STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, July 21, 2013

Maskini! Papii Kocha alilia tena Rais Kikwete

MUIMBAJI Nyota wa zamani wa bendi ya FM Academia, Papii Kocha amemuandikia ombi jingine maalum Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete kumuomba MSAMAHA wa kufutiwa adhabu yake ya kifungo cha maisha jela alichopewa yeye na wanafamilia yake kwa kesi ya kubaka.
Ujumbe huo unaelezwa ni wa mara nyingine tena kwa msanii huyo aliyepo gerezani na baba yake, japo hakujawa na hakika kama barua hizo zinamfikia Mheshimiwa na kuzisoma au la. Ebu isome mwenyewe barua hiyo ya 'Mwana Mfalme' Papii Kocha kwenda kwa Rais Jakaya Kikwete...inaumiza!
MF/NA: 836'04 Johnson Nguza
(Papii Kocha) Gereza Kuu Ukonga
S.L.P 9091
Dar es Salaam
Mh. Rais Jamuhuri ya Muungano Tanzania

YAH: MAOMBI YA KUPEWA MSAADA (MSAMAHA) WA KUFUTIWA ADHABU YA KIFUNGO NILIYOPEWA NA MAHAKAMA YA HAKIMU MKAZI KISUTU.

Husika na somo hilo hapo juu. Mimi ni mfungwa katika gereza kuu Ukonga. Kwa heshma na taadhima na kwa kutambua utu na huruma yako ya kiMUNGU ulionayo dhidi ya binadamu wenzako pamoja na mamlaka uliokabidhiwa na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Naanguka na kushika miguu yako mitukufu muheshimiwa rais....Nakuomba msaada (msamaha) kwako muheshimiwa rais, kwa njia hii ya maandishi kusudi niweze kuondolewa adhabu ya kifungo cha maisha gerezani, niliyohukumiwa na mahakama tajwa hapo juu. Mh.Rais mimi nimefungwa nikiwa bado kijana mwenye umri mdogo, na ukweli kutoka moyoni sikufanya kosa hilo.

Si mimi, baba yangu Nguza wala ndugu yangu yeyote aliyefanya kitendo kile. Lakini wenye mamlaka wakatuona tuna hatia na kuamua kuteketeza kizazi chetu gerezani.

Natamani kiama ifike ili mwenyezi Mungu aweke wazi ukweli wote uliojificha nyuma ya pazia. Mpaka sasa natambua wazi hatima pamoja na dhamana ya maisha yangu ipo katika mikono yako mitukufu Mh. Rais Naomba huruma yako muheshimiwa Rais maana mimi ni mtoto wako ninaehitaji huruma yako wewe mzazi. Lakini pia sisi ni binadamu wenye nafsi na miili kama wengine. Waliotumia mamlaka yao kutuweka gerezani nao ni binadamu pia, wenye miili na nafsi.

Ipo siku nafsi zetu zitapaswa kutoa hesabu ya tuliyoyafanya hapa duniani. wakati huo miili yetu tunayoitumia kunyanyasa wanyonge itakuwa imeoza mavumbini.

Natumaini kauli yako ya mwisho ndio itakayoleta pumzi ya uhai nafsini mwangu. Nakutakia kazi njema, afya njema na maisha marefu. Mungu akubariki. Wako mtiifu

Mfungwa NO:836'04 JOHNSON NGUZA (PAPII KOCHA)
 
Udaku Specially

Kumbe Msajili wa Vyama alibariki CHADEMA kuunda 'jeshi'?!


  Nakala za majibu ya Ofisi ya Tendwa kwa CHADEMA zilipelekwa kwa
  • Waziri wa Mambo ya Ndani wakati huo, Omar Mapuri,
  • Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, aliyekuwa anashughulikia Habari na Siasa, Muhammed    Seif Khatib;
  • Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu;
  • Inspekta Jenerali wa Polisi na
  • Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai

LICHA ya kuwapo kwa shutuma mbalimbali zinazopinga mpango wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuanzisha kikundi cha, kujihami cha Red Brigade kitakachotoa ulinzi kwa viongozi wao, imebainika kuwa msajili wa vyama vya siasa nchini, John Tendwa alitoa baraka za kuanzishwa kwake.

Tanzania Daima imeona nakala ya barua ya mwaka 2005 kutoka katika ofisi ya Tendwa, ikionyesha kubariki jambo hilo ambalo katika siku za hivi karibuni limezua gumzo kubwa na kusababisha Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, kuhojiwa na polisi kuhusiana na kauli zake.

Uchunguzi wa kina uliofanywa na Tanzania Daima umebaini kuwa Desemba 30, 2004 ofisi ya msajili wa vyama siasa ilimwandikia Katibu Mkuu wa CHADEMA barua yenye kumbukumbu Na. RPP/CHADEMA/72/29 ikitaka ufafanuzi baada ya kusikia kupitia vyombo vya habari kuwa chama hicho kinataka kuanzisha kikundi cha kujihami (Red Brigade). “Kulingana na Ibara ya 9 (2) (c) ya Sheria Na. 5 ya Vyama vya Siasa 1992, ibara ya 147 na 148 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sheria ya Jeshi la Polisi, kuanzishwa kwa kikundi hicho ni kinyume cha sheria hizo,” imeeleza sehemu ya barua hiyo.

Barua hiyo ambayo Tanzania Daima inayo iliyosainiwa na Hilda Lugembe kwa niaba ya msajili wa vyama vya siasa, inaeleza kuwa kuvunjwa kwa sheria hizo kutasababisha CHADEMA kufutwa. CHADEMA baada ya kupata barua hiyo, Januari 6 mwaka 2005 iliijibu kuwa kikundi kinachozungumziwa ni walinzi wa ndani ya chama, vijana wa kike na wa kiume, wanachama wa CHADEMA, watu wasio na silaha, chini ya usimamizi wa kurugenzi ya ulinzi na usalama ya chama hicho. “Kikundi kinachokusudiwa kuundwa ni kutokana na Katiba ya CHADEMA ambayo inaruhusu uundwaji wa Kurugenzi ya Ulinzi na Usalama chini ya Katiba ya CHADEMA, kifungu cha 7.6.4 (h),” inaeleza barua ya CHADEMA yenye kumbukumbu Na. C/HQ/ADM/64 iliyosainiwa na Suzan Kiwanga kwa niaba ya Katibu Mkuu wa CHADEMA. Chama hicho kiliilaumu serikali kwa vitisho ilivyotoa vya kutaka kukifuta endapo kingeendelea na kusudio la kuanzisha kikundi hicho.

Barua ya ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa nchini ya kuithinisha uanzishwaji

Hata hivyo, baada ya ufafanuzi huo, Januari 11 mwaka 2005, ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, ilipopata majibu hayo ya CHADEMA, ilieleza kuwa kwa madhumuni yaliyoelezwa na chama hicho inakubaliana na malengo ya kuanzisha kikundi cha ulinzi kwa ajili ya usalama wa ndani ya chama. “Ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, kwa madhumuni mliyoyatoa kwenye barua yenu C/HQ/ADM/62 inakubaliana na maelezo yenu ya kuanzishwa kwa kikundi cha ulinzi kwa ajili ya usalama wa ndani ya chama ingawa Katiba ya CHADEMA haijatoa ufafanuzi huo, vinginevyo tunawatakia kila la heri kwenye matayarisho ya uundwaji wa kikundi hicho,” ilisema barua ya msajili wa vyama vya siasa nchini.

Barua hiyo yenye kumbukumbu Na. RPP/CHADEMA/72/32 iliyosainiwa na Hilda Lugembe kwa niaba ya msajili wa vyama vya siasa nchini, pia iliwatakia kila la heri CHADEMA kwenye matayarisho ya uundwaji wa kikundi hicho.

Nakala za majibu ya Ofisi ya Tendwa kwa CHADEMA zilipelekwa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani wakati huo, Omar Mapuri, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, aliyekuwa anashughulikia Habari na Siasa, Muhammed Seif Khatib; Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu; Inspekta Jenerali wa Polisi na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai

TANZANIA DAIMA

Golden Bush Veterani waikwanyua Faru Dume x3

Golden Bush Veterani a.k.a 'Wazee wa Dozi' katika moja ya mechi zao
WAKALI wa soka la maveterani jijini Dar es Salaam, Golden Bush Veterani jana asubuhi wameikwanyua bila huruma, Faru Dume ya Manzese kwa kuicharaza mabao 3-1 katika pambano la kirafiki lililochezwa kwenye uwanja wa Kinesi, Ubungo jijini Dar es Salaam.
Golden Bush ilipata ushindi wake huo mnono kupitia mabao ya Waziri Mahadhi 'Mandieta', Kudra Omar na Ally Chuo yaliyotosha kuizima Faru katika pambano hilo.
Uongozi wa Golden Bush ulisema umeridhishwa na kiwango cha timu yake na kwa sasa wanaendelea kujipanga kwa ajili ya mechi nyingine za kirafiki ili kugawa 'dozi' kwa wapinzani wao watakaoshuka mbele yao.

Mr Bomba kuagwa kesho kuzikwa kwao Mpwapwa

REV. John Makanyagana
Msanii John Makanyaga (Mchungaji) 'Mr Bomba' enzi za uhai wake


http://www.bongocinema.com/images/products/dangerous_deal.jpg
Moja ya kazi za mwisho mwisho za marehemu Mr Bomba

MWILI wa msanii nyota wa zamani wa Kaole Sanaa, John Makanyanga maarufu kama Mr Bomba unatarajiwa kuagwa kesho jijini Dar es Salaam kabla ya kusafirishwa Mpwapwani, Dodoma kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika siku ya Jumanne.
Kwa mujibu wa mmoja wa wasanii wenzake ambaye hivi karibuni walitoka na filamu mpya iitwayo 'Dangerous Deal', Adam Malele 'Swebe Santana' ni kwamba mwili wa msanii huyo aliyerafiki jana katika Hospitali ya Taifa Muhimbili utaagwa kesho Jumatatu kabla ya kusafirishwa jioni kuepekwa Mpwapwa.
Swebe, ambaye anayemlilia Mr Bomba na kudai ni mtu aliyekuwa naye karibu tangu wakiwa wote Kaole, alisema mwili huo utaagwa nyumbani kwa marehemu Buguruni Malapa karibu na Kanisa la Anglikana, jijini Dar.
"Kwa taarifa ambazo mpaka muda huu nilizonazo ni kwamba marehemu ataagwa kesho kabla ya kusafirishwa kwao Mpwapwa Dodoma kwa ajili ya mazishi ambayo yatafanyika siku ijayofuata," alisema.
Mr Bomba, ambaye kitaaluma alikuwa ni mwalimu aliyewahi kufundisha Shule ya Sekondari Makongo na nyingine binafsi eneo la Mbezi, alifariki jana baada ya kusumbuliwa kwa muda mrefu na kansa ya uvimbe wa kwenye ini mbali na sanaa na ualimu pia alikuwa Mtumishi wa Mungu akiwa kama Mchungaji wa Kanisa la Anglikana.
Enzi za uhai wake msanii huyo aliyejaliwa mwili mkubwa alitamba na tamthilia mbalimbali akiwa na kundi la Kaole Sanaa iliyokuwa ikirushwa na kituo cha ITV, akimudu zaidi nafasi ya 'kibosile' na wakati mwingine kama 'mafia' anayehusika na biashara ya dawa za kulevya na alicheza filamu kadhaa ikiwamo 'Kidole Tumbo', iliyozuiwa kuingizwa sokoni.
Mbali na uigizaji, pia marewhemu alikuwa mtunzi, mwandishi wa miswada ya filamu na kazi ya karibu kuiandaa ni Dangerous Deal ambayo aliitunga na kuiandikia mswada mwenyewe na kuongoza na Swebe ambapo mbali na kuichezea yeye mwenyewe, pia aliigiza na Swebe, Chuchu Hans, Hashim Kambi, Sebastian Mwanangulo, Mama Sonia na wengine.

Mungu aiweke mahali pema roho ya marehemu Mr Bomba.

Waamuzi wa Madagascar kuzihukumu Stars, The Cranes

Stars na Uganda the Cranes walipoumana wiki iliyopita katika pambano lao la kwanza la CHAN na Stars kulala kwa bao 1-0
Na Boniface Wambura
SHIRKISHO la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeteua waamuzi kutoka Madagascar kuchezesha mechi kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Uganda (The Cranes) itakayochezwa Jumamosi (Julai 27 mwaka huu) Uwanja wa Mandela ulioko Namboole nje kidogo ya Jiji la Kampala.

Waamuzi wataongozwa na Kanoso Abdoul Ohabee wakati mwamuzi msaidizi namba moja ni Andirvoavonjy Pierre Jean Eric. Mwamuzi msaidizi namba mbili ni Jinoro Velomanana Ferdinand huku Andriamiharisoa Hubert Marie Bruno akiwa mwamuzi wa mezani (fourth official).

Kamishna wa mechi hiyo ya marudiano ya raundi ya mwisho kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) ni Ismail Kamal kutoka Ethiopia.

Mechi hiyo namba 38 itachezwa kuanzia saa 10 kamili jioni kwa saa za Afrika Mashariki. Taifa Stars ilipoteza mechi ya kwanza iliyochezwa Julai 13 mwaka huu jijini Dar es Salaam kwa bao 1-0.

Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager iko kambini jijini Mwanza ikijiandaa kwa mechi hiyo itakayoamua ni timu ipi kati ya hizo mbili itacheza Fainali za CHAN mwakani nchini Afrika Kusini.

Mmiliki wa Home Shopping Centre amwagiwa tindikali


Duka moja wapo la Home Shopping Centre lililopo jijini Dar es Salaam 

MTU asiyejulikana juzi usiku alimvamia mmiliki wa maduka ya Home Shopping Centre, Said Mohammed Saad  na kumwagia maji usoni yanayodhaniwa kuwa ni tindikali.
Tukio hilo lililotokea juzi saa 1 usiku karibu na kituo cha Polisi cha Oysterbay, lilithibitishwa na Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Ally Mlege kwa kusema kuwa bado polisi wanaendelea na uchunguzi wao ili kuwabaini waliohusika.
“Ni kweli tukio hili limetokea ila polisi wanaendelea na uchunguzi. Tukikamilisha uchunguzi tunatarajia kutoa taarifa kamili za tukio zima,” alisema na kuongeza;
“Hatuna haja ya kuficha ukweli wa tukio hili, uchunguzi wetu ukikamilika na watuhumiwa wakikamatwa kila mtu atajua.”
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya Jeshi la Polisi zilizolifikia gazeti hili zilieleza kuwa mtu huyo, alimkuta Saad akiwa anazungumza na mmoja wa wafanyakazi wake katika duka lake jipya lililopo karibu na Kituo cha Polisi cha Oysterbay.
“Wakati akizungumza na mfanyakazi wake, huyo mtu alikuwa kama anapita na alichomoa kitu fulani na kummwagia Saad usoni na kisha kukimbia,” zilieleza taarifa hizo na kuongeza;
“Baada ya tukio hilo alipelekwa katika Hospitali ya AMI, sasa hatujui kama bado yupo hapo au ameondoka, ila sisi tulizungumza naye na alitueleza mwonekano wa mtu aliyemwagia tindikali.”
Taarifa hizo zilifafanua kwamba polisi wanazitumia taarifa hizo walizopewa na Saad, ili kuweza kumkamata mhusika.
Taarifa hizo zilifafanua kuwa polisi wanapanga tena siku ya kumhoji kwa mara ya pili Saad, kwamba watataka kufahamu kama mfanyabiashara huyo alikuwa akipewa vitisho au ujumbe wowote, kabla ya kukutwa na tukio hilo.
Hata hivyo, habari nyingine zilizolifikia Mwananchi Jumapili zilieleza kuwa mtu huyo baada ya kummwagia Saad tindikali, alipanda pikipiki na kutokomea eneo hilo.
“Walikuwa wawili, mmoja alikwenda kufanya unyama na mwingine alibakia katika pikipiki, baada tu ya kumwagia tindikali mtu yule alikimbia mpaka pale alipokuwa imesimama pikipiki, alipanda na kuondoka kwa kasi,” zilieleza habari hizo.
Taarifa zilizopatikana jana asubuhi zilieleza kuwa ndugu na marafiki wa mfanyabiashara huyo, walikuwa katika mipango ya kumpeleka nje ya nchi kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi.

MWANANCHI

Picha za matukio ya miili ya wanajeshi waliouwawa Darfur


MKUU WA MAJESHI GENERALI DAVIS MWAMUNYANGE AKISUBIRI KUPOKEA MIILI YA VIJANA WAKE WALIOUAWA SUDAN
BAADHI YA VIONGOZI WA SERIKALI WAKIONGOZWA NA MAKAMU WA RAIS DR MOHAMMED GHARIB BILAL

MAMA SALMA KIKWETE NA MKUU WA MKOA WA DAR ES SALAAM NAO WALIKUWEPO


NDEGE ILIYOBEBA MIILI YA WANAJESHI MARA BAADA YA KUWASILI KUTOKA SUDAN


MIILI YA WANAJESHI 7 WALIOUAWA SUDAN IKIONEKANA KWENYE NDEGE MARA BAADA YA KUWASILI
WANAJESHI WA JWTZ WAKIBEBA MIILI YA WENZAO WALIOUAWA HUKO SUDAN
NDUGU JAMAA NA MARAFIKI WAKISUBIRI KUWASILI KWA MIILI YA WANAJESHI WALIOUAWA SUDAN
ILIKUWA NI VIGUMU KUVUMILIA HALI HII BAADA YA KUONA MIILI YA WAPENDWA WAO
HALI ILIKUWA YA MACHUNGU KWA NDUGU WA KARIBU
WANAJESHI WA JWTZ WAKIPOKEA MIILI YA WENZAO
MIILI IKITOLEWA KWENYE NDEGE
MMOJA KATI YA MIILI YA MAREHEMU UKIINGIZWA KWENYE GARI
MOJA KATI YA FAMILIA ZA MAREHEM WALIOUAWA SUDAN
FAMILIA ZA MAREHEM WAKISUBIRI KUWAPOKEA WAPENDWA WAO
Miili ya wanajeshi saba mashujaa wa Tanzania waliofariki wakiwa kazini wakitekeleza ulinzi wa amani wa kimataifa katika mkoa wa Darfur nchini Sudan, iliwasilia jana ndege maalumu ya Umoja wa Mataifa.

Kaimu Mkurugenzi wa habari wa JWTZ, Meja Joseph Masanja amesema miili hiyo iliwasili Jumamosi majira ya saa 9.45 alasiri katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa JNIA na imehifadhiwa katika hospitali ya jeshi ya Lugalo hadi Julai 22 ambapo itaagwa rasmi.

Miili iliyowasili ni ya Sajenti Shaibu Othuman, Koplo Oswald Chaula, Koplo Mohamed Juma, Koplo Mohamed Chikilizo, Pte. Rodney Ndunguru, Pte. Peter Werema na Pte. Fortunatus Msofe.

Shughuli za kuagwa miili ya wanajeshi hao zitafanyika katika viwanja vya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la kujenga taifa vilivyoko Upanga jijini Dar es salaam.

Kuwapoteza wanajeshi hawa ni la kwanza na kubwa kwa nchi ya Tanzania tangu Tanzania ilipoanza kuchangia walinzi wa amani chini ya Umoja wa Mataifa mwaka 2007. Wanajeshi wengine watatu wa Tanzania walifariki dunia mwezi uliopita baada ya chombo chao cha kusafiria kusombwa na maji ya mto uliokuwa umefurika huko nchini Sudan. 

 
BONGOCLAN

TFF YAMLILIA KOCHA WA ZAMANI WA TAIFA STARS

Bert Trautmann
Na Boniface Wambura
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha kocha wa zamani wa Taifa Stars, Bert Trautmann (89) kilichotokea jana (Julai 19 mwaka huu) nchini Hispania.

Kabla ya kuwa kocha, Trautmann aliyezaliwa 1923 mjini Bremen, Ujerumani alikuwa kipa wa timu ya Manchester City ya Uingereza ambapo anakumbukwa kwa kucheza mechi ya fainali ya Kombe la FA dhidi ya Birmingham City akiwa amevunjika shingo.

Manchester City ilishinda fainali hiyo iliyochezwa mwaka 1956 mabao 3-1. Trautmann ambaye aligongana na mshambuliaji wa Birmingham, Peter Murphy zikiwa zimesalia dakika 17 mechi hiyo kumalizika aligundua kuwa amevunjika shingo siku tatu baadaye.

Mbali ya kuwa kocha wa Taifa Stars mwanzoni mwa miaka ya 60, Trautmann pia alikuwa mkufunzi wa makocha ambapo hapa nchini aliendesha kozi mbalimbali zilizotoa makocha waliokuja kutamba baadaye.

TFF itamkumbuka Trautmann kwa mchango wake aliotoa katika maendeleo ya mpira wa miguu nchini ikiwemo wazo lake la kuanzishwa kwa Ligi Kuu (Daraja la Kwanza) ambalo alilitekeleza katikati ya miaka ya 60.

Msiba huo ni pigo kwa familia ya Trautmann, TFF na familia ya mpira wa miguu kwa ujumla nchini kutokana na mchango alioutoa kwa Tanzania hasa wakati akiwa kocha na mkufunzi wa makocha.

TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Trautmann, Chama cha Mpira wa Miguu cha Ujerumani (DFB), Chama cha Mpira wa Miguu cha Uingereza (FA) na kuwataka kuwa na uvumilivu katika kipindi hiki cha msiba huo mzito.

Mungu aiweke roho ya marehemu Bert Trautmann mahali pema peponi. Amina