STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, October 31, 2013

Je wewe ni msomi jisome uende kwenye usaili wa Polisi


Jeshi la Polisi Tanzania linawaita kwenye usaili wahitimu walioorodheshwa hapa chini wa vyuo vya Elimu ya Juu na  vya Ufundi  Stadi. 
Usaili utafanyika kuanzia tarehe 11/11/2003 hadi tarehe 15/11/2013 saa mbili asubuhi hadi saa kumi jioni kila siku kwa taaluma na maeneo yafuatayo;
  •  Fani za Menejimenti  ya Rasilimali Watu, Utawala, Uchumi, Usimamizi wa Sheria na Utekelezaji(BaLe), Ualimu, Sosholojia, Saikolojia na Ushauri Nasihi, Sheria, Takwimu, Lugha, Uhusiano wa Kimataifa, Uandishi wa habari na Mawasiliano ya Umma, Maendeleo ya Jamii, Ukutubi na Utunzaji Kumbukumbu. Usaili  wa fani hizi  utafanyika katika chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es salaam(DPA) kilichopo kando kando ya barabara ya Kilwa Kurasini Dar es salaam .
  • Fani ya Udereva ,Ufundi rangi za magari(spray and Painting /Panel Beating ), Ufundi wa matengenezo ya Magari Makubwa(Auto-Mechanics-Heavy Duty) na Ufundi wa Matengenezo ya Umeme wa Magari(Auto Elecrical ). Usaili wa  fani hizi utafanyika Kikosi cha Polisi Ufundi kilichopo kando kando ya barabara ya Kilwa Kurasini Dar es salaam.
  • Fani za Kompyuta. Usaili wao utafanyika nyuma ya kikosi cha Ufundi yaani  TEHAMA KEKO chini.
  • Fani ya Uhandisi Mitambo(Mechanical Engineering ). Usaili wao utafanyika Kikosi cha Polisi Anga kilichopo Uwanja wa Ndege JK Nyerere DSM.
  • Waataalam wa masuala ya Afya/Wauguzi usaili wao utafanyika katika kikosi cha afya kilichopo kando kando ya barabara ya Kilwa Kurasini Dar es salaam.
  • Orodha  ya majina inapatikana  pia katika Gazeti la habari Leo la tarehe  04/11/2013.
   Muhimu: 
  1. (i)Mwombaji afike kwenyeakiwa na nakala  halisi  pamoja na kivuli cha  vyeti vyote vya masomo/Taaluma [Academic Transcript (s)/Certificate(s)]yaani  kidato cha nne, sita ,Chuo na cheti cha kuzaliwa.Hati ya kiapo cha kuzaliwa haitakubalika. 
  1. (ii)Mwombaji aliyeitwa kwenye usaili atalipia gharamaupimaji afya  shilingi elfu kumi(10,000), usafiri, chakula na malazi kwa muda wote wa zoezi la usaili.
 (iii)Kwa kuwa  muda ni mchache  anaekuja kwa usaili ajiandae baada ya usaili atakaechaguliwa  atapelekwa katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Moshi siku nne baada ya usaili kwisha yaani tarehe 19/11/2013.
 Orodha ni kama ifuatavyo;

BOFYA HAPO CHINI UDOWNLOAD MAJINA

SOURCE: http://www.policeforce.go.tz

Maskini Mzee huyu afa ghafla mahakamani

Tiger Mwaigomole (70) Mkazi wa kata ya Masukulu wilayani Rungwe amefariki dunia ghafla akiwa katika chumba cha Mahakama ya Wilaya ya Rungwe akifuatilia mwenendo wa kesi inayomkabili mtoto wake wakati Mahakama ikiendelea.

MTU mmoja aliyefahamika kwa jina la Tiger Mwaigomole (70) Mkazi wa kata ya Masukulu wilayani Rungwe amefariki dunia ghafla akiwa katika chumba cha Mahakama ya Wilaya ya Rungwe akifuatilia mwenendo wa kesi inayomkabili mtoto wake wakati Mahakama ikiendelea.
Tukio hilo la aina yake lilitokea hivi karibuni majira ya saa 9 alasiri ndani ya Mahakama hiyo ambapo Marehemu alifika mahakamani hapo akiwa na mwanaye aliyejulikana kwa jina la Lusajo Tiger (40) wakiwa na lengo la kumwekea dhamana ndugu yao Gwakisa Tiger ambaye alifikishwa mahakamani hapo akituhumiwa kwa kosa la kupigana na kujeruhi katika ugomvi uliotokea kijijini kwao.
Kwa mujibu wa mtoto wa Marehemu aliyekuwa ameongozana nae Mahakamani hapo Lusajo Tiger alisema wakati kesi ikiendelea chini ya Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Rungwe, Kingwele, ndugu yao alipandishwa kizimbani kusomewa mashtaka yanayomkabili ndipo marehemu alipoanza kutetemeka kwa madai kuwa anajisikia baridi kali sana.
Alisema kutokana na marehemu kulalamikia baridi aliamua kumnunulia chai ya moto ili anywe na kupunguza baridi ambapo baada ya kufanya hivyo marehemu alikata roho muda mfupi baada ya kumaliza kunywa chai aliyokuwa amepelekewa huku akiwa amekaa ndani ya chumba cha mahakama hiyo.
Kutokana na tukio hilo Askari polisi waliokuwepo mahakamani hapo waliuchukua mwili wa marehemu na kuukimbiza katika Hospitali ya Wilaya ya Rungwe Makandana kwa ajili ya vipimo lakini hata hivyo mwili ulikabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya taratibu za mazishi ingawa ripoti ya kifo chake haikutolewa mapema.
Wakati huo huo Hukumu ya kesi ya mauaji dhidi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Rungwe, John Mwankenja inayowakabili Hakimu Mwakalinga na wenzie watatu huenda ikatolewa Novemba 11 mwaka huu baada ya Mahakama kuu kanda ya Mbeya chini ya Jaji Samwel Karua kumaliza kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka pamoja na utetezi kwa upande wa watuhumiwa.
Kwa mujibu wa Jaji Karua alisema baada ya kumaliza kusikiliza pande zote mbili atatumia muda wa siku mbili kwa ajili ya kuandika hukumu ambayo itaitoa Novemba 11, Mwaka huu, kesi ambayo inasimamiwa na Mwanasheria wa Serikali Archiles Mulisa huku watuhumiwa wakitetewa na Mawakili wawili wa kujitegemea ambao ni Simon Mwakolo na Victor Mkumbe.

Na Mbeya yetu

Simba yavutwa mkia jioni, mashabiki wang'oa viti FFU yawafurumusha kwa mabomu ya machozi

Kagera walioinyima raha Simba leo Taifa
BAO la mkwaju wa penati lililofungwa dakika za majeruhi na beki Salum Kanoni limeisaidia Kagera Sugar kunusurika kipigo toka kwa Simba baada ya kulazimisha sare ya 1-1 katika pambano la Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mwamuzi Mohammed Theophile wa Morogoro alitoa penati hiyo baada ya mabeki wa Simba kumuangusha Jumanne Daudi katika lango lao na kusababisha vurugu kubwa kutoka kwa mashabiki wa Simba ambao wanadaiwa walikuwa waking'oa viti na kulazimisha FFU kuvurumusha mabomu ya machozi.
Kabla ya penati, Simba ilionekana kuelekea kuibuka washindi katika pambano hilo lililokuwa kali kwa bao la dakika za majeruhi ya kipindi cha kwanza lililofungwa na Mrundi Amissi Tambwe.
Tambwe alifunga bao hilo kwa shuti kali na kuifanya Simba iende mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0 ambalo liliendelea mpaka ilipofika dakika nne za nyongeza wakati Kagera waliposhambulia lango na wekundu hao wa msimbazi na kumchezea vibaya Daud.
Kitendo cha kutolewa kwa penati hiyo ilionekana kuwakera benchi nzima la Simba pamoja na mashabiki wao, lakini mwamuzi alisimamia msimamo wake na Kanoni aliyewahi kuichezea Simba kufunga bao hilo na kufanya mashabiki wa Msimbazi kuanza kung'oa viti kwa hasira.
Kwa matokeo hayo ya sare hiyo, Simba imeshindwa kurejea kileleni kwa kufikisha pointi 21 inayowafanya wasalie katika nafasi yao ya nne waliokuwa wakiishikilia nyuma ya Yanga ambayo kesho itashuka kwenye uwanja huo kuvaana na JKT Ruvu.
Azam na Mbeya City zinaendelea kubaki kileleni zikiwa na pointi 23 na Yanga wakifuatia nafasi ya tatu wakiwa na pointi 22 na kama kesho watashinda wanaweza kukaa kileleni mpaka Jumamosi wakati Azam itakaposhuka dimbani kuvaana na Ruvu Shooting.

Gareth Bale aanza mambo Real Madrid, Ronaldo aweka rekodi

Bale na Ronaldo wakipongezana
Bale akishangilia moja ya mabao yake ya jana
 WINGA nyota wa Wales, Gareth Bale ameanza kuonyesha cheche zake baada ya usiku wa kuamkia leo kufunga mabao mawili na kutengeneza mengine wakati Real Madrid wakishinda mabao 7-3 dhidi ya Sevilla.
Wakati Bale akionyesha uhalisia wa thamani ya donge nono alilosajiliwa na klabu hiyo ya Hispania, Mreno Cristiano Ronaldo alitupia kambani mabao matatu na kuweke rekodi.
Kocha Carlo Ancelotti aliwachezesha kwa pamoja washambuliaji hao na kuifanyia maafa makubwa Sevilla iliyomaliza mchezo ikiwa pungufu.
Bale lilikuwa pambano lake la kwanza kucheza kwa muda wote wa dakika 90 tangu aliposajiliwa na timu hiyo hivi karibuni.
Winga huyo alifunga mabao yake katika dakika za 13 na 27, huku Ronaldo akifunga hat trick yake kwa mabao ya dakika ya 32 lililokuwa la penati na mengine ya dakika za 60 na 71,\ na kumfanya awe mchezaji wa nne aliyefunga mabao mengi katika La Liga kwa wachezaji wa Real Madrid alimpiku gwiji Ferenc Puskas.
Ronaldo amefikisha jumla ya mabao 157 moja zaidi la Puskas, nyota wa zamani wa klabu hiyo na nchi ya Hungary.
Mabao mengine wa washindi hao yaliwekwa kimiani na Mfaransa, Karim Benzema katika dakika za 53 na 80.
Wageni wa Real Madrid walipata mabao yao matatu kupitia kwa Rakitic  aliyefunga mawili moja likiwa la penati katika dakika ya 38 na lingine dk ya 63 huku Bacca akifunga pia.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo ya Hispania, Ososuna iliishindilia Rayo Vallecano kwa mabao 3-1 na usiku wa leo kutakuwa na michezo miwili itakayozikutanisha timu za Villarreal dhidi ya Gitafe na Granada itakayovaana na Atletico Madrid.


Hii ndiyo ratiba ya 8 Bora Capital One


MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya England Manchester United imepangiwa kucheza ugenini dhidi ya Stoke City katika pambano lake la Robo Fainali ya Kombe la Ligi (Capital One) baada ya FA kutangaza ratiba ya Nane Bora.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo ilivyo ni kwamba Manchester City nayo itacheza ugenini dhidi ya timu ya Daraja la Kwanza Leichester City, huku Tottenham Hotspur watakuwa nyumbani kuvaana na 'Wagonga Nyundo wa London' West Ham United.
Chelsea wenyewe wamepangiwa kuumana na mshindi wa mechi ya mwisho ya hatua ya nne ya michuano hiyo kati ya Sunderland na Southampton.

Tottenham, Manchester City zaifuata Chelsea, Man Utd Capital One League

Manchester City wakipongezana

Wachezaji wa Spurs wakipongeza baada ya kufuzu Roibo Fainali ya Capital One L:eague jana
TIMU za Tottenham Hotspur na Manchester City usiku wa kuamkia leo nazo zimefanikiwa kutinga hatua ya Robo Fainbaliu ya Kombe la League (Capital One) baada ya kupata ushindi kwa mbinde dhidi ya wapinzani wao kwenye mechi za raundi ya nne ya michuano hiyo.
Spurs ililazimika kusubiri mikwaju ya penati kuwavusha hatua hiyo mbele ya Hull City baada ya kumaliza dakika 120 zikiwa nguvu sawa ya kufungana mabao 2-2.
Ikicheza nyumba Spurs ilitangulia kupata bao la kuongoza dakika ya 16 kupitia kwa Gylfi Sigurdsson na kudumu hadi kipindi cha kwanza kinamalizika.
Kipindi cha pili kilianza kwa kipa wa Spurs, 'Babu' Brad Friedel kujifunga bao dakika ya 53 na kuisafanya Hull kupumua na kumaliza dakika 90 zikiwa bao 1-1 na katika dakika za 30 za nyongeza, McShane aliiandikia wageni bao dakika ya 99 kabla ya wenyeji kuchomoa dakika ya 108 baada ya Harry Kane kufunga bao na kuingia kwenye matuta ya penati.
Katika hatua hiyo Spurs ilifanikiwa kutumbukiza penati 8 na Hull City 7 na kufanya Spurs kuungana na vigogo vya Manchester United, Chelsea na Manchester City iliyopata ushindi wa mbinde ugenini dhidi ya  Newcastle United kucheza hatua ya Robo Fainali.
Man City iliishinda Newcastle 2-0 katika muda wa nyongeza baada ya awali kumaliza dakika 90 zikiwa nguvu sawa kwa kutofunagana.
Katika muda huo wa nyongeza mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu ya England walipata mabao yao dakikka za 99 na 105 kupitia kwa Negredo na Eden Dzeko.
Timu nyingine zilizofuzu hatua hiyo ya Robo Fainali ya Capital One ni Stoke City, West Ham United na Leicester City, huku timu ya mwisho kumalizia nafasi moja iliyosalia itasubiri matokeo ya wiki ijayo kati ya Sunderland dhidi ya Southampton itakayochezwa Novemba 6.

Serikali kuondoa kodi vifaa vya michezo


Waziri Makalla
SERIKALI imeahidi kulifanyia kazi suala la kuondolewa kodi kwa vifaa vya michezo vinavyoingizwa nchini, hususani kwa matumizi ya shule na taasisi ya michezo.
Kauli hiyo ilitolewa juzi bungeni na Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amosi Makalla alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Rage (CCM).
Mbunge huyo alitaka kujua serikali ina mpango gani wa kuhakikisha vifaa vya michezo vinafutiwa kodi.
Akijibu swali hilo, Makalla alisema serikali imechukua hoja hiyo kama changamoto na kwamba itawasilishwa kwa wanahusika, ili ione kama vifaa hivyo vinavyoagizwa kutoka nje ya nchi kama vinaweza kufutiwa kodi, wakati wa kuingizwa kwake.
Awali, katika swali la msingi Mbunge wa Singida Magharibi, Mohamed Missanga (CCM), alitaka kujua serikali imefikia hatua ipi katika kuendeleza mchezo wa riadha nchini, ikiwa ni pamoja na kupelekwa kwa wataalamu kwenye nchi za Ethiopia na Kenya ili kujifunza mchezo huo.
"Nchi za Kenya na Ethiopia zinafanya vizuri katika mchezo wa riadha wakati Tanzania haifanyi vizuri, je, serikali imefikia wapi katika kutekeleza ushauri wangu niliotoa mwaka 2011 wa kupeleka wataalamu katika nchi hizo hili kujifunza mbinu na mikakati ya kukuza mchezo huu nchini?" alihoji Missanga
Akijibu swali hilo, Makalla alisema wizara hiyo imebaini kuwa nchi hizo zina mafanikio katika mchezo huo kwasababu ya kuzingatia mambo mbalimbali muhimu.
Makalla alisema miongoni mwa mambo hayo ni uhamasishaji na msingi wa kushiriki mchezo huo kuanzia katika umri mdogo katika ngazi za shule za msingi ikiwa ni pamoja na serikali sekta binafsi kuwekezaji katika mchezo huo.
Aliongeza kuwa mambo mengine muhimu yafanywayo na nchi hiyo katika kukuza mchezo huo ni uwapo wa vituo na shule maalum za kuendeleza mchezo huo, pamoja na uongozi thabiti wa mashirika ya mchezo huo.
Makalla alisema kwa kuzingatia mambo hayo, serikali imeanza kuyafanyia kazi kwa kadri ya uwezo wake kwa kushirikiana na Chama cha Riadha Tanzania.

Rais JK kushiriki mbio za Uhuru Marathon

Rais Jakaya Kikwete

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete anatarajiwa kushiriki katika mbio maalum za Uhuru (Uhuru Marathon) zitakazofanyika Desemba 8 jijini Dar es Salaam imefahamika.
Mshindi wa jumla wa mbio hizo za marathoni (kilomita 42) atakabidhiwa zawadi ya Sh. milioni 3.5.
Akizungumza jana kwenye ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Katibu Mkuu wa kamati ya maandalizi ya mbio hizo, Innocent Melleck, alisema kuwa Rais Kikwete atakabidhiwa fomu namba moja ya kujisajili katika ushiriki wa mbio hizo huku akimtaja Spika wa Bunge, Anne Makinda kuwa atapewa fomu namba mbili.
Melleck alisema kuwa viongozi hao watashiriki mbio za kilomita tatu na kumtaja mshiriki mwingine wa mbio hizo ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni na Mbunge wa Jimbo la Hai, Freeman Mbowe.
Alisema kuwa tayari fomu za kujiandikisha zimeanza kutolewa katika vituo mbalimbali nchini jana huku zoezi hilo likitarajiwa kufanyika kwenye viwanja vya Bunge mkoani Dodoma Jumanne na Jumatano wiki ijayo.
Alisema ada ya fomu hizo kwa mbio za marathoni ni Sh. 6,000 huku za kilomita tano zikiwa ni Sh. 2,000 na zitashirikisha pia wanariadha kutoka nje ya nchi.
Alieleza kuwa lengo la kuanzisha mbio hizo ni kutaka kuenzi na kudumisha amani iliyopo nchini na kukumbushana kutochezea thamani hiyo.
"Kupitia mbio hizi tutaweka tofauti zetu pembeni, Tanzania kwanza, Amani Kwanza," alisema katibu huyo wa kamati ya maandalizi.
Aliwataka wadau na taasisi mbalimbali kujitokeza kudhamini mbio hizo zitakazokuwa zinafanyika kila mwaka nchini.