STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, March 17, 2013

Mario Balotelli aendelea kung'ara Italia

Mario Balotelli 'Super Mario'

MSHAMBULIAJI  wa Italia, Mario Balotelli 'Super Mario' ameendelea kuonyesha makali yake ya kufumania nyavu kwenye Ligi Kuu ya Seria A baada ya jioni hii kuifungia timu yake ya Ac Milan magoli mawili wakiizima Palermo 2-0 katika mfululizo wa ligi hiyo.
Balotelli aliyetua Milan akitokea Manchester City ya Uingereza, alifunga mabao hayo katika kila kipindi bao la kwanza akilipachika kwa njia ya mkwaju wa penati dakika ya nane tu ya pambano hilo lililochezwa kwenye dimba la San Siro mjini Milan.
Kuonyesha kuwa kwa sasa yeye ni nguzo ya Milan iliyotolewa kimaajabu kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa ya Ulaya na Barcelona waliowafunga mabao 4-0 katika mechi ya marudiano na kuzima ndoto zao za kutinga robo fainali baada ya awali kushinda magoli 2-0, Balotelli aliongeza bao la pili dakika ya 66.
Katika mechi nyingine za ligi hiyo inayoongozwa na vinara Juventus, Siena ikiwa nyumbani ilibanwa mbavu na Cagliari kwa kulazimishwa suluhu ya kutofunga, Napoli waliendelea kuwafukuzia mabingwa watetezi Juve kwa kupata ushindi wa magoli 3-2 nyumbani dhidi ya Atalanta, huku Chievo Verona wakiwa ugenini waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 mbele ya wenyeji wa Pescara na Fiorentina iliichapa Genoa magoli  3-2.

HIZI NDIZO SILAHA ZA AZAM MJINI MONROVIA JIONI HIIWachezaji wa Azam wakijifua mjini Monrovia, Liberia


Photo: Maandalizi Monrovia
Wachezaji wa Azam wakijifua nchini Liberia

KOCHA Mkuu wa klabu ya Azam, wawakilishi pekee wa Tanzania katika michuano ya kimataifa, Stewart Hall ametangaza silaha zake zitakazoshuka dimbani jioni hii katika pambano lao dhidi ya wenyeji wao Barrack YC II kuwania taji la Kombe la Shirikisho Afrika.
Kwa mujibu wa akaunti ya klabu ya Azam, ambao watashuka dimbani saa 1 jioni kwa saa za Afrika Mashariki sawa na saa 10 jioni za Monrovia, golini kama kawaida atakuwa Mwadini Ali akisaidiwa na 'kiraka' Himidi Mao na Waziri Salum upande wa kushoto na mabeki wa kati watakuwa David Mwantika na Jockins Atudo.
Dimba la kati lenyewe litashikiliwa na Michael Balou  na Ibrahim Mwaipopo, huku Kipre Tchetche John Bocco, Humphrey Mieno na Mcha Khamis 'Vialli' wataongoza safu ya ushambuliaji.
Kikosi kamili cha Azam ambacho kimeapa kufa na kupona kuweza kuitoa kimasomaso Tanzania baada ya kupoteza wawakilishi wake wengine ni kama kifuatavyo;
Mwadini Ali, Himidi Mao, Waziri Salum, David Mwantika, Jockins Atudo, Michael Bolou, Kipre Tchetche, Ibrahim Mwaipopo, John Bocco, Humphrey Mieno, Mcha Khamis.

Wachezaji wa akiba;  Aishi Salum, Malika Ndeule, Luckson Kakolaki, Abdulhalim Humud, Abdi Kassim, Jabir Aziz, Seif Karihe.

Mapinduzi Simba! Wanachama wamng'oa Rage

HABARI zilizotufikia hivi punde zinasema kuwa Mkutano wa Dharura ulioitishwa na wanachama wa klabu ya Simba umeung'oa uongozi wa juu wa klabu hiyo unaoongozwa na Mwenyekiti Ismail Aden Rage aliyepo kwenye matibabu nchini India.
Habari hizo zinasema maamuzi hayo yamefikiwa kwenye mkutano huo uliofanyika na kumalizika mchana huu kwenye ukumbi wa Starlight Mnazi Mmoja, Dar es Salaam na kukabidhi majukumu ya klabu kwa kamati maalum inayoongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Usajili, Zakaria Hanspope na Rahma Al Kharoos.
Hanspope na Bi Rahma maarufu kama Malkia wa Nyuki wataiongoza Simba mpaka pale utakapofanyika uchaguzi mkuu wa kupata viongozi wapya wa klabu hiyo.
Taarifa kamili juu ya mkutano huo tunazifuatilia kwa kuwa MICHARAZO haikuhabatika kuwepo ukumbini hapo na tutawajulisha hivi punde.

Waangola kuzihukumu Stars na Morocco J'pili


Na Boniface Wambura
SHIRIKISHO la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limeteua waamuzi kutoka Angola kuchezesha mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Morocco (Lions of the Atlas).

Mechi hiyo ya kundi C itachezwa Machi 24 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Ivory Coast ndiyo inayoongoza kundi hilo ikiwa na pointi nne na kufuatiwa na Taifa Stars yenye pointi tatu.

Mwamuzi wa mechi hiyo ni Helder Martins de Carvalho wakati mwamuzi msaidizi namba moja ni Inacio Manuel Candido huku Ricardo Daniel Cachicumi akiwa mwamuzi msaidizi namba mbili. Mwamuzi wa mezani (fourth official) ni Antonio Muachihuissa Caxala.

Waamuzi hao watawasili nchini saa 1.20 usiku Machi 22 mwaka huu kwa ndege ya Kenya Airways wakitokea Luanda, Angola kupitia Nairobi, Kenya.

Kamishna wa mechi hiyo atakuwa David Fani kutoka Botswana anatarajiwa kuwasili Machi 22 mwaka huu saa 1.45 usiku kwa ndege ya South African Airways.

Naye mtathmini wa waamuzi (referee assessor) Neermal Boodhoo kutoka Afrika Kusini atawasili nchini Machi 22 mwaka huu 1.45 usiku kwa ndege ya South African Airways.

Yanga, Ruvu Shooting wavuna Mil 62Na Boniface Wambura

PAMBANO la  Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Ruvu Shooting na Yanga lililochezwa jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam limeingiza sh. 62,228,000 kutokana na watazamaji 10,929.

Viingilio katika mechi hiyo namba 146 iliyomalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0 vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 14,336,764.95 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 9,492,406.78.

Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 7,289,880.48, tiketi sh. 4,136,390, gharama za mechi sh. 4,373,928.29, Kamati ya Ligi sh. 4,373,928.29, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 2,186,964.14, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) sh. 850,486.06 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 850,486.06.

Stars waingia kambini kuiwinda Morocco


Na Boniface Wambura
TIMU ya soka ya taifa, Taifa Stars imeanza kambi jana jioni (Machi 16 mwaka huu) ambapo wachezaji 14 kati ya 23 walioitwa wameripoti na kufanya mazoezi leo asubuhi chini ya Kocha Kim Poulsen.

Wachezaji walioripoti ni nahodha Juma Kaseja kutoka Simba na msaidizi wake Aggrey Morris wa Azam, Erasto Nyoni (Azam), Kelvin Yondani (Yanga), Nadir Haroub (Yanga), Nassoro Masoud Cholo (Simba), Shomari Kapombe (Simba) na Salum Abubakar (Azam).

Wengine ni Athuman Idd (Yanga), Amri Kiemba (Simba), Frank Domayo (Yanga), Mwinyi Kazimoto (Simba), Mrisho Ngasa (Simba) na Simon Msuva (Yanga).

Wachezaji Hussein Shariff, Issa Rashid na Shabani Nditi ambao timu yao ya Mtibwa Sugar jana ilicheza mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) mjini Turiani wataripoti kambini leo jioni.

Kikosi hicho kitakamilika Jumanne asubuhi baada ya wachezaji walio katika kikosi cha Azam nchini Liberia kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho kurejea nchini. Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaochezea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemorasi ya Congo (DRC) wanatarajiwa kutua nchini kesho usiku.

Kila la heri Azam mkisaka heshima Afrika

Kikosi cha Azam

Furaha ya Ushindi: Azam tuypeni raha kama hivi hata mkiwa ughaibuni
WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya kimataifa, Azam jioni ya leo itakuwa ugenini mjini Monrovia, Liberia kusaka heshima barani Afrika ikitarajiwa kuvaana na timu ya maafande ya Barrack YC II katika pambano la kwanza la raundi ya kwanza ya michuano ya Kombe la Shirikisho.
Kikosi cha timu hiyo kimeeleezwa kipo tayari kwa pambano hilo, japo itawakosa baadhi ya nyota wake ambao wamepatwa na matatizo ya kiafya wakiwa njiani, lakini waliosalia wameapa kupigana kuhakikisha wanapata ushindi katika mechi hiyo ya leo kabla ya kurudiana na wapinzani wao nchini wiki mbili zijazo.
Azam inahitaji ushindi wa aina yoyote ili kujiwekea mazingira mazuri kwa mechi ijayo mwezi Aprili, hasa ikizingatiwa kiu yao kubwa ni kuona inafika mbali na kuonyesha mfano kwa klabu nyingine za Tanzania ambazo kwa miaka nenda rudi zimekuwa zikiiwakilisha nchi bila ya tija yoyote ya maana.
Afisa Habari wa Azam alinukuliwa jana akisema kuwa kikosi chao kipo imara na wamekuwa wakichimbwa mkwara na mashabiki wa timu yao wakionyeshwa kuwa leo watagongwa mabao mawili au matatu.
"Mashabiki wa mpira wa hapa kila tunapopita wanatuonyesha vidole viwili wengine vitatu kama ishara kwamba tutanyukwa na timu yao mabao hayo, lakini sisi tumekuja hapa kwa ajili ya kupata matokeo mazuri," alisema Jaffar Idd Maganga 'Mbunifu'
Blog hii kwa niaba ya wasomaji wake wote wanaitakia kila la heri Azam iweze kupata ushindi mnono ili iendelee kuipeperuha bendera ya Tanzania kimataifa baada ya wawakilishi wetu wengine, Simba na Jamhuri Pemba kushindwa kuhimili vishindo mapema kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Wasauzi kuchapana kuwania nfasi ubingwa wadunia


MABONDIA wa Afrika ya Kusini Jeffrey Mathebula na Takalani Ndlovu watakutana katika ukumbi wa Carnival City Casino jijini Johannesburg jimbo la Gauteng nchini Afrika ya Kusini katika pambano la mchujo (Elimination Title) la ubingwa wa dunia uzito wa unyoya (Featherweight).
 
      
               Jeffrey Mathebula (kushoto) na Takalani Ndlovu (kulia) katika moja ya mapambano yao
Wawili hawa ni mahasimu wakubwa wanaojulikana nchini Afrika ya Kusini na walishakutana mara mbili ambapo Ndlovu alishhinda pambano la awali huku Mathebula akishinda pambano la mwisho.
Wakati huo huo mabondia Vusi Malinga wa Afrika ya Kusini na Diarh Gabutan wa Phillipines watakutana katika mpambano mwingine wa mchujo kuwania tiketi ya kukutana na bingwa wa dunia katika uzito wa Bantam.
Promota maarufu wa Afrika ya Kusini Branco Milenkovic wa kampuni ya Branco Boxing Promitions atakuwa ndiye mwandaaji wa mpambano huo utakaofanyika tarehe 23 mwezi wa tatu mwaka huu.
Huu ni mwendelezo wa Shirikisho la Ngumi la kKmataifa IBF katika programu yake ua “Utalii wa Michezo” barani Afrika ambapo imejiwekea lengo la mapambano 100 ya ubingwa mwaka huu.

Twanga Pepeta kuzindua Miss Tabata 2013 Pasaka


BENDI ya muziki wa dansi ya Africans Stars 'Twanga Pepeta' inatarajiwa kuzindua utambulisho wa warembo watakaochuana kwenye shindano la urembo la Tabata 'Miss Tabata 2013' siku ya Pasaka.
Utambulisho huo unatarajiwa kufanyika kwenye ukumbi wa Da West Park, Tabata jijini Dar es Salaam, ambapoa bendi hiyo maarufu kama 'Kisima cha Burudani' ndiyo itakayotoa burudani.
Mratibu wa shindano hilo Godfrey Kalinga alisema mashabiki na wapenzi wa fani ya urembo watapata fursa ya kuwaona warembo kabla ya fainali itakayofanyika Mei mwaka huu.
Utambulisho wa Miss Tabata 2013 imedhaminiwa na Konyagi, CXC Africa, Fredito Entertainment, Saluti 5 na Kitwe General Traders na kuandaliwa na Bob Entertainment na Keen Arts.
Mratibu huyo alisema warembo 25 wanaendelea na mazoezi kila siku katika ukumbi wa Da’ West Park, Tabata.
Washindi watano kutoka Tabata watafuzu kushiriki Miss Ilala baadaye mwaka huu.
Anayeshikilia taji la Miss Tabata ni Noela Michael ambaye pia ni Miss Ilala.