STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, September 26, 2011

Golden Boy, kuzinyuka na Miyeyusho

BINGWA wa UBO-Mabara, Mbwana Matumla 'Golden Boy' anatarajia kupanda ulingoni mwezi ujao kuzipiga na bondia Francis Miyeyusho katika pambano la kutetea taji lake litakalofanyika jijini Dar es Salaam.
Pambano hilo la uzani wa Bantam litakalokuwa la raundi 10, litafanyika Oktoba 30 kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, likisindikizwa na michezo kadhaa ya utangulizi.
Kwa mujibu wa kocha msaidizi wa kambi ya Kinyogoli Foundation inayowanoa mabondia watakaosindikiza pambano hilo la Matumla na Miyeyusho, Rajab Mhamila ni kwamba maandalizi ya pigano yanaendelea vema.
Mhamila, alisema pamoja na kwamba pambano hilo ni la kuwania taji la UBO, lakini pia limewagawa mashabiki wa ngumi kulingana na mahali wanapotoka mabondia hao nyota, ambapo Matumla yeye anatokea Temeke na Miyeyusho akitokea Kinondoni.
"Pambano la Matumla na Miyeyusho ni kama la watu wa Temeke na Kinondoni, huku yale ya utangulizi yatahusisha mabondia wa pande hizo mbili, hali inayofanya pigano hilo lijalo kuwa na msisimko wa aina yake," alisema Mhamila.
Mhamila, alisema pambano hilo la UBO limeratibiwa na Mood Bawazir wa kampuni ya Dar World Links na litasindikizwa na michezo ipatayo mitano ya utangulizi kati ya hiyo ni pigano linalosubiriwa kwa hamu kati ya Ramadhani Shauri wa Kinondoni dhidi ya Issa Sewe kutoka Temeke.
Pigano hilo la Matumla, linakuja miezi minne tangu bondia huyo alipopanda ulingoni na kulitetea taji lake hilo kwa kumchakaza Mkenya, Gabriel Ochieng katika pambano lililofanyika Mei Mosi, kwenye ukumbi wa PTA, jijini Dar es Salaam.
Mabondia wote wawili yaani Matumla na Miyeyusho kwa sasa wapo kambini wakijifua kwa ajili ya pambano hilo, kila mmoja akitamba kuibuka na ushindi siku ya pigano hilo.

Mwisho

Maugo kuzichapa na MkenyaBONDIA machachari wa ngumi za kulipwa nchini, Mada Maugo anatarajiwa kupanda tena ulingoni jijini Mwanza kuzipiga na Mkenya, ikiwa anatokea kuuguza kipigo toka kwa Francis Cheka.
Aidha bondia huyo amesema hayupo tayari kupigana tena na Francis Cheka, labda kama mwamuzi na majaji watakuwa ni wa kutoka nje ya nchi kwa kile alichodia waamuzi na majaji wa nchini humbeba mpinzani wake kila mara.
kizungumza na MICHARAZO, Maugo, alisema pambano hilo la Mkenya Mosses Odhiambo litafanyika Novemba kwenye uwanja wa CCM Kirumba.
Maugo, alisema pambano hilo lisilokuwa la ubingwa la raundi 10 na la uzani wa kati, ni maalum kwa maandalizi ya kwenda kupigana nje ya nchi katika pambano la kimataifa dhidi ya Mjerumani.
"Natarajia kupanda ulingoni mwezi Novemba kupigana na Mkenya katika pambano la raundi 10 la uzito wa kilo 72, lisilo la ubingwa kwa nia ya kujiweka fiti kabla ya kwenda kupigana ngumi za kimataifa dhidi ya Mjerumani," alisema Maugo.
Kuhusu kurudiana na Cheka, Maugo alisema atakuwa radhi kufanya hivyo kama majaji na waamuzi watatoka nje ya nchi kwa madai wa ndani humbeba mpinzani wake kama ilivyotokea kwenye mechi zao mbili ambapo zote alipigwa kwa pointi.
"Sintakuwa tayari kupigana tena na Cheka, labda kama waandaaji watawaleta majaji na mwamuzi kutoka nje, mpinzani wangu wamekuwa akibebwa ndio maana rekodi yake nje ya nchi ni mbovu tofauti na anavyotamba akicheza nyumbani," alisema.
Alisema wiki iliyopita akifuatwa na mmoja wa mapromota akiwataka wapigane na Cheka katika pambano la kusaka mbabe kati yao, na kuweka msimamo wake huo, hali iliyofanya muaandaji huyo kuamua kuachana na wazo la kuwapiganisha tena.
Maugo alipigwa kwa pointi na Cheka katika mapambano yaliyofanyika Januari Mosi, jijini Dar es Salaam na Septemba Mosi, mjini Morogoro, ambapo kote bondia huyo alikuwa akilalamikia 'kuchakachuliwa' matokeo.

Anti Fifi: Jimama linalotesa Bongo Movie, sasa ageukia utunzi wa vitabuWAKATI mastaa wenye majina na umaarufu mkubwa kama wake nchini hupenda kuishi maisha 'bandia' ya kuhofia kujishughulisha na kazi au kujichanganya na watu
wengine wa kawaida, kwa Tumaini Biligimana au 'Anti Fifi', hali ni tofauti.
Licha ya umaarufu alionao kupitia sanaa aliyoanza kuifanya zaidi ya miaka 20 akianzia kama promota wa urembo, disko na muziki wa kizazi kipya, Anti Fifi anauza 'genge' la chakula eneo la Mwananyamala, alipika na kuuza mwenyewe.
Pia, nyota huyo haoni aibu kula 'chips dume' (mihogo ya kukaanga) au kupanda daladala katika mizunguko yake jijini Dar, licha ya kumiliki gari zuri la kisasa.
"Siwezi kuhofia kuishi nilivyozoea kwa sababu ya jina kubwa, kuishi 'bandia' ndiko kunakoponza mastaa wengi kuishia kwenye machafu wakitafuta mkato ya maisha ili waonekane bab'kubwa," alisema.
Alisema, tangu alipoanza kupata umaarufu hajawahi kuona aibu kujichanganya na watu wengine, jambo alilodai limemrahisishia mambo yake mengiu kimaisha na kisanii.
Anti Fifi, aliyefanya kazi na madansa wa nyota wa zamani kama Black Mosses, Master
Flash na wengine, alisema kitendo cha kupika na kuuza chakula katika mgahawa wake kumemfanya apate wateja wengi, baadhi wakienda ili kujiridhisha kama kweli ni yeye au wanamfananisha na mtu wanayemuona kwenye filamu.
Msanii huyo alisema anavyofahamu yeye, ustaa wa mtu kujizuia na matendo machafu na ya aibu mbele ya jamii, ila sio kuogopa kujichanganya au kuishi vile mtu apendavyo au alivyozoea.
"Ustaa ni kujiheshimu, kujithamini na kujichanganya na watu ili kujifunza mengi toka kwao yanayoweza kumsaidia msanii katika kukuza sanaa yake, sio kuishi maisha bandia ya hadhi ya juu, ilihali uwezo huo mtu hana," alisema.
Muigizaji huyo ambaye pia, ni mtunzi, mtayarishaji na mwandishi wa vitabu, alisema mbali na kuuga mgahawa, pia anajiuza mayai ya jumla katika nchi jirani, sambamba na nguo na vipodozi vya wanawake na watoto.
Alisema anaamini wasanii wakiamua kuishi jinsi walivyo kabla ya kupata umaarufu wanaweza kujiepusha na skendo chafu ambazo zimekuwa ni mazoea kwao na kuitia doa sanaa yao kwa ujumla.
"Sijisifii, ila mie ni baadhi ya wasanii wanaojiheshimu kwa vile naishi jinsi nilivyo, hivyo sikumbwi na skendo kwa kusaka umaarufu, bali kazi zangu ndizo zinazonipa 'ujiko' mbele ya jamii, kama unavyojua majuzi tu filamu niliyotunga ya 'Senior Bachelor' ilitwaa tuzo ZIFF."
Anti Fifi anayependa kula ugali kwa samaki na dagaa na kunywa juisi ya karoti na passion, alisema tangu atumbukie kwenye sanaa amenufaika kwa mengi, ikiwemo umaarufu, kujenga nyumba, kumiliki gari na kiwanja alichoanza kukijenga nyumba nyingine eneo la Mbezi.
"Najivunia sanaa pia, imenisaidia kuweza kutunga na kuuza hadithi za filamu, huku kwa sasa nikiwa nimetumbukia kwenye utunzi wa vitabu, nikijiandaa kutoa kitabu kiitwacho 'Migogoro ya Ndoa na Suluhisho Lake'," alisema.
Anti Fifi, aliyewahi kuishi maisha ya ndoa ya kiislam kuanzia mwaka 1989-2001 alipoachika, alisema matarajio yake ni kutaka kujitofautisha na wasanii wengine nchini akitaka kuwa mtunzi mahiri wa vitabu na filamu kwa ujumla.
Anti Fifi, aliyeokoka kwa sasa, alisema kama angekutana na Rais angemuomba asaidie kuiinua sanaa nchini na kukomesha uharamia, ili inawanufaishe wasanii.
"Hata mimi ningekuwa Rais ningeyafanya hayo, pamoja na kuondoa kero ya umeme nchini, kwani ni aibu kwa Tanzania yenye vyanzo vingi vya kuzalisha nishati hiyo kuwa na tatizo la ukosefu wa umeme na kuliingiza taifa kwenye hasara kubwa,: alisema.
Tumaini Biligimana, aliyezaliwa Julai 17, 1965 mjini Kigoma, akiwa mtoto wa sita kati ya 13 wa Mzee Biligimana, alisema hakuna tukio la furaha kwake kama aliposhiriki filamu ya Dar es Salaam akiigiza kama Jimama la Kikongo, linaloendesha genge la mabinti wahalifu, kiasi cha kufuatiliwa na Polisi, waliodhani huenda ndivyo alivyo.
"Huwezi amini nilifuatiliwa na Polisi kwenye duka na saluni yangu wakinipeleleza kwa kile walichokiona kwenye filamu hiyo niliyoiigiza mara nilipotua Dar nikitokea Kigoma," alisema.
Kisanii, Anti Fifi mwenye watoto watatu, Mohamed, 24 anayesoma kidato cha tano nchini Uganda, Omari, 21 anayesomea ufundi VETA na Zamda, 17 aliyepo kidato cha pili Shule ya Sekondari Kunduchi Beach, alianza tangu shuleni akicheza ngoma, kuimba na kupiga filimbi.
Alisema pia alikuwa mahiri wa kuchora, kubinuka sarakasi wakati wakisoma Shule ya Msingi Muungano na baadae Ujiji Sec, kabla ya kuajiriwa serikalini kama Mhasibu katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma.
Baada ya miaka tisa ya utumishi wa umma, aliacha kazi hiyo na kujikita katika biashara akiwa promota wa fani ya urembo na disko, hadi mwaka 2001 aliposhiriki uzinduzi wa filamu ya Girlfriend na kupata kiu ya kuwa muigizaji baada ya kukutana na George 'Tyson' Otieno.
Alianza fani hiyo kwa kutunga na kuigiza filamu ya kwanza iitwayo Haraka ya Maisha ya mwaka 2002 kabla ya kuja Dar miaka miwili baadae kujiunga na kundi la Fukuto Arts na kushiriki filamu ya Dar es Salaam iliyomfungulia neema ya mafanikio.
Kazi nyingine alizoshiriki ni pamoja na Copy, Sound of Death, Senior Bachelor, I Deserve It, Kaburi la Mapenzi, Kizungumkuti, Fake Smile, Daddy, na nyinginezo baadhi akizitunga.
Anti Fifi anayechizishwa na rangi ya zambarau na pinki, alisema anawazimia Jacob Stephen 'JB', Irene Uwoya na Aunty Ezekiel, aliwaasa wasanii wenzake wajitume na kujichanganya kusaka maisha nje ya sanaa zao, kwa lengo la kuepusha kutumiwa ovyo.

Watanzania hawana utamaduni wa kusoma-EZAA

CHAMA cha Waandishi wa Vitabu Kanda ya Mashariki, EZAA, kimesema asilimia kubwa ya watanzania hawana utamaduni wa kupenda kusoma vitabu, jambo linalochangia kuwepo kwa ugumu wa soko la vitabu nchini.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Jackson Kalindimya, aliyasema hayo wakati wa semina ya siku tatu ya watunzi wa vitabu vya hadithi za watoto, iliyofanyika kwenye ukumbi wa Msukuma, mjini Mlandizi, Pwani.
Kalindimya alisema Tanzania ina tatizo la watu kupenda kusoma, kitu ambacho kwa kiasi kikubwa kimekuwa kikiathiri soko la vitabu na maandishi mengi.
Hata hivyo, aliwaasa waandishi na watunzi wa vitabu kutokata tamaa badala yake kuzidi kuandaa kazi zenye mvuto ambavyo zitachochea wananchi kubadilika na kuanza kupenda kusoma kama ilivyo kwa mataifa mengi.
Kalindimya alisema tofauti na wananchi wa mataifa mengine ambao wawapo safarini au mahali popote hubeba vitabu au majarida kwa ajili ya kujisomea, kwa wananchi wa Tanzania ni wachache wanaofanya hivyo, kitu alichotaka watanzania wabadilike.
"Wananchi wanapaswa kubadilika na kujenga tabia ya kupenda kusoma kwani itawasaidia kuelimika, sambamba na kusaidia soko la kazi za waandishi," alisema.
"Licha ya hali hiyo, watunzi na waandishi msikate tamaa, muikabili changamoto hiyo kwa kuandaa kazi zenye mzuri zenye mvuto ambazo zitawabadilisha wananchi, pia ikirahisisha soko la kazi zenu," alisema.
Baadhi ya washiriki wa semina hiyo, ambao ni chipukizi katika utunzi na uandishi wa vitabu, waliwapongeza waandaaji wake kwa namna walivyowasaidia kuelewa mambo ambayo kabla ya hapo walikuwa hawana ufahamu nayo katika fani hiyo.

CBP yataka mrithi wa Shaaban Robert apatikane
WATUNZI na waandishi wa kazi za Fasihi nchini, wamepewa changamoto ya kujibidiisha katika fani zao, ili kumpata 'Shaaban Robert' mpya miongoni mwao atakayeendeleza na kudumisha fasihi katika kiwango alichokuwa nayo gwiji huyo.
Aidha jamii imeaswa kujenga utamaduni wa kuwanunulia na kuwasomea vitabu vya hadithi watoto wao kama njia ya kuchochea uwezo wao kuelewa na akili ambao utawasaidia katika masomo ya kitaaluma.
Katibu Mtendaji wa Mradi wa Vitabu vya Watoto Tanzania, CBP, Pili Dumea, ndiye aliyetoa wito huo kwa waandishi wakati wa ufungwaji wa semina ya siku tatu ya Waandishi wa Vitabu Kanda ya Mashariki, EZAA, iliyofanyika Mlandizi, mkoani Pwani.
Dumea, alisema watunzi na waandishi chipukizi wa kazi za fasihi wanapaswa kufanya kazi zao kwa umahiri, ili waweze kuja kumrithi Shaaba Robert, ambaye licha ya kufariki kitambo kirefu, bado amekosa wa kufikia umahiri wake katika fani hiyo.
"Semina na mafunzo haya yawe chachu kwenu katika kujibidiisha na kujituma katika fani hii mkiwa na lengo la kutaka kuwa warithi wa Shaaba Robert, ambaye licha ya kutokuwepo kazi zake zimeendelea kudumu milele," alisema Dumea.
Katibu huyo alisema CBP, ipo kwa ajili ya kuwasaidia watunzi na waandishi wa vitabu kufikia lengo la kuendeleza fasihi hasa vitabu vya hadithi vitakavyochochea maendeleo ya nchi kuanzia kwa watoto hadi watu wazima.
Pia, alisema jamii ni lazima iwe na utamaduni wa kuwasomea na kuwanunulia watoto vitabu kuwazoesha kusoma na kuchochea ufahamu wao na uwezo wao wa kimasomo darasani, akidai kusoma ni njia ya kusaidia uelewa na akili za mtu.
Naye Katibu Mkuu wa EZAA, Jackson Kalindimya, aliwaasa waandishi hao watumie vema uwezo wao wa 'kimungu' walionao katika kuchochea maendeleo ya nchi pamoja na kuijenga jamii katika maadili mema.
Kalindimya, alisema watunzi wa vitabu ambao wana uwezo wa kuumba dunia yao na viumbe wengine wakiwapa pumzi, tabia na uhusika unaoweza kuibadilisha jamii kutoka mahali pamoja hadi kwingine kimaendeleo na hata kimaadili kupitia kazi zao.
"Lazima mjivunie uwezo wa kimungu mlionao, kwa kuisaidia jamii kubadilika mahali ilipo hadi kwenye maendeleo, cha muhimu ni kutoa kazi nzuri zenye mvuto ambazo zitawafanya watu wazinunue na kuzisoma, kisha kuwabadilisha," alisema.

Mwisho