STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, December 5, 2014

TFF yaionya Simba usajili wa Sserunkuma kwa Kiongera

Kiongera aliyetajwa kuachwa kinyemela

http://www.standardmedia.co.ke/images/wednesday/ssekum56768.jpg
Dan Sserunkuma
BAADA ya kumuondoa kiutata kikosini mshambuliaji Mkenya Paul Kiongera, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limeitaka Klabu ya Simba kuwa makini katika kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo.
Uongozi wa Simba juzi ulimsainisha mkataba wa miaka miwili mshambuliaji Mganda Danny Ssrerunkuma huku ukitangaza kusitisha kwa muda mkataba wa Kiongera hadi pale atakapofanyiwa upasuaji na kupona majeraha ya goti yanayomkabili.
Timu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) zinapaswa kuwa na idadi isiyozidi wachezaji watano wa kigeni kwa mujibu wa Kanuni za Ligi za TFF Toleo la 2014. Ujio wa Sserunkuma umeifanya Simba kuwa na wachezaji sita wa kigeni; Waganda watatu (Emmanuel Okwi, Joseph Owino na Sserunkuma, Warundi wawili (Amissi Tambwe na Pierre Kwizera) na Mkenya mmoja (Kiongera).
Katika mahojiano maalum  kwenye ofisi za Makao Makuu ya TFF zilizopo Posta jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Mashindano wa shirikisho hilo, Boniface Wambura, alisema Simba wanapaswa kusajili kwa kufuata Kanuni za Ligi za TFF na taratibu zinazoongoza soka.
"Kwa sasa (jana saa 6:37 mchana) hatujapokea kitu chochote kutoka Simba kuhusu usajili unaoendelea wa dirisha dogo, tunasikia tu wamemsajili Sserunkuma lakini hatujapata taarifa rasmi," Wambura alisema.
"Simba itaruhusiwa kusajili mchezaji mpya/wapya wa kigeni msimu huu endapo tu itavunja mkataba/mikataba na wachezaji wa kigeni ilio nao kwa sasa.
"Kuna mambo matatu yanayothibitisha kuvunjwa kwa mkataba wa mchezaji; mchezaji mwenyewe kuvunja mkataba, mchezaji kufariki au klabu kuamua kuvunja mkataba wa mchezaji husika. Hili la Kiongera na Sserunkuma hawajatueleza maamuzi yao."
Simba kupitia kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hanspope imeeleza kuwa imesitisha mkataba wake na Kiongera na kumuondoa kwenye orodha ya wachezaji wake kwa ajili ya msimu huu na atakapopona, mkataba huo utaendelezwa, kauli ambayo inaonekana kama Kiongera bado ni mchezaji wa Simba. Dirisha dogo la usajili lilifunguliwa Novemba 15 na litafungwa Desemba 15.
NIPASHE

Robbie Keane ang'ara Marekani

http://www.trbimg.com/img-547ffbde/turbine/la-sp-keane-mls-mvp-20141204-001/500/500x281MSHAMBULIAJI nyota wa timu ya Los Angeles Galaxy Robbie Keane ametajwa kuwa mchezaji mwenye thamani zaidi maarufu kama MVP katika Ligi Kuu ya Soka nchini Marekani-MLS kwa mwaka huu. 
Nyota huyo wa kimataifa wa Ireland amefunga mabao 19 katika mechi 29 hivyo kuwapita washambuliaji wengine akiwemo Lee Nguyen wa New England Revolution na Obafemi Martins wa Seattle Sounders. Akihojiwa Keane amesema hakwenda nchini Marekani kwa ajili ya likizo bali kufanya kazi hivyo anafurahi kunyakuwa tuzo hiyo. 
Keane mwenye umri wa miaka 34 ambaye ndiye mfungaji mwenye mabao mengi katika timu yake ya taifa aliendelea kudai kuwa bado anapenda kuendelea kucheza kwa kiwango cha juu.

Pellegrini amvulia kofia kun Aguero

KOCHA wa Manchester City, Manuel Pellegrini amemmwagia sifa lukuki mshambuliaji wake Sergio kun Aguero akisema ni mmoja kati ya wachezaji watano bora duniani.
Meneja huyo aliyasema hayo baada ya mshambuliaji huyo wa Argentina, kuisaidia timu yake kupata ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Sunderland juzi. 
Katika mchezo huo City walitoka nyuma na kufanikiwa kushinda mchezo huo muhimu kwa kufunga mabao mawili na kumfanya Aguero kufikisha jumla ya mabao 14 msimu huu. 
Pellegrini amesema anadhani Aguero yuko katika orodha ya wachezaji watano bora duniani na kwa umri wa miaka 26 alionao bado ana nafasi ya kuimarika zaidi. 
Mbali na Aguero, kocha huyo pia aliwapongeza viungo wake Yaya Toure na Samir Nasri kwa juhudi zao kubwa kuhakikisha wanajiimarisha katika nafasi ya pili ya msimamo wa Ligi Kuu.

Chelsea kumpa kibarua cha kudumu Drogba

Mourinho akiwa na Drogba
MENEJA wa klabu ya Chelsea, Jose Mourinho amesema mshambuliaji wake Didier Drogba bado atakuwa na kazi Stamford Bridge wakati akiamua kustaafu rasmi kucheza soka. 
Drogba mwenye umri wa miaka 36 kwasasa anaichezea kwa mara ya pili klabu hiyo huku akifunga bao katika mchezo wa jana ambao Chelsea waliibugiza Tottenham Hotspurs kwa mabao 3-0. 
Akihojiwa Mourinho amesema jambo ni kwamba nyota huyo atamalizia soka lake akiwa na Chelsea na inavyoonekana anaweza kubakia akifanya mambo mengine pindi atakapostaafu. 
Drogba amefanikiwa kushinda mataji 10 akiwa na Chelsea mara ya kwanza kati ya mwaka 2004 mpaka 2012 huku akifunga mabao 157 katika mechi 341 alizocheza. 
Nyota huyo alijiunga tena na Chelsea katika kipindi cha majira ya kiangazi mwaka huu baada ya kuondoka klabu ya Galatasaray ya Uturuki.

Simba, Yanga kula shushu Mtani Jembe, viingilio vyatajwa

Vikosi vya Simba na Yanga
KLABU za Simba na Yanga watapata nafasi ya kubadili hadi wachezaji watano katika mechi ya kirafiki ya Bonanza, maarufu kama Mtani Jembe, ambayo viingilio vya mechi hiyo vimkitangazwa hadharani.

Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Boniface Wambura amesema wamefikia uamuzi huo kuwa wachezaji wanaoruhusiwa kuingia katika dakika 90 ni hadi watano kwa kila timu.
“Sub imeongezwa siku hiyo, badala ya wachezaji watatu, itakuwa hadi wachezaji watano.
“Kama mechi itaisha ndani ya dakika tisini bila ya kupata mshindi, basi zitapigwa penalti tano tano kwanza.
“Kikubwa katika mechi hiyo ni lazima siku hiyo mshindi apatikane,” alisema Wambura.
Wambura alisema pambano hilo litachezwa kwa dakika 90 tu na kama muda huo hatapatikana mshindi, mikwaju ya penalti itatumika na kwamba mshindi na marefa watakaolisimamia wanatarajiwa kutajwa leo na Kamati ya Waamuzi ya shirikisho.
Pia aliweka bayana viingilio vya mechi hiyo ya Jumamosi ijayo kuwa kiingilio cha chini kitakuwa Sh 7000 na cha juu Sh 30,000.

"Viingilio vya mechi hiyo ni Sh. 30,000 kwa VIP B, Sh. 20,000 kwa VIP C, 15,000/- kwa viti vya rangi ya chungwa na Sh. 7,000 kwa viti vya bluu na kijani. Tiketi zitakazotumika ni za kawaida na zitauzwa kwenye vituo ambavyo vitatangazwa baadaye," alisema Wambura.Mechi hiyo ya Bonanza inasubiriwa kwa hamu kubwa.

Tom Oloba apewa jukumu ya kunasa msaidizi wa Mombeki

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEiYcQ4GKfL84y4L09fZetG_9-iVLkU_gy6fWn9b2LjkoG-I89l_VehzDBlZEEPOxfcGAfGdq90_0rMu0KqwI3yOU4rTJc6B2UkJ6pWcErF0K-kEibqKmTapUgHCgW67ki5XFunEQjgRTfQ/s1600/IMG_6927.JPG
Mombeki alipokuwa Simba
UONGOZI wa klabu ya Ruvu Shooting, umesema hatma ya mshambuliaji mpya wa pili anayehitajiwa na kikosi chao ipo mikononi mwa kocha wao Tom Olaba, kwani tayari wachezaji zaidi ya watatu wanaendelea kufanyiwa majaribio kwenye mazoezi ya timu hiyo.
Msemaji wa Ruvu, Masau Bwire alisema baada ya kumsainisha mkataba wa mwaka mmoja mshambuliaji wa zamani wa Simba, Betram Mombeki kwa sasa wanasaka mchezaji wa mwisho na tayari chipukizi kadhaa wanafanyiwa majaribio kabla ya kocha Oloba kuamua.
Bwire alisema, Mkenya Olaba ndiye mwenye jukumu la kuamua nani anayemfaa katika kikosi chake kama alivyoamua kwa Mombeki ambaye alisainishwa mkataba wake mapema wiki hii.
"Tumefanikiwa kumnasa Mombeki na sasa kocha anaendelea kuwapima wachezaji waliojitokeza kwenye mazoezi, atakayemfaa ndiye atakayetueleza tumsainishe kwa ajili ya kukipa katika timu yetu, ila tunaamini tutafunika ligi ikiendelea kwa namna kikosi chetu kinavyoendelea kujifua," alisema.
Bwire alisema timu yao ipo kambi ya mazoezi tangu Novemba 24 na walianza mapema kwa ajili ya kutoa nafasi kwa kocha wao kurekebisha mapungufu yaliyoiangusha timu kwenye mechi za raundi saba zilizopita ambapo timu hiyo ilijikuta ikienda mapumziko wakiwa kwenye nafasi ya 11 kati ya timu 14 zinazoshiriki ligi hiyo kwa kukusanya pointi saba tu.
Ruvu inatarajiwa kuendelea na ligi Desemba 28 kwa kuvaana na ndugu zao wa JKT Ruvu wanaonolewa na kocha Fred Felix Minziro wanaokamata nafasi ya sita wakiwa na pointi 10.

Simba kuivaa Express bila Mkude, Sserunkuma ndani

Dan Sserunkuma anayeterajiwa kuonekana na uzi mwekundu leo
Kikosi cha Simba kitakachoshuka dimbani leo dhidi ya Express
MSHAMBULIAJI wa Simba Jonas Mkude anatarajia kuikosa mechi ya leo ya majaribio dhidi ya timu ya The Express  kutoka nchini Uganda kutokana na kuwa majeruhi, huku pia Dan Sserunkuma akitarajiwa kuonekana uwanjani na timu hiyo kwa mara ya kwanza.
Akizungumza jana Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Phiri alisema, Mkude, Ivo Mapunda na Hussein Shariff 'Casilas' wote wataikosa mechi hiyo ambayo ni muhimu kwa timu kujipima uwezo kabla ya mchezo wa 'Nani Mtani Jembe 2' dhidi ya Yanga Desemba 13, mwaka huu.
"Mechi ya leo ni muhimu kwetu, kwa sababu itatuonesha kipimo cha wachezaji kabla ya mchezo wetu wa Nani Mtani Jembe dhidi ya watani wetu Yanga,"alisema Phiri.
Alisema lengo la mchezo huo ni pamoja na kujiweka sawa kabla ya mchezo huo na Yanga na ule wa mzunguko wa nane wa Ligi Kuu Bara inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Desemba 26, mwaka huu katika viwanja tofauti hapa nchini.
Alisema mchezo huo pia utatumika kumpima mchezaji kutoka Gambia Omary Mboob ambaye anafanya majaribio kwa ajili ya kusajiliwa katika dirisha dogo la usajili linalofikia ukingoni Desemba 15, mwaka huu.
Akizungumzia mazoezi kwa ujumla alisema yanaendelea vizuri ambapo alisema wachezaji wameonyesha moyo wa kujituma pale wanapokuwa uwanjani kuendelea na mazoezi.

Maokola, MP Minoma kumaliza ubishi Desemba 19

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEi2DnzKJGvRGtEhB1V2Y09n6CRWs1Qt2k8RO129VGkP8domwzd7Qm7S2j22fN_8byoAanbCE1dOXeQuGqyfZL8iyAHSvvq8FQcnkAuxOo_2eVfUR0EAtGwI2zAtLZxL8f51cHY02Lq5eXTB/s1600/IMG_0408.JPG
Maokola na Mkalakala watakaorudiana tena kuwania ubingwa wa TPBC
BINGWA wa ngumi za kulipwa wa uzito wa Light Middle anayetambuliwa na Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC), Ibrahim Maokola anatarajiwa kupanda ulingoni Desemba 19, mwaka huu kwa ajili ya kutetea ubingwa wake huo dhidi ya Seleman Mkalakala 'MP Minoma'.
Rais wa TPBC, Chaurembo Palasa aliliambia MICHARAZO kuwa pambano hilo litakalokuwa la raundi 10 na litakalosindikizwa na michezo kadhaa ya utangulizi, litachezwa kwenye Ukumbi wa Vigae Pub, Mbagala Dar es Salaam.
Palasa alisema sababu ya kupeleka pambano hilo Mbagala ni kutaka kuhamasisha mchezo huo wa ngumi katika maeneo mengine badala ya kuendelea kuchezwa katika kumbi zile zile zilizozoeleka.
"Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC), tumeidhinisha pambano la ngumi kati ya Ibrahim Maokola atakayekuwa akitetea taji lake dhidi ya Seleman Mkalakala, mchezo huo utasindikizwa na michezo mingine kadhaa ya utangulizi," alisema Palasa.
Palasa alitaja baadhi ya michezo ya utangulizi kuwa ni lile la wapinzani wa jadi, Abdallah Mohammed 'Prince Nassem' dhidi ya Salehe Mkalekwa.
"TPBC inataka kuleta mvuto kwa mchezo huo kwa kupelekwa katika maeneo mengine nje ya kumbi zilizozoeleka, ili kuwavutia wadhamini sambamba na kuhakikisha vipaji vipya vinaibuka ndani na nje ya jijini la Dar es Salaam ili kuendeleza ngumi," alisema Palasa.
Aidha, Palasa alitoa tahadhari kwa mabondia, waratibu na mapromota ambao watakiuka sheria na kanuni za mchezo kuwa watachukuliwa hatua kali za kinidhamu ili kuhakikisha ustaarabu unaendelea kuwepo katika mchezo huo.

Zahoro Pazi kumbadili Mrwanda Polisi Moro

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgeIFO6Ts0oOYH-zSbZQpHtdE3LBHVEuBeH3qRPbnGO4jkbsbTrXqiLajnsS3YTyKidqQxsd0gZR9d434iV_lBuB4lrqz1F_FDTjFIQMRqaHqCmd338YusINEHVosFi2MAeESOCzguCrgXd/s1600/pazi.JPG
Zahoro Pazi alipokuwa Simba
TIMU ya Polisi ya Morogoro inayoshiriki Ligi Kuu imemsajili mshambuliaji wa Simba, Zahor Pazi, mtoto wa kipa wa zamani wa wekundu hao, Idd Pazi 'Father' katika kipindi hiki cha dirisha dogo linalotarajiwa kufugwa Desemba 15, mwaka huu.
Zahor ambaye anacheza nafasi ya ushambuliaji, amesaini mkataba wa kuichezea timu ya Polisi ya Morogoro kwa kipindi cha mwaka mmoja katika ofisi ya Kamanda wa Polisi mkoani hapa, ambaye pia ni mlezi wa timu hiyo.
Hatua ya Polisi kumsajili mchezaji huyo ni kujibu mapigo baada ya timu ya Simba kuwa mbioni kumsajili mshambualiaji wao tegemeo, Danny Mrwanda.
Akizungumza na waandishi wa habari, mwenyekiti wa timu hiyo ya Polisi, Issa Bushir alisema kuwa wameamua kumchukua mshambuliaji huyo kutokana na uwezo alionao na kwamba wanaamini kuwa ataisaidia timu hiyo katika ligi inayotarajiwa kuendelea wiki mbili zijazo.
Naye mlezi wa timu hiyo ya Polisi, ambaye ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonald Paul, alisema wanaamini mshambuliaji huyo ataweza kuziba pengo la Mrwanda anayehamia timu ya Simba.
Kwa upande wake Zahor alihaidi wanachama na wapenzi wa timu ya Polisi Morogoro kuwa atajituma kwa kushirikiana na wachezaji wenzake ili kuiletea ushindi timu hiyo ya 'maafande'.

Ndanda kuanza kuiwinda Mbeya City Jumatatu Dar

Kikosi cha Ndanda Fc
TIMU ya Ndanda ya Mtwara inayoshiriki Ligi Kuu kwa mara ya kwanza msimu huu inatarajiwa kuanza kambi ya mazoezi keshokutwa jijini Dar es Salaam, huku uongozi wake ukiendelea kuficha majina ya wachezaji wapya iliyowasajili kwenye dirisha dogo.
Mkurugenzi na Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Edmund Njowoka aliliambia MICHARAZO mapema leo kuwa, kambi yao ya mazoezi kwa ajili ya kujiwinda na mzunguko wa nane wa ligi hiyo itaanza siku ya Jumatatu badala ya Desemba 4 kama walivyokuwa wametangaza awali na itakuwa jijini Dar es Salaam.
Njowoka alisema uongozi wao umeamua kuiweka kambi hiyo jijini Dar es Salaam ili kutoa nafasi nzuri kwa kocha wao Meja Abdul MIngange kuwanoa vizuri wachezaji wapya ambao wamenyakuliwa na klabu hiyo katika dirisha dogo.
Hata hivyo alipoulizwa juu ya wachezaji wapya iliowaongeza, Njowoka alisema hawezi kuwataka kwa madai ni mapema mno kwa sasa na atafanya hivyo baada ya kufungwa kwa dirisha hilo Jumatatu ijayo.
"Hatuwezi kuzungumza vitu nusu nusu, wapo tuliofanikiwa kuwanyakua na wengine tunamalizana nao, hivyo subirini tumalize usajili wote kisha tuutangaze umma kitu kilichokamilika," alisema Njowoka.
Hata hivyo tayari timu hiyo ilishamtangaza kumsajili kiungo mshambuliaji wa Mtibwa, Masoud Chile na ilikuwa mbioni kuwanyemelea nyota wengine toka Yanga akiwamo kipa Ally Mustafa 'Barthez'.
Timu hiyo iliyopanda msimu huu sambamba na timu za Stand United na Polisi-Moro inatarajiwa kuvaana na Mbeya City katika mechi yao ijayo na mpaka ligi inasimama waliwakuwa katika nafasi ya pili toka mkiani ikiwa na pointi 6, moja zaidi ya wanaoshika mkia Mbeya City.