STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, February 27, 2014

Titina wa Extra Bongo ajiandaa kuacha kunengua

Mnenguaji Titi Mwinyi 'Titina' akiwa katika pozi
MNENGUAJI mahiri wa bendi ya Extra Bongo, Titi Mwinyiamir maarufu kama 'Titina' amesema anajipanga kuachana na fani hiyo baada ya kuitumikia kwa zaidi ya miaka 10.
Akizungumza na MICHARAZO, Titina aliyewahi kutamba na Double M Sound, Twanga Pepeta na FM Academia, alisema anataka kuachana na fani hiyo ili kujikita kwenye uimbaji.
Titina alisema muda aliotumika kama dansa tangu mwaka 2000 umeufanya mwili wake kuchoka na sasa anadhani ni muda muafaka kuhamia kwenye uimbaji ili kuendeleza kipaji alichonacho.
"Natarajia kuachana na unenguaji ili nijikite kwenye uimbaji, kipaji hicho ninacho tangu utotoni sema kunengua kuliniathiri na kukisahau, ila sasa sina jinsi zaidi ya kukiendeleza," alisema.
Dansa huyo alisema tayari ameanza mazoezi ya kuimba ili akiwiva vyema ahamie huko kufuata nyazo za akina Tshallah Mwana na Mbilia Bel waliowahi kutanga kwenye unenguaji kabla ya kuhamia kwenyue uimbaji na kuishika Afrika.
Titina, alisema anaamini bidii yake katika kujifunza kuimba kwa sasa ndiko kunakoweza kumfikisha pale walipofikia wakali hao kutoka Kongo au baadhi ya wanamuziki wa kike wanaotamba nchini kama akina Luiza Mbutu na wengine ambao walianzia kwenye unenguaji kabla ya kuwa waimbaji.

NEC yatoa ratiba uchaguzi mdogo Jimbo la Chalinze

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza ratiba ya uchaguzi mdogo wa jimbo la CHALINZE, mtakumbuka kuwa jimbo hilo limekuwa wazi baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo bwana Said Bwanamdogo kufariki dunia tarehe 22 Januari 2014 kwenye hospitali ya MOI jijini Dar es salaam.

Ratiba ya uchaguzi kwenye jimbo hilo iko kama ifuatavyo:-

1. Uteuzi wa wagombea  - Tarehe 12 Machi 2014

2, Kampeni na Uchaguzi - Tarehe 13 Machi 2014

3. Siku ya Uchaguzi - Tarehe 6 April, 2014


Tarehe ya wagombea ubunge kuchukua Fomu za uteuzi kwa msimamizi wa uchaguzi ni kuanzia tarehe 03 Machi, 2014 hadi tarehe 12 Machi, 2014(Siku ya uteuzi) Kabla ya saa 10:00 Alasiri.


Wagombea wanatakiwa kuwasilisha fomu za uteuzi kwa msimamizi wa uchaguzi siku ya uteuzi si zaisi ya saa 10:00 Alasiri

Da! Mwanamke ajifungua Barabarani


Mwanamke aliyejifungua barabarani
MWANAMKE mmoja raia wa Uingereza amejifungulia katika barabara moja mjini New Yorkakiwa njiani kuelekea hospitali kutokana na uchungu wa uzazi.
Polly McCourt, mwenye umri wa miaka 39,aliondoka nyumbani kwake katika mtaa wa East Side siku ya jumatatu na kujaribu kukodisha taxi hadi alipogundua kuwa mwanawe asingeweza kusubiri.
Wapita njia walimpa mama huyo koti na vitambaa walivyokuwa navyo kumfunika mwanawe hadi wahudumu walipofika kumsaidia na kumpeleka hospitaliini. Mama na mtoto walikuwa salama walipofikishwa hospitalini.
"alipiga mayowe akisema Mungu wangu mtoto wangu yuaja ,'' alisema shahidi mmoja.
Na niliweza kuona kichwa cha mtoto. Tulipomlaza mama chini kumsaidia, mtoto akawa tayari ametoka.''
Bi McCourt, anayetoka nchini Uingereza alijifungua mwanawe kando ya barabara.
Mama huyo alionekana akitabasamu alipoingia katika gari la ambulensi na kupelekwa katika hospitali ya Lennox Hill mjini New York.
Mumewe mama huyo alikuwa amekwama barabarani kutokana na msongamano wa magari alipopata simu kutoka kwa mkewe.
Wawili hao tayari wana watoto wengine wawili, Conor mwenye umri wa miaka sita na Adele mwenye umri wa miaka minne kulingana na jarida la New York Daily News.
Inaarifiwa walihamia mjini New York miaka minne iliyopita kutoka Dublin nchini Ireland.
BBC

27 warejesha fomu Uchaguzi wa Taswa, Shafii Dauda 'achomoa'

Shafii Dauda aliyeshindwa kurejesha fomu ya uchaguzi wa Taswa
JUMLA ya waombaji 27 kati ya 28 wamerejesha fomu kuomba kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kwenye uchaguzi wa Kamati mpya ya Utendaji ya Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) utakaofanyika Machi 2, 2014 jijini Dar es Salaam.

Mwisho wa kuchukua na kurudisha fomu hizo ilikuwa leo Alhamisi (Februari 27 mwaka huu) saa 9 alasiri.

Waliorejesha kwa nafasi ya ujumbe ni Arone Benedict Mpanduka, Elizabeth Rashid Mayemba, Emmanuel Augustino Muga, Hassan Maulid Bumbuli, Ibrahim Mkomwa Bakari, Masau Kuliga Bwire, Mbozi Ernest Katala, Mroki Timothy Mroki, Mussa Juma, Mwani Omary Nyangassa, Rehure Richard Nyaulawa, Salum Amiri Jaba, Tullo Stephen Chambo na Urick Chacha Maginga.

Mhazini Msaidizi ni Elius John Kambili, Zena Suleiman Chande wakati Mhazini Mkuu ni Shija Richard Shija na Mohamed Salim Mkangara.

Katibu Msaidizi ni Alfred Lucas Mapunda, Grace Aloyce Hoka na Patrick Raymond Nyembera. Katibu Mkuu ni Amir Ally Mhando pekee.

Waombaji nafasi ya Makamu Mwenyekiti ni Egbert Emmanuel Mkoko, Maulid Baraka Kitenge na Mohamed Omary Masenga. 
Waliojitosa kwenye nafasi ya Mwenyekiti ni George John Ishabairu, Juma Abbas Pinto.

Mgombea mwingine wa nafasi hiyo, Shaffih Kajuna Dauda hakurudisha fomu kwa madai ya kubanwa na moja ya vipengele vya katiba ya chama hicho na yeye ameonyesha kuridhika kujiweka kando bila kinyongo.

Wazambia watua, Twiga Stars yaapa kuing'oa Afrika

Twiga Stars wanaotarajiwa kuwapa raha watanzania kesho

WAKATI Zambia (Shepolopolo) imewasili leo mchana (Februari 27 mwaka huu), Twiga Stars imesema mazoezi yamewaingia barabara tayari kwa mechi dhidi ya Wazambia hao itakayochezwa kesho (Februari 28 mwaka huu). Mechi hiyo ya marudiano ya raundi ya kwanza ya michuano ya Afrika kwa Wanawake (AWC) itafanyika Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi kuanzia saa 10 kamili jioni, na hakutakuwa na kiingilio. Wakizungumzia mechi hiyo, Kocha wa Twiga Stars, Rogasian Kaijage na nahodha wa timu hiyo Sophia Mwasikili wamesema kikosi chao kimewiva kwa ajili ya mpambano huo baada ya kufanyia kazi upungufu uliojitokeza katika mechi ya kwanza.
Twiga Stars ilipoteza mechi ya kwanza iliyochezwa Februari 14 mwaka huu jijini Lusaka kwa mabao 2-1, na inahitaji ushindi ili iweze kusonga mbele kwenye michuano hiyo ambayo fainali zake zitafanyika Oktoba mwaka huu nchini Namibia.
Iwapo Twiga Stars itafanikiwa kuitoa Zambia katika mechi hiyo itakayooneshwa moja kwa moja na Azam Tv itacheza raundi ya mwisho na Zimbabwe.
Msafara wa Shepolopolo una watu 26 ambapo wachezaji ni Anita Mulenga, Annie Kibanji, Carol Howes, Debora Chisanga, Emelda Musonda, Esther Mukwasa, Grace Zulu, Hazel Nali, Hellen Mubanga, Lweendo Chisamu, Meya Banda, Mirriam Katamanda, Misozi Zulu, Mupopo Kabange, Noria Sosala, Rachel Lungu na Susan Banda.
Viongozi ni Maclean Daka, Charles Bwale, Kaluba Kangwa, Enala Phiri, Cornelia Chazura, James Nyimbili, Besa Chibwe, Dorothy Sampa na Kabungo Katongo.

Kim Poulsen 'byebye' Taifa Stars, TFF yavunja mkataba wake

Kim Poulsen aliyevuniwa mkataba na TFF
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) na Kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen wamekubaliana kuvunja mkataba katika makubaliano ambayo ni siri kwa pande zote mbili.
Uamuzi huo umetangazwa leo (Februari 27 mwaka huu) jijini Dar es Salaam kwa pamoja na Rais wa TFF, Jamal Malinzi na Kocha Poulsen mbele ya waandishi wa habari.
Rais Malinzi kwa niaba ya TFF ametoa shukrani za dhati kwa Kocha Poulsen kwa ushirikiano na mchango ambao ameutoa kwa Tanzania kuanzia kwenye mpira wa miguu wa vijana.
Naye Kim amewashukuru Watanzania kwa ushirikiano waliompatia kwa kipindi cha miaka mitatu alichokaa nchini kuanzia Mei 2011 alipoteuliwa kuwa kocha wa timu za Taifa za vijana, na baadaye Taifa Stars.
Akizungumzia benchi jipya la ufundi la Taifa Stars, Rais Malinzi amesema linatarajiwa kutangazwa hivi karibuni likiongozwa na kocha kutoka nje ya Tanzania.
Amesema kwa upande wa mechi dhidi ya Namibia itakayochezwa Machi 5 mwaka huu jijini Windhoek, Stars itaongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Ufundi, Salum Madadi akisaidiwa na kocha Hafidh Badru kutoka Zanzibar.

Nyota wa Yanga waenguliwa Stars, Kado wenzake waula

Juma Luizio 'Ndanda' ameongezwa Taifa Stars


Baadhi ya nyota wanaotarajiwa kuiongoza Stars dhidi ya Namibia

Na Boniface Wambura
KAIMU Kocha Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Salum Madadi amewaondoa wachezaji watano wa Yanga katika kikosi kilichotajwa awali ili wapate fursa ya kuitumikia timu yao kwenye mechi mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al-Ahly ya Misri.
Wachezaji hao ni Athuman Idd, David Luhende, Deogratius Munishi, Frank Domayo, Kelvin Yondani na Mrisho Ngasa. Pia kipa Ivo Mapunda ameondolewa katika kikosi hicho baada ya kupata msiba.

Nafasi zao zimezibwa na wachezaji Abdi Banda (Coastal Union), Himid Mao (Azam), Juma Luizio (Mtibwa Sugar), Said Moradi (Azam) na Shabani Kado (Coastal Union).
Taifa Stars itaingia kambini keshokutwa (Machi 1 mwaka huu) jioni kwenye hoteli ya Accomondia jijini Dar es Salaam, na itaondoka Machi 3 mwaka huu alfajiri kwa ndege ya South African Airways na kurejea nchini Machi 7 mwaka huu saa 8.15 mchana.

Kingwendu aja na Faza Hausi

MSANII wa filamu nchini Athumani Lali 'Budege' baada ya kucheza filamu za watu sasa ameamua kuja na filamu zake mwenyewe na kuwawezesha wasanii wenzie kuwa na kipato kizuri baada ya kuamua kufungua kampuni yake binafsi inayokwenda kwa jina la AJM Entatainment ambayo ina husika na maswala ya filamu za kibongo
Athumani Lali 'Budege'
akizungumza na mwandishi wa habari hizi Lali amesema kuwa kwa sasa yupo katika atua za mwisho kwa ajili ya kutoa filamu mpya inayokwenda kwa jina la Faza Hausi ambayo imeshilikisha wasanii wakongwe ndani yake akiwemo Mohamed Nurdini 'Chekbudi' ,Esha Buheti, Rashidi Mwishehe 'Kingwendu' Muogo Mchungu 
Filamu hiyo itakayo tolewa na Kampuni hiyo ya jijini Dar es salaam itakuwa moto wa kuotea mbali kwani si ya kukosa kabisa kwa mashabiki wa filamu nchini
filamu hiyo ya Faza Hausi itakuwa mtaani wakati wowote kuanzia sasa kwani takribani vitu vyote muhimu vimeshafanyika hivyo wadau wakae mkao wa kula kwani filamu hii si yakuikosa
Ambapo itapatikana Tanzania nzima nikianzia Dar es salaam na mikoa yote filamu hiyo itawafikia

Inspekta Harun kutambulisha mpya, akisdaka mrembo Mbeya

Inspekta Harun 'Babu' katika pozi
MSANII mkongwe wa muziki wa kizazi kipya nchini, Haruna Kahena 'Inspekta Harun' a.k.a Babu anatarajiwa kuitambulisha albamu yake mpya ya 'Sharubu za Babu' sambamba na video ya wimbo wake wa 'Hujachelewa' jijini Mbeya wikiendi hii.
Akizungumza na MICHARAZO, Inspekta alisema kuwa, utambulisho huo utafanyika siku ya Jumapili kwenye ukumbi maarufu jijini humo ambao utaambatana pia na shindano la kusaka kimwana wa kucheza filamu ya 'Mtoto wa geti Kali'.
Staa huyo wa nyimbo kama 'Nje Ndani', 'Simulizi la Ufasaha', 'Mtoto wa Geti Kali' na nyingine, alisema shindano hilo la kusaka mrembo wa kucheza filamu hiyo ya Mtoto wa Geti Kali utafanyika kila mahali atakapoenda kutambulisha albamu na video hiyo.
Alisema mwishoni watakaopatikana watashindanishwa kwa pamoja ili kupata kisura mmoja ambaye ndiye atakayekuwa mhusika mkuu wa filamu hiyo ambayo inatokana na wimbo wake uliowahi kutamba miaka ya nyuma wenyue jina hilo.
"Natarajia kuzindua video ya wimbo wangu mpya wa 'Hujachelewa' sambamba na kutambulisha albamu ya 'Sharubu za Babu'," alisema na kuongeza;
"Onyesho hilo litafanyika Machi 2, jijini Mbeya na litaenda sambamba na shindano la kusaka mrembo wa kucheza filamu yangu ya Mtoto wa Geti Kali na nitasindikizwa na wasanii kadhaa nyota wa jijini humo na wale wa Dar," alisema Inspekta Harun.
Msanii huyo alisema orodha ya watakaomsindikiza anatarajiwa kutangaza kesho ili kuwaweka tayari mashabiki wake kuwapokea vyema katika onyesho hilo la Jumapili.

Ikulu yabadilisha mwandishi wa hotuba za Rais

THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512, 2116898
              press@ikulu.go.tz             

Fax: 255-22-2113425

PRESIDENT’S OFFICE,
      THE STATE HOUSE,
              P.O. BOX 9120,  
DAR ES SALAAM.
Tanzania.
 
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
        Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Bwana Togolani I. Mavura kuwa Msaidizi wa Rais (Hotuba) kuanzia Februari 8, mwaka huu, 2014.
Taarifa iliyotolewa leo, Jumanne, Februari 25, 2014, mjini Dar Es Salaam na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue inasema kuwa Bwana Mavura anachukua nafasi ya Bwana Msafiri Marwa ambaye amehamishimiwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na kupangiwa kazi nyingine.
Kabla ya uteuzi huo, Bwana Mavura ambaye ni Ofisa wa Mambo ya Nje alikuwa Katibu wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
 “Mwisho”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
25 Februari, 2014

Azam warejea kileleni, Mwaikimba adhihirisha bado wamo!

MSHAMBULIAJI 'ngongoti' wa Azam, Gaudence Mwaikimba jana alidhihirisha kuwa bado wamo baada ya kuifungia timu yake mabao mawili na kuiwezesha kurejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakiishusha mabingwa watetezi Yanga.
Mwaikimba aliyewahi kutamba na Yanga, Kagera Sugar, Moro United, Tukuyu Stars na Ashanti, alifunga mabao hayo katika kila kipindi wakati Azam wakiizamisha Ashanti United kwa mabao 4-0 kwenye mechi pekee ya ligi hiyo iliyochezwa kwenye uwanja wa Chamazi jijini Dar.
Kwa muda mrefgu mchezaji huyo maarufu kama 'Andy Carroll' hakuwa akipangwa na makocha wa timu yake mbele ya washambuliaji mahiri wa timu hiyo, John Bocco 'Adebayor' aliye majeruhi na Kipre Tchetche anayetumikia kadi nyekundu na aliitumia nafasi aliyopewa na kocha Joseph Umog kwa kufunga mabao hao.
Mabao mengine ya Azam yaliwekwa kimiani na mabeki wake wa kati Aggrey Morris aliyefungwa kwa mkwaju wa penati lililokuwa bao la kwanza la timu hiyo na jingine likiwekwa wavuni na Said Morad na kuifanya Azma kufikisha pointi 40, mbili zaidi na ilizonazo Yanga yenye pointi 38 na kurejea tena kileleni.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea wikiendi kwa michezo kadhaa lakini pambano linalosubiriwa kwa hamu kubwa ni lile la Simba itakayoumana na Ruvu Shooting zote zikiwa na maumivu wa vipigo ilivyopewa katika mechi zao zilizopita, Simba ikilala kwa maafande wa JKT Ruvu kwa mabao 3-2 na Ruvu Shooting wakifumuliwa na Yanga kwa magoli 7-0.

Real Madrid 'yaua', Chelsea angalau Ligi ya Mabingwa Ulaya

Didier Drogba akionyesha manjonjo yaike mbele ya John Terry wa Chelsea jana ambapo timu zao zilitoka sare ya 1-1

Bale na Ronaldo wakipongezana wakati wakiiua Schalke 04 nyumbani kwao Ujerumani jan
REAL Madrid ikiwa katika kiwango cha hali ya juu msimu huu imevunja mwiko wa kushindwa kushinda kwenye ardhi ya Ujerumani baada ya usiku wa kuamkia leo kuifumua Schalke 04 kwa mabao 6-1 na kunusu hatua ya Robo Fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku Chelsea ya England ikibanwa ugenini na Galatasaray na kutoka sare ya 1-1 nchini Uturuki.
Mabao ya Karim Benzema katika dakika ya 13, kisha Gareth Bale kwenye dakika ya 21 yaliifanya Madrid kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 2-0 kabla ya kurudi kipindi cha pili wakiwa moto zaidi na kuongeza mabao mengine manne.
Cristiano Ronaldo alifunga bao dakika ya 52 kabla ya Benzema kurudi tena nyavuni dakika mbili baadaye na Bale kuongeza jingine dakika ya 69 na Ronaldo kumalizi udhia dakika ya 89.
Wenyeji waliambulia bao lao la kufutia machozi dakika moja ya nyongeza (90+1) kupitia kwa mdachi,  Klaas-Jan
Huntelaar na kuifanya Schalke 04 kuwa na kibarua kigumu cha kuweza kupata ushindi wa mabao 5-0 ugenini ili kuing'oa vinara hao wa Ligi ya Hispania.
Katika pambano jingine la kuhitimisha mechi za mkono wa kwanza za 16 Bora Chelsea ikiwa ugenini ilitangulia kuwafunga wenyeji kwa bao la Fernando Torres dakika ya 9 tu ya mchezo na kutoa matumaini huenda vinara hao wa Ligi ya England wangeibuka na ushindi ugenini na kuifuta machozi nchi yao ambayo imeshuhudia timu zake nyingine tatu zikifungwa katika mechi zake za mkondo huo.
Hata hivyo Chelsea walishindwa kulinda bao hilo kwani wenyeji Galatasaray walikuja kuchomoa bao dakika ya 65 kupitia kwa Mcameroon,  Aurélien Bayard Chedjou  aliyemalizia mpira wa kona uliochongwa na Mdachi Wesley Sneijder na mabeki wa Chelsea wakazembea kumkaba na kumfunga kirahisi kipa wao Petr Cech .

Wednesday, February 26, 2014

Tanzia! Nyota wa zamani Coastal afariki, kuzikwa leo Tanga

KWA niaba ya uongozi wa Coastal Union, tunatangaza msiba wa mchezaji wa zamani wa timu hii Bakari Jeki, pichani, aliefariki usiku wa kuamkia jana katika hospitali ya rufaa Bombo.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa kaka wa marehemu ndugu Ally Jeki, ndugu yetu aliugua kwa muda mfupi ambapo alilazwa katika hospitali ya Bombo wiki iliyopita mpaka mauti yalipomfika siku tatu baada ya kuanza kuugua.
Mwandisi wetu alizungumza na mchezaji wa zamani wa Coastal Union, ambae alipata bahati kumuona Bakari Jeki akiitumikia Coastal Union, Razak Yusuf ‘Careca’ ambae alibainisha kuwa marehemu alikuwa na mchango mkubwa katika timu.

“Coastal Union imekosa mtu muhimu katika soka ambae alikuwa msaada mkubwa akitoa mawazo, vilevile alikuwa hakosi katika mechi na mazoezi ya timu,” Careca.
Aidha beki namba tano wa zamani Coastal Union, Mzee Salim Amir ambae alicheza na marehemu katika michuano ya UFUMA, iliyoandaliwa na Chama Cha Soka nchini (FAT), ambao ulikuwa ni ushauri wa Rais wa kwanza wa Tanzania, Julius Nyerere.

Nyerere alitoa ushauri huo ili kuisaidia FAT iliyokuwa chini ya Said El Maamry, kuondokana na madeni. Michuano hiyo ikapewa jina la Operesheni Futa Madeni (OFUMA).
Ilishirikisha timu nne ambazo ni Simba (Dar es Salaam), Nyota (Mtwara), Coastal Union (Tanga) na Nyota Afrika (Morogoro), Coastal Union waliibuka mabingwa marehemu Bakari Jeki akiwa beki mbili na langoni alikuwa mdogo wake Said Jeki ambae pia alikuwa golikipa wa Taifa Stars.

Baadhi ya wachezaji waliokuwa katika kikosi kilichotwaa kombe la OFUMA, ambalo lilichezwa mara moja tu na kutoendelea tena ni Zacharia Kinanda, Mohammed Makunda, Bakari Rashid, Kuzu Mbwana, Salim Amir, Mohammed Salim, Zaharan Makame, Said Jeki na Mguruko.
“Alikuwa ni beki mzuri, Coastal Union ilinufaika na uchezaji wake kwani alicheza kwa moyo wote beki mbili ambayo ilipanda na kushuka bila kuchoka. Mbali na hayo aliishi vizuri na wenzake hakuwa mtu wa matatizo muda mwingi alipenda utani.

“Alinikuta mwaka1976 nikitokea Misri na timu ya Taifa, tukashiriki kombe la OFUMA tukiwa pamoja katika safu ya ulinzi lakini baadae nilistaafu baada ya kuumia, yeye aliendelea mpaka mwanzoni mwa miaka ya 1980 ndipo akaachana na soka, lakini hakuacha kuwa karibu na Coastal Union, muda mwingi alijitokeza kutoa ushauri na kila alipohitajika hakusita kuitikia mwito, huyo ndie Bakari Jeki ninaemfahamu,” alisema Salim Amiri.

Marehemu, alianza kucheza Coastal Union mwaka 1976 akitokea timu ya Magunia Moshi, alipotua Coastal Union alicheza kwa moyo wake wote mpaka alipostaafu soka, mpaka mauti yanamfika alikuwa kocha wa timu za mchangani mjini tanga na mshauri mkubwa wa benchi la ufundi Coastal Union.

Vilevile marehemu alitoka katika familia yenye vipaji vya soka kwani walikuwa ndugu watatu wa baba mmoja na mama mmoja ambapo Said Jeki alikuwa golikipa wa Coastal Union na timu ya Taifa, mwingine ni Hassan Jeki ambae alikuwa akichezea Reli Morogoro, lakini kwa sasa wote watatu ni marehemu.

Mwili wa Marehemu utatolewa Hospitali ya Rufaa Bombo mjini Tanga kuelekea nyumbani kwa kaka yake Ally Jeki maeneo ya Majengo, ifikapo saa tisa alasiri mwili wa marehemu utasaliwa katika msikiti wa Majengo kabla ya kupelekwa kijijini kwa Masuguru Wilayani Muheza Mkoani Tanga saa kumi alasiri.
Kaka wa marehemu hakuweka wazi kuhusu familia ya marehemu hasa upande wa mke ama watoto lakini alibainisha kuwa marehemu alizaliwa mwaka 1953 wilayani Muheza, Tanga. 
KWETU HANDENI

Yanga wapo kamili kuiua Al Ahly Jumamosi

Tegemeo la Tanzania michuano ya Afrika kwa sasa, Yanga
WAWAKILISHI pekee  wa Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga imeingia kambini katika hotel ya Laico Ledger iliyopo eneo la Bahari Bahari Beach Kunduchi  tayari kwa ajili ya pambano la Jumamosi dhidi ya ya Al Ahly kutoka Misri.
Mchezo huo wa Yanga dhidi ya Al Ahly utachezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Ofisa Habari wa Yanga Baraka Kizuguto alisema kikosi cha Yanga  chenye wachezaji 25 pamoja na benchi la Ufundi kilianza mazoezi juzi jioni katika Uwanja wa Kaunda Makao Makuu ya Klabu na jana asubuhi kimeendelea kujinoa katika Uwanja wa Boko Beach.
“Wachezaji wote wapo katika hali nzuri, mpaka sasa hakuna mchezaji majeruhi kuelekea mchezo huo,”alisema.

Alisema  Kocha  anatambua mchezo huo utakua ni mgumu, kwani Al Ahly wana uzoefu na michezo ya kimataifa lakini na wao wana malengo na zaidi  ni kufanya mapinduzi kwa kushinda
“Kwa vile Kocha anawafahamu Al Ahly  vizuri hakuna kitakachoshindikana kwasababu tayari tumepata  mbinu zao kutoka kwa  Kocha Msaidizi Boniface Mkwasa, kilichobaki ni kuwaandaa wachezaji kiakili,”alisema.

Katika mchezo huo, Mshambuliaji wa Kimataifa Emanuel Okwi atakuwa ni miongoni mwa wachezaji tegemeo katika kikosi kitakachotua dimbani siku hiyo. Kizuguto alithibitisha ushiriki huo kwa kuonyesha leseni yake iliyotoka Shirikisho la Soka Afrika(CAF) .



Al Ahly imewasili leo alfajiri saa 12 kasorobo kwa Shirika la Ndege la Misri Egypt Air kikiwa na watu 35 wakiwemo wachezaji 22, bechi la Ufundi 8 pamoja na viongozi 5 na wamefikia katika Hotel ya Hyatt Kempsinki ambapo ndio itakuwa ikiweka kambi.

Siku ya Jumatano na Alhamisi  jioni watafanya mazoezi katika Uwanja wa IST uliopo Upanga, na Ijumaa jioni watapata fursa ya kufanya mazoezi katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam tayari kwa mchezo huo wa Jumamosi.


Tiketi zitauzwa kwenye vituo mbalimbali kuanzia Ijumaa ambapo kiingilio cha juu ni  Shs 35,000,  25,000,  13,000 na cha chini kwa viti vya kijani na bluu ni Sh. 7000.

Rekodi ya Al Ahly:
Wana mataji 19 moja zaidi ya mataji 18 ya Ac Milan
Imeshinda mara 8 kombe la mabingwa barani Afrika, mwaka 1982,1987,2001,2005,2006, 2008, 2012, na 2013. Makombe 4 ni ubingwa wa Kombe la washindi 1984,1985,1986, 1993.

Mara sita imetwaa kombe la CAF Super Cup 2002, 2006,2007,2009, 2013, na 2014 na mmoja likiwa la Afro-Asian Cup mwaka 1988.

Shepolopolo kutua kesho kuivaa Twiga Stars Ijumaa


Timu ya Taifa ya Zambia (Shepolopolo) inatua nchini kesho mchana (Februari 27 mwaka huu) kwa ajili ya mechi ya marudiano ya michuano ya Afrika kwa Wanawake (AWC) dhidi ya Tanzania (Twiga Stars) itakayochezwa keshokutwa (Februari 28 mwaka huu).

Shepolopolo yenye msafara wa watu 29 itawasili kwa ndege ya Fastjet ikitokea Lusaka na itafikia kwenye hoteli ya Accomondia kwa ajili ya mechi hiyo itakayochezwa Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi kuanzia saa 10 kamili jioni.

Waamuzi wa mechi hiyo kutoka Burundi wakiongozwa na Ines Niyosaba wamewasili nchini leo asubuhi wakati Kamishna Fran Hilton-Smith kutoka Afrika Kusini atawasili kesho (Februari 27 mwaka huu) saa 8 kamili mchana kwa ndege ya South African Airways.
Katika hatua nyingine Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi atakuwa na mkutano na waandishi wa habari juu ya benchi la ufundi la timu ya Taifa ya wakubwa (Taifa Stars).

Mkutano huo utafanyika kesho (Februari 27 mwaka huu) saa 4 asubuhi kwenye ofisi za TFF zilizopo ghorofa ya 3 katika Jengo la PPF Tower, mtaa wa Garden na Ohio.

Symbion kusaidia programu za vijana za TFF


SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Symbion Power Tanzania Limited zimesaini makubaliano ambapo kampuni hiyo itasaidia kwenye maeneo matatu ya mpira wa miguu wa vijana.
Makubaliano hayo yametiwa saini leo (Februari 26 mwaka huu) kwenye ofisi za TFF jijini Dar es Salaam. Rais wa TFF, Jamal Malinzi amesaini kwa niaba ya shirikisho wakati upande wa Symbion aliyesaini ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo Peter Gathercoles.
Maeneo ambayo Symbion itasaidia ni ujenzi wa vituo viwili vya kuendeleza vipaji vitakavyojengwa Kidongo Chekundu na Kinondoni mkoani Dar es Salaam, mashindano ya Taifa ya wachezaji wenye umri wa chini ya miaka 12 (U12) yatakayofanyika mwaka huu na kuisaidia timu ya U17 ya Tanzania (Serengeti Boys).
Serengeti Boys itacheza na Afrika Kusini, Julai mwaka huu katika mechi za mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa wachezaji wa umri huo zitakazofanyika mwakani nchini Niger.
Hivyo Symbion imetoa dola 60,000 (zaidi ya sh. milioni 96) kwa ajili ya mashindano ya U12, na dola 50,000 (zaidi ya sh. milioni 80) kwa ajili ya maandalizi ya Serengeti Boys kwa mechi dhidi ya Afrika Kusini.
Rais Malinzi ameishukuru Symbion kwa kukubali kushirikiana na TFF katika mpira wa miguu wa vijana, lakini vilevile amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete kwani ndiye chachu ya kampuni hiyo kuamua kujishirikisha na mpira wa miguu wa vijana.

Ushawahi kula Kuku mwenye ngozi nyeusi tii?!


Kuku weusi
Aina kadhaa za kuku weusi  hupatikana barani Asia, lakini  kuku au ndege aina ya Silkie wa huko China, ndiyo maarufu zaidi.  Ndege hao, kama majina yao yalivyo, huwa wana manyoya yanayofanana na hariri.
Hata hivyo, chini ya uzuri wote huo, ndege hao wana ngozi nyeusi tii!  Ndege hao huuzwa katika nchi za magharibi kama mapambo, ambapo nchini China ni kitoweo cha hali ya juu kwani nyama yake  hupendwa sana.  Pia ndege hao huchukuliwa kama ‘mama wema’ kwani wanaweza kuatamia mayai ya ndege wengine bila kinyongo.
Black-Chicken
Wachina huwaelezea ndege hao kama “kuku wenye mifupa myeusi” au  “wu gu ji” na wamekuwa wakiwala kwa kuamini nyama yao ina tiba tangu karne ya saba au ya nane ambapo wanawake huila kwa ajili ya kuimarisha afya zao baada ya kujifungua. 
 Pia nyama hiyo inaaminika kuimarisha mapafu, tumbo na damu ikiliwa.  Wachina huitumia nyama ya ndege hao kwa kutengeneza supu yake na kuichanganya na viungo na matunda mbalimbali kwa ajili ya tiba.

Utafiti uliofanywa na kuchapishwa mwaka 2011 ulionyesha kwamba hali hiyo ya kipekee ya ndege hao aina ya Silkie ambayo inajulikana kama ‘fibromelanosis’ inatokana na mabadiliko katika jeni.  Mabadiliko hayo kisayansi  huenda sambamba na kuongezeka kwa chembechembe za  rangi ambazo huzifanya sehemu za ndani (mwilini) na mifupa kuwa nyeusi.

Ndege hao pia wana chembechembe za aina ya ‘carnosine’ ambazo huongeza nguvu mwilini.  Watu wenye kutaka kuongeza ukubwa wa misuli huwatumia kwa wingi kwa nia hiyo na kama chakula chenye kuleta nguvu.  Pia hutumika katika kupambana na ugonjwa wa akili wa watoto (autism), kisukari na kupambana na matatizo yanayotokana na uzee.
 
Kwa jumla ndege hao hutumiwa kama tiba ya maumivu ya viungo na kuzuia ugonjwa wa akili ujulikanao kama Alzheimer.
 
Kwa mujibu wa  utafiti wa kisayansi kuhusu kuku nchini Uingereza, mayai ya kuku weusi  ni bora kwa afya hasa yakitumika katika kupika keki.  Yakilinganishwa na mayai mengine, mayai ya kuku weusi yana kiwango kidogo cha tindikali  katika mafuta yake. 
 
 Kwa waliowahi kuila nyama yake, wanasema ina ladha kama ya kuku wa kawaida, lakini baadhi hudai ni tamu zaidi.  Je, ungependa kula nyama ya Silkie ili ufahamu utamu.
Credit:KALUNDE

Ivo Mapunda apatwa pigo zito, afiwa na baba

KIPA namba moja Tanzania, Ivon Philip Mapunda amefiwa na baba yake mzazi Mzee Philip Mapunda jana jioni na anatarajiwa kuzikwa kesho kijijini kwao, Tukuyu Mbeya.
Kipa huyo wa Simba SC, Ivo ameiambia BIN ZUBEIRY leo asubuhi kwamba, Mzee Mapunda aliyekuwa ana umri wa miaka 86 amefariki akiwa katika hospitali ya Ikonda, iliyopo Njombe ambako alikuwa amelazwa kwa takriban miezi miwili na nusu.
Pole mpiganaji; Ivo Mapunda amefiwa na baba yake mzazi jana 

Ivo alisema Mzee Mapunda alikuwa anasumbuliwa na maradhi ya kibofu cha mkojo, sukari na vidonda vya tumbo. 
Ivo aliyekuwa akizungumza akiwa njiani kuelekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam, amesema mwili wa marehemu kwa sasa upo kijijini Tukuyu tangu usiku wa jana. Pole Ivo na famili yake. Mungu ampumzishe kwa amani Mzee Mapunda.
BIN ZUBEIRY

Jahazi la Manchester Utd lazama Ugiriki, Chelsea kazi leo Uturuki

50/50: Olympiacos' Leadro Salino (left) fights with United's Ashley Young
Manchester Utd walipokuwa wakihenyeshwa uwanjani jana
Nowhere to be seen: United were outplayed in every area in Greece on Wednesday night
Wachezaji wa Manchester United wakiwa hawaamini kilichjowakuta Ugiriki jana
JAHAZI la Manchester United bado linaendelea klukumbwa na dhoruba baada ya usiku wa jana kukubali kipigo cha mabao 2-0 ugenini dhidi ya Olympiacous ambayo ipo kwenye kiwango cha juu.
Kipigo hicho ni cha kwanza kwa Mashetani Wekundu kwa timu hiyo ya Ugiriki katika miaka minne iliyopita kwani Olympiacous ilikuwa haijawahi kuifunga Manchester Utd katika michuano ya kimataifa.
Vijana wa David Moyes,  walishindwa kuhimili vishindo vya vinara hao wa Ligi Kuu ya Ugiriki, kwa kufungwa mabao hayo moja kila kipindi na kupata kibarua kigumu cha kushinda nyumbani kwao kwa mabao 3-0.
Mabao yaliyoiangamiza Manchester Utd na kutimiza tambo za kocha wa timu hiyo ya Ugiriki kwamba wangeshinda mchezo huo, yalifungwa na Alejandro Dominguez aliyefunga dakika ya 38 kabla ya nyota wa Arsenal anayecheza kwa mkopo Olympiacos, Joel Campbell kumaliza udhia katika dakika ya 55.
Kipigo cha Mashetani Wekundu imekuwa kama muendelezo wa aibu kwa timu za England katika hatua hiyo ya 16 baada ya wiki iliyopita Arsenal na Manchester City kufungwa idadi kama hiyo nyumbani na timu za Bayern Munich na Barcelona.
Timu nyingine ya England Chelsea leo itajaribu bahati yake kwa kuvaana na Galatasaray uwanja wa ugenini nchini Uturuki, huku mechi nyingine ya leo ni ile ya Schalke 04 itakayoikaribisha Real Madrid.
Katika mechi nyingine ya mapema jana,  wenyeji Zenit ya Urusi ilifumuliwa mabao 4-2 na wanafainali wa mwaka jana Borussia Dotmund ya Ujerumani ambapo hadi mapumziko walikuwa nyuma 2-0.
Mabao yaliyoiweka Dotmund katika nafasi ya kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa ya mwaka huu yalifungwa na Mkhitaryan, Reus kabla ya Robert Lewandowski kufunga mawili na wenyeji yaliwekwa kimiani na Shatov na Hulk.

Azam, Ashanti United hapatoshi leo Chamazi

Ashanti United

Azam Fc
LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inaendelea leo kwa pamoja moja tu kati ya Azam itakayoumana na Ashanti United kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam.
Azam yenye pointi 37 itakutana na Ashanti yenye pointi 14 ikiwa na kumbukumbu ya kulazimishwa sare ya 2-2 na Prisons na kushindwa kurejea kwenye kilele cha msimamo wa ligi hiyo inayoongozwa kwa sasa na Yanga yenye pointi 38.
Ushindi wowote itakayoupata leo itairejesha Azam katika kiti cha uongozi, japo Ashanti siyo timu ya kubeza kwani katika mechi yao ya mkondo wa kwanza walitoshana nguvu ya kutoka sare ya 1-1.
Katika mechi iliyopita Ashanti inayonolewa na King KIbadeni ilifumuliwa mabao 2-1 na Mtibwa Sugar na pia ipo kwenye nafasi mbaya ya kushuka daraja ikiwa nafasi ya 13 juu ya Rhino Rangers inayoburuza mkia.
Bila shaka pambano hilo litakuwa kali kwa kila timu kutaka kupata ushindi ili kujiweka pazuri katika nafasi walizopo Azam kukwea kileleni, Ashanti kuondoka mkiani.
Wakati huo huo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limewaagiza wanachama wake- vyama vya mpira wa miguu vya mikoa kuwapatia orodha ya klabu zote za mpira wa miguu zilizosajiliwa katika mikoa yao.
Orodha hiyo inatakiwa kujumuisha namba ya usajili wa klabu, viongozi waliopo madarakani kwa sasa pamoja na mawasiliano yao (namba za simu na anuani za email) na eneo yalipo makao ya klabu husika.
Kwa utaratibu huo, vyama vya mikoa vitakusanya taarifa za klabu zinazocheza ligi ya mikoa, lakini wakati huo vinatakiwa kuwasiliana na wanachama wake (vyama vya wilaya) kupata taarifa za klabu zinazocheza ligi za wilaya na baadaye kuziwasilisha TFF.
Klabu ambazo taarifa zake zitakuwa hazijawasilishwa TFF hadi Agosti mwaka huu hazitaruhusiwa kushiriki ligi ya msimu wa 2014/2015 katika ngazi yoyote ile.
Naye Rais wa TFF, Jamal Malinzi atakuwa na mkutano na waandishi wa habari juu ya programu ya mpira wa miguu kwa vijana.
Mkutano huo utafanyika kesho (Februari 26 mwaka huu) saa 5 asubuhi kwenye ofisi za TFF zilizopo ghorofa ya 3 katika Jengo la PPF Tower, mtaa wa Garden na Ohio.

Kaseja atemwa Taifa Stars, 22 waitwa kuivaa Namibia

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limetangaza kikosi cha wachezaji 22 kwa ajili ya mechi ya kirafiki ya kalenda ya FIFA dhidi ya Namibia (Brave Warriors) itakayochezwa Machi 5 mwaka huu jijini Windhoek, Namibia, ndani yake wakiwemo wachezaji sita wa Yanga SC.
Hata hivyo kipa tegemeo na nahodha wa zamani wa timu hiyo, Juma Kaseja akiwa ameachwa nje.
Kikosi hicho kilichotangazwa na TFF badala ya kocha mkuu wa timu hiyo, Kim Poulsen na kuashiria kupewa 'mkono wa kwaheri' kwa kocha huyo kutoka Denmark na kitakachoingia kambini Machi Mosi na kuondoka nchini Machi 3 kwenda kuivaa wenyeji wao ni pamoja na makipa watatu ambao ni  Deogratius Munishi (Yanga), Ivo Mapunda (Simba) na Mwadini Ally (Azam). 
Wengine waliotajwa ni mabeki wa pembeni ni Edward Charles (JKT Ruvu), Erasto Nyoni (Azam), Hassan Mwasapili (Mbeya City) na Michael Aidan (Ruvu Shooting).
Mabeki wa kati ni Aggrey Morris (Azam) na Kelvin Yondani (Yanga) wakati viungo ni Amri Kiemba (Simba), Athuman Idd (Yanga), David Luhende (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Jonas Mkude (Simba) na Mwinyi Kazimoto (Markhiya Sports Club, Qatar).
Washambuliaji ni Athanas Mdamu (Alliance Mwanza), Haruna Chanongo (Simba), Khamis Mcha (Azam), Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), Mrisho Ngasa (Yanga), Ramadhan Singano (Simba) na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC).
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itaingia kambini Machi 1 mwaka huu, kwenye hoteli ya Accommondia inatarajiwa kuondoka Machi 3 mwaka huu kwenda Windhoek.
TFF imesema wachezaji ambao timu zao zinacheza mechi za mashindano ya kimataifa na ligi wikiendi hii wataripoti kambini mara baada ya mechi zao kumalizika.

Kuziona Yanga na Al Ahly Buku 7 tu

http://gatemedia.ahram.org.eg/english/News/2012/10/29/2012-634871100531794113-179.jpg
Al Ahly ya Misri
Yanga ya Tanzania
WAKATI Al Ahly wakitua nchini leo, viingilio vya pambano mkondo wa kwanza raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya watetezi hao kutoka Misri na Yanga litakalofanyika Jumamosi hii uwanja wa Taifa, Dar es Salaam huku kile cha chini kabisa kitakuwa ni Sh. 7,000.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na klabu ya Yanga ni kwamba watu watakaoketi jukwaa la viti vya rangi ya Chungwa, wakati VIP A tiketi moja itauzwa kwa Sh. 35,000 na kwa viti vya VIP B na C Sh. 25,000.
Na kwamba wapinzani wa yaani Al Ahly wanatarajiwa kuwasili asubuhi hii na watafikia katika hoteli ya Hyatt Regency, Kempinsky au Kilimanjaro Hotel, iliyopo maeneo ya Kivukoni.
Waarabu hao wanaweza kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Gymkhana, uliopo kando ya bahari ya Hindi na kikosi wanachotarajiwa kuja nacho Dar es Salaam ni makipa; Sherif Ekramy, Ahmed Adel Abdel-Monem na Mahmoud Abou El-Sooud.
Mabeki ni; Wael Gomaa, Sherif Abdel-Fadil, Ahmed Fathi, Mohamed Naguib, Saad El-Din Samir, Sayed Moawad na Ahmed Shedid Qenawy.
Viungo ni; Hossam Ashour, Shehab El-Den Ahmed, Ahmed Nabil Manga, Ahmed Shokry, Mahmoud ‘Trezeguet’, Rami Rabia, Walid Soliman, Abdullah El-Said na Mohamed Abou-Treika na washambuliaji El-Sayed Hamdy, Dominique  Da Silva, Emad Meteb na Amr Gamal ambaye ndiye tegemeo la mabao la timu hiyo kwa sasa.

Tuesday, February 25, 2014

Ajali tena! Watu watano wafa Kilimanjaro, wanne taaban


PIcha hii haihusiki na habari hii, ila ni kati ya ajali ambazo zimekuwa zikichukua roiho za watanzania wenzetu kila uchao
AJALI za barabarani zimeendelea kuteketeza roho za watanzania baada ya watu watano kufariki katika ajali iliyohusisha magari mawili katika eneo la Boma Ng'ombe wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.
Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa na jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro, watu hao walifariki jana jioni katika njia ya mzunguko ya uwanja wa ndege wa kimataifa ya KIA ikihusisha magari mawili yaliyogongana ubavuni ambapo watu wengine wanne walijeruhiwa.
Inadaiwa mwendo kasi ya magari hayo ndiyo yaliyosababisha vifo vya watu hao watano wakiwamo wanaume watatu na wanawake wawili ambao miili yao iliharibika.
Abiria wanne walionusurika kufa wapo katika hali mbaya na wamelazwa katika hospitali ya mkoa ya Maweni kwa ajili ya matibabu.

Man Utd kuvuna nini Ugiriki katika UEFA Champion League?!


ATHENS, Ugiriki
KIVUMBI cha Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA Champion League) kinatarajiwa kuendelea tena leo na kesho kwa mechi nne za kumalizia mkondo wa kwanza wa hatua ya 16 Bora kuwania kucheza Robo Fainali ya michuano hiyo.
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya England, Manchester United ambayo imefufuka kwenye ligi ya nyumbani leo itakuwa ugenini nchini Ugiriki kuvaana na Olympiakos Piraeus wiuki moja baada ya timu za Manchester City na Arsenal kupoteza mechi zao za nyumbani dhidi ya Barcelona na Bayern Munich.
Mechi nyingine ya leo itazikutanisha timu za Zenit St Petersburg dhidi ya wana fainali wa mwaka jana,  Dortmund ya Ujerumani.
Katika mechi ya Manchester United dhidi ya Olympiakos Piraeus, wagiriki hao hawajawahi kufanya vyema mbele ya Mashetani Wekundu, japo wenyewe wamenukuliwa wakiapa kwamba piga ua leo ni lazima waigaragaze vijana wa David Moyes.
Mashetani Wekundu waliopata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Crysral Palace kwenye mechi yao ya ligi mwishoni mwa wiki, itahitaji kufanya vyema leo ugenini ili kufufua matumaini ya timu za England kuvuka katika hatua hiyo.
Hata hivyo itakuwa na kazi ngumu kuhakikisha wanaifunga  vinara hao wa Ligi Kuu ya Ugiriki ambao wamefika hatua hiyo ya mtoano kwa mara ya kwanza ndani ya kipindi cha miaka minne.
Wagiriki hao wataweka historia kama wataifunga United baada ya kupoteza mara nne katika michuano ya hivi karibuni ilipokutana nayo.
Hata hivyo, kwa sasa Olympiakos Piraeus ipo katika kiwango kizuri baada ya kucheza mechi 26 za ligi bila kupoteza huku ikiongoza kileleni mwa Ligi Kuu ya Ugiriki maarufu kama Super League.
Wakati United Jumamosi ikishinda 2-0 dhidi ya Crystal Palace, Olympiakos iliichapa OFI Crete mabao 4-0 huku Mserbia Marko Scepovic aliyesajiliwa hivi karibuni akifunga mara tatu ‘hat-trick’ yake ya kwanza katika maisha yake kisoka.
"Ningependa kuona hali kama hii, na hamu ya wachezaji wangu dhidi ya United kama walivyoonyesha dhidi ya OFI," kocha Michel alisema wakati timu yake ikipata ushindi wa 24 katika mechi 26 za ligi ilizocheza.
"Kila mechi tunakabiliana nayo kwa umakini sana na tunaamini tutapata matokeo mazuri sana Jumanne (leo)," alisema mshambuliaji huyo wa zamani na wa Real Madrid na Hispania ambaye kwa sasa ana miaka 50.
"Tumegeuza ukurasa mpya na akili zetu sasa tunazielekeza katika Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya United, ninaweza kuona hamu ndani ya macho na katika sura ya wachezaji wangu; wako tayari kwa hilo," aliahidi katika ukurasa wake wa Facebook juzi.
Michel atawakosa baadhi ya wachezaji wake wakongwe baada ya mshambuliaji wa zamani wa Argentina Javier Saviola kuwa majeruhi wa mguu. Kukosekana kwa Saviola inamaana Mnigeria Michael Olaitan mwenye miaka 21 kwa sasa, ambaye amefunga mabao nane katika mechi 15 alizocheza, atapata nafasi ya kuanza sambamba na kiungo mshambuliaji wa Argentina Alejandro Dominguez atakayecheza nyuma yake.
United imesafiri kwenga Ugiriki hiyo ikiwa nafasi pekee kwao msimu huu ya kutwaa kombe lakini hata hivyo matarajio hayo ni madogo sana kwa ubora wao kwa sasa.
Katika mechi hiyo, United itakuwa ikimtegemea zaidi Wayne Rooney (pichani) aliyepewa mkataba mnono wa paundi 300,000 kwa wiki huku akifunga bao safi mwishoni mwa wiki.
Pia, kocha David Moyes atakuwa na uwanja mpana zaidi wa kumjumuisha Marouane Fellaini katika kikosi chake cha kwanza baada ya kuwa majeruhi kwa muda mrefu.
Juu ya pambano la Zenit dhidi ya Dotmund, mashabiki wa timu ya Ujerumani watapewa ofa ya chai na vitafunwa kwa Zenit St Petersburg leo, lakini ukarimu huo hautakuwapo dimbani kwani miamba hiyo ya Urusi imepania kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza.
Kocha wa Zenit, Luciano Spalletti anafurahia kiwango cha timu yake kwa sasa; "Tumecheza Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa muda mrefu sasa, na tumepigana vema msimu huu. Tumekuwa na wachezaji wengi bora jambo linalomaanisha tunaweza kucheza kwa kiwango hiki."
Aliongeza: "Tulitoka sare nyumbani na Porto tulipopaswa kushinda, na ilikuwa hali kama hiyo dhidi ya Austria Vienna, tulipocheza tukiwa 10 uwanjani zaidi ya sasa moja.
"Tulipaswa kunyakua pointi nyingi zaidi, lakini kwa ujumla tunaweza kuwa na furaha kwa kiwango chetu."
Dortmund ilisonga mbele baada ya kuwa kinara wa kundi lao lilokuwa likizijumuisha Napoli, Arsenal na Olympique Marseille kwa kufikisha pointi 12 sawa na vijana wa Arsene Wenger na wa Rafa Benitez lakini wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa ndiyo yaliyoibeba miamba hiyo ya Ujerumani ambayo msimu huu haitisha kwenye ligi ya nyumbani.
Baada ya kutwaa ubingwa wa Bundesliga 2011 na 2012 na kumaliza ya pili msimu uliopita, imekuwa ikipanda na kushuka msimu huu na kwa sasa inashika nafasi ya tatu.
Jumamosi ilipata kipigo kikubwa zaidi ugenini msimu huu baada ya kuchapwa 3-0 na Hamburg SV lakini kocha Juergen Klopp anaamini watafanya vizuri leo.
"Tumewahi kufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kufanya vibaya kwenye ligi ya nyumbani," alisema.
"Ni mashindano tofauti kabisa," aliongeza kiungo Nuri Sahin. "Tutajiandaa vema huko St Petersburg na tunahitaji kupata matokeo mazuri na kurudi nayo Dortmund."