STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, February 26, 2014

Azam, Ashanti United hapatoshi leo Chamazi

Ashanti United

Azam Fc
LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inaendelea leo kwa pamoja moja tu kati ya Azam itakayoumana na Ashanti United kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam.
Azam yenye pointi 37 itakutana na Ashanti yenye pointi 14 ikiwa na kumbukumbu ya kulazimishwa sare ya 2-2 na Prisons na kushindwa kurejea kwenye kilele cha msimamo wa ligi hiyo inayoongozwa kwa sasa na Yanga yenye pointi 38.
Ushindi wowote itakayoupata leo itairejesha Azam katika kiti cha uongozi, japo Ashanti siyo timu ya kubeza kwani katika mechi yao ya mkondo wa kwanza walitoshana nguvu ya kutoka sare ya 1-1.
Katika mechi iliyopita Ashanti inayonolewa na King KIbadeni ilifumuliwa mabao 2-1 na Mtibwa Sugar na pia ipo kwenye nafasi mbaya ya kushuka daraja ikiwa nafasi ya 13 juu ya Rhino Rangers inayoburuza mkia.
Bila shaka pambano hilo litakuwa kali kwa kila timu kutaka kupata ushindi ili kujiweka pazuri katika nafasi walizopo Azam kukwea kileleni, Ashanti kuondoka mkiani.
Wakati huo huo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limewaagiza wanachama wake- vyama vya mpira wa miguu vya mikoa kuwapatia orodha ya klabu zote za mpira wa miguu zilizosajiliwa katika mikoa yao.
Orodha hiyo inatakiwa kujumuisha namba ya usajili wa klabu, viongozi waliopo madarakani kwa sasa pamoja na mawasiliano yao (namba za simu na anuani za email) na eneo yalipo makao ya klabu husika.
Kwa utaratibu huo, vyama vya mikoa vitakusanya taarifa za klabu zinazocheza ligi ya mikoa, lakini wakati huo vinatakiwa kuwasiliana na wanachama wake (vyama vya wilaya) kupata taarifa za klabu zinazocheza ligi za wilaya na baadaye kuziwasilisha TFF.
Klabu ambazo taarifa zake zitakuwa hazijawasilishwa TFF hadi Agosti mwaka huu hazitaruhusiwa kushiriki ligi ya msimu wa 2014/2015 katika ngazi yoyote ile.
Naye Rais wa TFF, Jamal Malinzi atakuwa na mkutano na waandishi wa habari juu ya programu ya mpira wa miguu kwa vijana.
Mkutano huo utafanyika kesho (Februari 26 mwaka huu) saa 5 asubuhi kwenye ofisi za TFF zilizopo ghorofa ya 3 katika Jengo la PPF Tower, mtaa wa Garden na Ohio.

No comments:

Post a Comment