilala, Hugho Sseseme Makocha Ilala walionyesha uwezo wa hali ya juu licha ya wapinzani wao kuonyesha upinzani na kusababisha ushindi katika mechi hiyo ya leo kuwa kiduchu.

Taifa Stars, Sudan zashindwa kutambiana Ethiopia


TIMU ya soka ya taifa, Taifa Stars jioni hii imetoshana nguvu na Sudan katika pambano la kimataifa la kirafiki lililochezwa mjini Addis Ababa, nchini Ethiopia ilipoweka kambi yake ya kujiandaa na michuano ya kufuzu Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika nchini Brazili.
Kwa mujibu wa Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Boniface Wambura Stars ilionyesha uwezo mkubwa licha ya kuchezesha vijana katika pambano hilo kwa nia ya kuwapa uzoefu zaidi katika kikosi hicho ambacho kwa sasa wapo kwenye hafla nyumbani kwa Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia.
Kikosi hicho kitaondoka kesho nchini Ethiopia kwa ajili ya kuanza safari ya kwenda Morocco kwa kupitia Misri ili kukwaruzana na wenyeji wao katika pambano la marudiano la kundi C kwa nia ya kuwania kucheza fainali hizo za Brazili.
Katika mechi ya kwanza  Stars iliinyuka Morocco mabao 3-1 na ushindi huo iliifanya Stars kuendelea kusalia nafasi ya pili ikijikusanyia pointi 6, moja nyuma ya Ivory Coast yenye pointi saba ambayo nayo wikiendi ijayo itakuwa dimbani klupambana na Gambia.

Abajalo yang'oka RCL, yalala 1-0 Ilulu

TIMU ya soka ya Abajalo imeng'olewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) baada ya kulazwa bao 1-0 na Kariakoo Lindi katrika mechi ya marudiano lililochezwa uwanja wa Ilulu.
Katika pambano lililochezwa wiki iliyopita timu hizo zilishindwa kutambiana baada ya kufungana mabao 2-2 na hivyo,  Abajalo iomeng'olewa kwenye hatua hiyo ya pili kwa jumla ya mabao 3-2.

Borussia Dortmund yamtolea macho Podolski

http://img.thesun.co.uk/multimedia/archive/01595/PODOLSKI_1595719a.jpg
Lucas Podolski



KLABU ya Arsenal inakabiliwa na changamoto kubwa ya kumbakisha mshambuliaji wake nyota Lucas Podolski, baada ya mchezaji huyo aliyesaidia timu yake kupata ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Ecuador kunyemelewa na wana fainali za Ligi ya Mabingwa Ulaya, Borussia Dortmund.
Podolski, aliyewahi kuripotiwa na gazeti la The Sun mwezi Aprili kuhitajiwa na Atletico Madrid, alitua Emirates mwaka jana kwa kitita cha Pauni Mil. 11, lakini kwa sasa atupiwa macho na Dortmund iwap[o Arsenal inaridhia kumuachia.
Klabu hiyo ya Ujerumani imepata jeuri ya kumtaka Podolski aliyesajiliwa na Arsenal akitokea timu nyingine ya Bundesliga ya Cologne kutokana na kuvuna mamilioni ya fedha kwa kumuuza Mario Gotze kwa kitita cha Pauni Mil. 31.5 na nyota wake mwingine Robert Lewandowski akiwa njiani kumfuata mwenzake kwa mabingwa hao walioweka rekodi msimu huu kutwaa taji la Ligi ya Ulaya, Bundesliga na Kombe la Ujerumani.
Hata hivyo Dortmund itabidi ifanye kazi ya ziada kumshawishi Arsene Wenger kumtoa mchezaji huyo wakati akiwa ameaminiwa na mabosi wake kuendelea kukisuka upya kikosi hicho ili angalau kufuta 'ukame' wa mataji katika klabu hiyo uliodumu kwa miaka kadhaa sasa.
Mshambuliaji huyo mwenye asili ya Poland na aliyeichezea timu ya taifa ya Ujerumani mara 109 na kuifungia mabao 46, tangu alipotua Arsena; ameichezea mechi 33 za Ligi na kuifungia mabao 11 na amekuwa akinukuliwa akifurahia maisha Emirates.

Stars kujipima nguvu na Sudan kabla ya kesho kwenda Morocco


KIKOSI cha timu ya taifa, Taifa Stars kilichopo kambini mjini Addis Ababa, Ethiopia kujiandaa na mechi ya kuwania tiketi ya Kombe la Dunia dhidi ya Morocco Juni 8, leo itacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Sudan.
Stars chini ya Kocha wake, Kim Poulsen, iliyopiga kambi katika Hoteli ya Hilton kujiandaa na mechi hiyo, ipo nafasi ya pili kwenye kundi la C; nyuma ya Ivory Coast yenye pointi saba.
Kwa mujibu wa Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura aliyehojiwa na kituo kimoja cha redio nchini alisema kuwa pambano hilo litatumiwa na kocha Poulsen kukiangalia kikosi chake kabla ya kesho kuondoka kueleka Morocco.
Wambura alisema mara baada ya mechi hiyo wachezaji na viongozi wa Stars watakwenda Ubalozi wa Tanzania nchini humo walikoalikwa na Balozi Joram Biswaro, ambapo watapata fursa ya kukutana na baadhi ya Watanzania wengine waishio nchini huo kwa ajili ya kuwaaga.
Kikosi cha nyota 22 kitaondoka Ethiopia alfajiri ya kesho kwenda Marrakech, Morocco kupitia Cairo, Misri ambao ni Juma Kaseja, Aggrey Morris, Mwadini Ally, Ally Mustafa, Shomari Kapombe, Kevin Yondani, Erasto Nyoni, Haroub Nadir, Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Khamis Mchana, Amri Kiemba, Salum Abubakar, Simon Msuva, John Bocco, Vincent Barnabas, Mudathiri Yahya, Athuman Idd, Haruni Chanongo na Zahoro Pazi.


Ruvu Shooting waanza kuimarisha kikosi chake

Kikosi cha Ruvu Shooting Stars

KLABU ya soka ya Ruvu Shooting ya Pwani imemsajili mchezaji Cosmas Ader Lewis kwa mkataba wa miaka miwili wa kuitumikia klabu hiyo katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
Cosmas aliyeichezea kwa mkopo African Lyon msimu uliopita akitokea Azam, alisaini mkataba huo mwishoni mwa wiki kwenye ofisi za klabu hiyo ya jeshi zilizopo Kikosi cha Jeshi 832 Ruvu JKT Mlandizi, Kibaha-Pwani.
Mchezaji huyo alikuwa na mkataba wa mwaka mmoja na klabu ya Azam ambao umeisha na kuifanya Ruvu kufanikiwa kumnyakua na kuzizidi kete timu nyingine zilizokuwa zikimnyemelea ikiwamo Simba.
Msemaji wa timu hiyo Masau Bwire aliiambia MICHARAZO kuwa usajili wa mchezaji huyo ambaye ni mshambuliaji kinda aliyezaliwa Novemba 1995, una lengo la kuifanya Ruvu Shooting ifanye vyema kwa msimu ujao baada ya msimu uliosha hivi karibuni kushindwa kutimiza malengo yao ya kumaliza kwenye 5 Bora.
Bwire alisema kunyakuliwa kwa mchezaji huyoa ni mwanzo wa timu yao kujiimarisha kwa msimu ujao ambao huenda ukaanzxa kati ya Agosti na Septemba mwaka huu.
"Tunaamini kutua kwa Lewis Ruvu Shooting kutakuwa na tija na ufanisi mkubwa kwa msimu ujao kwani ni mmoja wa wachezaji mahiri na ndiyo maana tumeamua kumnyakua, "alisema Bwire.
Bwire alisema usajili wao kwa kikosi cha msimu ujao ufanywa kwa umakini mkubwa ili kuondoa dhana kwamba timu za majeshi ni wasindikizaji tu katika Ligi Kuu Tanzania Bara, ambayo kwa sasa bingwa wake ni Yanga ambao walinyakua nafasi ya kwanza na kufuatiwa na Azam kisha Simba.

Simba, Yanga kutoshiriki Kagame, kisa....!

 
Simba

Mabingwa watetezi wa Kagame, Yanga
VIONGOZI wa klabu ya soka ya Simba na Yanga wanatarajiwa kukutana haraka iwezekanavyo kwa nia ya kutoa msimamo wao juu ya kwenda Sudan kushiriki michuano ya Kombe la Kagame ambayo inatarajiwa kuanza katikati ya mwezi huu.
Michuano hiyo ilitangazwa na Baraza la Vyama vya soka Afrika Mashariki na Kati - CECAFA kuwa ingefanyika mjini Darfur -Sudan, lakini serikali ya Tanzania imetoa tamko kuhusu timu za Simba na Yanga kwenda kushiriki michuano hiyo huko Sudan kwenye eneo ambalo limekuwa likiandamwa na vurugu kwa miaka kadhaa sasa.
 Kwa mujibu wa msemaji wa klabu ya Simba Ezekiel Kamwaga ni kwamba serikali haidhani ni busara kwa vilabu vya Simba na Yanga kwenda kwenye eneo hilo kushiriki Kagame Cup kutokana hali mbaya ya usalama iliyopo Darfur.
Kamwaga aliadnika hivi katika ukurusa wake wa Facebook;
Breaking News...... Serikali imesema haioni busara ya Kagame Cup kupigwa Darfur.... Hakuna hoteli ya maana na watu wanashauriwa kutembea na fulana zinazozuia risasi kupenya... Nadhani hii ndiyo stori kubwa ya kimichezo kwa leo.... Je, mnadhani itakuwa busara kwa Simba na Yanga kushiriki?
Hata hivyo taarifa zilizopatikana mchana huu ni kwamba viongozi wa Simba na Yanga kwa nafasi zao wanatarajiwa kukutana kujadili tamko hilo na kutoa msimamo wao kama wataenda Sudan au la, kwa hofu ya machafuko yanayoendelea huko.
Kagame ili[elekwa huko kwa nia ya kuhamasisha amani katika mji huo, lakini hali haionyeshi matumaini na wadau wengi wanadhani si busara timu za Tanzania kwenda kwa kuhofia kutokea maafa ywa wachezaji wa timu hizo. TUSUBIRI Tuone

Dorice Mollel ndiye Miss Tabata 2013

Miss Tabata Dorice akipozi na Mshindi wa pili Upendo Lema (kulia) na mshindi wa tatu Recho Mushi (kushoto).
MWANAFUNZI wa mwaka wa pili katika chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Dorice Mollel (22) usiku wa kuamkia jana alishinda taji la Miss Tabata kwenye shindano lililofanyika katika ukumbi wa Dar West Park, Tabata.
Dorice aliwabwaga  warembo wengine 14 kumrithi Noela Michael aliyekuwa anashikilia taji hilo. Noela ndiye anayeshikilia taji la Miss Ilala kwa sasa.
Mshindi huyo alizawadiwa Sh 600,000 na king’amuzi kutoka Multichoice pamoja na warembo waliyoshika tano za juu watawakilisha Tabata katika shindano la Miss Ilala baadaye mwaka huu.
Warembo hao ni Upendo Lema (22) aliyezawadiwa sh 400,000 baada ya kushika nafasi ya pili na Recho Mushi (20) alipata Sh 300,000 baada ya kushika nafasi ya tatu.  Wengine ni Kazunde Kitereja (19) alishinda nafasi ya nne na kuzawadiwa Sh 200,000 na Kabula Juma Kibogoti (20) alipataSh 150, 000 kwa kushika nafasi ya tano.
Warembo wengine waliyoingia kumi bora kila moja alipata shilingi laki moja. Nao ni Madgalena Bhoke (21), Eunice Nkoha (19), Rehema Kihinja (20), Brath Chambia (23) na Joaniter Kabunga (21). Warembo waliyosalia walipata kifuta The rest got consolation prize of Sh 50,000 each.
Miss Tabata iliandaliwa na Bob Entertainments na Keen Arts chini ya udhamini wa Dodoma Wine, Redd’s Original, Nipashe, Vayle Springs, Multichoice, Fredito Entertainment, Integrated Communications Limited, CXC Africa, Brake Point na Saluti5.

Mwili wa Ngwair wakwama tena, sasa kutua Jumanne

https://fbcdn-sphotos-e-a.akamaihd.net/hphotos-ak-ash3/p480x480/579293_526768957387103_1440212486_n.jpg
Ngwair

MWILI wa aliyekuwa nyota wa muziki wa Hip hop nchini, Albert Mangwea 'Ngwair' uliokuwa uwasili nchini huu umeshindikana na sasa utawasili nchini Jumanne ukitokea Afrika Kusini ambapo ndipo msanii huyo alipopatwa na mauti.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Mazishi ya msiba wa msanii huyo, umewaomba radhi Watanzania ambao wamekuwa na shauku ya kuupokea mwili wa kipenzi chao huyo, aliyekuwa ametangazwa awali angetua jana mchana kabla ya kubadilishwa na kuelezwa ungetua leo saa 8 mchana.
Taarifa rasmi ya kamati hiyo inasomeka hapo chini, ingawa taarifa zaidi kutoka Afrika Kusini zinasema kuwa mwili wa Ngwair utawasili nchini Jumanne mchana na kuagwa siku inayofuata kabla ya kwenda kuzikwa Morogoro Alhamisi.
Kwa mujibu wa ujumbe wa mtangazaji wa Clouds Millard Ayo aliyepo Johannesburg, Afrika Kusini aliotwitte kwenye akaunti yake ni kwamba mwili wa Ngwair utawasilia Jumanne mchana.

                  TAARIFA YA KAMATI NDIYO HII HAPA:
Kamati ya msiba tunaomba kutoa ya taarifa kwamba mwili wa Ndugu yetu Albert Mangwea hautoweza kufika siku ya jumapili ya tarehe 2/06/2013 kama ilivyo taarifa hapo awali, hii ni kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wetu.Kwa sasa tunasubiri taarifa kamili kutoka kwa wenzetu/wawakilishi wetu waliopo nchini Afrika Kusini, mara tutakapopata taarifa hizo tutawafahamisha zaidi.Tunaomba radhi watanzania wote kwa usumbufu wote uliojitokeza tushirikiane na uvumilivu kwa hili.
Asante
Mwenyekiti wa Kamati
Kenneth Mangweha
…………………………………
Msemaji wa Kamati
Adam Juma
……………………….

Mwanamke aishi kama mkimbizi baada ya kunusurika kuchinjwa


Mary Mbosa aliyenusurukia kuchinjwa na mtalaka wake na kulzaimika kuishi porini kama mkimbizi.

Na Gustav Chahe, Iringa



MAMA mmoja mkazi wa Itunundu – Pawaga katika Mkoa wa Iringa Mery Mbosa anaishi kama digidigi baada ya kunusurika mara kadhaa kuchinjwa na mtalaka wake na kulazimika kuhama kijiji kwa ajili ya kunusuru maisha.



Akiongea na mtandao huu jana, Bi Mbosa alisema maisha yake yapo hatarini kutokana na kuvamiwa na mtalaka wake mara kadhaa akiwa nyumbani na kumuumiza.



Alisema alilazimika kutalakiana baada ya mwanamume huyo kuwa mkorofi kiasi cha kupigwa, kutokuwa huru kutumia mazao ambayo walilima wote na hata kutokuwa huru kuongea na watu hata kama ni ndugu zake kwa madai kuwa ni wivu wa kimapenzi.



Alisema mtalaka wake amegeuka kuwa mnyama na kufika nyumbani kwake usiku wa manane na pindi anapokuta mlango umefungwa huanza kurusha mawe madirishani huku akitaka kuvunja mlango ili kuingia kumdhuru.



Amemtaja mtalaka wake kuwa ni Phabiani Msilamgunda ambaye miezi ya hivi karibuni alikutana na ye njiani akielekea shambani akamvamia akiwa na kisu kwa kutaka kumchinja na kuokolewa na watu ambao walikuwa jirani.



“Ilikuwa 23 Machi mwaka huu nilikuwa nikielekea shambani nikakutana na mtalaka wangu akiwa na kisu mkononi akanivamia huku akisema nakuchinja laeo lakini kwa bahati nzuri kulikuwa na watu jirani wakaniokoa vinginevyo ningekuwa marehemu.



“Lakini hata hivyo amekuwa akimtukana hata mama yangu mzazi (mama mkwe) akitaka kupiga pia na kila wakati nimekuwa nikishtaki hadi ofisi zinanichoka pamoja na kuwa ninapokelewa na akiitwa haendi kwa sababu amekuwa mbabe” alisema bi Mbosa.



Hata hivyo Mbosa alisema kuwa aliwahi kupigwa na kuumizwa vibaya na kulazimika kushtaki mahakamani japo kuwa hukumu ilivyotolewa haikuwa ya haki na kuhatarisha zaidi maisha yake.



“Nilipigwa na kuumizwa vibaya kesi ikapelekwa mahakamani lakini hukumu ilivyotolewa haikuwa ya haki kwangu na baada ya hukumu maisha yangu yamekuwa ni ya hatari zaidi” alisema.



Kwa mujibu wa maelezo ya wananchi wa kijiji hicho ambao wameeleza kushuhudia mama huyo akinusurika kuuawa na jinsi maisha yake yanavyozidi kuwa mabaya, walisema kiburi cha Msilamgunda kinatokana na dada yake ambaye ni diwani wa viti maalum (CCM).



Gazeti hili limebaini kesi ambayo mama huyo hajaridhika na hukumu ni Jinai No. 22/2013, mshitakiwa Phabiani Msilamgunda ambayo ilitolewa hukumu Mei 21 Mwaka huu.



Imeelezwa kuwa katika utoaji huku hiyo hakimu aliyetajwa kwa jina moja la Masuwe alimtaka mtuhumiwa alipoe faini ya shilingi laki mbili pamoja na gharama ya kesi shilingi 45 elfu jambo ambalo lilifanyika hivyo na mtuhuhumiwa kuwa huru kwa vitisho kuwa lazima ammalize mwanamke huyo.



Pamoja na kutokuridhika na hukumu iliyotolewa, Mkuu wa kituo cha Polisi cha Pawaga Fedrick Nyavilwe anatuhumiwa kumdhurumu mama huyo na kuiomba serikali kumsaidia ili aishi kama wanavyoishi wananchi wengine.



Nyavilwe anatuhumiwa kumdhurumu mwanamke huyo mbegu ya mpunga na kumfanya kuwa mtumwa kwa kukosa chakula bila kujua hatima ya maisha yake.



“Baada ya hukumu nilikwenda shambani nilikokuwa ninaanda mbegu ya mpunga kwa ajili ya kupanda nikakuta watu wananing’oa, nilipouliza walisema wametumwa na Mkuu wa kituo cha polisi. Hivi sasa naishi kama ndege jamani sijui nitakula nini kwa sababu hata mashamba niliyokuwa nalima nilinyang’anywa na mbegu niliyokuwa nimeandaa kwa ajili ya kupanda polisi wameninyang’anya” alisema.



Alipotafutwa kwa njia ya simu kwa ajili ya kutolea maelezo, Veronica Msilamgunda ambaye ni ndugu na Phabian Msilamgunda alisema hawezi kuzungumza chochote kwa kuwa yupo kwenye mkutano.



Kwa upande wake mwenyekiti wa kijiji hicho Joseph Malinga alipotafutwa kwa ajili ya ufafanuzi Alikiri kuwa mama huyo ni mhanga mkubwa na anaishi kama mkimbizi kwa hofu ya kuuawa.



“Nalijua sana hilo na ninashukuru kwa kuwa umenitafuta ili nikueleze. Maisha ya huyo mama hatuji yataishia wapi kwa sababu hali ilivyo kwa sasa ni ngumu na anaishi kama mkimbizi.




“Hata akiwa sehemu yenye ulinzi anaona kama hakuna ulinzi kwa sababu ya kile anchofanyiwa. Kiujumla hata sisi viongozi wa kijiji tunaishi kwa mashaka kwa sababu tunatishiwa kuuawa tunapotaka kutafutas suluhu ya huyo mama. Huyu mwanaume tunashindwea kuelewa kama ni mtu wa kawaida maana amegeuka kuwa kamas samba” alismea Malinga.



Hata hivyo alisema anaomba kwa watu wanaoweza kumsaidia mama huyo kupata hifadhi ili aondokane na maisha ya kuishi kama digidigi kule kijijini.