STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, September 6, 2010

Mpeni kura Mkullo, namuamini mno-Dk KIkwete


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni mgombea wa nafasi hiyo kwa tiketi ya CCM, Dk Jakaya Kikwete, amewaomba wakazi wa Jimbo la Kilosa, kumpa tena ubunge mgombea wa chama hicho na Waziri wa Fedha, Mustafa Mkullo kwa madai anamuamini.
Aidha mgombea huyo aliwaomba wapiga kura wa majimbo mengine yaliyopo wilayani Kilosa kuhakikisha wanaipa kura CCM kupitia viti vya ubunge na udiwani ili kumrahisishia kazi ya kuongoza nchi kwa mara ya pili mfululizo.
Akiwahutubia wakazi wa wilaya ya Kilosa kwenye mkutano wake wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja uliopo njia panda Ilonga na Kimamba, Rais Kikwete alisema angependa kuona wakazi wa Kilosa wakimpa tena ubunge waziri Mkullo kwa vile ni mmoja wa mawaziri anayewaamini.
"Naombeni mnichagulie tena Mkullo kuwa Mbunge wa Kilosa kwa kuwa kumuamini kwangu ndiko kulikonifanya nimpe dhamana ya kuwa Waziri wa Fedha na Uchumi," alisema Dk Kikwete.
Dk Kikwete alisema, chini ya Mkullo Kilosa imeweza kupiga hatua kubwa ya maendeleo kwa serikali yake kushawishika kuidhinisha fedha za miradi ya maendeleo katika sekta za elimu, afya, maji, umeme na barabara.
Pia mgombea huyo wa Urais, aliwaomba wakazi wa wilaya hiyo kuwachagua pia wagombea wengine wa majimbo ya Gairo na Mikumi pamoja na wale wa udiwani wa kata zilizopo wilayani humo ili kumrahisishia kazi katika kuwaletea maendeleo katika maeneo yao.
Naye Mkullo, alipopewa nafasi ya kuwasalimia wapiga kura wake, aliwaomba wampigie kura na kumpa ubunge kwa mara ya pili ili aweze kukamilisha baadhi ya ahadi zake alizowatolea kwenye uchaguzi uliopita wa mwaka 2005.
"Sina cha ziada ila kuwaomba mnichague tena kwa awamu ya pili ya kiti cha jimbo la ubunge la Kilosa ili kutekeleza ahadi zangu na kuwaletea maendeleo kwa ujumla kwa sababu nia na sababu ninayo," alisema Mkullo.
Akisoma Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2005, Katibu wa CCM wilayani Kilosa, Gervas Makoye, alisema asilimia kubwa zimetekelezwa au kuanza kutekelezwa na hivyo ni fursa ya wakazi wa mji humo kuhakikisha wanaichagua tena CCM Oktoba 31, ili kujiletea maendeleo ya kweli.

Mwisho